Post on 19-Oct-2018
1
HOTUBA YA MWENYEKITI WA CHAMA CHA
MAPINDUZI NA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, MHESHIMWIA JAKAYA MRISHO KIKWETE
WAKATI WA KUFUNGA SEMINA YA MAKATIBU WA
CCM MIKOA NA WILAYA NA WENYEVITI WA CCM WA
WILAYA, INAYOFANYIKA DODOMA
TAREHE 24 OKTOBA, 2013
Ndugu Phillip Mangula, Makamu Mwenyakiti wa CCM;
Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM;
Ndugu Manaibu wa Katibu Mkuu;
Ndugu Makatibu wa Sekretariat Mliopo;
Ndugu Wanasemina;
Ndugu Watoa Mada;
Mabibi na Mabwana;
Nakushukuru na kukupongeza sana Katibu Mkuu kwa
uamuzi wa busara wa kuwa na mafunzo haya kwa
Wenyeviti wa Wilaya, Makatibu wa Wilaya na Makatibu wa
Mikoa wa Chama chetu. Nafurahi kwamba mafunzo haya
yamefanyika wakati muhimu katika safari yetu ya kuelekea
2
mwaka 2015. Hivi sasa tupo takriban katikati ya safari hiyo.
Naamini mafunzo haya yatasaidia kujiweka sawa katika
ngwe ya pili ya kipindi cha pili cha uongozi wa Awamu ya
Nne ya uongozi wa CCM katika nchi yetu. Awamu ambayo
mimi ndiye kiongozi wake kwa niaba ya Chama chetu.
Ni mategemeo yangu kuwa baada ya mafunzo haya,
mijadala iliyofuatia na mapendekezo mliyoyatoa
mnaondoka hapa mkiwa manahodha bora zaidi wa
kuongoza vyema Chama cha Mapinduzi kwenda na kufika
salama katika safari yetu ya kuelekea 2015. Mnatoka kwenye
mafunzo haya mkiwa na kauli mbiu moja tu kwamba
“Ushindi ni Hakika mwaka 2014 na 2015”.
Lengo Kuu la Chama cha Siasa
Ndugu viongozi wenzangu;
Sote tunafahamu kwamba lengo kuu la Chama cha
Mapinduzi kama ilivyo kwa vyama vyote vya siasa nchini
na duniani ni kushika dola. Hivyo ndivyo Katiba ya CCM
inavyotamka wazi katika Ibara ya 5 kwamba malengo na
3
madhumuni ya CCM ni; Nanukuu “Kushinda katika
uchaguzi wa Serikali Kuu na Mitaa, Tanzania Bara
na Zanzibar ili kuunda na kushika Serikali Kuu na Mitaa
katika Jamhuri ya Muungano kwa upande mmoja na
Zanzibar kwa upande wa pili”. Katika mazingira ya nchi
yetu ni kushinda uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Wabunge,
Wawakilishi, Madiwani na ule wa viongozi wa Serikali za
Mitaa, Vijiji na Vitongoji. Hivyo pamoja na majukumu
mengine mengi mliyonayo lazima mtambue kwamba
hatimaye shabaha yetu kuu ni kuhakikisha kuwa wagombea
wa Chama chetu wanashinda katika chaguzi hizo.
Nyie kama viongozi na watendaji wakuu wa maeneo
yenu lazima mtambue kuwa chombo cha kutuongoza,
kutuimarisha na kutufikisha kwenye ushindi ni Chama cha
Mapinduzi. Hivyo basi, lazima Chama kiwe na nguvu ya
kutosha ya kutufikisha kwenye lengo letu kuu. Hamna budi
kila mnapofanya jambo mpime kama jambo hilo linakisaidia
4
Chama chetu kuwa na nguvu za kushinda uchaguzi au la.
Msifanye mambo yatakayoipunguzia CCM nguvu na
yanayojenga mazingira yatakayosababisha wagombea wa
CCM kushindwa na hivyo Chama chetu kushindwa.
Mkifanya hivyo mtakuwa hamkisaidii Chama chetu. Wakati
wote kila mmoja wetu ajiulize je hili nilifanyalo linasaidia
CCM kushinda? Au kwa lugha nyingine tujiulize ni kitu
gani nikifanya kinasaidia Chama cha Mapinduzi kushinda.
Uhai na Uimara wa Chama
Ndugu viongozi wenzangu;
Kwa maoni yangu kuna mambo matatu muhimu
ambayo yakifanyika yatasaidia Chama cha Mapinduzi
kushinda:-
(1) Uimara wa Chama;
(2) Tabia na mwenendo wa viongozi na wanachama wa
CCM; na,
(3) Utendaji wa Serikali ya CCM.
5
Inatupasa kuhakikisha kuwa Chama chetu kinashiriki
katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi
Mkuu kikiwa na nguvu kubwa, hai na imara kwa kila hali
toka ngazi ya shina, tawi, kata, jimbo, wilaya, mkoa hadi
taifa. Siku za nyuma nilishasema kuwa Chama ni kama
ulivyo mwili wa mwanadamu, uimara wake unategemea
sana ukamilifu na uzima wa viungo vyake. Kikipungua
kiungo kimojawapo Chama kina ulemavu na kikidhoofika
chochote kinakuwa na afya mbaya. Kwa ajili hiyo basi
uimara wa Chama cha Mapinduzi unategemea kuwepo kwa
wanachama, viongozi, watendaji, vikao, rasilimali na
jumuiya za Chama na vyote vikiwa vinafanya kazi zake
ipasavyo.
Ninyi mliopo hapa yaani Wenyeviti wa Wilaya,
Makatibu wa Wilaya na Makatibu wa Mikoa ndiyo
mnaotegemewa zaidi kuliko mtu mwingine yeyote
kuhakikisha kuwa viungo vya Chama vinakamilika na
kwamba viko hai kwa maana ya kufanya kazi kama
6
inavyotarajiwa kwa mujibu wa Katiba ya Chama cha
Mapinduzi, sera na maamuzi mbalimbali.
Ndugu viongozi;
Ni matumaini yangu na nimehakikishiwa hivyo
kwamba katika mafunzo haya mmepewa maarifa ya
kuhakikisha kuwa Chama cha Mapinduzi kinakuwa hivyo.
Mmejifunza juu ya nini mnachowajibika kufanya ili Chama
chetu kiwe imara, hai na chenye nguvu. Nimeambiwa pia
kuwa katika majadiliano mlipata nafasi ya kubadilishana
uzoefu kutoka kwa wale waliofanikiwa na hata wale
walioshindwa. Ndugu zangu mpate nini zaidi ya hayo.
Mfanyiwe nini tena lililo bora zaidi kuliko hilo. Ndiyo
maana sipati kigugumizi kusema kuwa sasa ninyi
mmekuwa wapiganaji bora zaidi. Haya nendeni mkaoneshe
umahiri wenu kwenye medani ya kujenga Chama. Nendeni
mkaoneshe mtindo bora wa uongozi na utendaji. Nendeni
mkakipe Chama chetu sura mpya, uhai mpya na kasi mpya
ya maendeleo.
7
Kuingiza Wanachama
Ndugu Viongozi;
Hatuna budi kwanza kabisa kuhakikisha kwamba
Chama chetu kinapata wanachama wapya wengi na
kuwaimarisha waliopo. Wanachama ndiyo kielelezo cha
awali cha kuwepo kwa Chama. Wingi wa wanachama ndio
nguvu ya kufanya kazi ya Chama na mtaji wa uhakika wa
kuanzia katika kutafuta ushindi. Hivyo basi, lazima wakati
wote Chama chetu kiendelee kuingiza wanachama wapya.
Tusisubiri mpaka karibu au wakati wa uchaguzi ndipo
tuongeze nguvu ya kusajili wanachama wapya. Twende
tukafanye kazi ndani ya umma kuwashawishi na
kuwahamasisha wananchi, hususan vijana, kujiunga na
Chama cha Mapinduzi. Mnapaswa kuwa na mikakati
madhubuti ya kupata wanachama wapya katika maeneo
yenu. Kupata wanachama wapya ni kazi ya kudumu ya
Chama.
8
Ndugu viongozi;
Kimsingi uimara wa Chama chetu unategemea uhai wa
wanachama wake. Mwanachama hai wa CCM ni yule
anayelipa ada na kushiriki kwa ukamilifu katika shughuli za
Chama, mojawapo ikiwa kuwashawishi watu wasiokuwa
wanachama kuunga mkono CCM. Ili wanachama wawe
hivyo ni wajibu wa viongozi kuwa na mikakati maalum ya
kuwawezesha kufanya hivyo. Kuwatembelea mara kwa
mara kuzungumza nao na kuwaelimisha mambo
mbalimbali yanayohusu Chama na nchi kwa ujumla ni
mbinu muhimu sana kwa ajili hiyo. Tukifanya hivyo
Chama chetu kitakuwa na wanachama wengi wanaojua
mambo na wenye moyo wa kukitumikia. CCM itakuwa na
uwezo mkubwa wa kujiendesha na kufanya mambo yake.
Kitakuwa kimeimarika zaidi. Viongozi wa Chama lazima
tujenge mazoea ya kuwatembelea wanachama na
kuzungumza nao. Hili ndilo jukumu la msingi na asiyefanya
hivyo ameshindwa kutimiza wajibu wake.
9
Ndugu zangu;
Ni ukweli ulio wazi kuwa si viongozi na watendaji
wengi wanaofanya hivyo. Lazima mjisahihishe. Zamani
mlidai hamna magari sasa mnayo. Kwa kweli
kutowatembelea wanachama ni jambo lisilokuwa na
maelezo. Nilishaagiza siku za nyuma na narudia kusisitiza
tena leo kuwa katika Taarifa ya kazi za Chama ya kila
mwezi kila Wilaya itoe taarifa ya kuhusu viongozi
kutembelea matawi na kuzungumza na wanachama. Hivyo
hivyo kwa Mikoa, nao watoe taarifa ya kutembelea Wilaya
zao na kuzungumza na viongozi wa Wilaya, Kata, Matawi
na Mashina pamoja na kuzungumza na wanachama. Ndugu
Katibu Mkuu naomba hili lazima tulidai lifanyike kwani
manufaa yake kwa uhai wa Chama cha Mapinduzi hayana
mfano wake.
10
Ndugu viongozi;
Jambo la pili muhimu kwa uhai na maendeleo ya
Chama chetu ni kuwatembelea wananchi na kuzungumza
nao. Ni vyema mkatambua kuwa tunapotaka kuongoza dola
kwa mfumo wa vyama vingi kazi yetu kubwa ni ile ya
kuwavutia watu upande wetu. Tushinde mioyo na akili zao.
Tuwafanye watu waelewe sera na siasa ya Chama cha
Mapinduzi, wazikubali na kutuunga mkono. Tufute maneno
hasi na uongo wa wapinzani dhidi ya CCM na serikali yake.
Lazima viongozi mtoke muwatembelee wananchi,
mzungumze nao kuhusu Chama chetu na taifa kwa ujumla.
Tumekuwa wazito sana kufanya hivyo, lazima tujirekebishe.
Utendaji wa Serikali
Ndugu viongozi na Watendaji;
Kwa vile hivi sasa CCM ndicho Chama tawala,
viongozi wa Chama wanaowajibu wa namna mbili. Kwanza,
kuhakikisha kuwa serikali yao inatekeleza Ilani ya Uchaguzi
11
na pili, kuwaelezea wananchi masuala mbalimbali ya
utendaji wa serikali. Viongozi wa Chama mmepewa
dhamana ya kuyasimamia hayo katika maeneo yenu.
Lazima mfuatilie utekelezaji wa Ilani kupitia vikao vyenu
hususan Kamati za Siasa na Halmashauri Kuu za Wilaya na
Mikoa. Ndiyo maana Wakuu wa Wilaya na Mikoa ni
wajumbe wa vikao hivyo na hutoa taarifa ya kazi nyakati
mbalimbali.
Ili muweze kufanya hivyo, lazima ninyi wenyewe
mfahamu vizuri Ilani ya CCM inasema nini kuhusu Mikoa
na Wilaya zenu. Pili, lazima mfahamu ahadi za wagombea
wa Chama chetu na za viongozi wa Chama katika ngazi
mbalimbali. Lengo ni kujua na kufuatilia utekelezaji wa
ahadi hizo ili zisije zikageuka kuwa tatizo katika uchaguzi
ujao. Tujue zipi zimetekelezwa, zipi hazijatekelezwa na
zilizotekelezwa zimetekelezwa kwa kiwango gani. Tujue
mipango iliyopo na nini kinapaswa kufanyika ili kutekeleza
au kukamilisha ahadi hizo. Tukumbushane mambo ambayo
12
hayajatekelezwa. Wakumbusheni Marais, Mawaziri,
Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Madiwani
na viongozi wa Serikali za Mitaa juu ya ahadi zao
walizozitoa ambazo hazijatekelezwa ili wazitekeleze au
wawe na mipango thabiti ya kutekeleza.
Pia, ziambieni serikai katika ngazi zote husika kuhusu
masuala mapya yaliyojitokeza ambayo wananchi wanataka
tuyatekeleze. Tukiweza kuyafanya na hayo pia
yatatuongezea kuaminika, kupendwa na kutuongezea
uhakika wa kuchaguliwa tena. Naomba mshirikiane na
viongozi wa Serikali katika maeneo yenu kutengeneza
utaratibu mzuri ili masuala hayo yajulikane na
kutengenezwa mkakati maalum wa kuyatekeleza.
Ndugu viongozi;
Tumieni vikao vyenu au njia nyingine za mawasiliano
kuyafikisha masuala hayo na mengine. Katika vikao hivyo
pia, Wakuu wa Wilaya na Mikoa wanao wajibu wa kuelezea
na kufafanua masuala mbalimbali yahusuyo Serikali au
13
Mkoa au Wilaya husika. Wajumbe waulize ili wapate
maelezo ya kusaidia kujibu hoja za wananchi au
wapotoshaji kwa kazi nzuri za serikali ya CCM.
Vikao
Ndugu Viongozi;
Hatuna budi kuhakikisha kuwa vikao vya Chama
vinafanyika na vinaendeshwa vizuri ili viweze kutekeleza
ipasavyo jukumu lake la kufuatilia utendaji wa serikali ya
CCM na uendeshaji wa Chama. Lazima vikao vya Kikatiba
vifanyike bila kukosa na pawepo na kalenda maalum kwa
ajili hiyo. Kuwa na kalenda inayojulikana ni muhimu kwa
wajumbe kwani wanashughuli zao zinazowapatia riziki
hivyo wakijua mapema vikao vya Chama watajua namna
bora ya kujipanga. Si vizuri taarifa ya vikao vya Kikatiba
ikatolewa kwa muda mfupi kana kwamba ni vikao vya
dharura.
Jambo lingine muhimu kuhusu vikao ni kuwa na
agenda za maana na zilizoandaliwa vizuri. Kwa mfano,
14
mnaweza mkaamua kila kikao kiwe na agenda ipi kuu
katika Wilaya na Mkoa wenu. Mathalani mnaweza kupanga
kuwa kikao cha mwezi fulani kiwe cha kupokea taarifa ya
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, cha mwezi fulani kupokea
taarifa ya uhai wa Chama na kadhalika. Mkifanya hivyo
mnajipa muda wa kushughulikia masuala muhimu. Hata
hivyo haizuiliwi kuzungumzia au kushughulikia masuala
mengine muhimu. Ni muhimu pia kuhakikisha kuwa vikao
vinaendeshwa vizuri na wajumbe wanapata nafasi ya kutoa
maoni yao kwa uhuru. Kumbukumbu za vikao ziandikwe
vizuri na kuhifadhiwa vizuri.
Ndugu Katibu Mkuu;
Chama lazima kiwe na utaratibu wa kuwafundisha
Makatibu Tawi, Makatibu Kata, Makatibu Wasaidizi,
Makatibu wa Wilaya na Mikoa kuhusu uandishi wa
kumbukumbu na namna ya kuzihifadhi na kuzifanyia kazi.
Lazima pia kiwe na utaratibu wa mafunzo kwa watumishi
na watendaji wake wa kada mbalimbali katika ngazi zote za
15
utumishi na utendaji. Chama kina mifumo yake na taratibu
zake za kuendesha shughuli ambazo lazima zifuatwe. Ni
lazima watu wafundishwe ili wazielewe na kuzifuata. Vile
vile ni muhimu Chama kuwekeza katika kuwaendeleza
watumishi na watendaji wake kielimu na kitaaluma. Aidha,
tuwalipe maslahi mazuri.
Mali za Chama
Ndugu Viongozi na Watendaji;
Jambo lingine muhimu sana katika kuimarisha Chama
ambalo naamini mmelizungumzia kwa undani ni rasilimali
za Chama kwa Chama kuwa na fedha, majengo, vyombo
vya usafiri na vifaa vingine vya kuendeshea shughuli zake
ni jambo la kufa na kupona. Lazima tuwe na fedha za
kutosha, majego mazuri ya kufanyia kazi, magari na
vyombo vingine vya usafiri na vifaa mbalimbali. Lazima
tuwe na mipango na mikakati dhabiti ya kuwa na rasilimali
hizo na hasa fedha. Katika historia ya Chama chetu vyanzo
vikuu vya fedha ni ada za wanachama, uuzaji wa vitabu na
16
mali nyingine za Chama na michango ya hiari. Hali ilivyo
sasa ni kwamba wanachama wamekuwa wazito kulipa ada,
vitabu na mali za kuuza hazipo za kutosha. Na michango ya
hiari haibuniwi. Kwa kweli, Chama siku hizi kinaendeshwa
kwa taabu. Wilaya na Mikoa hutegemea Makao Makuu
tofauti na ilivyokuwa zamani. Pale ambapo kuna wafadhili
ambao ni wabunge wajumbe wa NEC wenye uwezo na
wapenzi wa Chama mambo huwa mazuri. Pale ambapo
hawapo kuna shida. Aghalabu baadhi ya wafadhili au
wapenzi wa Chama ni watu wenye agenda zao. Ama wana
tamaa za kugombea uongozi fulani hivyo wananunua
kuungwa mkono au wanatafuta msaada fulani.
Mtakubaliana nami kuwa jambo hili muhimu sana kwa
uhai wa Chama lakini halijapata mwelekeo mzuri. Lazima
tubadilike tena tubadilike haraka vinginevyo mbele ya safari
hali itakuwa mbaya zaidi. Hatuna budi kuwa wabunifu na
kuongeza jitihada za kukijengea Chama uwezo wa kifedha
na rasilimali katika ngazi zote. Tulishatoa maagizo kwa kila
17
ngazi kuwa na mfuko wa uchaguzi, sijui ni wangapi wanao
na wana kiasi gani. Na watu hawashtuki. Hali hii
haikubaliki lazima tujirekebishe, hatujachelewa.
Mtakumbuka katika Mkutano Mkuu uliopita niliagiza
majengo na viwanja vyote vya Chama vipatiwe hati. Je,
limekalimika?
Maadili
Ndugu viongozi na Watendaji;
Tabia na mwenendo mwema ni sifa ya msingi ya kuwa
kiongozi na mtendaji wa Chama cha Mapinduzi. Kwa
namna ya pekee kiongozi hutoa taswira ya CCM kwa
wananchi na wanachama. Mkiwa wachapa kazi hodari,
watu wenye nidhamu na waadilifu ni sifa njema kwa Chama
chetu. Mkiwa tofauti na hayo ni sifa mbaya kwa CCM.
Naamini haya ninayoyasema yameelezwa vizuri na
kusisitizwa sana katika mafunzo haya. Naomba
muwayazingatie na kuyatekeleza.
18
Nendeni sasa mkadhihirishe kuwa ni mfano bora kwa
wanachama na wananchi tunaowaongoza. Mkifanya hivyo
mtakubalika na kuungwa mkono na wanachama na jamii
kwa ujumla. Na hivyo basi chama chetu kitanufaika.
Ndugu viongozi;
Si jambo jema hata kidogo kwa viongozi au watendaji
wa Chama kuwa na tabia na mwenendo mbaya
wanakiumiza Chama. Jiepusheni kuwa waombaji na
wapokeaji wa rushwa. Epukeni kuwa mawakala na
wasambazaji wa fedha chafu za wagombea wanaotaka
kununua uongozi. Tukifanya hivyo tutaiharibu sana sifa ya
CCM. Mtashindwa kusimamia haki na mtakigawa Chama
chetu. Ninyi mnategemewa kuwa wasimamizi wa
michakato ya uchaguzi lazima mtende haki na muwe
waadilifu. Mkikubali kuhongwa au kuwa wakala wa
mgombea mtawanyima haki baadhi ya wagombea na
itakuwa vigumu kwenu kutatua malalamiko yanayotokea
kwa sababu ninyi wenyewe ni sehemu ya tatizo. Isitoshe
19
wagombea watapoteza imani kwa viongozi na watendaji wa
Chama chao, jambo ambalo ni la hatari. Linalofanya watu
kupata hasira na wengine kufanya uamuzi usiotarajiwa na
kukiathiri Chama. Katika maeneo mengi tuliyopoteza
katika uchaguzi uliopita upendeleo wa viongozi kwa
wagombea ulichangia sana. Hakikisheni kasoro za chaguzi
zilizopita hazijirudii tena siku za usoni. Msije mkakiingiza
Chama kwenye matatizo yanayoweza kuepukika.
Ndugu viongozi na Watendaji;
Kabla ya kumaliza, ningependa kuwakumbusha kuwa
Chama chetu kupitia serikali yake kimefanya mambo mengi
mazuri kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Sina
shaka ifikapo 2015 tutakuwa tumefanya vizuri zaidi na
hivyo hatutasutwa kwa kutokuwa wakweli. Kwa ajili hiyo
sioni sababu kwa nini tusifanye vizuri katika chaguzi za
2014 na 2015. Lakini, tutaweza kutokufanya vizuri iwapo
tutafanya makosa katika uteuzi wa wagombea. Tukiteua
watu wasiokubaliwa na jamii kwa sababu ya urafiki, ujamaa
20
au kwa kupewa chochote binafsi zetu, jamii itatuadhibu.
Anayedhani kuwa kila aliyeteuliwa na CCM atachaguliwa
anajidanganya. Wakati huo umepita. Tupate wagombea
wazuri tusiendekeze rushwa. Tusiwaonee au kuwadhulumu
watu na kuwafanya wajenge chuki dhidi ya Chama chetu na
hata kususa au kufanya matendo ya kukidhuru Chama.
Tusiwasukume watu ukutani bila ya sababu acheni mambo
yawe wazi, ushindi uwe wa haki ili mtu akishindwa ajue
kuwa haikuwa bahati yake. Mtu mwenye upungufu
aambiwe kasoro zake kama ilivyo mila na desturi ya CCM.
Si vizuri mtu ajione kaonewa au kadhulumiwa na viongozi
wa Chama waliopokea rushwa kutoka kwa wagombea au
wanaomchukia. Nalisema hili kwa sababu habari zimezagaa
za watu wanaojipanga kugombea uongozi kuwa wanahonga
sana viongozi na watendaji wa CCM. Mzee Mangula
analishughulikia hilo. Nawasii mjiepushe nao msije
mkakutwa kuhusika, mtapata matatizo makubwa. Lazima
tulinde na kudumisha heshima ya Chama chetu.
21
Ndugu viongozi na watendaji;
Nimalizie kwa kuwapongeza watoa mada kwa kazi
nzuri waliofanya ya kutoa mafunzo kwa viongozi wetu
hawa. Viongozi wenzangu tusiwaangushe wakufunzi wetu
kwa kutoonesha mabadiliko katika uongozi na utendaji
wetu baada ya mafunzo hayo. Nawatakia safari njema na
utendaji ulio bora zaidi.
Baada ya kusema haya, natamka rasmi kwamba,
semina yenu imefungwa. Asanteni kwa kunisikiliza.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI.