Post on 30-Mar-2019
Miaka Miwili ya Urais wa Magufuli: Safari Ya Matumaini Au
Nyota Iliyofifia?
Hakimiliki 2017 Evarist Chahali
Kimechapishwa na Evarist Chahali kupitia Smashwords
Smashwords Edition License Notes
This ebook is licensed for your personal enjoyment only. This ebook may not be re-sold or
given away to other people. If you would like to share this book with another person, please
purchase an additional copy for each recipient. If you’re reading this book and did not purchase
it, or it was not purchased for your enjoyment only, then please return to Smashwords.com or
your favorite retailer and purchase your own copy. Thank you for respecting the hard work of
this author.
Farahasi
Kumbukumbu
Shukrani
Kuhusu Mwandishi
Utangulizi
Sura Ya Kwanza
Sura Ya Pili
Sura Ya Tatu
Sura Ya Nne
Sura Ya Tano
Sura Ya Sita
Hitimisho
Vitabu Vingine
Ungana Na Mwandishi Mtandaoni
Kumbukumbu
Kwa Marehemu Mzee Philemon Chahali na marehemu Adelina, wazazi wangu mliotangulia
mbele ya haki wakati ninawahitaji sana. Asanteni kwa kunizaa, kunilea, na kunipa imani ya
kuwa mtu ninayetaka kuwa.
Shukrani
Kitabu hiki kinachofanya tathmini ya kina ya miaka miwili ya utawala wa Rais Dokta John
Magufuli ni mwendelezo wa uchambuzi wa siasa za Tanzania kwa mfumo wa vitabu. Kitabu cha
kwanza ‘Uchaguzi Mkuu Tanzania 2015: Magufuli vs Lowassa,’ kilichotoka Oktoba 2015
kilijadili kwa kina kuhusu uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani nchini Tanzania,
uliofanyika mwezi huo. Kitabu cha pili, ‘Dokta John Magufuli: Safari ya Urais, Mafanikio na
Changamoto Katika Urais Wake,’ kilijadili kipindi cha awali cha utawala wa Dokta Magufuli.
Kilichonisukuma kuandikia kitabu hicho cha pili ni pamoja na ukweli kwamba kile cha kwanza
kilichapishwa takriban wiki mbili tu kabla ya Uchaguzi Mkuu na hivyo kuwanyima fursa
wasomaji wengi watarajiwa. Vilevile, kulionekana kuna haja ya kufanya tathmini ya uchaguzi
huo ulioshuhudia mgombea wa chama tawala, Dokta Magufuli akiibuka mshindi.
Kadhalika, mimi ni mwanafunzi wa stadi za siasa, na mara zote nimekuwa nikiamini kwamba
njia mwafaka zaidi ya kuitumia elimu yangu ipasavyo ni kuitumikia nchi yangu kwa njia ya
maongezi, aidha kupitia maandishi ya kwenye makala gazetini au bloguni au kwa makala za
sauti ninazozitoa mara kwa mara. Ninasema ‘maongezi’ kwa vile mimi si mwandishi kitaaluma,
na ninajitambulisha kama mfanya-maongezi (conversationalist) kuliko mwandishi. Kwahiyo,
kitabu hiki ni sehemu na mwendelezo wa maongezi hayo.
Licha ya kuwa mwanafunzi wa stadi za siasa, kitabu hiki, kama zilivyo makala zangu gazetini na
bloguni, sio cha kitaaluma. Ni maongezi kati yangu na Mtanzania wa kawaida, awe mwenye
shahada ya uzamifu kutoka chuo kikuu au mhitimu wa elimu ya msingi. Hii isitafsiriwe kama
kukosa imani katika kujadili masuala mbalimbali kitaaluma bali nimeonelea kuwa ndio njia
mwafaka ya kuongea na watu wengi pasi kuwepo kwa vikwazo vinavyoweza kuwanyima fursa
wenzetu ambao hawakubahatika kielimu. Kitabu hili ni kwa ajili ya kila Mtanzania wa rika
lolote, jinsia yoyote na wa kada yoyote – mwanasiasa au raia anayeichukia siasa, ‘mama ntilie’
au mwanasheria, mwanafunzi au mwalimu, nk.
Kama ilivyokuwa kwa toleo la kwanza, ninatunuku (dedicate) kitabu hiki kwa baba yangu
mpendwa, Marehemu Mzee Philemon Chahali, ambaye pamoja na mkewe, mama yangu
mpendwa, marehemu Adelina Mapango, ambao japo hawapo nasi kimwili, ninaamini kiroho
wanafurahishwa na kazi hii yangu mtoto wao.
Ninamshukuru dada yangu Mary, na wadogo zangu, Sr Maria-Solana na mapacha Peter na Paul
(Kulwa na Doto) kwa upendo wao ulionisaidia mno kuandika kitabu hiki.
Pia, ninawashukuru watu mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, hususan Twitter na
Facebook, kwa kulipokea vema wazo langu la uandishi wa vitabu.
Mapungufu yoyote yaliyomo katika kitabu hiki ni yangu mwenyewe na ninabeba lawama zote.
Kama nilivyotanabaisha hapo juu, mimi si mwandishi kitaaluma. Na pia ninakichukulia kitabu
hiki kama maongezi (conversation) niliyoamua kuyaweka katika maandishi.
Ni matumaini yangu makubwa kuwa licha ya faida tarajiwa ya mjadala wa undani kuhusu
uchaguzi huo mkuu, kitabu hiki kitawahamasisha Watanzania wenzangu kuhusu haja ya kuweka
fikra au mitizamo yetu katika maandishi, sambamba na kuendeleza filosofia isiyo rasmi ya
‘sharing is caring.’
Ninawatakia usomaji mwema.
Evarist Chahali.
Glasgow, Uskochi.
Desemba 9, 2017.
Kuhusu Mwandishi
Mwandishi wa kitabu hiki, Evarist Chahali, ni Mtanzania mwenye makazi yake jijini Glasgow,
Uskochi. Ni mhitimu wa Shahada ya kwanza katika Sosholojia (BA in Sociology) aliyoipata
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania, Shahada ya Uzamili katika Stadi za Vita
(Master of Letters in War Studies) na Shahada ya Uzamili katika Utafiti wa Siasa (Master of
Research in Political Research) alizopata katika Chuo Kikuu cha Aberdeen, Uskochi, ambapo
bado anaendelea na Shahada ya Uzamifu katika Stadi za Siasa (PhD in Political Studies – Part-
Time).
Kwa zaidi ya miaka 10, amekuwa akiandika makala katika magazeti mbalimbali nchini
Tanzania, ambapo huko nyuma aliandikia magazeti ya ‘Kulikoni’ na ‘Mtanzania,’ na kwa sasa ni
mwandishi wa makala katika gazeti la kila wiki linaloongoza nchini Tanzania, la ‘Raia Mwema.
Kadhalika, mwandishi anamiliki blogu ya ‘Kulikoni Ughaibuni’ iliyoanzishwa mwaka 2006.
Awali, mwandishi alikuwa mwalimu katika Shule ya Sekondari ya Ecknforde, Tanga, Tanzania
kabla ya kujiunga na utumishi serikalini katika Ofisi ya Rais wa Jamhuri wa Munngano wa
Tanzania. Hivi sasa, licha ya kuendelea na masomo yake ya Shahada ya Uzamifu (part-time)
anajihusisha ushauri wa kitaalamu katika masuala ya intelijensia na usalama (intelligence and
security consulting), mikakati ya siasa (political strategy consulting) na mahusiano na
mawasiliano ya kimkakati (International PR and strategic communications), akiwa mwanzilishi
na mmiliki wa kampuni ya ushauri wa kitaalam ya AdelPhil Consultancy iliyopo Glasgow,
Uskochi.
Utangulizi
Oktoba 5 mwaka juzi – 2015 – Dokta John Magufuli aliapishwa kuwa Rais wa tano wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Kabla yake nchi hiyo iliongozwa na Marehemu Julius Nyerere, Ali
Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.
Kitabu hiki ni mwendelezo wa vitabu vingine viwili vinavyozungumzia siasa za Tanzania
hasa kuhusu uchaguzi na uongozi. Kitabu cha kwanza kilizungumzia uchaguzi mkuu wa mwaka
2015 kabla hakujafanyika, tathmini ya fursa kwa kila mgombea na chama chake.
Kitabu cha pili kilihusu safari ya Dokta Magufuli kutoka kwenye mchakato wa kupitishwa
kuwa mgombea wa chama chake hadi kushinda uchaguzi huo. Kadhalika, kilichambua
mafanikio na changamoto kwa urais wake.
Kitabu hiki kinaendelea vilipoishia vitabu hivyo viwili, kwa kufanya tathmini ya kina ya
miaka miwli tangu Dokta Magufuli aingie madarakani.
Sura Ya Kwanza
Tarehe 25 Oktoba mwaka 2015, Watanzania walipiga kura ya kumchagua Rais mpya Dokta John
Magufuli aliyemrithi mtangulizi wake, Rais wa Nne wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete. Japo
uchaguzi mkuu haukuwa wa kwanza katika historia ya nchi yetu, mazingira yaliyouzunguka na
hali halisi ya Tanzania wakati unafanyika, yaliufanya uwe na umuhimu wa kipekee.
Kisiasa, angalau kwa chama tawala, CCM, yayumkinika kuhitimisha kuwa uchaguzi mkuu
huo ulikuwa wa kwanza kufanyika ambapo ‘nguvu za Baba wa Taifa, Marehemu Mwalimu
Julius Nyerere, hazikuwepo moja kwa moja (directly).’ Mara baada ya kung’atua, Nyerere
‘alimteua’ Ali Hassan Mwinyi kuwa Rais, akitumia nafasi yake kama mwanasiasa mwenye
nguvu zaidi nchini Tanzania. Baada ya Rais Mwinyi kumaliza mihula yake mawili mwaka 1995,
Nyerere alitumia tena nguvu zake kisiasa na kuwezesha msaidizi wake wa zamani, Benjamin
Mkapa kupitishwa na CCM, na hatimaye kushinda urais, madaraka aliyoshikilia kwa mihula
mawili, kama mtangulizi wake, yaani Rais Mwinyi.
Hata hivyo, duru za kisiasa zinaelezwa kuwa nguvu ya kisiasa aliyotumia Nyerere
kumpitisha Mkapa iliwaathiri wanasiasa wawili vijana, Jakaya Kikwete na Edward Lowassa,
ambao miaka 10 baadaye, walifanikiwa kmwingiza mmoja wao Ikulu.
Kwahiyo japo Nyerere hakuwa hai wakati Kikwete anaingia madarakani mwaka 2005, safari
yake ya kuingiza Ikulu ilicheleweshwa kwa miaka 10 na nguvu za kisiasa za Nyerere. Kadhalika,
kushinda urais kwa Kikwete akisaidiwa na rafiki yake Lowassa mwaka huo kulitazamwa kama
‘manufaa’ ya kutokuwepo Nyerere.
Mwaka 2010, Kikwete alishinda tena urais, kama ilivyo kanuni isiyo rasmi ndani ya chama
tawala CCM kwa rais aliye madarakani ‘kuruhusiwa’ kumaliza mihula miwili. Kwahiyo, hata
kama ‘nguvu za Nyerere’ zilikuwepo wakati huo bado zisingemzuwia Kikwete kushinda tena.
Katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu huu hali ilikuwa
tofauti kabisa. ‘Nguvu za Nyerere’ zilionekana bayana kuondoka kabisa. Hata wanasiasa
waliokuwa waamini wa itikadi zake, kwa mfano mkongwe Kingunge Ngombale Mwiru, sio tu
walionekana wenye mtizamo tofauti lakini baadhi yao, ikiwa ni pamoja na Kingunge
mwenyewe, waliohama CCM na kujiunga na upinzani. Jina la Nyerere limebaki kama heshima
tu lakini lisilo na uwezo wa kubadili chochote ndani ya CCM.
Lakini, tukiacha kumhusisha Nyerere, kinyang’anyiro cha kumpata mgombea wa CCM
wake ambapo hatimaye Dkt Magufuli ‘aliibuka kidedea’ kiliweka historia mpya, ambapo
makada zaidi ya 40 walijitokeza kuwania kuteuliwa. Kuna waliotafsiri iwngi huo ya idadi ya
‘watangaza nia’ kama kukua kwa demokrasia ndani ya chama hicho, huku wengine wakieleza
kuwa wingi huo ni ishara ya uchu wa madaraka, na wengine wakienda mbali zaidi na kudai
kuwa Rais Kikwete aliishusha hadhi ya urais kiasi kwamba ‘kila Dick, Tom na Harry’ alidhani
anaweza kuwa Rais.
Kwa mara ya kwanza, CCM na Watanzania walishuhudia kampeni zisizo rasmi za makada
waliotangaza nia za kuomba kupitishwa na chama hicho hata kabla kutangazwa rasmi kuanza
kwa mchakato huo. Kampeni hizo zilikuwa kali, kana kwamba ni kampeni rasmi za kuwania
urais. Awali, kuna waliohoji iwapo ukali wa mchuano huo ungepelekea chama hicho kupata
mgombea bora au la, lakini hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Dkt Magufuli tangu aanze
rasmi urais wake zinaweza kutoa jibu kuwa wingi wa waliojitokeza kuwania nafasi hiyo
umeisaidia sana CCM kumpata mgombea, na hatimaye rais, bora.
Jingine kisiasa, ni athari za mchakato wa chama hicho tawala kupata mgombea wake,
ambapo jina la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa halikupitishwa, na hatimaye akaamua
kuhama chama hicho na kujiunga na chama cha upinzani, Chadema. Kuhama kwa Lowassa
kutabaki kuwa moja ya kumbukumbu muhimu za uchaguzi huo. Japo kinyume na ilivyotarajiwa
kuwa kuhama kwake kungeambatana na kuhama kwa wanasiasa wengi wa CCM waliokuwa
wanamuunga mkono, ukweli tu kuwa mwanasiasa huyo ambaye kura mbalimbali za maoni
zilimwonyesha akiongoza kwenye uwezekano wa kupitishwa kuwa mgombea wa chama hicho,
kuamua kujiondoa katika chama tawala kulikuwa si jambo dogo hata chembe.
Na baadaye, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye naye alitangaza kujiunga na
Upinzani, na kuweka historia mpya ya mawaziri wakuu wa zamani kuhama CCM na kujiunga na
Upinzani. Baadaye kidogo, mwanasiasa mkongwe na mwasisi wa CCM, Kingunge Ngombale
Mwiru, nae alitangaza kukihama chama hicho tawala, na japo hakujiunga na chama kingine cha
siasa, alipanda majukwaani kumnadi Lowassa.
Uamuzi wa Lowassa kuhamia Chadema, ambayo awali ilifikia maafikiano ya kusimamisha
mgombea mmoja wa urais na vyama vya CUF, NCCR Mageuzi na NLD ambavyo kwa pamoja
viliunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), na kuteuliwa kuwa mgombea urais kwa
tiketi ya UKAWA kulibadili kabisa mwelekeo wa uchaguzi mkuu huo. Yayumkinika
kuhitimisha kuwa kwa mara ya kwanza kabisa, vyama vya upinzani, hususan vilivyounda
UKAWA, na wanachama wake, walionekana kuwa na matumaini makubwa ya kuing’oa CCM
madarakani. Hata hivyo, kuwa na matumaini ni suala moja, na matumaini hayo kutimia ni jambo
jingine kabisa kama ilivyoshuhudiwa katika matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo ambapo
Lowassa alishindwa na Dkt Magufuli.
Lakini eneo jingine lilioufanya uchaguzi mkuu huu kuwa tofauti na chaguzi zilizotangulia ni
matumizi ya teknolojia ya kisasa, hususan mitandao ya kijamii. Kama ilivyokuwa wakati CCM
inafanya mchakato wa kupata mgombea wake wa tiketi ya urais, ambapo watangaza nia
mbalimbali walijiunga na mitandao ya kijamii na baadhi yao kufanya ‘kampeni’ za waziwazi,
kampeni za vyama mbalimbali vya siasa, hususan CCM na UKAWA zilitawala mno katika
mitandao mbalimbali ya kijamii, hususan Twitter, Facebook, Instagram na kwenye blogu.
Kadhalika, teknolojia ya mawasiliano ya kutumiana ujumbe, hususan Whatsapp, ilikuwa nyenzo
kubwa ya ushirikishwaji wa umma katika siasa zinazohusiana na uchaguzi huo. Yayumkinika
kuhitimisha kuwa huo ulikuwa uchaguzi mkuu wa kwanza ambapo teknolojia ya kisasa ilikuwa
na nafasi kubwa, kulinganisha na chaguzi zilizotangulia.
Matumizi ya teknolojia hayakuishia kwenye kampeni tu bali pia hata shughuli nyingine
zilizohusiana na uchaguzi huo na siasa za Tanzania kwa ujumla. Kwa mfano, wakati fulani
niliweza kushiriki moja kwa moja (kwa njia ya Skype) katika mjadala kuhusu hatma ya nchi
uliofanyika jijini Dar es Salaam, wakati mimi nipo Glasgow, hapa Uingereza. Japo kwa mujibu
wa Katiba ya Tanzania, raia wa nchi hiyo walio nje hawaruhusiwi kupiga kura, ukweli kwamba
baadhi yao walishiriki kikamilifu katika mijadala mbalimbali ya mustakabali wa taifa iliwezesha
ushiriki wao katika shughuli za kisiasa (political participation).
Lakini tukiweka kando mazingira hayo ya kisiasa na kiteknolojia, uchaguzi mkuu huu
ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa kila Mtanzania, hasa kwa kuzingatia hali halisi iliyokuwepo
wakati unafanyika. Pamoja na taarifa mbalimbali zilizoashiria kuwa Tanzania ilikuwa ikifanya
vizuri kiuchumi, mamilioni ya Watanzania bado ni masikini mno. Na kana kwamba hiyo
haitoshi, pengo kati ya ‘wenye nacho’ na ‘wasio nacho’ linazidi kuongezeka.
Kibaya zaidi, kadri pengo hilo linavyozidi kukua ndivyo hisia miongoni mwa ‘wasio nacho’
kuwa wengi wa ‘wenye nacho’ ni mafisadi. Kwa lugha nyingine, kwa kiasi kikubwa, utajiri
nchini Tanzania umekuwa ukiangaliwa kwa jicho la mashaka. Hisia hizi zinaathiri umuhimu wa
watu kujituma na pengine kuweza kuingiza kwenye kundi la ‘wenye nacho.’
Wakati hakujawahi kutolewa maelezo ya kueleweka kwanini Tanzania ni masikini licha ya
utajiri mkubwa wa raslimali ilionao, yayumkinika kuhitimisha kuwa ufisadi ni moja ya sababu
ambazo sio tu zinachangia umasikini wa nchi wa nchi yetu bali pia unazidisha hali hiyo.
Kwahiyo moja ya changamoto kwa serikali ya Awamu ya Tano ni kupambana kwa dhati na
ufisadi.
Suala la kukosekana maelezo kuhusu umasikini unaoikabili nchi yetu lipo pia katika hisia
kuhusu mafanikio ya watu binafsi. Kama kuna wahanga wakubwa wa hisia hizo basi ni wasanii,
ambapo msanii akifanikiwa katika kazi zake, zinasikika tetesi kuwa ni muumini wa kundi la
‘Freemason.’ Kama ilivyo kwa wengi wa wanasiasa wetu kutanabaisha bayana kwanini nchi
yetu ni masikini ndivyo ambavyo baadhi ya wananchi wanashindwa kuelewa kwamba
inawezekana kwa mtu kuwa na mafanikio pasipo kujihusisha na ufisadi au kuwa ‘Freemason.’
Lakini licha ya umasikini mkubwa uliowakabili Watanzania wengi, ambao kwa mtizamo
wangu ninaamini ulichangiwa zaidi na ufisadi, nchi pia ilikabiliwa na matatizo mengine lukuki,
ikiwa ni pamoja na tatizo sugu la nishati isiyo na uhakika kutokana na mgao ‘wa kudumu’ wa
umeme. Matatizo mengine ni pamoja na ukosefu wa ajira, ambapo idadi kubwa ya wahitihimu
hukumbana na soko la ajira lisilowahitaji, matatizo kwenye sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na
miundombinu duni ya elimu na walimu kucheleweshewa mishahara yao. Kadhalika, maeneo
mengi ya Tanzania bado yalikabiliwa na tatizo la huduma ya uhakika ya maji, huku sekta ya afya
nayo ikiwa na matatizo mengi.
Uhalifu pia ulishamiri huku biashara ya madawa ya kulevya ikiimarika mno kiasi cha
kudhani mihadarati ni miongoni mwa ‘exports’ muhimu kwa nchi yetu. Vita dhidi ya madawa ya
kulevya ilikwazwa sio tu na viongozi wa serikali na wanasiasa kwa kutochukua hatua dhidi ya
wahusika bali pia mtizamo wa jamii kwa wahusika ni wa kuwatukuza zaidi (kwa mfano
‘kuwapamba’ kwa jina la ‘wazungu wa unga’ badala ya kuwaona kuwa ni wahalifu).
Sambamba na tatizo la madawa ya kulevya ni ujangili ambao ulichangia sana kuchafua
taswira ya nchi yetu kimataifa. Mabadiliko ya mara kwa mara ya mawaziri wanaoongoza Wizara
na idara zenye dhamana ya maliasili yalishindwa kabisa japo kupunguza tatizo hilo.
Tatizo jingine linalohusiana na uhalifu ni biashara ya ‘kuchukiza’ inayohusisha viungo vya
watu wenye ulemavu wa ualbino. Kama kuna kitu ambacho kiliichafua mno Tanzania ni biashara
hiyo ambapo vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa vilifanya vipindi maalumu kuelezea
kuhusu tatizo hilo. Tatizo hilo lilichangiwa zaidi na ukweli kuwa imani za ushirikina zimeota
mizizi mno katika nchi yetu, na hakuna jitihada za dhati kukabiliana nalo.
Kuna baadhi ya wananchi walikuwa wanaongea kwa mzaha kuwa ‘shughuli pekee
inayolipa, yaani yenye faida, katika nchi yetu ni uhalifu.’ Licha ya biashara ya madawa ya
kulevya na ujangili, nchi yetu pia ilikabiliwa na matatizo ya utakasishaji fedha sambamba na
biashara ya kusafirisha binadamu isivyo halali (human trafficking).
Kwa upande wa umoja wa kitaifa, kusuasua katika kuyashughulikia matatizo yanayoikabili
muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar kuliendelea kuweka muungano huo katika hali ya
hatihati. Na kama ilivyogusiwa katika toleo la kwanza la kitabu hiki, kwamba uchaguzi huo
unngeweza kuwa kama ‘referendum’ ya Muungano, kwa sababu wakati CCM ilibainisha katika
ilani yake ya uchaguzi kuwa ingeendelea kudumisha muundo uliopo wa serikali mbili, UKAWA
waliweka wazi kwamba miongoni mwa vipaumbele vyao ni muundo wa serikali tatu kama
ulivyopendekezwa na Tume ya kupokea maoni kuhusu Katiba Mpya, maarufu kama ‘Tume ya
Warioba.’ Katika kitabu hicho nilitoa angalizo kuwa hatma ya muundo wa muungano uliopo
ingetegemea chama gani kingechoshinda kati ya CCM na UKAWA, hususan huko Zanzibar.
Kwa bahati mbaya, na kimsingi, kutokana na kasoro za Muungano kutoshughulikiwa kwa
ukamilifu, hadi wakati ninaandika kitabu hiki, hatma ya uchaguzi mkuu huko Visiwani ni tete
kufuatia uamuzi wa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar kufuta uchaguzi wa Rais wa Zanzibar. Hadi
wakati ninaandika kitabu hiki, bado mgogoro wa kisiasa Visiwani humo unaendelea pasipo dalili
za kupatikana ufumbuzi mapema. Hata hivyo, licha ya kutoa taswira isiyopendeza kuhusu
uchaguzi mkuu kwa Jamhuri nzima, mgogoro huo wa kisiasa huko Zanzibar haukuathiri Dkt
Magufuli kutangazwa mshindi wa urais wa Muungano.
Lakini moja ya vichocheo vya kuporomoka kwa umoja wa kitaifa ilikuwa kupungua kwa
kasi kwa uzalendo. Ni wazi kwamba ni vigumu kwa uzalendo kushamiri kwenye jamii yenye
pengo linalozidi kukua kati ya ‘wenye nacho’ na ‘wasio nacho.’ Kwa bahati mbaya au makusudi,
programu za miaka ya nyuma zilizochangia kukuza uzalendo kama vile wahitimu kujiunga na
Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria zilikuwa za kusuasua.
Umoja wa kitaifa ulihatarishwa pia na tatizo lililozidi kukua pasipo kushughulikiwa
ipasavyo la migogoro ya kidini. Kubwa zaidi katika tatizo hilo ni malalamiko ya muda mrefu ya
Waislam kuwa wenzao Wakristo wanapendelewa na serikali. Japo katika siku za hivi karibuni
tatizo hili limekuwa kimya, ukweli mchungu ni kwamba bado lipo na kuna uwezekano wa
kuibuka tena huko mbeleni. Wakati Awamu zilizotangulia ziliamua kulikwepa tatizo hilo kwa
kutolizungumzia waziwazi, ilani ya uchaguzi ya CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005
ilibainisha wazi dhamira yake ya kushughulikia kero za Waislamu, na kuahidi kuwa ingewapatia
Mahakama za Kadhi. Hata hivyo, ahadi hiyo imeendelea kuwa ahadi tu na haijatekelezwa hadi
muda huu. Ni wazi kwamba suala hili litajitokeza tena huko mbeleni.
Kushamiri kwa udini pia kulichangia kuathiri umoja wa kitaifa. Udini hujitokeza katika sura
tofauti, na mfano mmojawapo ni hiyo ahadi ya CCM mwaka 2005 kuwa ingewapatia Waislamu
mahakama za kadhi, lengo likiwa ni kuvuta kura za waamini wa dini hiyo. Uchaguzi Mkuu
uliopita, mwaka 2010, ulishuhudia udini ukitumika tena kama turufu ya kisiasa, ambapo
wanasiasa mbalimbali wa CCM waliojaribu kujenga picha kuwa mgombea urais kwa tiketi ya
Chadema, Dokta Willbrord Slaa ni ‘padri anayewakilisha Kanisa, na hafai kuwa rais.’ Mbinu
chafu kama hiyo iliwahi kutumika kwenye chaguzi za nyuma dhidi ya chama cha CUF ambapo
zilifanyika jitihada za kujenga picha kuwa chama hicho ni cha kidini, cha Kiislamu.
Tofauti za kiitikadi ziliendelea kuchangia mpasuko katika nchi yetu ambapo baadhi ya
viongozi wa ngazi za juu wa chama tawala walikuwa wakifanya jitihada za waziwazi kujenga
taswira potofu kuwa vyama vya upinzani ni kama taasisi za kihaini. Tulishuhudia huko nyumba
jinsi baadhi ya viongozi na wanachama wa Chadema walivyonyanyaswa na vyombo vya dola
kwa tuhuma za ugaidi. Kumekuwa na jitihada kubwa za kuwaaminisha Watanzania kuwa
Wapinzani si Watanzania kamili na hawaitakii mema nchi yetu.
Kingine kinachoweza kuingizwa katika kipengele hiki cha mmomonyoko wa umoja wetu
wa kitaifa ni mtizamo fyongo miongoni mwa wanasiasa na wananchi wa kawaida dhidi ya
Watanzania wenzao walio nje ya nchi kwa sababu moja au nyingine. Kama kuna kipindi hali hii
ilijiweka bayana zaidi basi ni wakati wa mjadala kwenye Bunge Maalum la Katiba ambapo suala
la uraia pacha liliigawa jamii, huku wengi wakiwaangalia Watanzania waliopo nje kama wenye
mapungufu katika sifa za utaifa, au kwa lugha nyepesi ‘Watanzania nusu,’ kwa maana kuwa sio
kamili. Mchango wa Watanzania walio nje, au Diaspora kama inavyohamika, umekuwa
ukipuuzwa kwa hoja mbalimbali, kubwa ikiwa ni tishio kwa usalama wa taifa letu, kana kwamba
matishio yaliyopo yamechangiwa na watu wa Diaspora.
Rekodi ya Tanzania katika kuheshimu haki za binadamu ilikuwa sio ya kupendeza hata
kidogo. Vyombo vya dola, hususan Jeshi letu la Polisi, vilikuwa mstari wa mbele katika
kutoheshimu haki za binadamu. Licha ya suala hili kuchangia katika kumomonyoa umoja wetu
kitaifa ambapo mara nyingi wahanga wakubwa walikuwa viongozi na wanachama wa vyama vya
upinzani, pia liliathiri sana imani ya Watanzania wengi kwa vyombo vyao vya dola.
Yayumkinika kuamini kuwa laiti nguvu iliyotumiwa na Jeshi la Polisi katika kudhibiti
maandamano halali ya vyama vya upinzani, kwa mfano, ingeelekezwa katika kukabili uhalifu,
basi tatizo hilo lingepungua kwa kiasi kikubwa.
Kimataifa, Tanzania ya zama za Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, na hii ya miaka ya hivi
karibuni ilikuwa ni vitu viwili tofauti. Wakati nchi yetu sio tu ilikuwa miongoni mwa
wapiganiaji wa umoja na ushirikiano katika Bara la Afrika lakini pia ilishiriki katika mapambano
ya ukombozi kusini mwa bara hilo, kwa sasa ni vigumu kuielewa sera ya nje ya Tanzania, kama
ipo. Japo bado tuliendelea kuwa na mchango katika utatuzi wa migogoro kwa nchi jirani, kwa
mfano huko Burundi, sambamba na kuchangia harakati za kimataifa katika utatuzi wa migogoro,
kwa mfano uwepo wa majeshi yetu nchini D.R.C, hatukuweza kurudi kwenye ramani ya
kimataifa kama ilivyokuwa zama za Nyerere, na tatizo kubwa limekuwa kutokuwa na msimamo
imara.
Uwepo wetu katika eneo la Maziwa Makuu na hali ya mashaka inayotawala katika eneo hilo
inatupasa kutukumbusha umuhimu wa kujiimarisha kiulinzi na kiusalama, sambamba na
kudumisha amani yetu kwa kuzingatia kuwa ‘hatuna pa kukimbilia.’ Kulikuwa na shutuma
nyingi dhidi ya taasisi muhimu kwa usalama wa taifa letu, yaani Idara ya Usalama wa Taifa.
Kisiasa, taasisi hiyo ilikuwa ikituhumiwa kutekeleza majukumu yake kana kwamba ni kitengo
cha usalama cha chama tawala. Lakini shutuma kubwa kwa Idara hiyo ni jinsi ilivyoonekana
kushindwa kukabiliana na matishio kadhaa ya usalama kama vile ufisadi. Uimara wa taasisi
hiyo ni muhimu sana kwa mustakabali wa nchi yetu kwa sababu uimara wa ndani ndio
unaowezesha kukabiliana vizuri na matishio kutoka nje ya nchi.
Moja ya changamoto zilizotarajiwa kumkabili mshindi wa kiti cha urais katika uchaguzi huo
ni kuyumba kwa thamani ya sarafu yetu. Kwa kuzingatia kuwa uchumi wetu unategemea sana
misaada ya nchi kama China, ambayo wakati Tanzania inaingia kwenye kipindi cha uchaguzi,
ilikuwa kwenye matatizo ya kiuchumi baada ya soko lake la hisa kuyumba, ilimaanisha haja ya
mikakati imara ya kuinusuru sarafu yetu. Hata hivyo, wakati wa kampeni za uchaguzi, suala la
kuyumba kwa thamani ya shilingi halikupewa uzito stahili.
Ni vigumu kuorodhesha matatizo yote yaliyokuwepo wakati Tanzania inaingia kwenye
uchaguzi huo (yanahitaji kitabu kizima) lakini kilicho wazi ni kwamba uchaguzi huo ulikuwa
fursa muhimu kwa Watanzania kumchagua kiongozi atakayewasaidia kuboresha mazingira ya
safari ya kuifikisha nchi yetu mahala inapostahili kuwa.
Kitabu hiki kina sura sita. Sura ya kwanza inamtambulisha kwa kifupi Dokta John Magufuli,
alipotoka na hadi alipofikia hatua ya kuchukua fomu kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na hatimaye kushinda.
Sura fupi ya pili inazungumzia mchakato wa CCM kumpata mgombea wake wa kiti cha
urais, na jinsi Dokta Magufuli alivyofanikiwa kuibuka mshindi katika kinyang’anyiro hicho
ambacho kilishuhudia makada 43 wa chama hicho wakichukua fomu kuwania nafasi hiyo.
Sura ya tatu inazungumzia fursa mbalimbali ambazo ziliitengenezea CCM na mgombea
wake Dokta Magufuli mazingira mazuri ya ushindi ktika uchaguzi huo.
Sura ya nne inazungumzia vikwazo mbalimbali kwa CCM na Dokta Magufuli katika
kinyang’anyiro cha urais ambapo kwa mara ya kwanza tangu Tanzania iingie katika mfumo wa
vyama vingi, chama hicho tawala kilikuwa kikikabiliana na muungano wa vyama vinne vya
upinzani, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, huku mgombea wao akiwa mwanasiasa
ambaye kabla ya kuhama CCM alikuwa mwanasiasa maarufu kuliko wote, yaani Lowassa.
Sura ya tano inazungumzia urais wa Dokta Magufuli tangu atangazwe mshindi, hadi muda
huu kitabu hiki kinaandikwa, na jinsi alivyobadilisha kwa kiasi kikubwa, pamoja na mambo
mengine, taswira ya Tanzania ndani na nje ya nchi.
Sura ya sita inajadili changamoto mbalimbali zinazomkabili Dokta Magufuli, ikiwa ni
pamoja na haja ya jamii kubadilika ili kuendana na falsafa ya ‘Hapa ni Kazi Tu,’ sambamba na
mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar. Sura hiyo pia inagusia umuhimu wa mabadiliko katika
sekta ya usalama wa taifa hasa ikizingatiwa kuwa vita aliyotangaza Dokta Magufuli dhidi ya
mafisadi, wauza madawa ya kulevya, majangili, nk inagusa watu wenye nguvu kubwa na ambao
wanaweza kuhatarisha usalama wake binafsi na pengine taifa kwa ujumla.
Sura ya fupi ya mwisho ni ya kuhitimisha kitabu hiki, na kwa kiasi kikubwa inafanya
majumuisho ya masuala mbalimbali yaliyojadiliwa katika sura zilizotangulia.
Sura Ya Pili
Dokta Magufuli na mchakato wa CCM kumpata mgombea wake wa kiti cha urais: Sura hii
inajadili kwa undani mchakato wa chama tawala CCM kumpata mgombea wake kwa tiketi ya
urais ambapo hatimaye Dokta Magufuli aliibuka mshindi, na mwishowe alifanikiwa kushinda
kiti cha urais.
Tofauti na chaguzi zilizopita, kwa mara ya kwanza tangu Tanzania iingie kwenye mfumo
wa vyama vingi, CCM ilikuwa na jina la kada mmoja lililozungumwa mno kuwa na uwezekano
wa kugombea urais katika uchaguzi huu. Jina hilo si jingine bali la kada wa siku nyingi wa
chama hicho aliyeshika nyadhifa mbalimbali katika awamu tofauti, na hatimaye kuwa Waziri
Mkuu, Edward Lowassa. Licha ya utumishi wake wa muda mrefu serikalini, na kama
ilivyoelezwa katika sura zilizopita, mwanasiasa huyo alikuwa sehemu muhimu ya kampeni za
Rais Kikwete kuingiza madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2005. Pamoja na
mfanyabiashara Rostam Aziz, Lowassa na Kikwete walifahamika kama viongozi wa
kinachoitwa ‘Mtandao wa Kikwete,’ kikundi kisicho rasmi kilichojumuisha watu kutoka kada
mbalimbali, kikiwa na lengo la kumwingiza Kikwete madarakani kumrithi Raia wa Awamu ya
Tatu, Benjamin Mkapa.
Taarifa zisizo rasmi zinaelezwa kuwa ‘Mtandao’ huo uliundwa mara baada ya Kikwete na
Lowassa kushindwa azma ya mmoja wao kuingiza Ikulu katika uchaguzi wa mwaka 1995,
ambapo inaelezwa kuwa Nyerere alitumia nguvu zake kubwa kisiasa kuwazuwia wanasiasa hao
na papo hapo ‘kumbemba’ mwanasiasa chaguo lake, yaani Mkapa.
Taarifa hizo zilieleza kuwa kulikuwa na makubaliano kati ya Kikwete na Lowassa
kupokezana urais aidha baada ya miaka mitano ya Kikwete madarakani aua atakapomaliza
mihula yote miwli. Hata hivyo, kashfa ya Richmond iliyopelekea Lowassa kujiuzulu ilionekana
kujenga mpasuko sio tu katika ‘makubaliano’ hayo bali pia katika kinachoelezwa kuwa urafiki
wa muda mrefu kati yao.
Tetesi kuwa Lowassa angewania urais zilianza kitambo, lakini zilipata nguvu zaidi wakati
CCM ikijiandaa kwa uchaguzi wa mwaka 2010 ambao kwa mujibu wa taratibu zisizo rasmi
ndani ya chama hicho, rais aliyekuwa madarakani alistahili kupitishwa kugombea tena ili
amalizie awamu yake ya pili. Wakati huo, kulikuwa na tetesi zisizo rasmi kuhusu uwezekano wa
Lowassa kuachana na Kikwete ili nae agombee, lakini tetesi hizo zilipotea haraka kama
zilivyozuka.
Hata hivyo, dalili za Lowassa kujiimarisha kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka
zilijidhihirisha zaidi katika chaguzi za ndani za CCM mwaka 2012, ambapo makada waliokuwa
wakimuunga mkono walifanikiwa kushinda nyadhifa mbalimbali, huku ikidaiwa kuwa wengi
wao walisaidiwa kifedha na Lowassa na washirika wake. Ushindi huo ulionekana kama mwanzo
wa kilichokuja kufahamika kama ‘kambi ya Lowassa’ ndani ya CCM.
Kadri siku zilivyokwenda ndivyo tetesi za Lowassa kuwania urais zilivyozidi kupamba
moto. Hata hivyo, kadri tetesi hizo zilivyopamba moto ndivyo upinzani dhidi yake, hususan
ndani ya CCM, ulivyozidi kujitokeza, kubwa zaidi likiwa wazo la ‘CCM kujivua magamba,’
lilishikiliwa kwa nguvu kubwa na kada kijana, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye. Wazo
hilo lilionekana kuwavutia sio wana-CCM tu bali hata wananchi wengine wasiojihusisha na
chama hicho tawala. Kimsingi, ilionekana kuwa chama hicho kimetambua makosa yake na kina
nia ya kujirekebisha. Kadhalika, hatua hiyo ilonekana kutambua jinsi ajenda ya ufisadi
ilivyokuwa ikivipaisha vyama vya upinzani hususan Chadema, huko CCM ikitumia muda
mwingi kujitetea.
‘Kujivua gamba’ ilikuwa moja ya fursa adimu na muhimu kwa chama hicho tawala
kurejesha imani kwa wanachama wake na Watanzania kwa ujumla. Yayumkinika kuhitimisha
kuwa laiti mpango huo ungefanikiwa, CCM isingekuwa inapitia wakati mgumu kwenye kampeni
za kuwania uraia wakati huu ninapoandika kitabu hiki. Urahisi katika utekelezaji wa mpango huo
ulikuwa kwenye ukweli kwamba kuna wana-CCM wengi waliokuwa wakiuafiki, na wananchi
kwa ujumla walikuwa na mtizamo chanya.
Lakini licha ya mpango huo kufanikiwa kiasi kwa kupelekea mmoja ya wanasiasa
waliokuwa na nguvu kubwa ndani ya CCM, Rostam Aziz, kuamua kujiuzulu ubunge na nyadhifa
zake ndani ya chama hicho, kwa kiasi kikubwa kinachotajwa kama ‘nguvu ya Lowassa’
kilifanikiwa kuuzima. Kikwazo kingine kwa mpango huo kilikuwa Rais Kikwete, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa CCM Taifa, kuonekana kumtumia Nape kufanikisha mkakati huo pasipo ushiriki
wake yeye (Kikwete) mwenyewe.
Hoja kubwa dhidi ya ‘kujivua gamba’ zilikuwa ni pamoja na kuushutumu mpango huo kuwa
ungepelekea kuigawa CCM, sambamba na kumtuhumu Nape kuwa anamwandama Lowassa kwa
sababu binafsi. Kwa ujumla, wazo hilo zuri liligeuzwageuzwa hadi kuonekana kuwa lingekuwa
na athari zaidi kuliko faida kwa chama hicho.
Kipenga cha mbio za kuwania urais kwa tiketi ya CCM kilipulizwa na rasmi na kada kijana,
Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia na msaidizi wa zamani wa Rais Kikwete, January
Makamba, kutangaza nia ya kuwania urais, takriban mwaka mmoja kabla ya kuanza rasmi kwa
mchakato kamili wa CCM. Tangazo hilo la January liliingiza CCM kwenye zama mpya kwani
huko nyuma suala la kuwania urais lilifanywa kwa siri hadi ulipokaribia muda kwa chama hicho
kuanza mchakato wake.
Licha ya hofu kuwa kwa kutangaza nia ya kuwania urais mapema hivyo January angeweza
kuwapa ‘silaha’ maadui zake kisiasa, Watanzania wengi walilipokea vema tamko lake huku
wengi wakiona kuwa ni vema kwa wanasiasa wanaotaka kuwania urais kujitokeza hadharani
mapema ili wananchi wawafahamu vema. Kwa upande mwingine, tangazo hilo la January
lilikuwa changamoto kubwa kwa Lowassa ambaye jina lake lilikuwa likihusishwa na urais kwa
miaka kadhaa.
Pamoja na kuulizwa mara kadhaa iwapo atawania urais, Lowassa aliendelea kukaa kimya,
hatua inayoweza kuwa ilichangia kutofanikiwa kwa dhamira yake ya kuwa mrithi wa ‘rafiki
yake wa zamani,’ Kikwete. Katika mazingira ya kawaida tu, ilionekana kuwa iwapo mwanasiasa
kijana kama January anapata ujasiri kuwatangazia Watanzania kuwa anataka kuwania urais,
kwanini mkongwe kama Lowassa ashindwe kuwa muwazi kwa wananchi? Yawezekana alikuwa
hajaamua kwa dhati kuchukua hatua hiyo au huenda ulikuwa ni mkakati wenye lengo la
kuwashtukiza watu, lakini vyovyote ilivyokuwa, safari yake ya muda mrefu kutaka urais kupitia
CCM iliisha baada ya jina lake kukatwa na vikao vya mchujo.
Uamuzi wa January kutangaza mapema kuwa atawania urais hatimaye ulipelekea wanasiasa
wengine nao kuanza kuzungumzia hadharani kuwa wana nia ya kufanya hivyo japo hawakuwa
wawazi sana. Pengine kutokana na ugeni wa utaratibu wa wanasiasa kutangaza nia ya urais
kitambo kabla ya mchakato wa uchaguzi kuanza, au pengine kwa sababu za kihafidhina tu,
tangazo la January lilikumbana na vikwazo ndani ya chama chake ambapo ziliibuka tuhuma
kuwa mwanasiasa huyo, na baadaye makada wenzie watano, Lowassa, Bernard Membe, Stephen
Wassira, Waziri Mkuu wa zamani Frederick Sumaye, na William Ngeleja, kukaripiwa na chama
hicho kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kukiuka taratibu na kanuni za CCM za uchaguzi. Pamoja
na kukaripiwa, makada hao ‘walihukumiwa kifungo’ cha miezi kadhaa, japo kiuhalisia takriban
wote waliendelea kujinadi wakati wa ‘kifungo’ hicho.
Mara baada ya chama hicho kufungua rasmi mchakato wa kuomba ridhaa ya kuwania urais
kwa tiketi ya chama hicho, Juni 6, 2015, makada kadhaa walijitokeza kuchukua fomu. Kwa mara
ya kwanza katika historia ya CCM, na ya Tanzania kwa ujumla, makada 43 walichukua fomu.
Orodha ya makada hao ni kama ifuatavyo:
1. Amos Robert Siyatemi
2. Augustine Ramadhani.
3. Balozi Ali Karume
4. Balozi Amina Salum Ali
5. Bernard Membe
6. Boniface Ndengo
7. Charles Makongoro Nyerere
8. Dk. Asha Rose Migiro
9. Dk. Augustine Mahiga
10. Dk. Harrison Mwakyembe
11. Dk. John Magufuli
12. Dk. Khamis Kigwangallah
13. Dk. Mwele Malecela
14. Dk. Titus Kamani
15. Dk. Mohamed Gharib Bilal
16. Dk. Muzzamil Kalokola
17. Edward Lowassa
18. Frederick Sumaye
19. Hassy Kitine
20. Hellen Elinawinga
21. January Makamba.
22. Lazaro Nyalandu
23. Leonce Mulenda
24. Lidephonce Bilohe
25. Luhaga Mpina
26. Maliki Marupu
27. Mathias Chikawe
28. Mizengo Pinda
29. Mohamed Gharib Bilal
30. Monica Mbega.
31. Musa Mwapango
32. Mwigulu Nchemba
33. Patrick Chokala
34. Peter Isaiah Nyalali
35. Peter Nyalali.
36. Prof Mark Mwandosya
37. Prof. Sospeter Muhongo
38. Ritha Ngowi
39. Samuel Sitta
40. Samwel John
41. Stephen Wassira
42. Veronica Kazimoto
43. William Ngeleja
Hata hivyo, kati ya wagombea hao 43, wanne kati yao hawakurejesha fomu na hivyo
kufanya majina yaliyopelekwa kwenye vikao vya mchujo vya CCM kubaki 38 tu. Wagombea
hao walioshindwa kurejesha fomu ni Dkt Kalokola, Elinawinga, Chalamila na Nyalali.
Zoezi hilo la kuchukua na kurejesha fomu lilishuhudia sehemu kubwa ya watendaji wa
serikali wakiwania kumrithi Rais Kikwete, ambapo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, mawaziri
10 na Manaibu Waziri wawili, sambamba na Jaji Mkuu Mstaafu mmoja, Wakurugenzi wakuu
wawili wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa, na wengineo.
Wingi huo wa makada ulizua mjadala wa aina yake. Kwa upande mmoja, kuna waliotafsiri
idadi hiyo kubwa kuwa ni dalili za kushamiri kwa demokrasia ndani ya chama hicho, wakirejea
historia ya zama za chama kimoja ambapo jina moja tu la mwanachama mmoja tu liliwasilishwa
kwa ajili ya kupigiwa kura katika vikao vya CCM.
Hata hivyo, baadhi ya watu walitafsiri wingi huo kuwa ni ‘athari’ ya wazi ya miaka 10 ya
Kikwete madarakani. Wenye mtizamo huo walidai kuwa urais wa Kikwete ulishusha hadhi ya
taasisi ya urais kiasi kwamba ‘kila mtu alidhani anaweza kuwa rais.’
Tukirejea kwenye jitihada binafsi za makada kuwania nafasi hiyo, kuna mambo kadhaa
yaliyojitokeza yanayopaswa kugusiwa hapa. Kubwa zaidi lilikuwa jinsi Lowassa alivyoonekana
kupata ufuasi mkubwa, mara baada ya kutangaza nia na katika muda wote aliopita maeneo
mbalimbali kusaka wadhamini. Na japo kanuni za chama hicho zilimtaka mgombea kupata
wadhamini 450 katika mikoa 15, mwanasiasa huyo alipata wadhamini 1,600,000. Kwa jinsi hali
ilivyokuwa wakati huo, isingekuwa jambo la kushangaza kuhisi kuwa kilichokuwa kikisuburiwa
ni Lowassa kuapiashwa tu na kuwa rais.
Hata hivyo, pamoja na dalili hizo za kukubalika na wengi, ndani ya CCM kulikuwa na sauti
kadhaa za upinzani dhidi yake. Kwa mfano, mara kadhaa, ‘hasimu’ wake wa muda mrefu, Nape,
alitoa matamshi yalioashiria kuwa kuna jitihada za kumzuwia Lowassa kuteuliwa kuwa
mgombea urais kwa tiketi ya CCM. Kadhalika, baadhi ya wagombea, kwa mfano Makongoro
Nyerere, Waziri Mkuu wa zamani Sumaye, na Waziri Sitta, walitumia hotuba zao mbalimbali
zilizoashiria kuwa na ujumbe kuwa “Lowassa hafai.”
Katika muda wote huo Rais Kikwete hakuonyesha dalili yoyote iwapo anamuunga mkono
Lowassa au la. Hilo lilichangia kwa kiasi kikubwa kuugeuza mchakato huo kuwa kama
‘referendum’ kwa wanasiasa hao, ambapo kwa upande mmoja, swali lilikuwa, “Je Kikwete
‘atamtosa’ rafiki yake au ‘atambemba’?” Na kwa upande mwingine, swali kuhusu Lowassa
lilikuwa, “atakatwa (katika vikao vya mchujo vya CCM) au hatokatwa?”
Pengine moja ya dalili za awali kuwa licha ya ufuasi mkubwa alioupata wakati anasaka
wadhamini sehemu mbalimbali, na licha ya kutajwa kwa muda mrefu kuwa angegombea urais,
Lowassa hakuwa na hakika iwapo Kikwete atamuunga mkono, ni katika kurejea mara kwa mara
katika mikutano yake kauli kwamba anaamini ‘rafiki yake huyo atamsapoti kama yeye
alivyomsapoti mwaka 2005.’ Haihitaji uelewa mkubwa wa ‘jinsi urafiki unavykuwa’ kutambua
kuwa ‘marafiki walioshibana hawahitaji kukumbushana fadhila walizofanyiana huko nyuma.’
Kwamba kama kweli urafiki wa wawili hao ni wa dhati basi watasaidiana tu pasi haja ya
Lowassa kukumbushia msaada wake kwa Kikwete miaka 10 iliyopita.
Kwa upande mwingine, ukimya wa Kikwete tangu ‘rafiki yake’ huyo alipotangaza nia ya
kuwania urais, na kurejea kauli kwamba ‘hana mgombea wake,’ ilianza kujenga hisia kuwa
huenda tetesi kuwa urafiki kati ya wanasiasa hao wawili si mzuri zina ukweli. Hata hivyo, kwa
vile kwa kiasi kikubwa urafiki kati yao umekuwa ni suala la kuhisiwa zaidi kuliko kuthibitishwa
nao hadharani, baadhi ya watu waliamini sio rahisi kwa Kikwete ‘kumtosa’ Lowassa, na
kinachotajwa kama ‘tofauti kati yao’ ni sehemu tu ya mkakati wao.
Wakati ‘safari ya urais wa Lowassa’ ilichangiwa zaidi na jina lake kutajwa kuwa mrithi wa
Kikwete kwa muda mrefu kuliko mwanasiasa mwingine yeyote yule, kada aliyeendesha
‘kampeni’ zake kwa umahiri mkubwa ni January. Awali, alipotangaza nia, takriban mwaka
mmoja kabla ya CCM kuanza rasmi mchakato wa kumpata mgombea wake, baadhi ya watu
walidhani kuwa hakuna na dhamira ya dhati, na pengine ‘anamsafishia njia mgombea
mwingine.’ Hata hivyo, kadri siku zilivyokwenda, na licha ya ‘kebehi’ za mara kwa mara
alizokumbana nazo, mwanasiasa huyo kijana alionekana kutotetereka katika dhamira yake.
Baadaye, January alichapisha visheni yake aliyoiita ‘Tanzania mpya,’ ambayo kwa kiwango
kikubwa ilibainisha matatizo yanayoikabili nchi yetu na namna ya kuyatatua. ‘Kampeni’ ya
January ilifanikiwa zaidi kutokana na mambo makuu mawili, kwanza, ukaribu aliojenga na
vijana hususan katika mitandao ya kijamii, na pili, kuwa mtu anayefikika (approachable) na
wengi. Licha ya sababu hizo mbili, mwanasiasa huyo kijana amejaaliwa kipaji cha kuongea
lugha inayoeleweka kirahisi kwa mtu wa rika na kada yoyote. Jinsi ‘alivyouza’ ajenda yake ya
‘Tanzania mpya’ iliwafanya watu wengi kumwelewa na pia kumsaidia kupata ufuasi mkubwa.
Sambamba na hilo, wasanii kadhaa walionekana kumuunga mkono na hiyo ilisadia kuwavuta
wafuasi wa wasanii hao kumkubali mwanasiasa huyo, msaidizi wa zamani wa Rais Kikwete na
mtoto wa Katibu Mkuu wa zamani wa CCM.
Lakini mchakato huo wa CCM kumpata mgombea wake uliambatana na ‘vituko’ pia,
kikubwa kikiwa uamuzi wa Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
kuwania nafasi hiyo. Miezi machache tu kabla, jina la mwanasiasa huyo msomo lilivuma mno
kufuatia kashfa ya Tegeta Escrow ambayo hatimaye ilipelekea kujiuzulu licha ya awali kudai
kuwa asingefanya hivyo. Lakini pengine hata kama Profesa Muhongo asingehusishwa na kashfa
hiyo, Watanzania wengi walikuwa wanamkumbuka kwa kauli yake kuwa uwezo wa Watanzania
kuwekeza unaishia kwenye juisi na matunda. Alisema hayo alipoombwa na taasisi moja asitishe
zoezi la kutoa vitalu vya gesi asilia kwa wageni hadi sera ya gesi na mafuta iwe tayari ili
kuwezesha Watanzania nao kuingia ubia au kushiriki umiliki wa uchumi wa gesi. Wengi
walijiuliza, “hivi huyu mtu ambaye majuzi tu kulazimika kujiuzulu kwa kashfa ya Tegeta
Escrow, amepata wapi ujasiri wa kuwania urais?” Ni katika mazingira kama hayo, hoja kwamba
kujitokeza kwa wana-CCM wengi kuwania urais imechangiwa na ‘thamani ya urais kushuka’
ilionekana kupata nguvu.
Kingine kilichojitokeza wakati wa ‘kampeni’ za makada mbalimbali wa CCM kuwania urais
ni matumizi ya mitandao ya kijamii. Kama kuna suala moja litakaloingia kwenye historia ya
uchaguzi mkuu nchini Tanzania basi ni hili la jinsi matumizi ya teknolojia ya kisasa, hsusan
mitandao ya kijamii, yalivyowezesha ushirikishwaji wa kisiasa kwa wananchi wengi, wanasiasa
waliokuwa wakiwania kuteuliwa kuwa wagombea urais na wananchi wa kawaida kwa ujumla.
Kwa mara ya kwanza, wananchi waliokuwa mtandaoni walipata fursa ya kuwahoji
wanasiasa hao, sambamba na wao kutumia fursa hiyo kuwaeleza Watanzania mikakati yao
iwapo wangepewa ridhaa na chama hicho kuwa wagombea. Kwa bahati mbaya, kwa kiasi
kikubwa suala hili halijapewa uzito mkubwa, labda pengine kutokana na ukweli kuwa idadi
kubwa ya watumiaji wa mitandao ya kijamii ‘hawachukulii mambo ya mtandaoni kwa uzito
mkubwa.’ Hisia kuwa ‘Watanzania wanaotumia mtandaoni ni asilimia ndogo tu ya Watanzania
wote’ imekuwa kigezo muhimu kwa watu wengi kutoyachukulia yanayojiri mtandaoni kwa uzito
unaostahili. Hata hivyo, ukweli kwamba wanasiasa kadhaa walitambua umuhimu wa teknolojia
hiyo kuwasiliana na wananchi unaonyesha kuwa Tanzania imepiga hatua ya kuridhisha katika
matumizi ya teknolojia ya mawasiliano.
Suala jingine muhimu kabisa ni idadi ya wanawake waliojitokeza kuomba ridhaa ya CCM
kuwania urais, ambapo makada sita wa kike walijitokeza. Makada hao ni Dkt Mwele Malecela,
Dkt Asha-Rose Migiro, Balozi Amina Salum Ali, Monica Mbega, Ritha Ngowi na Hellena
Elinawinga. Kujitokeza kwa idadi hiyo ya kuridhisha ya wanawake kulijenga hisia kuwa iwapo
Tanzania haitopata Rais mwanamke basi kuna uwezekano mkubwa wa kupata mgombea
mwenza, na pengine hatimaye mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa umakamu wa rais.
Hata hivyo, jambo la kusikitisha ni kwamba kwa kiasi kikubwa makada hao hawakupewa
sapoti ya kutosha na wanawake wenzao, kwenye chama chao na hata ‘mtaani.’ Hii ni
changamoto kubwa kwa wanawake nchini Tanzania kwa sababu licha ya ukweli kwamba
uongozi ni suala la uwezo lakini jamii nyingi duniani, hususan Barani Afrika, zimekuwa
zikikandamiza nafasi za wanawake katika uongozi, na hii ilikuwa fursa nzuri kwa wanawake wa
Tanzania kuwasapoti wanawake wenzao.
Hatimaye, Julai 2,2015 zoezi la kusaka wadhamini na kurejesha fomu za kuwania ridhaa ya
CCM kumteua mgombea wake wa urais lilifikia ukingoni na makada walioweza kurejesha fomu
walifanya hivyo. Kilichosubiriwa kwa hamu kilikuwa uamuzi wa vikao vya chama hicho tawala
kuchuja wagombea wake na hatimaye kumpata mmoja atakayekiwakilisha chama hicho katika
uchaguzi mkuu.
Mara baada ya kikao cha kwanza, cha Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM kumaliza
kikao chake, kulisikika uvumi kuwa jina na Lowassa halikupitishwa. Uthibitisho sahihi kuhusu
tetesi hizo ulipatikana Julai 11, 2015 baada ya chama hicho kutangaza rasmi majina matano ya
makada wake waliopitishwa, na ambayo yangepigiwa kura katika Mkutano Mkuu wa CCM.
Taarifa za kukatwa kwa jina la Lowassa zilizokelewa kwa mshtuko mkubwa, na wakati fulani
zilisikika tetesi kuwa ‘wafuasi wa Lowassa’ walipanga kufanya mapinduzi ya kumng’oa
Kikwete na Kamati Kuu ya Chama hicho. Baadhi ya ‘wafuasi’ hao, walijitokeza hadharani
kupinga maamuzi ya chama chao kukata jina la mwanasiasa huyo.
Taarifa zisizo rasmi zinaelezwa kuwa marais wa zamani, Mwinyi na Mkapa walifanya kazi
kubwa kumnusuru Kikwete na uhai wa chama hicho kwa ujumla kwa maelezo kwamba kanuani
na taratibu za chama hizo ziwekwe mbele ya maslahi ya mtu binafsi (Lowassa). Inadaiwa Mkapa
alikwenda mbali na kuwatakia wajumbe wa vikao hivyo wanaodhani kuwa Lowassa
hakutendewa haki aidha warejeshe kadi zao za uanachama wa CCM, kwa maana ya kujiondoa
wenyewe kwenye chama hicho, au waafiki maamuzi ya vikao hivyo.
Hatimaye Julai 11, 2015 Dokta Magufuli alifanikiwa kupita mchujo wa kwanza baada ya
jina lake kuwa miongoni mwa majina matano yaliyopitishwa na Kamati Kuu ya CCM. Makada
wengine walikuwa January Makamba, Bernard Membe, Balozi Amina Salum Ali, na Dokta
Asha-Rose Migiro.
Nyota ya urais kwa Dokta Magufuli iliendelea kung’ara baada ya kufanikiwa kupita mchujo
wa pili ambapo yeye, Balozi Amina na Dokta Asha-Rose walipitishwa, na kuwashinda January
na Membe. Na dalili ya uwezekano wa yeye kuibuka mshindi katika hatua ya mwisho ilionekana
kwenye idadi ya kura walizopata makada ahao, ambapo Dokta Magufuli alipata kura 290,
akifuatiwa na Balozi Amina (kura 284), Dokta Asha-Rose (kura 280), January (kura 124), na
Membe (kura 120).
Taarifa zinaeleza kuwa kwa vile kambi ya Lowassa iliamini kuwa Membe ndio chaguo la
Kikwete, na January alionyesha upinzani mkubwa kwa ‘mgombea wao,’ kura zao nyingi
zilielekezwa kwa Magufuli, Dkt Asha-Rose na Balozi Amina. Katika duru la mwisho, Magufuli
aliibuka mshindi kwa kura 1560, akifuatiwa na Dkt Asha-Rose alaiyepata kura 702 na Balozi
Amina kuambulia kura 349.
Awali kulikuwa na hisia kuwa kwa vile ‘tatu bora’ ilikuwa na makada wawili wa kike basi
huenda mshindi angekuwa mwanamke pia. Hata hivyo, wachunguzi wa siasa wanadai wakati
Dkt Asha-Rose hakuwa na ushawishi mkubwa wa kumwezesha kusinda nafasi hiyo,
kilichomwangusha Balozi Amina ni hotuba yake ya kuomba kura ambapo alionekana kama
anayetaka ‘kura za huruma kutoka kambi ya Lowassa,’ sambamba na dalili kuwa huenda
‘angamvuta’ Lowassa kuwa nae kama mgombea mwenza endapo mwanamama huyo angeshinda
katika kinyang’anyiro hicho.
Yayumkinika kuhitimisha kuwa mafanikio ya Magufuli hadi kuteuliwa kuwa mgombea
rasmi wa chama hicho yalichangiwa zaidi na ‘siasa za kumzuwia Lowassa’ kwa upande mmoja,
na ‘hasira za kambi ya Lowassa dhidi ya Membe.’ Hata hivyo, kwa kumchagua Magufuli, CCM
iliweza kumpata mgombea ambaye wa kiasi kikubwa alikuwa mmoja wa watendaji wachache
kabisa katika chama hicho wenye kusifika kwa uchapakazi. Tangu jina lake lilipotangazwa
rasmi, sambamba na kada aliyemteua kuwa mgombea mwenza, Samia Suluhu, taswira
iliyojitokeza mtaani iliashiria kuwa chama hicho tawala kisingekuwa na kazi ngumu kumnadi
mgombea huyo ambaye licha ya kusifika kwa uchapakazi, alisifika kwa kuweka mbele maslahi
ya taifa badala ya kuendekeza itikadi za kisiasa, sambamba na kipaji cha kujieleza kwa ufasaha
Kwa upande mwingine, ‘sintofahamu’ ilijitokeza kuhusu hatma ya Lowassa, kada ambaye
sio tu jina lake lilianza kusikika mapema kuwa angewania nafasi hiyo na kujizolea ufuasi
mkubwa lakini pia hadi muda huo alikuwa mwanasiasa mwenye nguvu zaidi ndani na nje ya
chama hicho. Swali kubwa lililotawala vichwa vya Watanzania liligeuka kutoka ‘atakatwa au
hatakatwa (na vikao vya mchujo vya CCM)’ na kuwa ‘atahama CCM au atabaki katika chama
hicho (hasa ikirejewa kauli zake za awali kuwa wanaomtaka atoke katika chama hicho watoke
wao na sio yeye).
Hatimaye, Julai 28, 2015, takriban wiki mbili baada ya jina lake kukatwa na vikao vya
CCM, Lowassa alitangaza kuihama CCM na kujiunga na Chadema. Siku chache baadaye, vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), vilimpitisha Lowassa kuwa mgombea
wao wa nafasi ya urais.
Katika kuhitimisha sura hii, ni muhimu kupigia mstari jinsi ushindi wa Magufuli, na
kushindwa kwa Lowassa, kulivyoenda kinyume na ubashiri wa wachambuzi mbalimbali wa siasa
za Tanzania, ikiwa ni pamoja nami mwandishi wa kitabu hiki. Kwa upande wangu, nilibashiri
uwepo wa makundi makuu matatu ambayo yangeweza ‘kuzaa’ mgombea urais kwa tiketi ya
CCM. Makundi hayo ni, kwanza, makada wenye nafasi kubwa, ya kati na wenye nafasi ndogo.
Katika kundi la kwanza Katika kundi la kwanza niliwaweka Jaji Ramadhan, Lowassa,
January, Makongoro, Dkt Bilal, Pinda na makada watatu wanawake, yaani Dkt Mwele, Dkt
Asha-Rose na Balozi Amina.
Jaji Ramadhani aliingia kundi hilo kutokana na sababu za wazi. Ushahidi wa kimazingira
wakati huo ulionyesha kama ndio alikuwa mgombea ‘turufu’ kwa CCM, hasa katika kile
kilichotajwa kama ‘kumdhibiti Lowassa.’ Pia kulionekana dalili kuwa Jaji huyo Mkuu mstaafu
alikuwa chaguo la Kikwete kwa kurejea baadhi matamshi yake huko nyuma. Kadhalika, uhaba
wa makada wa CCM wenye rekodi ya kupendeza japo kidogo ulimfanya Jaji Ramadhani
kuonekana mwenye na nafasi ya juu zaidi.
Kuhusu Lowassa, sababu mbili zilizopelekea kuingizwa kundi hilo la kwanza ni, kwanza,
historia yake na Kikwete, angalau hadi wakati huo. Mtizamo maarufu wakati huo ulikuwa
kwamba laiti sakata la Richmond lisingetokea na Lowassa kulazimika kujiuzulu, basi muda huo
ingekuwa inasubiriwa kutawazwa kwake tu, yaani kupasisha utawala kwa mtu pasi haja ya
uchaguzi.
Mengi ya yalikuwa yakisemwa kuhusu uhusiano wake na Kikwete hayakuwahi
kuthibitishwa, lakini iliyumkinika kuhisi kuwa kadri Lowassa alivyomsaidia Rais Kikwete
mwaka 2005 ndivyo Kikwete alivyotarajiwa ‘kulipa fadhila’ katika uchaguzi mkuu huu.
Sababu ya pili ilikuwa uwezo wake mkubwa kifedha ambao kwa kiasi kikubwa ulichangia
kile kilichoonekana kama kukubalika kwake kwa wananchi wengi. Ilikuwa muhimu sana
kutopuuza nafasi ya fedha katika kinyang’anyiro hicho hasa kwa kuwa chaguzi nyingi za CCM
hutawaliwa mno na nguvu ya fedha kiasi hata uchaguzi wa viongozi wa chipukizi wa chama
hicho uliwahi kuhusishwa na matumizi makubwa ya fedha.
Kwa upande wa January, aliingia katika kundi hili kwa sababu kuu mbili. Kwanza, alikuwa
kada wa kwanza kutangaza hadharani nia yake ya kuwania urais. Hatua hii ilionekana kumsaidia
sana kutambulika kwa watu wengi hususani miongoni mwa vijana wanaotumia mitandao ya
kijamii. Sambamba na hilo, kada huyo kijana alijizolea ufuasi mkubwa miongoni mwa wasanii
maarufu na wenye mashabiki wengi ambao licha ya kumsapoti pia walikuwa wakimnadi
hushusan katika mitandao ya kijamii.
Sababu ya pili ilikuwa nguvu kubwa mno aliyotumia ‘kujinadi’. Licha ya kuandika kitabu
kinachoelezea ajenda yake ya ‘Tanzania Mpya,’ mwanasiasa huyo alifanya kazi kubwa ya
kujinadi, huku akisaidiwa na wasanii kadhaa ‘wenye majina makubwa.’ Kimsingi, kada
mwingine pekee anayelingana na Makamba kwa ‘kampeni’ kubwa alikuwa Lowassa, ambaye
hata hivyo, tofauti na Makamba, alikuwa akifanyiwa zaidi ‘kampeni’ hizo na wapambe kuliko
yeye mwenyewe.
Kuhusu Makongoro, kikubwa kinachomwingiza Makongoro katika kundi hili ni ukweli
kwamba yeye ni mtoto wa Nyerere, na takribani kila Mtanzania anayeitakia mema nchi yetu
bado anamlilia Mwalimu Nyerere. Kwa kuwa mtoto wa Baba wa Taifa, kulikuwa na hisia
kwamba ‘tunaweza kumpata Nyerere mwingine,’ jambo ambalo ilikuwa kama ndoto njema ya
Watanzania wengi.
Lakini kingine ni ukweli kuwa Makongoro alikuwa muwazi mno katika kuikosoa CCM, na
alijitahidi sana kutotoa ahadi kwa kigezo kuwa ahadi za mgombea wa chama hicho shurti
ziendane na ilani ya uchaguzi ya chama hicho ambayo ilikuwa haijatolewa hadi muda huo.
Kuhusu Bilal na Pinda, kitu pekee kilichofanya waingie katika kundi hilo ni ukweli kwamba
walikuwa wasaidizi wa karibu wa Rais Kikwete katika miaka 10 iliyopita. Kwa taratibu zisizo
rasmi katika siasa za Afrika, hakuna Rais anayemaliza muda wake atakayethubutu kumkabidhi
madaraka kwa mtu asiyemjua, na Kikwete na makada hao walikuwa wakijiuana vizuri kutokana
na ukaribu wao kikazi. Kadhalika, Uzanzibari wa Bilal ulitarajiwa kuwa ‘mtaji’ kwake pia iwapo
ingeamuliwa na CCM kuwa mgombea wake ajaye wa urais ajaye Zanzibar.
Kwa Pinda, mara kadhaa alionekana ‘kubebeshwa lawama’ katika masuala ambayo pengine
lawama zilipaswa kwenda kwa bosi wake, yaani Rais Kikwete. Ilidhaniwa kwamba kwa
‘kukubali ‘kurushiwa risasi ili kumkinga Rais wake, huenda Kikwete angelipa fadhila kwa
kumnadi awe mrithi wake.
Kwa upande wa makada watatu wanawake, niliwapa nafasi sawa Dkt Mwele, Dkt Asha-
Rose na Balozi Amina kutokana na kila mmoja kuwa na ‘turufu’ zake. Kwa Dkt Mwele, licha ya
kuendesha ‘kampeni’ yake kistaarabu sana, alikuwa na faida ya kuwa ‘mgeni’ katika siasa, kwa
maana isingikuwa rahisi kuhusishwa na mapungufu yaliyoelekezwa kwa makada wengine
waliokwishashika nyadhifa katika chama hicho. Kwa Migiro, ilitarajiwa kuwa wasifu wake
kama mmoja wa wanawake wachache wenye nguvu katika ngazi za juu za chama hicho, na
wadhifa wake wa zamani kama Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ungeweza
kumsaidia.
Kwa Balozi Amina, ‘turufu’ zake ilitarajiwa kuwa Uzanzibari wake, utumishi wake wa
muda mrefu katika taasisi za kimataifa, na ukweli kwamba hilo lilikuwa jaribio lake la pili
kwania fursa hiyo.
Kundi la pili lilijumuisha makada walioonekana kuwa na nafasi ya kati. Binafsi, nilibashiri
kuwa kundi hilo lingeweza kutoa ‘surprise candidate’ angalau kuingiza kwenye ‘tano bora,’ na
nilikuwa sahihi kwani Dokta Magufuli alitoka kwenye kundi hilo, kada ambaye licha ya
kutanguliza maslahi ya taifa mbele ya itikadi za kisiasa, alikuwa akisifika kwa uchapakazi.
Pamoja na Dokta Magufuli, kada mwingine katika kundi hilo alikuwa na Membe, ambaye tetesi
zilikuwa zikidai kuwa alikuwa akiungwa mkono na familia ya Kikwete, sambamba na ukweli
kuwa nafasi yake ya Uwaziri wa Mambo na Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilimweka karibu
sana na mkuu huyo wa nchi. Hata hivyo, licha ya awali kupewa nafasi ya kutoa upinzani mkali
kwa Lowassa, kauli zake angalau mara mbili kuwa angekuwa tayari kumuunga mgombea
mwingine endapo yeye asingepitishwa zilitoa taswira kuwa huenda alishajikatia tamaa.
Mwigulu aliingia katika kundi hilo kutokana na ukweli kwamba kulinganisha na ‘watangaza
nia wengine,’ alikuwa na rekodi ya kipekee katika kupambana na vyama vya upinzani.
Kada wingine alikuwa Balozi Mahiga, ambaye licha ya kuwa mwanadiplomasia wa
kimataifa kwa muda mrefu aliwahi pia kuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa. Tatizo kwa
Balozi Mahiga lilikuwa kutojulikana sana katika medani za siasa za Tanzania, na japo ukweli
kuwa aliwahi kuwa bosi wa ‘mashushushu’ ulitarajiwa kumsaidia kama ‘mgombea mwenye
uwezo wa kukabiliana na tatizo la ufisadi,’ lakini pia ilidhaniwa kuwa sifa hiyo ingeweza
kumkwamishwa na waliohofia kuwa na ‘rais shushushu.’
Mwingine katika kundi hilo alikuwa Profesa Mwandosya, mmoja wa makada waliojaribu
bila mafanikio kuchuana na Kikwete katika kinyanga’anyiro cha CCM kumpata mgombea wake
mwaka 2005. Hata hivyo, nguvu aliyokuwa nayo wakati huo ilikuwa imepungua sana
kulinganisha na mwaka 2015.
Kundi la tatu lilijumuisha makada wengine wote waliochukua fomu kuwania ridhaa ya
chama hicho tawala kuwateua kuwa mgombea wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Katika kundi hili kulikuwa na wanasiasa kama Waziri Mkuu wa zamani, Sumaye ambaye
aliingia kundi hili kwa sababu tayari alikuwa ‘na maadui wengi’ ndani ya CCM, hivyo ni
ingekuwa vigumu mno kupitishwa kuwa mgombea wa chama hicho. Baadaye Sumaye alitangaza
kuhama chama hicho na kujiunga na UKAWA, na suala hilo litajadiliwa kwa kirefu katika sura
ijayo.
Makada wengine, kama Ngeleja na Profesa Muhongo, waliingia katika kundi hilo la
wagombea wenye nafasi finyu kutokana na ukweli kwamba hadi muda huo majina yao yalikuwa
yakifahamika zaidi kuhusiana na skandali kuliko utendaji kazi wao. Kwa upande wa Dk.
Mwakyembe na Sitta, nafasi zao zilionekana kuwa finyu kutokana na kilichotajwa mara kadhaa
kuwa na ‘uhasama wake na Lowassa’ ambao ulitarajiwa ungepelekea upinzani mkali dhidi yao.
Moja ya maswali ambayo hadi leo ‘hajayajapatiwa majibu’ ni jinsi Jaji Ramadhan
alivyoishia kukatwa jina lake licha ya kupewa nafasi kubwa kama ‘mtu pekee anayeweza
kupambana na Lowassa.’ Kimsingi, uamuzi wake wa kutangaza nia ya kugombea urais
uliwashtua wengi hasa ikizingatiwa kuwa rekodi yake ‘safi’ kama Jaji Mkuu wa zamani, afisa
wa zamani wa ngazi ya juu jeshini, na kiongozi wa kidini, ingeweza aidha kuchafuliwa wakati
wa kampeni au kuingiza doa iwapo jina lake lingeishia kukatwa. Kwa bahati mbaya, Jaji
Ramadhan anaweza kukumbukwa zaidi kwa kutamani urais lakini jina lake halikupitishwa,
kuliko rekodi yake ya kuvutia.
Kwa hitimisho, sura hii imezungumzia kwa undani mchakato wa Chama cha Mapinduzi
CCM kumpata mgombea wake Dokta Magufuli, ambaye baadaye aliibuka mshindi wa kiti cha
urais; masuala kadhaa yaliyojitokeza kabla, wakati na baada ya chama hicho kuruhusu makada
wake kuwania nafasi hiyo, na jinsi vikao vya chama hicho vilivyowexza kumpitisha mgombea
wao, Magufuli.
###
Sura Ya Tatu
Changamoto zilizomkabili Magufuli (na CCM) katika uchaguzi mkuu: Pamoja na fursa nyingi
zilizoitengenezea mazingira mazuri ya ushindi CCM na mgombea wake Dokta Magufuli, chama
hicho kiliingia katika uchaguzi huo huku kikikabiliwa na changamoto na vikwazo kadhaa.
Kikwazo kikubwa zaidi ni kilikuwa kwa chama hicho kuhusishwa kwake na kila ‘baya’
lililoihusu Tanzania. Orodha ilikuwa ndefu, lakini kama kuna tuhuma ‘iliyoitafuna’ zaidi CCM
ni suala la ufisadi. Na licha ya tuhuma hizo za ufisadi kuiandama CCM katika awamu zake
mbalimbali, hali katika awamu mbili za Rais Kikwete ilikuwa mbaya mno.
Licha ya yeye binafsi kuonekana kama mwanasiasa ‘msafi’ na mchapakazi, mtihani
mkubwa kwa Dokta Magufuli (na chama chake kwa ujumla) ulikuwa katika kuwaaminisha
wapigakura uwezekano kwa chama hicho kingeweza kubaki hai pasipo kujihusisha na ufisadi.
Kwa muda mrefu, hali ndani ya CCM ilikuwa mbaya mno kiasi kwamba wakati chama hicho
kilipokuja na mkakati wa ‘kujivua magamba,’ watu wengi walidai jaribio hilo lingekiuwa chama
hicho katika namna ileile ya ‘kumuua kobe ukijaribu kumng’oa gamba.’
Kama kuna ajenda moja iliyodhaniwa ingeweza kumnyima Dokta Magufuli na CCM
ushindi ni suala hilo la ufisadi. Na licha ya Lowassa kuandamwa na tuhuma za ufisadi alipokuwa
CCM, chama hicho tawala kilipata wakati mgumu kuzungumzia ‘ufisadi mmoja tu’ huku
chenyewe kikiandamwa na lundo la tuhuma za ufisadi. Na kwa upande mwingine, hoja mbadala
dhidi ya chama hicho ilikuwa ‘ufisadi wa Lowassa si usafi wa CCM.’
Moja ya virutubisho vilivyoufanya ufisadi kuwa kama sehemu ya uhai wa CCM ni
kulindana. Kimsingi, laiti ‘sera ya kulindana’ isingekuwepo, basi CCM isingehangaishwa na
Lowassa katika uchaguzi huo kwa sababu ingeweza kuchukua hatua katika nyakati mbalimbali
dhidi yake kutokana na kuhusishwa kwake na tuhuma za ufisadi.
Kushindwa kwa chama hicho na serikali yake kuchukua hatua dhidi ya ufisadi kulitajwa
kuwa ni moja ya sababu za kukua kwa tatizo hilo, kwa sababu ‘mafisadi watarajiwa’ hawakuwa
na cha kuwaogopesha kufanya majaribio ya ufisadi mpya, kwa kuzingatia kuwa wengi wa
waliokwishafanya hivyo hawakuchukuliwa hatua zozote.
Kibaya zaidi, CCM iliingia kwenye uchaguzi huo huku tuhuma nyingi za ufisadi zikiwa
hazijapatiwa majibu wala hatua kuchukuliwa. Licha ya suala la Richmond kujitokeza mwaka
2006, taarifa mbalimbali kuhusu suala hizo hazikuwa na majibu ya maswali kadhaa
yaliyowasumbua Watanzania wengi. Kwa mfano, wakati Lowassa akituhumiwa kuwa ‘mhusika
mkuu’ katika kashfa hiyo, wapo waliohoji je ‘bosi’ wake, yaani Rais Kikwete, hakuwa na
ufahamu wowote kuhusiana na suala hilo?
Kwa upande wa kashfa ya EPA, hadi wakati wa uchaguzi huo serikali ya CCM ilikuwa
imegoma katakata kuwajulisha Watanzania kuhusu mmiliki wa kampeni ya Kagoda, iliyotajwa
kuwa mnufaika mkubwa wa ufisadi huo. Kwenye kashfa ya Escrow, bado kulikuwa na lundo la
maswali kuhusu, kwa mfano, wakati majina ya waliopewa mgao kupitia Benki ya Mwananchi
yalifahamika, wanufaika wa mgao uliotajwa kuwa mkubwa zaidi kupitia benki ya Standard
Chartered walikuwa hawajatajwa hadharani. Katika kashfa ya Operesheni Tokomeza, Serikali ya
CCM ilifanya ‘kioja cha mwaka’ kwa kuwasafisha wahusika pasipo kutoa maelezo ya
kuridhisha.
Kushamiri kwa ufisadi, sambamba na kutokuwepo jitihada za dhati kupambana na tatizo
hilo kulionekana kungeweza kuwashawishi baadhi ya wapiga kura, hata waliokuwa wana-CCM,
kukinyima kura chama hicho tawala au mgombea wake Dokta Magufuli.
Licha ya ufisadi wa EPA, Richmond, Escrow na kashfa ya Operesheni Tokomeza, kulikuwa
pia na kashfa nyingine kama ya Meremeta, Tangold, Mwananchi, mgodi wa Kiwira, na
nyinginezo zilizoonekana ‘kuzikwa kienyeji’ bila serikali ya CCM kubainisha majina ya
wahusika wala kuchukua hatua stahili dhidi yao. Tatizo hapo lilikuwa sio tu kashfa hizo
zingeweza kuiathiri CCM katika uchaguzi huo bali pia hofu kuwa zingeweza kuibuka upya huko
mbeleni.
Tukiweka kando kashfa za ufisadi, tangu kustaafu kwa Nyerere, Tanzania iliendelea
kushuhudia ongezeko la uhalifu mkubwa, hususan tatizo sugu la biashara ya madawa ya kulevya,
biashara ya usafirishaji binadamu, utakatishaji fedha na ujangili. Matatizo haya ambayo
yalikuwepo hata kabla ya Kikwete kuingiza madarakani, yalishamiri zaidi katika utawala wake,
ambapo licha ya kuchafua jina la Tanzania kimataifa, nchi yetu ilifikia hatua ya kuonekana kama
ina-export uhalifu (kwa mfano, kuna idadi kubwa tu ya Watanzania waliofungwa katika
magereza ya nchi mbalimbali duniani kwa makosa ya madawa yakulevya)
Kana kwamba matatizo hayo hayakuwa mabaya kwa hadhi ya nchi yetu, kwa muda mrefu
Tanzania ilijikuta ikipata sifa mbaya kutokana na mauaji ya albino, ambapo vyombo vya habari
mbalimbali vya kimataifa vilikuwa vikifuatilia unyama uhalifu huo wa kinyama kwa karibu.
Jitihada za serikali kupambana na tatizo hilo zilikuwa hafifu, huku tuhuma zikielekezwa kwa
wanasiasa ambao baadhi yao walituhumiwa kuwa wateja wa waganga wa kienyeji wanaotumia
viungo vya albino kutengeneza dawa za asili. Japo CCM haikuweza kuhusishwa moja kwa moja
na tatizo hili, ukweli kwamba lilijiri wakati wa utawala wake ungeweza kuwapa nguvu UKAWA
kukibana chama hicho, kwa hoja kwamba kilishindwa kuwalinda maalbino.
Licha ya kuonekana kama ‘kisiwa chama amani na utulivu,’ Tanzania chini ya utawala wa
CCM ilikuwa na rekodi isiyopendeza kuhusu haki za binadamu. Wakati uhalifu wa mauaji ya
albino uliangukia katika eneo hilo, jeshi la polisi lilikuwa likilaumiwa mara kwa mara, hususan
na vyama vya upinzani, kwa ‘kutumia nguvu kubwa zaidi ya akili’ katika matukio kadhaa
yaliyopelekea vifo na majeruhi. Kwa vile CCM ilikuwa kama ina ‘kinga’ dhidi ya vitendo hivyo
vya polisi, ilionekana kutofanya jitihada za kutosha kupambana na ukiukwaji huo wa haki za
binadamu. Kimsingi, chama hicho tawala kilikuwa kikionekana kama kinafurahia mwenendo wa
jeshi la polisi, ambapo wakati fulani, aliyekuwa Waziri Mkuu (2008-2015) Mizengo Pinda alitoa
ruhusa kwa polisi kuwapiga raia badala ya kusisitiza haja ya kuzingatia haki za binadamu.
Yayumkinika kuhitimisha kuwa moja ya sababu za uhusiano hafifu kati ya wananchi wengi
na jeshi la polisi ilikuwa kwa chombo hicho cha dola kupuuzia haki za binadamu hususan pale
maslahi ya chama tawala yalipoguswa. Ni katika mazingira hayo, jeshi hilo lilibandikwa jina la
‘poli-CCM’ likimaanisha ‘polisi wa CCM.’ Chuki za wananchi dhidi ya jeshi hilo lililoonekana
kuipendelea CCM zilihofiwa kuwa zingeweza kukiathiri chama hicho kwenye uchaguzi huo.
Kiuchumi, wakati CCM iliweza kujinadi kwa kutumia takwimu mbalimbali zilizoonyesha
kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kuboresha uchumi wake, hali halisi ‘mtaani’ ilikuwa
tofauti kabisa. Ukosefu wa ajira, mfumuko wa bei, kipato kisichoendana na hali halisi ya maisha
pamoja na matatizo mengine kama hayo yalipelekea kushamiri kwa rushwa na uhalifu
mwingine. Tofauti za kipato kati ya ‘wenye nacho’ na ‘wasio nacho’ sio tu ilizidi kukua mwaka
hadi mwaka lakini pia iliongeza hamasa kwa ‘wasio nacho’ kutafuta njia za kuweza kumudu
maisha yao, ambapo mara nyingi kimbilio lilikuwa kwenye uhalifu, ufisadi na rushwa.
Utawala wa CCM ulishuhudia watu kutoka kada mbalimbali katika jamii wakikimbilia
kwenye siasa, kutokana ana siasa kugeuka kuwa ‘ajira ya uhakika zaidi’ kuliko zote. Wasomi
mbalimbali wamekuwa wakiachwa kazi za taaluma na kuingiza kwenye siasa, na kinyume cha
matarajio ya wengi kuwa ujio huo wa wasomi ungechochea maendeleo, wengi wao wameishia
kukumbwa na kashfa za ufisadi kiasi cha kushamiri kwa hisia miongoni mwa Watanzania kuwa
‘wasomi wetu ni miongoni mwa wanaomchangia matatizo katika nchi yetu.’ Ilidhaniwa kuwa
UKAWA ingeweza kuinyooshea kidole CCM ikiituhumu kwa ‘kuzalisha ukame wa
wanataaluma’ na kisha ‘kuwaharibu wanataaluma wanaoingia katika siasa kupita chama hicho,
kwa kuweka kando eilu yao na kukumbatia ufisadi.’
Changamoto nyingine kwa Dokta Magufuli na CCM ilikuwa kuhusu kutochukuliwa hatua
madhubuti kutatua baadhi ya kero sugu zilizokuwa zikiikabili Tanzania. Na moja ya kero hizo
sugu ilikuwa ‘mgao wa kudumu wa umeme.’ Tatizo la mgao wa umeme lililochangiwa kwa kiasi
kikubwa na ufisadi mfululizo linawaathiri na kuwakera Watanzania wengi. Kibaya zaidi, badala
ya utawala wa CCM kuwekeza nguvu kumaliza tatizo hilo, jitihada za baadhi ya watendaji wake
zilielemea zaidi katika kutumia tatizo hilo kama njia ya kufisadi zaidi. Kimsingi, Shirila la
Umeme Tanzania (TANESCO) lilikuwa kama ‘ng’ombe asiye na lishe lakini aliyekamuliwa
maziwa mfululizo hadi kutoa damu badala ya maziwa.’ Hujuma mfululizo dhidi ya Shirika hilo,
katika awamu mbalimbali za utawala wa CCM zilichangia mno kufanya mgao wa umeme kuwa
kama ‘stahili’ ya Watanzania. Wakati wa kampeni za uchaguzi, haikuwa jambo la kushangaza
kukutana na mabandiko kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii yakieleza bayana ‘nitainyima
kura CCM kwa sababu ya mgao wa umeme.’
Wakati wa kampeni za kuwania urais mwaka 2005, moja ya ahadi za CCM na Kikwete
ilikuwa kuzalisha ajira milioni mbili. Kama lengo hilo lilifikiwa au la, tafsiri ya mtaani ilikuwa
kama kuzalishwa kwa ‘ajira’ nyingi za uhalifu kuliko ‘ajira halali.’ Kulikuwa na ongezeko la
idadi ya waliojiingiza katika siasa na kugeuka mamilionea kutokana na marupurupu makubwa
kwenye ubunge, ongezeko la ‘wauza unga,’ majangili, mafisadi, na wahalifu wengine kwa
ujumla. Ugumu wa maisha na ukosefu wa ajira ulipelekea uhalifu kuwa kama ‘ajira halali’ na
njia halali ya kutengeneza kipato.
Uchaguzi mkuu huo utabaki kwenye kumbukumbu kama uliohusisha matumizi makubwa ya
teknolojia, hususan mitandao ya kijamii. Wakati maendeleo hayo yalitoa fursa sawa kwa CCM
na UKAWA, ilitarajiwa kuwa umoja huo wa Wapinzani ungeweza kunufaika zaidi kwa sababu
mitandao hiyo ya kijamii inatumika kama nyenzo muhimu ya mawasiliano kati ya viongozi na
wanachama, na miongoni mwa wanachama, na hivyo kukabiliana na kikwazo cha vyombo vya
habari vya umma kuelemea CCM.
Hata hivyo, pengine kwa kujiamini kuwa walikuwa na fursa kubwa kuishinda CCM, na
kudhani umaarufu wa mgombea wao, Lowassa, ungejinadi wenyewe na hatimaye kumudu
kumshinda mpinzani wake, Dokta Magufuli, wana-UKAWA hawakuitumia ipasavyo mitandao
ya kijamii kulinganisha na wana-CCM.
Kadhalika, wakati kabla ya uchaguzi huo, CCM na wafuasi wake ilikuwa ikilaumiwa na
wapinzani kuwa ‘ilipendelea kutumia vitisho au lugha kali kila ilipohojiwa kuhusu tuhuma
mbalimbali,’kampeni za uchaguzi huo zilishuhudia kinyume cha hali hiyo, ambapo wengi wa
wafuasi na baadhi ya viongozi wa UKAWA waligeuka hodari wa matusi na kumwandama kila
mtu aliyejaribu kuibua maswali halali kuhusu sera zao, Lowassa, nk.
CCM ilifanikiwa mno katika matumizi ya mitandao ya kijamii kwenye kampeni zao,
ambapo kwa kiasi kikubwa walielemea zaidi kumnadi mgombea wao Dokta Magufuli na
wagombea ubunge, tofauti na UKAWA walionekana sio tu kujiamini kwa kutomnadi Lowassa
vya kutosha bali ‘kuwekeza’ zaidi kwenye matusi huku wakisahau wagombea wao wa ubunge na
udiwani.
Changamoto nyingine kwa Dokta Magufuli na CCM ilikuwa kile Waingereza wanaita
‘guilty by association,’ yaani kuhusishwa na kosa kutokana na kuhusiana na mtenda kosa. Katika
hilo, utawala wa CCM ulibebeshwa lawama za ubadhirifu mkubwa uliofanywa kwenye taasisi
mbalimbali, hususan vyama vya ushirka ambavyo baadhi ya viongozi wake walionekana kama
wakilindwa na chama hicho tawala, hususan kutokana na michango yao ya fedha kwa chama
hicho. Tatizo la ubadhirifu katika vyama vya ushirika sio tu liliwaathiri sana wakulima vijijini
bali pia lilikuwa na athari kwa uchumi wa taifa letu ambalo linategemea kilimo kama uti wa
mgongo. Vyama vingi vya ushirika vilionekana huko vijijini kama taasisi za CCM, na ilikuwa
rahisi makosa yaliyofanywa na vyama hivyo kuhusishwa na chama hicho tawala.
Licha ya vyama vya ushirika, uendeshaji wa serikali za mitaa ulikuwa umegubikwa na
tuhuma mbalimbali za ufisadi, sambamba na watendaji wa serikali hizo kujiona kama miungu-
watu, na kutokuwa na msaada wa kutosha kwa wananchi. Chuki za wananchi dhidi ya watendaji
wa serikali za mitaa wenye tuhuma za ubadhirifu au wasio na utendaji kazi bora zilionekana
kuwa zingeweza kuiathiri CCM pia, hasa ikizingatiwa kuwa ni vigumu kuchora mstari
unaotenganisha chama hicho tawala na serikali za mitaa.
Tatizo la umungu-mtu lilikuwepo pia ndani ya CCM yenyewe na katika serikali zake. Kwa
upande mmoja tatizo hili lilichangiwa na ufisadi ambapo ‘jeuri ya fedha’ iliwapa kiburi
watendaji wakiamini kuwa fedha walizonazo ni kinga dhidi ya kuchukuliwa hatua. Kwa upande
mwingine, utoaji ajira kwa misingi ya undugu au urafiki uliwajengea kiburi baadhi ya watendaji
wanaoamini kuwa hata wakiboronga ‘watalindwa na aliyewaweka hapo.’ Sababu kama hizi
zilihisiwa kuwa zingeweza kuwafanya baadhi ya wapigakura waamue ‘kufanya majaribio kwa
utawala wa UKAWA’ hasa kutokana na kutapakaa kwa hisia kuwa ni vigumu kwa CCM
kupambana na mengi ya matatizo yanayoikabili yenyewe kama chama, na nchi kwa ujumla.
Umungu-mtu na viongozi kuwa mbali na wananchi pia ulikuwa matokeo ya mfumo
uliorithiwa kutoka zama za chama kimoja. Wakati huo, kauli ya kiongozi ilikuwa kama ‘amri ya
mungu,’ ni sahihi na isiyoweza kupingwa. Ujio wa mfumo wa vyama vingi haukufanikiwa
kuondoa kasumba hiyo, ambayo pia ilichangia viongozi kutofahamu fika matatizo ya wananchi
kutokana na kutokuwa karibu nao.
Kadhalika, mabadiliko yaliyoitoa CCM kutoka ‘chama cha wakulima na wafanyakazi’ na
kuwa ‘chama cha wafanyabiashara na wasomi’ yalionekana kuwa yageaweza kutoa fursa kwa
vyama vya upinzani, hususan UKAWA, kuwaunganisha ‘wakulima na wafanyakazi
waliotelekezwa na CCM,’ na kupata kura kutoka kwa makundi hayo mawili yenye asilimia
kubwa ya Watanzania.
Ukweli kwamba huo ulikuwa uchaguzi mkuu wa kwanza kwa CCM kukumbana na
muungano imara wa upinzani, ulioongozwa na Lowassa, mwanasiasa aliyekuwa na nguvu
kubwa alipokuwa ndani ya CCM, ulitarajiwa ungeweza kukifanya chama hicho tawala kisijue
jinsi ya kuukabili upinzani huo ‘wa aina mpya.’ Kwa kiasi fulani, ushindi wa CCM dhidi ya
vyama vya upinzani katika chaguzi mbalimbali huko nyuma ulichangiwa na mazingira ya
‘chama kikongwe na imara’ kuchuana na upinzani dhaifu na uliogawanyika. Ilidhaniwa kuwa
mbinu zilizotumiwa na CCM katika chaguzi za mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010 zisingeweza
kufanikiwa kwenye uchaguzi wa mwaka huo kutokana ushirikiano wa vyama vya upinzani
vilivyounda UKAWA.
Lakini kwa upande mwingine, ilidhaniwa kuwa mazowea ya kushinda kila uchaguzi mkuu
yangeweza kuijengea CCM hali ya kujiamini kupita kiasi, na hivyo kuzembea, na kutoa fursa
kwa UKAWA kushinda uchaguzi huo.
Licha ya tuhuma za mara kwa mara za ufisadi zilizouandama utawala wa Kikwete, moja ya
matatizo yaliwagusa wengi ni ombwe la uongozi wa taifa. Wakati Wapinzani walimtuhumu Rais
Kikwete kuwa ni dhaifu, wananchi wengi walimwona kama ‘mpole kupita kiasi,’ japo wakati
anaingia madarakani kwa mara ya kwanza, mwaka 2005 alitahadharisha kuwa ‘tabasamu lake
lisieleweke vibaya.’ Ombwe hilo la uongozi ambalo lilijitokeza mara baada ya Nyerere kustaafu
na hatimaye kufariki, lilizidi kukua, awamu moja baada ya nyingine. Kuna nyakati ambapo nchi
ilionekana kama ‘inajiendesha kwa auto-pilot,’ aidha kwa vile Rais alikuwa kwenye safari zake
mfululizo nje ya nchi au watendaji wa serikali walikuwa ‘wamebanwa na jukumu la kuvuna
shamba la bibi, kula keki ya taifa,’ yaani kufanya ufisadi. Ilitarajiwa kuwa UKAWA wangeweza
kunufaika katika hili iwapo wangemudu kuonyesha mlolongo wa kukua kwa ombwe la uongozi,
na kujenga hisia kuwa CCM ikishinda itaendeleza ombwe hilo badala ya kuliondoa.
Hata hivyo, licha ya changamoto hizo zote kwa Dokta Magufuli na CCM kwa ujumla,
mpinzani wake, Lowassa, na UKAWA walioshindwa kabisa kulishawishi kundi muhimu la
wapigakura – wasiofungamana na chama chochote – ambalo yayumkinika kuamini kuwa ndilo
lililomwezesha Dokta Magufuli na CCM kushinda uchaguzi huo uliojaa ushindani mkubwa.
Kama kuna kitu kilichomwangusha sana Lowassa, na UKAWA kwa ujumla, katika
uchaguzi huo ni viongozi na wafuasi wake kujiamini kupita kiasi. Kujiamini huko kuliandamana
na jeuri ya aina flani, ambapo viongozi na wafuasi hao hawakutaka kusikia ushauri wowote hata
kama ulikuwa wa manufaa kwao.
Kujiamini huko ‘kulikopitiliza’ kulichangiwa na sababu kuu mbili. Kwanza, umaarufu wa
Lowassa kabla hajajiunga na Upinzani. Ni kweli kwamba hadi wakati anajiondoa CCM,
mwanasiasa huyo alikuwa maarufu kuliko yeyote yule ndani ya chama hicho tawala. Hata hivyo,
UKAWA walipotoka kudhani kuwa umaarufu wa Lowassa akiwa CCM ungeendelea baada ya
kuhamia Upinzani. Hilo lilithibitika katika ukweli kwamba ahadi kuwa ‘mamia ya viongozi wa
CCM wangemfuata Lowassa huko UKAWA’ iliisha kuwa porojo tu. Makada waliomfuata huko
Upinzani hawakuwa na nguvu ya kutosha kuiyumbisha CCM au kuiimarisha UKAWA.
Sababu ya pili, ni imani potofu kuwa ‘CCM ilikuwa inachukiwa mno’ kiasi kwamba
wapigakura wangemchagua Lowassa hata asingejinadi vya kutosha. Na kwa hakika, kampeni ya
Lowassa ilikuwa kama mzaha mbaya kwenye uchaguzi. Licha ya hotuba zake kuwa fupi mno,
alishindwa kabisa kuelezea kaulimbiu yake kuu ya ‘mabadiliko.’ Wakati kwa hakika Watanzania
wengi walikuwa wakihitaji mabadiliko, lakini ilihitajika zaidi ya maneno matupu jukwaani
kuwaaminisha wananchi kuwa watu walewale kama Lowassa na Sumaye walioitwa mafisadi na
wapinzani haohao wanaowanadi, wangeweza kweli kuleta mabadiliko waliyohubiri.
Kwa kuhitimisha, sura hii imejadili changamoto mbalimbali zilizomkabili Dokta Magufuli
na chama chake katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Kama sura hii na
iliyotangulia zinavyoonyesha, uchapakazi wa Dokta Magufuli ulikuwa turufu muhimu kwake na
kwa CCM pia. Alikuwa mgombea ambaye ‘anauzika’ kirahisi licha ya ukweli kwamba chama
chake kiliwekeza nguvu kubwa kumnadi. Lakini kama kanuni za kisiasa zinavyotanabaisha,
uimara wa mgombea hutegemea udhaifu wa mpinzani wake. Na kwa bahati nzuri, mpinzani
mkuu wa Dokta Magufuli, yaani Lowassa, alikuwa mgombea dhaifu aliyekuzwa na sifa za
kufikirika ambazo ziliishia kumuumbua wakati wa kampeni. Kimsingi, ushindani kati ya Dokta
Magufuli na Lowassa aulikuwa kati ya mwanasiasa ‘msafi’ anayesifika kwa uchapakazi dhidi ya
mwanasiasa aliyesifika zaidi kwa tuhuma za ufisadi, zilizopelekea kujiuzulu Uwaziri Mkuu
mwaka 2008.
Kana kwamba ubora huo wa Dokta Magufuli dhidi ya udhaifu wa Lowassa ulikuwa
hautoshi, ukweli kwamba Chadema, chama kilichompokea Lowassa na kumfanya mgombea
wake wa urais kwa tiketi ya UKAWA, kilikuwa mstari wa mbele kwa takriban miaka 9
kumwandama Lowassa kwa kumuita fisadi sugu, ulitosha kabisa kuwarahisishia maamuzi
wapigakura kuhusu mgombea gani ni sahihi kwao.
Usaliti wa Chadema ulionekana pia katika jinsi ‘ilivyomtenda’ aliyekuwa Katibu wake
Mkuu, na mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Dokta Willbrord
Slaa. Baada ya kujiweka kando kwa takriban mwezi mzima mara baada ya Lowassa kujiunga na
Chadema, Dokta Slaa alijitokeza hadharani na kueleza sababu zilizopelekea yeye kutoafikiana na
uamuzi wa chama chake kumpitisha Lowassa kuwa mgombea wake wa urais. Pamoja na mambo
mengine, Dokta Slaa alielezea bayana kuwa kada huyo wa zamani wa CCM aliihadaa Chadema
kwa kuahidi kuwa idadi kubwa ya viongozi wa chama chake cha zamani wangejiunga na chama
hicho, na hivyo kuiongezea uwezekano wa kuiangusha CCM. Dokta Slaa, ambaye alikuwa na
mchango mkubwa katika kuiimarisha Chadema na kuifanya ionekane mtetezi wa wanyonge
hususan dhidi ya ufisadi, alihitimisha kuwa Lowassa alikuwa ni ‘liability’ na sio ‘asset’ kwa
Chadema na UKAWA, kitu ambacho hatimaye kilithibitika baada ya matokeo ya uchaguzi huo
kutangazwa.
Hatua hiyo ya Dokta Slaa kujitokeza hadharani kueleza kilichojiri hadi akajiweka kando
ilipelekea viongozi wakuu wa Chadema na wafuasi wao kumwandama na kumdhalilisha kwa
kiasi kikubwa, huku wakimtuhumu kuwa alinunuliwa na CCM ili kumkwamisha Lowassa. Kosa
walilofanya Chadema, na pengine UKAWA kwa ujumla ni kupuuzia umuhimu wa Dokta Slaa
katika siasa za upinzani nchini Tanzania. Kutokana na umakini wake na msimamo wake
usioyumba, uamuzi wake wa kutangaza hadharani ‘usaliti wa Chadema’ ulikuwa na athari
kubwa kwa chama hicho kikuu cha upinzani, na umoja wa UKAWA kwa ujumla. Katika
mazingira ya kawaida tu, mwanasiasa anayeheshimika kitaifa anapokikosoa chama chake
hadharani hususan wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, inaweza kukigharimu chama husika.
Kwa upande mwingine, kosa la msingi walilofanya Chadema na UKAWA kwa ujumla
kumpitisha Lowassa kuwa mgombea wao wa kiti cha urais ni ukweli kwamba ni miujiza pekee
ingeweza ‘kumsafisha’ Lowassa ndani ya miezi mitatu, ilhali wapinzani haohao waliojitwisha
kibarua cha kumsafisha ndio waliokuwa mstari wa mbele kwa miaka tisa mfululizo ‘kumchafua.’
Suala jingine la muhimu kuhusu uchaguzi huo lililkuwa nafasi ya utafiti wa kura za maoni
(opinion polls). Baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, taratibu tafiti za kura za
maoni zilianza kujichomoza, lakini zilikabiliwa na upinzani mkali kwa madai ya kukibeba
chama tawala. Iwapo madai hayo yalikuwa na ukweli au la, suala lililojitokeza wazi ni kuwa
wananchi wengi hawakutilia maanani matokeo ya tafiti hizo, pengine kutokana na hisia za
upendeleo kwa chama tawala au ugeni tu wa utaratibu huo.
Katika uchaguzi huo kulifanyika tafiti tatu za kura za maoni. Katika tafiti hizo, ya taasisi za
Twaweza, IPSOS (Synovate) na TADIP, mbili zilionyesha CCM na mgombea wake anaongoza
kwa mbali huku tafiti ya tatu ikionyesha mgombea wa UKAWA akiongoza.
Katika utafiti wa kura za maoni wa Twaweza, Magufuli aliongoza kwa asilimia 65 ilhali
Lowassa akipata asilimia 25, na katika utafiti wa IPSOS (Synovate) Magufuli alipata asilimia 62
na Lowassa asilimia 31, huku utafiti wa kura za maoni wa taasisi ya TADIP ukionyesha Lowassa
akipata asilimia 54 dhidi ya asilimia 40 kwa Magufuli.
Tafiti zote hizo za kura za maoni zilishutumiwa vikali, huku mbili zilizoonyesha Magufuli
akiongoza zikituhumiwa kuwa ‘zilipikwa na CCM,’ ilhali ule ulioonyesha Lowassa anaongoza
ukilaumiwa kwa madai kuwa taasisi iliyofanywa utafiti huo ilikuwa inamilikiwa na Chadema.
Matokeo ya uchaguzi huo yalipotangazwa, yaliakisi kwa kiasi kikubwa matokeo ya utafiti
wa kura za maoni wa Twaweza na IPSOS (Synovate). Katika matokeo hayo, Dokta Magufuli
alipata jumla ya kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46 ya kura 15,589,639 huku Lowassa
akiambulia kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 ya kura zote.
Kwa mujibu wa takwimu, takriban Watanzania milioni 23,161,440 walijiandikisha kupiga
kura katika uchaguzi huo. Kwa kuzingatia kwamba idadi kubwa ya wapigakura hao sio
wanachama wa chama chochote cha siasa, yayumkinika kuhitimisha kuwa ushindi kwa Magufuli
na CCM au Lowassa na UKAWA ungeamuliwa na kundi hilo. Kimahesabu, takwimu
zilizokuwepo zilionyesha kuwa idadi ya jumla ya wanachama wa CCM ni milioni 8 hivi, ambao
ni sawa na takriban asilimia 34.5 ya jumla ya Watanzania waliojiandikisha kupiga kura. Kwa
makadirio, idadi ya jumla ya wanachama wa vyama vinavyounda UKAWA ni pungufu ya hao
wa CCM, na hiyo ingeweza kufanya kundi la wapigakura wasiofungamana na chama chochote
kuwa zaidi ya asilimia 50.
Kilichoupa uzito zaidi kundi hilo la wapigakura wasiofungamana na upande wowote ni
ukweli kwamba lingeweza kuwa kubwa zaidi kutokana na mabadiliko yaliyojitokeza ndani ya
CCM na UKAWA kabla ya uchaguzi. Kwa upande wa CCM, kuondoka kwa Lowassa
kungeweza kuwafanya baadhi ya wana-CCM kutoiunga mkono CCM lakini bila kuchukua
uanachama huko UKAWA. Hawa wangeweza kuingia katika kundi hilo la ‘wasioungamana na
chama chochote,’ licha ya kuendelea kuwa wana-CCM.
Kwa upande wa UKAWA, ilihisiwa kuwa kuna baadhi ya wanachama wa vyama
vilivyounda umoja huo ambao sio tu hawakuridhishwa na suala la ushirikiano wa vyama hivyo,
lakini pia wale ambao walichukizwa na ujio wa Lowassa, au kukerwa na sababu zilizopelekea
Prof Ibrahim Lipumba (mwenyekiti za zamani wa CUF) na Dkt Slaa kujiengua katika uongozi.
Katika hawa, ilidhaniwa kuna ambao wangeweza kuamua kujiunga na CCM, lakini uwezekano
mkubwa ulikuwa ni kwa wengi wao kubaki wanachama wa vyama hivyo lakini wasiounga
mkono ugombea wa Lowassa. Kwahiyo nao wangeweza kuingizwa katika kundi la
‘wasiofungamana na chama chochote,’ licha ya kuendelea kuwa wananchama katika vyama
vyao.
Hadi kufikia hatua ya kuhitimisha toleo la kwanza la kitabu hiki, ambalo lilichapishwa
takriban wiki mbili kabla ya uchaguzi huo, mimi kama mwandishi nilisimamia kwenye kufanya
uchambuzi bila kuelemea upande wowote. Nilijitahidi kuelezea mapungufu ya pande zote mbili,
sambamba na fursa walizonazo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Nilifanya hivyo kwa
sababu lengo la kuandika toleo hilo halikuwa kufanya simulizi, au kukampenia chama au
mgombea fulani bali kuweka kumbukumbu sawia, pamoja na kuwasaidia wasomaji kufanya
maamuzi sahihi wakati wa kupiga kura.
Na uamuzi wa kuvizungumzia vyama viwili tu, yaani CCM na UKAWA (kama muungano
wa vyama) ulitokana na ukweli kuwa kwa vyovyote vile, mshindi katika kiti cha urais angekuwa
aidha Dokta Magufuli au Lowassa, huku ushindi kwa upande wa vyama kwa jumla kingekuwa
aidha CCM au UKAWA katika umoja wao. Kwahiyo, ilionekana bayana kuwa hatma ya
Tanzania ilikuwa mikononi mwa Magufuli na CCM yake na Lowassa na UKAWA yake, na
hivyo kulazimika kuwajadili wagombea hao na vyama hivyo.
Hata hivyo, na bila kupendelea upande wowote, nilibainisha bayana kuwa mazingira
yaliyokuwepo yaliipa nafasi kubwa CCM na mgombea wake Dokta Magufuli kuibuka mshindi
katika uchaguzi huo. Nilielezea sababu kadhaa ambazo zingezoweza kuisadia CCM na Dokta
Magufuli kushinda. Na nilifanya hivyo pia kwa UKAWA na Lowassa. Kwa kukilinganisha fursa
na vikwazo kwa kila upande haikuwa ngumu kubashiri ushindi kwa CCM na Dokta Magufuli.
Nilieleza pia kwamba ushindi kwa CCM na mgombea wake ungeweza kutokana zaidi na
nilichokiita ‘sababu za kimfumo,’ kwamba mfumo uliokuwepo katika kipindi cha kuelekea
uchaguzi ulimtengenezea mazingira mazuri Dokta Magufuli na chama chake, ilhali ushindi kwa
Lowassa na UKAWA ulitegemea zaidi mapungufu ya CCM, sio tu katika kujinadi bali pia
kupata mwanya wa kuwashawishi wapigakura wengi zaidi katika kundi muhimu la
‘wasiofungamana na chama chochote,’ ambalo niliamini kuwa lingeamua mshindi katika
uchaguzi huo.
Nilieleza pia kuwa kwa vile ‘wapigakura wasiofungamana na chama chochote’ ndio
wangeamua mshindi katika uchaguzi huo, ilikuwa rahisi zaidi kwao kumwamini Dokta Magufuli
kutokana na rekodi yake, kuliko Lowassa. Kwa kuwalinganisha wagombea hao wawili, Dokta
Magufuli angeweza na aliweza kutembea ‘kifua mbele’ kuonyesha mafanikio ya utendaji kazi
wake, kubwa zaidi likiwa kumudu kutumikia awamu mbili tofauti kwa ufanisi mkubwa. Hali
ilikuwa tofauti kwa Lowassa, kwa sababu vyovyote ilivyokuwa, tuhuma dhidi yake kuhusu
kashfa ya Richmond sio tu ilikuwa vigumu kufutika bali pia ilikuwa sio rahisi kwa Chadema na
UKAWA kwa ujumla kumsafisha mwanasiasa huyo ndani ya miezi matatu ilhali walitumia
takriban miaka tisa ‘kumchafua.’
Kibaya zaidi, wakati Dokta Magufuli aliungwa mkono na takribani wana-CCM wote,
tukiweka kando waliojiweka kando kutokana na jina la Lowassa kukatwa na vikao vya mchujo
vya chama hicho, na baadaye kukihama chama hicho tawala, Lowassa hata kama angeungwa
mkono na asilimia kubwa ya wana-UKAWA, wengi wa hao waliomuunga mkono walitumia
muda mrefu huko nyuma ‘kumchafua’.
Hoja hapa ni kwamba, wakati waliomuunga mkono Dokta Magufuli ni watu ‘waliomuunga
mkono muda wote,’ kwa maana ya ufuasi wao kwa CCM, kwa upande wa Lowassa, wengi wa
waliomuunga mkono ni ‘watu wapya,’ ambao huko nyuma walifanya kila jitihada ‘kumchafua.’
Ilikuwa rahisi kwa kundi la ‘wapigakura wasiofungamana na chama chochote’ kushawishiwa na
‘waliomuunga mkono Magufuli tangu mwanzo’ kuliko hao ‘waliomuunga mkono Lowassa muda
huo lakini huko nyuma walimbomoa.’
Kimsingi, CCM haikuhitaji kuwashawishi wanachama wake kumuunga mkono Dokta
Magufuli, kwa sababu alikuwa ‘mwenzao.’ Kwa upande wa Lowassa, sio tu zilihitajika jitihada
za kuwashawishi baadhi ya wana-UKAWA kuwa ‘actually tulikosea kumwita huyu mtu fisadi,’
lakini pia kuwaaminisha kuwa ‘atasimama nao hadi dakika ya mwisho,’ kwa kuzingatia hofu
kwamba ‘huenda Lowassa ametumwa na CCM ili kuuwa upinzani.’
Ndio, ilikuwa rahisi kwa UKAWA kudai kuwa ‘fisadi pekee hakuwa Lowassa tu, na ufisadi
CCM haukuwa Richmond pekee,’ lakini kwa upande mwingine, ukiangalia watu waliotajwa
kuwa karibu na Lowassa na wale walio karibu na Dokta Magufuli, mpigakura ‘asiyefungamana
na chama chochote’ angeweza kushawishika kirahisi kumchagua mgombea huyo wa CCM
kuliko Lowassa, kwa sababu wengi wa ‘waliomzunguka Lowassa,’ waliomfuata kutoka CCM na
baadhi ya waliotajwa kumuunga mkono bila kujitangaza hadharani, walikuwa watu wenye
rekodi zisizopendeza. Hili liliweza kujenga hofu kwamba, laiti mgombea huyo wa UKAWA
angeshinda, angeweza kuwawekea kando ‘wenye vyama vyao,’ na kuwateua ‘maswahiba zake’
waliotajwa kumsaidia katika kampeni zake.
Kwenye suala la mgombea gani kati ya Lowassa na Dokta Magufuli alikuwa na nafasi ya
kuleta mabadiliko halisi ndani ya chama chake na kwa taifa kwa ujumla, ilionekana kuwa
ingekuwa rahisi kwa Dokta Magufuli angalau kuahidi hilo kwa sababu kimsingi tatizo la CCM
lilikuwa ukosefu tu wa nia ya kufanya mabadiliko kusudiwa, kwani uwezo na sababu
zilikuwepo. Kwa upande wa Lowassa, hiyo tu kuamini kwamba kuwa hivi sasa yeye ni mtu
tofauti na yule aliyekuwa CCM ilikuwa ‘mtihani’ tosha.
Lakini kingine, Lowassa alishindwa kabisa kuelezea kwa undani kuhusu ajenda yake ya
mabadiliko, hali iliyopelekea hisia kuwa huenda yeye mwenyewe hakuamini katika mabadiliko
aliyohubiri. Kimsingi, mabadiliko yaliyotarajiwa na Watanzania, hususan wafuasi wa UKAWA,
sio jambo jepesi kama lilivyozungumzwa majukwaani.
Ingekuwa sio jambo la faida kwa wapigakura na Watanzania kwa ujumla pekee bali
lingeweza kumsaidia Lowassa na UKAWA endapo dhana hiyo ya mabadiliko ingefafanuliwa
kwa upana zaidi. Kwa mfano, mgombea huyo angeweza kueleza kuhusu ratiba ya mabadiliko
hayo, sambamba na kutanabaisha ni maeneo yapi yatakayoanza kushughulikiwa. Orodha ya
maeneo yaliyopaswa kukumbwa na mabadiliko hayo ni ndefu, na pasipo mipango ya kueleweka,
basi hata Lowassa angeshinda katika uchaguzi huu, angeweza kumaliza vipindi viwili vya urais
pasipo kutimiza ahadi ya kuleta mabadiliko.
Kulikuwa na haja kwa Lowassa na UKAWA kwa ujumla kujifunza kutoka katika ahadi ya
Kikwete wakati wa kampeni zake kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 ambapo alitoa
ahadi ya ‘jumla jumla’ ya ‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania.’ Japo ‘maisha bora’ ni rahisi
kuchanganuliwa kuliko ‘mabadiliko,’ kwa kiasi kikubwa Kikwete alimaliza mihula yake miwili
huku wananchi wengi wakidhani ahadi hiyo ya maisha bora ilikuwa ‘hadaa’ tu. Hata hivyo,
tatizo lililoifanya ahadi hiyo kutoonekana kama imetekelezwa ni kutokana na ‘ujumla jumla’
wake.
Kwa kuhubiri mabadiliko pasipo kuelezea kwa undani, ilihisiwa kuwa ‘urais wa Lowassa’
ungekumbwa na matatizo mapema kutoka kwa wananchi ambao wangekuwa wakitarajia, kwa
mfano, mara baada ya mwanasiasa huyo kuingiza Ikulu, kila mwananchi angeweza kujimudu
kiuchumi, ajira zingepatikana mara moja kwa wasio na ajira, na matarajio mengine lukuki. Si
kwamba wazo la mabadiliko lilikuwa baya au lisilohitajika bali lilistahili kutolewa maelezo ya
kina hususan mipango na ratiba thabiti ya utekelezwaji wake.
Lakini hata kama ingekuwa rahisi kwa Lowassa kueleza kuhusu ajenda ya mabadiliko kwa
upande wa kiutawala au sera, kikwazo kingeweza kuwa upande wa mabadiliko kijamii. Kwa
mfano, mwanasiasa huyo angepaswa kueleza ana mkakati gani ya kubadili kasumba iliyoota
mizizi katika nchi yetu ya ‘kuwapa wahalifu heshima wasiyostahili’? Ilikuwa jambo la kawaida
katika maeneo mengi ya Tanzania yetu kuona muuza madawa ya kulevya akitukuzwa na kupewa
‘wadhifa’ wa ‘mzungu wa unga’ badala ya kuitwa mhalifu. Kadhalika, ilizoeleka kuona
wabadhirifu makazini wakipewa ‘wadhifa’ wa ‘mapedejee.’
Licha ya tabia hizo, kuna masuala yanayopewa uzito mkubwa katika jamii ilhali yale ya
muhimu yakipuuzwa. Kwa mfano, watu wapo tayari kuchangia mamilioni ya shilingi kama
michango ya harusi lakini wanashindwa kuchangiana ada za watoto wao mashuleni. Laiti
ushirikiano unaoonyeshwa kwenye klabu za starehe, kile wenyewe wanaita ‘kuzungusha raundi
za kinywaji’ ungehamishiwa kwenye ushirika kwenye miradi ya maendeleo, basi pengine
mabadiliko yaliyohubiriwa na Lowassa yangekuwa yameanza kitambo.
Kuna tatizo la vijana wengi kutafuta njia za mkato za mafanikio, hali inayowavutia matapeli
kubuni miradi mbalimbali ya ‘kula fedha za bure.’ Ni watu wangapi waliopoteza fedha zao
katika ‘miradi ya kitapeli’ kama vile ‘Dollar Jet,’ ‘DECI,’ na mingineyo?
Licha ya miradi ya kitapeli wa utajiri wa ‘chapu chapu,’ kuna imani katika vitu visivyo na
mwelekeo kama ilivyokuwa katika suala la ‘kikombe cha babu,’ mtumishi wa Kanisa huko
Samunge, mkoani Arusha aliyeahidi tiba ya magonjwa mbalimbali, na kupelekea maelfu kwa
maelfu ya Watanzania kujazana huko. Hadi leo idadi ya waliopoteza maisha kwa kuamini ‘tiba
ya kikombe cha babu’ haijawekwa hadharani lakini yayumkinika kuhisi kuwa ni kubwa.
Kuna tatizo kubwa la imani za ushirikina ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi
zinazoongoza duniani kwa imani hiyo. Je mabadiliko ya kisera yanaweza kuwafanya waamini
wa ushirikina wabadilike? Licha ya ushirikina, kuna vijana lukuki wanaoamini kuwa njia ya
mkato ya mafanikio ni kujiunga na kikundi cha ‘Freemasons,’ huku takriban kila kijana
anyejituma na kufanikiwa kimaisha akihisiwa kuwa mfuasi wa kundi hilo. Kibaya zaidi, ilifika
mahala baadhi ya vijana kujizushia kuwa wao ni freemasons ili ‘waonekane kuwa wanakaribia
kupata utajiri punde.’
Kama kuna eneo linalohitaji mabadiliko ya haraka ni katika suala la rushwa. Utafiti mmoja
uliofanyika mkoani Arusha ulionyesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya waliohojiwa waliamini
kuwa ‘rushwa ilikuwepo, ipo na itaendela kuwepo milele.’ Sawa, rushwa ilikuwepo kitambo na
itaendelea kuwepo lakini si kwa kiwango kilichokuwepo wakati huo. Na uwepo wake wa muda
mrefu haukumaanisha wananchi wakubaliane nayo, kwani hata maradhi kama malaria na ukimwi
yamekuwapo kitambo lakini jitihada za kupambana nayo zinaendelea.
Kwahiyo, ajenda ya Lowassa kuhusu mabadiliko, licha ya uzuri wake, licha ya kuwa na
mkanganyiko mkubwa, haikupatiwa maelezo ya kutosha. Na ni katika mazingira haya,
waliomlaumu Lowassa kuhusu ‘hotuba zake za dakika chache’ walipata uzito katika lawama
hizo kwa sababu kuna masuala kadhaa yaliyohitaji kuelezwa kwa kirefu, kubwa likiwa ni hilo la
ajenda ya mabadiliko.
Katika kuhitimisha toleo la kwanza la kitabu hiki, nilieleza bayana ugumu wa kufanya
ubashiri wa uhakika kuwa nani kati ya Dokta Magufuli na Lowassa angeibuka mshindi. Hata
hivyo, ‘nilijifunga kitanzi’ kwa kueleza waziwazi kuwa mazingira yaliyokuwepo muda huo
yaliashiria kuwa mgombea huyo wa CCM na chama chake walikuwa na nafasi kubwa ya
ushindi. Nilikumbushia kuwa japo kulikuwa kuna idadi kubwa ya Watanzania waliochoshwa na
CCM lakini kuchoshwa pekee hakutoshi kukiondoa chama madarakani. Na kama alivyosema
Dkt Slaa wakati anatoa maelezo kuhusu kujitenga kwake na Chadema, mabadiliko ya kweli
yanahitaji mikakati makini ya watu makini. Na kwa kiasi kikubwa tu, si Lowassa wala UKAWA
waliokuwa watu makini wenye mikakati makini kuleta mabadiliko waliyoyahubiri.
Sura Ya Nne
Urais wa Dokta Magufuli na utekelezaji wa ‘Hapa ni Kazi Tu’: Siku moja tu baada ya kuapishwa
kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta Magufuli alionyesha dalili
kuwa kaulimbiu yake ya ‘Hapa Ni Kazi Tu’ haikuwa porojo. Badala ya kutumia siku ya kwanza
ofisini kwake Ikulu, Rais alifanya ziara ya kushtukiza katika Wizara ya Fedha, na alitembea kwa
miguu.
Siku nne baadaye, Dokta Magufuli alifanya tena ziara ya kushtukiza, safari hii katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambako alishuhudia utoaji mbovu wa huduma na kuchukua
uamuzi wa kuvunja bodi ya hospitali hiyo na kumtimua kazi Kaimu Mkurugenzi Mkuu.
Kadhalika, Rais aliagiza mashine za vipimo vya CT-Scan na MRI zitengenezwe haraka.
Akiwa madarakani ndani ya wiki tatu tu, Dokta Magufuli alichukua hatua kadhaa za kubana
matumizi yasiyo ya lazima. Hatua hizo ni pamoja na kufuta safari zote za nje kwa watumishi wa
serikali isipokuwa kwa kibali maalum kutoka kwake au Katibu Mkuu Kiongozi. Uamuzi huo wa
kufuta safari za nje ulipelekea kufutwa kwa majina 50 ya watumishi wa serikali waliotakiwa
kuhudhuria Mkutano wa Nchi za Jumuiya ya Madola, na kuwabakiza wanne tu, hatua iliyookoa
takriban shilingi bilioni 700.
Kadhalika, mara baada ya kuzindua Bunge, Rais aliamua kuwa shilingi milioni 225
zilizochangwa kwa ajili ya sherehe ya uzndizu wa bunge hilo zitumike kununulia vitanda kwa
ajili ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Akionyesha dhamira ya dhati ya kubana matumizi, Dokta Magufuli alifuta sherehe za
maadhimisho ya miaka 54 ya uhuru na badala yake akaagiza sherehe hizo ziazimishwe kwa
kufanya usafi wa mazingira nchi nzima. Uamuzi huo wa kufuta sherehe za uhuru uliokoa shilingi
bilioni 4, ambazo Rais aliagiza zielekezwe kwenye matengenezo ya Barabara ya Morocco, jijini
Dar es Salaam.
Historia ya utendaji kazi wa Dokta Magufuli yaonyesha kuwa ni mtu wa vitendo zaidi
kuliko maneno. Hata hivyo, historia pia yaonyesha kuwa anapoongea, maneno yake huwagusa
wengi. Na katika kuthibitisha hilo, hotuba aliyoitoa wakati anazindua Bunge inabaki kuwa moja
ya hotuba za kihistoria.
“Hotuba hii ya Rais Magufuli ni moja ya hotuba bora kabisa katika historia ya siasa za
Tanzania.” Hili lilikuwa hitimisho langu katika mtandao wa kijamii wa Twitter mara baada ya
hotuba hiyo.
Na kwa hakika watu kadhaa waliafikiana na hitimisho hilo. Kilichovutia wengi waliosikia
hotuba hiyo sio tu mpangilio wa hotuba yenyewe bali pia jinsi kila alilotamka lilivyoonyesha
bayana kuwa lilitoka moyoni mwake kwa dhati kabisa.
Rais alianza hotuba yake hiyo kwa kuorodhesha matatizo mbalimbali aliyobaini wakati wa
kampeni zake Urais ambapo alizunguka takriban Tanzania nzima. Alitoa uchambuzi wa kina wa
matatizo hayo kabla ya kuelezea kwa undani ni kwa jinsi gani serikali yake itayashughulikia.
Ilikuwa ni zaidi ya hotuba ya kisiasa, na pengine ingeweza kabisa kuwa mhadhara wa kitaaluma
uliofanyika katika lugha nyepesi na ya kueleweka.
Moja ya vitu vilivyovutia sana katika hotuba hiyo ni jinsi Rais Dokta Magufuli alivyoweza
kutoa jibu la swali ambalo kwa miaka kadhaa lilionekana kuwatatiza viongozi wetu mbalimbali:
“Kwanini Tanzania ni masikini licha ya utajiri lukuki wa raslimali ilionao.” Alieleza bayana na
kwa kirefu jinsi ufisadi, rushwa na uhalifu vilivyochangia kukwamisha maendeleo ya taifa letu.
Kadhalika, alifafanua, kwa kutumia takwimu halisi, jinsi mabilioni ya fedha yalivyotumika
visivyo kwa matumizi yasiyo muhimu na yaliyo nje ya uwezo wa taifa letu masikini.
Kwa hakika ilikuwa hotuba ya kihistoria iliyofunika kabisa utovu wa nidhamu wa hali ya
juu ulioonyeshwa awali na wabunge wa upinzani ambao walitumia muda mwingi kabla ya
hotuba hiyo kuzomea na baadaye kuamiriwa kutoka nje ya ukumbi huo.
Lakini kwa vile sio rahisi kumridhisha kila mtu, baadhi ya waliosikiliza hotuba hiyo walidai
kuwa eti “haina tofauti na hotuba nyingine kadhaa zilizokuwa nzuri kuzisikiliza lakini zikaishia
kuwa maneno matamu tu.” Wengine walikwenda mbali zaidi na kudai kuwa hata mtangulizi wa
Dokta Magufuli, yaani Rais Mstaafu Kikwete, naye pia alianza urais wake kwa hotuba za kutia
moyo kama hizo lakini mengi ya aliyoahidi, hususan lile la ‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania,’
yaliishia kuwa ahadi tu.
Sikukubaliana kabisa na wakosoaji hao, japo hoja zao zinaweza kuwa na mantiki kidogo. Ni
kweli kwamba ukosefu wa hotuba za kuvutia si moja ya matatizo yanayoikabili nchi yetu. Wengi
wa wanasiasa na viongozi wetu ni mahiri sana wa maneno lakini tatizo huwa katika kutafsiri
maneno yao kuwa vitendo.
Wakosoaji hao hawapo sahihi kwa sababu hotuba hiyo ilikuwa ya kutoka moyoni mwa
Dokta Magufuli, na haikuhitaji ‘sayansi ya roketi’ kubaini hilo. Ilikuwa hotuba ya kiongozi
anayeguswa na yanayoisibu nchi yake, kiongozi mwenye uelewa wa changamoto zinazoukabili
uongozi wake, na mwenye dhamira thabiti ya kukabiliana na changamoto hizo.
Kuna mbinu moja muhimu ya kubaini iwapo mtu anaongea ukweli au anahadaa, nayo ni
kumwangalia usoni. Tangu kuanza kwa kampeni zake za urais na hadi wakati wa hotuba hiyo
Bungeni, uso wa Dokta Magufuli wakati anaongea unaonyesha bayana kuwa kila neno linalotoka
mdomoni mwake ni la dhati, linatoka moyoni na si sehemu ya porojo tulilozowea kutoka kwa
wengi wa wanasiasa na viongozi wetu. Mtaalam yeyote wa kubaini ukweli na uongo
hatoshindwa kubaini uthabiti wa kauli za Dokta Magufuli upo wazi kwa yeyete anayemwangalia
usoni wakati anaongea.
Lakini pia, hotuba hiyo ilikuwa mwendelezo wa ishara nzuri zilizoanza kujitokeza siku moja
tu tangu Rais Magufuli aingie ofisini, ambapo alifanya ziara ya kushtukiza Wizara ya Fedha,
kabla ya kufanya ziara nyingine kama hiyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Na siku hiyo
ya uzinduzi wa Bunge, aliwakumbusha Watanzania enzi za (Waziri Mkuu wa zamani) hayati
Edward Sokoine, aliyesifika kwa uchungu wa mali za umma, baada ya kuamuru zaidi ya shilingi
milioni 200 zilizochangwa kwa ajili ya hafla ya mchapalo ya sherehe za uzinduzi wa Bunge
jipya zielekezwe kwenye ununuzi wa vitanda katika hospitali ya Muhimbili, na kiasi kidogo tu
kitumike kwa ajili ya hafla hiyo.
Kimahesabu, chini ya wiki tatu tangu aingie madarakani, Rais Magufuli aliokoa jumla ya
shilingi milioni 900 kutokana na hatua alizochukua dhidi ya matumizi yasiyo ya lazima. Kwa
kasi hii, kulikuwa na kila sababu ya kutarajiwa kuiona Tanzania ikipaa kiuchumi, na hatimaye
Watanzania kunufaika na neema lukuki ambayo nchi yao imejaaliwa kuwa nayo.
Wakati tangu wakati alipoteuliwa na CCM kuwa mgombea wa chama hicho katika nafasi ya
urais, Watanzania wengi hawakuwa shaka kuhusu uchapakazi wa Dokta Magufuli, ‘mtihani’ wa
awali ulikuwa kuhusu nani angemteua kuwa Waziri Mkuu. Hatimaye alimteua mwasiasa
asiyefahamika sana lakini anayesifika kwa uchapakazi, Khassim Majaliwa. Na haikuchukua
muda kuthibitishwa kuwa chaguo la Dokta Magufuli kwa Waziri Mkuu Majaliwa lilikuwa sahihi
kwani mara tu baada ya kuapishwa, alichukua hatua kadhaa zilizoonyesha kuwa yeye na ‘bosi’
wake ni ‘dream team.’
Moja ya hatua za awali za Waziri Mkuu Majaliwa ni ziara ya ghafla katika Bandari ya Dar
es Salaam, ambako alibaini upotevu wa makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya shilingi
bilioni 80. Baadaye alifanya kikao na uongozi wa Bandari hiyo na ule wa Mamlaka ya Mapato
(TRA) na kuwasimamisha kadhi maofisa kadhaa wa taasisi hizo mbili, ikiwa ni pamoja na
Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade. Kadhalika, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Jehsi la
Polisi kuwakamata maofisa hao ili waisaidie polisi katika uchunguzi.
Ufanisi mkubwa uliopatikana kwa Dokta Magufuli na Waziri Mkuu Majaliwa wakisaidiwa
na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefui, kumudu kufanya kazi bila ya baraza
la mawaziri, ulipelekea baadhi ya wananchi kutamani kusiwepo kabisa baraza hilo kwani
matunda ya viongozi hao yalionekana bayana. Hofu kubwa kuhusu baraza la mawaziri ilikuwa
katika uwezekano wa kurejea sura zilizozoeleka aidha kwa uzembe au ufisadi.
Japo hili litaongelewa kwa kirefu baadaye, kinachoweza kuelezwa kama ‘doa la kwanza’
katika utawala wa Dokta Magufuli ni pale alipotangaza baraza lake la mawaziri. Kwa vile
ilichukua zaidi ya mwezi mzima kuunda baraza hilo, matarajio ya wananchi wengi yalikuwa
makubwa katika kuona ‘sura za kuleta matumaini’ na zenye uwezo wa kuendana na kasi ya Rais
wao.
Baraza hilo lilitangazwa kwa awamu mbili, huku wizara chache zikiachwa ‘viporo.’ Jina la
waziri lililoonekana kugusa hisia za wengi, huku baadhi wakihoji busara za Dokta Magufuli, ni
la Profesa Sospeter Muhungo, mwanasiasa msomi ambaye alilazimika kujiuzulu katika utawala
wa Rais Kikwete kufuatia kashfa ya Tegeta Escrow.
Kilichowakera baadhi ya wananchi kuhusu Profesa Muhongo sio tu kuhusishwa kwake na
kashfa hiyo ya Escrow, ambayo baadaye ilipelekea kujiuzulu kwake, bali pia kauli yake maarufu
ya dharau kuwa Watanzania wanaweza kufanya biashara ya juisi tu na sio kumudu uwekezaji
mkubwa kama katika sekta ya gesi na mafuta. Hadi alipoteuliwa tena na Dokta Magufuli,
Profesa Muhongo hakuwahi kuikana kauli hiyo wala kuifafanua. Kwa maoni ya wengi, alipaswa
kuwaomba msamaha Watanzania kwa kuwadhalilisha.
‘Doa’ jingine kwa Dokta Magufuli ni pale alipotangaza majina ya kuziba ‘wizara viporo,’
ambapo miongoni mwa walioteuliwa alikuwa Profesa Jumanne Maghembe, aliyekabidhiwa
Wizara ya Maliasili na Utalii. Si tu kwamba Waziri huyo mpya alishawahi kushika wadhifa huo
huko nyuma pasipo mafanikio makubwa, na baadaye alihamishwa kutoka Wizara hiyo, bali pia
aliwahi kutajwa na uongozi wa CCM kuwa ni mmoja wa ‘mawaziri mizigo,’ yaani wasio na
ufanisi katika utendaji kazi wao.
Pengine kuthibitisha kuwa uteuzi wa maprofesa hao wawili ulikuwa na walakini, wote
wawili wameshatoka madarakani wakati kitabu hiki kinaandikwa. Profesa Muhongo alilazimika
kujiuzulu tena (kama alivyolazimika kujiuzulu katika serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais
Kikwete) baada ya Kamati iliyoundwa na Rais kuchunguza mchanga wenye madini (makinikia)
kutoa taarifa inayoonesha upotevu wa Sh trilioni 1.439 baada ya uchunguzi, kupima mchanga
ulio kwenye kontena 277 zilizozuiwa kusafirishwa nje ya nchi tangu Machi mwaka huu.
Kwa upande wa Profesa Maghembe, jina lake halikuwemo katika mabadiliko madogo ya
Baraza la Mawaziri la Dokta Magufuli yaliyofanyika Oktoba mwaka huu. Japo hakuna maelezo
yaliyokwishatolewa kuhusu uamuzi wa Dokta Magufuli kumwondoa Profesa huyo katika
Uwaziri, yayumkika kuamini kuwa uamuzi huo ulitokana na uendaji kazi usioridhisha.
Hata hivyo, pamoja na uwepo wa Profesa Muhongo na Profesa Maghembe katika kabineti
ya kwanza ya Dokta Magufuli, taarifa kwamba mawaziri wote walisainishwa mikataba maalum
‘inayowanga,’ kwa maana kuwa pindi wizara zao zikiboronga wao ndio watakuwa wa kwanza
kuwajibishwa, ziliwapa matumaini wananchi kuwa hata mawaziri wanaoangaliwa ‘kwa jicho la
walakini’ wangeweza kuwa wachapakazi wazuri kwani kinyume cha hivyo wangetimuliwa.
Na katika kuonyesha mabadiliko angalau ya kimtizamo, Profesa Muhongo alitangaza
kuwakaribisha wazawa katika uwekezaji katika sekta ya umeme, hatua iliyotafsiriwa kuwa
huenda amebadili mtizamo wake kuhusu uwezo wa Watanzania kuishia kwenye kutengeneza
juisi tu na si katika uwekezaji mkubwa.
Kwa upande wake, Profesa Maghambe alinukuliwa akieleza bayana kuzitambua
changamoto zinazoikabili sekta ya maliasi na utalii na kuapa kupambana nazo vilivyo, huku
akipigia mstari matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kukabiliana na tatizo sugu la ujangili.
Kadhalika, uamuzi wa Dokta Magufuli kumteua Dokta Philip Mpango, mchumi wa zamani
katika Benki ya Dunia, na mchapakazi ‘aliyefanya miujiza’ kwa kuiwezesha Mamlaka ya
Mapato kukusanya zaidi ya shilingi trilioni 1.3 kwa mwezi mmoja tu baada ya kuteuliwa ukaimu
Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, uliwapa matumaini makubwa Watanzania kuwa baraza lake
la mawaziri lingeendana na faslafa yake ya ‘Hapa Ni Kazi Tu.’
Kumpatia Dokta Mpango Wizara nyeti ya Fedha na Mipango ilionekana kama ‘kuuwa
ndege wawili kwa jiwe moja.’ Kwa upande mmoja, mafanikio aliyoyaonyesha katika muda
mfupi tu akiwa kaimu Kamisha Mkuu wa TRA, yaliashiria kuwa Dokta Magufuli ameipatia
Tanzania mtu sahihi kabisa anayeweza kulisaidia taifa kiuchumi, hususan kukabiliana na tatizo
sugu la ukwepaji kodi. Kanuni za kiuchumi kuhusu ukusanyaji kodi zipo bayana: taifa lisilo na
ufanisi katika ukusanyaji kodi na matumizi yake lazima litayumba kiuchumi. Kwa muda mrefu,
tatizo kwa nchi hiyo halikuwa kwenye makusanyo ya kodi pekee bali pia matumizi yasiyoendana
na kidogo kilichokusanywa katika kodi. Mara baada ya kuingia madarakani, Dokta Mpango
alieleza bayana kuwa asingekubali kuona ama kuendelea kuwafumbia macho watu ambao
wangebainika kuitumia TRA kama pango la kujinufaisha kiuchumi.
Kwa upande mwingine, ukweli kwamba mchumi huyo aliwahi kufanya kazi kwa ufanisi
katika Benki ya Dunia ulimaanisha kuwa Tanzania sio tu ilimpata mtu mwenye uelewa mkubwa
wa masuala ya uchumi kimataifa bali pia mwenye uzoefu na hadhi iliyotarajiwa kuleta matokeo
chanya katika mahusiano na nchi nyingine katika uchumi wa dunia.
Kama kulikuwa na hofu yoyote kuhusu baadhi ya walioteuliwa kuwa mawaziri au manaibu
waziri, basi uteuzi wa makatibu wakuu na manaibu wakuu uliongeza matumaini zaidi kwa
Watanzania. Timu ya watendaji hao wakuu kitaalamu katika wizara ilijumuisha maprofesa 7,
madokta 14, wahandisi 6, ma-meja jenerali wastaafu wawili na mabalozi wa zamani wawili.
Kuchanganya na maprofesa, madokta na wahandisi kadhaa waliosheheni katika kabineti yake ya
kwanza, ilitarajiwa kuwa hakutokuwa na fursa ya uzembe katika serikali ya Dokta Magufuli.
Kitu kimoja kikubwa muda mfupi tu baada ya Dokta Magufuli kuingia madarakani ni
matumaini ya wananchi wengi kurejea kwa kasi. Matumaini hayo yalitokana na dalili za awali
kuwa kiongozi huyo alikuwa akitekeleza kaulimbiu yake ya ‘Hapa Ni Kazi Tu’ kwa vitendo
pasipo porojo.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge, Rais alitanabaisha kuwa kazi yake ni ‘kutumbua
majipu,’ na ghafla neno hilo likatokea kupata umaarufu mkubwa, huku mafisadi, wala rushwa,
wazembe na kadhalika wakianza kuitwa ‘majipu.’
Sambamba na umaarufu wake ulionekana kukua kwa kasi nchini Tanzania, Dokta Magufuli
pia alijipatia umaarufu mkubwa duniani kufuatia hatua zake mbalimbali za ufanisi alizochukua
tangu alipoingia madarakani. Licha ya hatua kadhaa za kubana matumizi, Dokta Magufuli pia
alichukua hatua dhidi ya watendaji wenye mapungufu, huku miongoni mwa ‘wahanga’ wa awali
akiwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuwia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU), Dokta Edward Hoseah, ambaye wadhifa wake huo ulitenguliwa na Rais.
Wiki tatu tu tangu baada ya kuapishwa kuwa Rais, mtandao wa kijamii wa Twitter
‘ulitikiswa’ na ‘trend’ maarufu kabisa ya #WhatWouldMagufuliDo, yaani ‘Je Magufuli
angefanyaje,’ ambapo watumiaji wa mtandao huo kutoka sehemu mbalimbali duniani
walionyesha mapungufu yanayofanywa na viongozi wa nchi zao, na kujiuliza Magufuli
angefanya pindi angekuwa kiongozi katika nchi hizo.
Kana kwamba hiyo haitoshi, vyombo mbalimbali vya habari duniani viliripoti kuhusu
ufanisi wa Dokta Magufuli, huku baadhi ya wanahabari wakiwashauri viongozi wa nchi zao
kuiga mfano wa kiongozi huyo.
Katika hali inayoweza kuonekana kama miujiza, ilifikia hatua kundi la wananchi nchini
Kenya kuandamana wakidai ‘Magufuli awe rais wao’ wakionyesha kuchoshwa na tuhuma
mbalimbali zinazouandama utawala wa Rais Uhuru Kenyatta.
Kadhalika, watumiaji mbalimbali wa mitandao ya kijamii kutoka kila kona ya dunia
walimtumia Dokta Magufuli kama ‘reference’ (kielelezo) kudai uwajibikaji kwa viongozi katika
nchi zao.
Kwa hakika ukiondoa zama za ‘mwanasiasa wa kimataifa’ marehemu Baba wa Taifa, Julius
Nyerere, Tanzania ilikuwa haijawahi kushuhudia kiongozi wake akipata umaarufu dunia nzima
kama inavyotokea kwa Dokta Magufuli katika siku zake za mwanzo za urais wake. Na hisia
miongoni mwa Watanzania wengi siku hizo zilikuwa kwamba huenda nchi yao ilikuwa
imefanikiwa kupata mrithi halisi wa Nyerere, sambamba na mrithi wa marehemu Sokoine,
Waziri Mkuu aliyesifika kwa uchapakazi na kuichukia rushwa kwa dhati.
Kilichotia matumaini makubwa zaidi kuhusu uchapakazi wa Dokta Magufuli,
kilijidhihirisha katika hotuba yake aliyoitoa alipokutana na uongozi wa Jumuiya za
wafanyabiashara wakubwa, ambapo licha ya kuwaamuru waliokwepa kodi kujisalimisha ndani
ya siku 7, aliwasihi watumie uwezo wao kuiletea Tanzania maendeleo kusudiwa. Alieleza kuwa
anaamini kabisa kuwa nchi yetu ina uwezo wa kuwa mingoni mwa nchi wafadhili, na
kutanabaisha anatamani kuona hilo linatokea huko mbeleni.
Sura ya sita katika kitabu ‘Dokta John Magufuli: Safari Ya Urais, Mafanikio Na
Changamoto Katika Urais,” kilichochapishwa siku 55 tu baada ya Rais Magufuli kuingia
madarakani, iligusia changamoto mbalimbali ambazo mwandishi alidhani zingeweza kumkabili
kiongozi huyo, licha ya kilichoonkena mafanikio makubwa katika siku zake za awali.
Moja ya changamoto hizo ilikuwa ukweli kwamba Dokta Magufuli asingeweza kufanikiwa
peke yake pasipo ushirikiano wa Watanzania wote. Mfano ulikuwa kwenye mapambano dhidi ya
rushwa, ambapo mwandishi alikumbusha kuwa mara nyingi Watanzania wamekuwa
wakikumbushwa kuhusu umuhimu wa kujenga kasumba ya kudai haki na stahili zao (kwa
amani) badala ya kuona haki au stahili zao ni kama fadhila au upendeleo flani. Kwa kutambua na
kudai haki au stahili zao, wananchi wangeweza kumsaidia Rais wao kwa ‘kulazimisha’ huduma
bora na ufanisi pasipo haja ya yeye au wasaidizi wake kuingilia kati. Na uzuri wa kufanya hivyo
ni kwamba ingezua ‘domino effect,’ kwamba mafanikio katika eneo moja yangeweza
kuhamasisha taasisi nyingine zilizozembea kubadilika pia.
Ilielezwa kwamba isingekuwa rahisi kwa Rais Magufuli au wasaidizi wake kwenda kila
sehemu kuwezesha au kuharakiasha upatikanaji wa huduma. Jukumu hilo lingepaswa kusaidiwa
na wananchi wenyewe ambao mara nyingi ndio wahanga wakubwa wa huduma mbovu.
Kadhalika, watoa huduma wangeanza kutambua kuwa hizo ni zama mpya, mambo yamebadilika,
kwahiyo shurti nao wabadilike.
Kadhalika, mchango wa wananchi wote ungehitajika katika kupambana na ufisadi, rushwa
na uhalifu mwingine. Wakati Rais aliahidi kukabiliana na ‘mapapa’ wa uhalifu kama kwenye
biashara hatari ya madawa ya kulevya, pasipo wananchi kumsaidia kwa kuwatenga wahusika na
kuwaripoti - badala ya kuwasujudia na kuwapa majina ya heshima kama ‘wazungu wa unga’ au
‘mapedejee’ – ingepunguza ufanisi wa jitihada hizo, na Tanzania ingeendelea kuumizwa na
vitendo hivyo viovu.
Kadhalika, ilishauriwa kuwa ili kauli-mbiu ya ‘Hapa Ni Kazi Tu’ iweze kuleta matokeo
kusudiwa na kuwa ya ufanisi ingebidi kila Mtanzania kuachana na dhana fyongo ya kusaka
mafanikio kwa njia za mkato, kwamba kungekuwa na haja ya kurejea zama za Ujamaa na
Kujitegemea ambapo waliokula bila kuvuja jasho waliitwa ‘kupe.’ Kila mtu alipaswa achape
kazi, kuacha kufanya ‘ujanja ujanja,’ kuona fahari kuwa na shughuli halali badala ya kuamini
kuwa ufisadi, rushwa, uhalifu, nk ndio njia rahisi na sahihi za kufikia mafanikio kwa haraka.
Changamoto nyingine kubwa, na iliyotarajiwa kugusa mahusiano kati ya Tanzania na nchi
wahisani ilikuwa mgogoro wa kisiasa huko Zanzibar uliosababishwa na uamuzi wa Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kufuta matokeo ya uchaguzi wa Rais wa huko, na kuagiza uchaguzi
huo urudiwe tena. Na uliporudiwa, chama kikuu cha upinzani cha CUF kilisusia uchaguzi huo,
na hadi muda huu chama hicho kimegoma kuitambua serikali ya CCM huko Zanzibar..
Licha ya Katiba ya Muungano na ile ya Zanzibar kumnyima Dokta Magufuli nafasi kubwa
ya kuliingilia tatizo hilo kwa undani, si yeye wala Rais wa Zanzibar Dokta Ali Mohammed
Shein anayeonekana na kuwa na nia ya kusaka suluhisho la kudumu la mgogoro huo wa kisiasa.
Kwa upande mwingine, mgogoro mkubwa unaoendelea CUF ambao umezua makundi
makuu mawili – linalomuunga mkono Mwenyekiti wa Taifa aliyotangaza kujiuzulu kabla ya
kurejea madarakani ‘kimabavu,’ Profesa Ibrahim Lipumba, na lile la Katibu Mkuu wa chama
hicho, Seif Sharif Hamad – unaweka mazingira magumu ya kusaka mwafaka katika mgogoro wa
kisiasa huko Visiwani.
Changamoto nyingine ya wazi kwa Dokta Magufuli na serikali yake ilikuwa tatizo la
ufisadi, rushwa na uhalifu kwa ujumla. Japo katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge, Dokta
Magufuli aliongelea changamoto hiyo kwa urefu na mapana, na kueleza bayana kuwa vita hiyo
ni ngumu na anahitaji Watanzania wamwombee, bado kulikuwa na hofu kwamba huenda
asingepata kuungwa mkono vya kutosha na baadhi ya wana-CCM waliokuwa wakikumbatia
ufisadi, rushwa, na uhalifu mwingine.
Katika kitabu hicho, mwandishi alishauri kwamba ili Dokta Magufuli afanikiwe kukabiliana
na changamoto hizo, licha ya dua na sala za Watanzania kwake, na licha ya wao kumuunga
mkono kwa kuchukia vitendo hivyo na kupambana navyo, silaha kubwa ambayo angeihitaji zaid
ni Idara ya Usalama wa Taifa. Tasnia ya usalama wa taifa ina kanuni moja kuu: ‘kukua kwa
matishio kwa usalama wa taifa (kama ufisadi, rushwa, madawa ya kulevya, ujangili, nk) ni ishara
ya wazi ya mapungufu ya kiufanisi ya idara ya usalama ya taifa husika.’
Kwa maana hiyo, kushamiri kwa maovu hayo katika Tanzania yetu kulikuwa ishara za wazi
za mapungufu ya kiutendaji ya taasisi hiyo nyeti. Kwa muda mrefu, mwandishi, kama mtumishi
wa zamani wa taasisi hiyo, na kwa sasa msadi (consultant) katika fani hiyo, amekuwa akihimiza
haja ya kufanyika mageuzi ya kimfumo na kiutendaii kwa taasisi hiyo muhimu.
Moja ya mapendekezo hayo ni haja ya kuwepo kile wazungu wanaita ‘oversight,’ yaani
chombo au utaratibu unaoweza angalau kuwahoji watendaji wakuu wa Idara hiyo. Kwa hali
iliyokuwepo, taasisi hiyo inaonekana kutumia nyenzo yake muhimu kiutendaji kazi, ya usiri,
kuficha mapungufu yake, sambamba na kutochukua hatua stahili dhidi ya matishioya usalama
kwa taifa.
Kwa uelewa wa mwandishi, miongoni mwa vikwazo vya ufanisi kwa taasisi hiyo ni ajira
zilizokuwa zinazotolewa kiupendeleo. Mwandishi alishauri kwamba njia rahisi ya kukabiliana na
tatizo hili ni kuwa na utaratibu wa wazi wa ajira kama ilivyo kwa taasisi kubwa za usalama
duniani, kwa mfano CIA, NSA, MI6, MI5 na GCHQ. Ajira ya uwazi maana yake ni matangazo
ya ajira hizo kuwekwa bayana, na taratibu za ajira kuzingatia sifa, vipaji na uwezo badala ya
undugu au kujuana. Afisa usalama wa taifa anayeamini kuwa ajira yake ni matokeo ya ‘msaada
wa flani’ anaweza kuwa na mapungufu makubwa katika uzalendo, ambao ni nguzo kuu katika
utumishi kwa taasisi za usalama wa taifa dunian kote.
Kadhalika, ilishauriwa kwamba kuna haja kwa Idara hiyo kupewa nguvu zaidi ya kuishauri
tu serikali. Kama ilivyo kwa taasisi nyingi kubwa za usalama wa taifa duniani, kulikuwa na haja
ya kuangalia uwezekano wa kuiwezesha Idara ya Usalama wa Taifa kuwa na mamlaka ya
kukamata (power of arrest), hasa ikizingatiwa kuwa mbinu zinazotumiwa na maafisa usalama wa
taifa ni za hali ya juu zaidi ya polisi, TAKUKURU au taasisi nyingine za usalama.
Ilielezwa kuwa umuhimu wa mabadiliko kwa taasisi hiyo si tu kwa minajili ya kumsaidia
Dokta Magufuli katika utekelezaji wa majukumu yake, lakini pia ukweli kwamba vita
aliyotangaza dhidi ya mafisadi, wafanyabiashara ya madawa ya kulevya, majangili, nk ilikuwa
dhidi ya watu hatari. Ukweli kwamba uhalifu waliokuwa wanafanya watu hao ni sehemu
muhimu ya uhai wa watu hao ulimaanisha kwamba wangemtazama Dokta Magufuli kama
kizingiti katika maisha yao ya kihalifu, na wangeweza kuwa na dhamira ya kumdhuru.
Ili kuwadhibiti, taasisi pekee ambayo ingeweza kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi ni Idara
hiyo ya Usalama wa Taifa. Lakini ili iweze kufanya hivyo kwa ufanisi, sharti yenyewe iwe ‘safi.’
Taarifa za ndani zilionyesha kuwa kwa muda mrefu baadhi ya watendaji wa taasisi hiyo
walikuwa wakitumika kwa maslahi ya watu binafsi. Pasipo kuchukua hatua madhubuti, ‘rogue
elements’ ndani ya taasisi hiyo zilionekana kuweza sio tu kukwaza jitihada za Dokta Magufuli
kupambana na wahalifu bali pengine hata kujaribu kumdhuru.
Kimfumo, mwandishi alishauri kuwa ni muhimu kwa Idara ya Usalama wa Taifa
kutojihusisha na siasa. Hili lilikuwa tatizo la muda mrefu na liliathiri sana ‘professionalism’
katika taasisi hiyo muhimu. Wakati siasa ni moja ya maeneo ya kushughulikiwa na taasisi hiyo,
kuchanganya taaluma na siasa kulipelekea kile kinachoitwa kibaiolojia kama ‘symbiotic
relationship,’ yaani uhusiano wa kutegemeana kati ya wanasiasa na taasisi hiyo. Moja ya athari
kubwa ilikuwa uwezekano wa taasisi hiyo kutumika kwa maslahi binafsi ya wanasiasa au
watendaji wa serikali.
Changamoto nyingine ni ndani ya CCM, chama ambacho kwa muda mrefu kimewakumbatia
mafisadi, wauza madawa ya kulevya, majangili, na wahalifu wengineo. Kama ilivyo kwa Idara
ya Usalama wa Taifa na siasa, uhusiano kati ya CCM na baadhi ya watu wasio na wasifu wa
kupendeza katika ujamii nao umekuwa symbiotic, ambao baadhi ya watu wanaofahamika kuwa
ni mafisadi au wanaojihusisha na uhalifu wamewekeza fedha zao katika chama hicho tawala kwa
aidha kukichangia fedha au kuwafadhili wagombea wa chama hicho katika kuwania nyadhifa
mbalimbali.
Hata hivyo, pamoja na changamoto hizo nilizoainisha hapo juu, mwandishi alikuwa na
matumaini makubwa kuwa Dokta Magufuli na timu yake ingefanikiwa sio tu kukabiliana na
changamoto hizo bali pia kumudu kuifikisha Tanzania mahala inapostahili kuwa. Ilitarajiwa
kuwa chini ya utawala wa Dokta Magufuli, zama za Tanzania kuwa miongoni mwa nchi
masikini kabisa duniani licha ya utajiri lukuki iliojaaliwa kuwa nao, zingeanza kuelekea
ukingoni. Pia zilianza kujitokeza hisia kwamba huenda huko mbeleni Tanzania ingeweza kuwa
moja ya mataifa yenye nguvu kubwa kiuchumi duniani, na pengine kuingia katika kundi la nchi
wafadhili.
Kitabu hicho kilihitimishwa kukumbushia kuwa takriban muda wote akiwa kwenye kampeni
zake, na takriban katika hotuba zake alizotoa baada ya kuapoishwa kuwa rais (hadi wakati kitabu
hicho kinachapishwa), neno ambalo Dokta Magufuli alikuwa akilitaja sana ni MUNGU. Hii
ilionekana kuwa ishara nzuri na muhimu, kwa sababu takriban robo tatu ya Watanzania ni
washika dini wanaomtumainia Mwenyezi Mungu katika maisha yao ya kila siku. Kwa hiyo, kwa
Dokta Magufuli kumtaja Mungu mara kadhaa katika hotuba zake, ilileta hisia kuwa sio tu taifa
hilo limepata kiongozi mchapakazi lakini pia mcha Mungu. Na hiyo ilipelekea kumkumbuka
marehemu Nyerere ambaye inaelezwa kwamba moja ya sababu za mafanikio katika uongozi
wake ilikuwa ucha-Mungu wake.
Sura Ya Tano
Kwa jinsi hali ya Tanzania ilivyokuwa hususan kabla Dokta Magufuli haijaingia madarakani,
kulikuwa na ulazima kwa kiongozi huyo kuja na mikakati kabambe ya kuiondoa Tanzania katika
mwelekeo mbaya. Pamoja na viongozi wakuu wawili wa Awamu ya Nne, Rais Jakaya Kikwete
na Waziri Mkuu wake Mizengo Pinda kutamka bayana kuwa hawaelezwi kwanini Tanzania ni
masikini, haikuhitajika japo utafiti kubaini kwamba kushamiri kwa rushwa na ufisadi
kulichangia umasikini kwa taifa na wananchi kwa ujumla.
Kwa upande mmoja, sera za kiuchumi za watangulizi wa Rais Magufuli, yaani marais
Mwinyi, Mkapa na Kikwete, ziliwapendeza nchi na taasisi wahisani, na Tanzania ilikuwa moja
ya nchi iliyonufaika kwa kiasi kikubwa na misaada ya kimataifa. Wakati fulani, Tanzania
ilikuwa nchi ya tatu nyuma ya Afghanistan na Iraq kunufaika na misaada ya kimataifa. Hata
hivyo asilimia kubwa ya misaada hiyo iliisha mifukoni mwa mafisadi.
Kwa upande mwingine, watangulizi hao wa Dokta Magufuli hawakufanya jitihada za
kutosha kuandaa na kutekeleza sera madhubuti za kuondoa masikini. Pamoja na kutofanikiwa
vya kutosha, sera mbalimbali za kiuchumi katika serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya
Nyerere zililenga kuondoa umasikini kwa kuweka njia kuu za kiuchumi katika miliki ya umma.
Japo kuna wanasiasa ‘wajanja’ waliotumia fursa hiyo kujinufaisha, Tanzania chini ya utawala wa
Nyerere ilikuwa nchi ambayo ya usawa kwa kiasi cha kuridhisha.
Wakati serikali ya Awamu ya Pili chini ya Rais Mwinyi ilihusika na ‘kifo cha itikadi ya
Ujamaa na Kujitegemea’ kupitia kiitwacho ‘Azimio la Zanzibar,’ serikali ya Awamu ya Tatu
chini ya Rais Mkapa iliweka mbele zaidi maslahi ya wawekezaji kuliko wananchi wazawa. Na
baada ya Rais Mkapa kuondoka madarakani, ilibainika kuwa nyuma ya pazia la uwekezaji
kulikuwa na dalili za ufisadi.
Kama hali ilikuwa mbaya katika Awamu ya Pili na ya Tatu, basi hali ilikuwa mbaya zaidi
katika serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Kikwete. Moja ya sababu kubwa zilizotengeneza
mazingira mabovu kwa utawala huo ni kampeni ya Kikwete kuingia Ikulu ambayo ilihusisha
kundi lililofahamika kama ‘wanamtandao,’ lililojaa watu wa aina mbalimbali, wengi wao
wakiwa na wasifu usiopendeza. Kundi hilo lilipigana kufa na kupona kuhakikisha kuwa
mgombea wao Kikwete anaingia madarakani. Inaelezwa kuwa jitihada za kundi hilo zilianza
mara baada ya jaribio lililoshindikana la Kikwete na aliyekuwa mshirika wake mkubwa,
Lowassa, kuwania urais mwaka 1995. Inaelezwa kuwa Nyerere aliingilia kati jaribio hilo na
hatimaye ‘kumpitisha mgombea wake’ yaani Mkapa.
Baadhi ya wanamtandao walimpigania Kikwete kwa matarajio ya kulipwa fadhila mara
baada ya mwanasiasa huyo kuingia madarakani. Na kwa upande mwingine, Kikwete aliingia
madarakani akiwa na deni kubwa la fadhila kwa wanamtandao. Ndio maana haikushangaza
kuona miezi michache tu baada ya kuingia madarakani, serikali yake ikaanza kuandamwa na
kashfa mbalimbali za ufisadi.
Yayumkinika kuhitimisha kuwa japo tatizo la ufisadi lilianza kuchipuka kwa kasi katika
serikali ya Awamu ya Pili chini ya Rais Mwinyi, na kupata nguvu zaidi kupitia sera za uwekezaji
za serikali ya Awamu ya Tatu ya Mkapa, zama za Kikwete sio tu ziliimarisha ufisadi bali pia
ziliufanya kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku ya Mtanzania.
Ni katika Awamu hiyo ambapo uhalifu kwa maana ya rushwa na ufisadi, ujangili, biashara
ya madawa ya kulevya, nk viligeuka kuwa kama shughuli halali. Katika utawala wa Kikwete,
kuna wakati bidhaa kwa iliyosafirishwa nje (export) na iliyoingizwa Tanzania kutoka nje
(import) ilikuwa madawa ya kulevya.
Kushamiri kwa vitendo vya kihalifu katika utawala huo vilijenga saikolojia isiyopendeza
mingoni mwa Watanzania kwamba njia yenye ufanisi zaidi kufikia mafanikio ni kujihusisha na
vitendo hivyo vya kihalifu. Kwa kushindwa kuchukua hatua stahili dhidi ya mafisadi, wauza
madawa ya kulevya, majangili, nk ilifika mahala ikaonekana kana kwamba vitendo hivyo
vimehalalishwa, na hiyo ikahamaisha watu wengi zaidi – hususan vijana – kujiingiza kwenye
vitendo hivyo.
Kwahiyo kimsingi hayo ndio mazingira ambayo Dokta Magufuli alikumbana nayo wakati
anaingia madarakani. Lakini ukweli kwamba mwanasiasa huyo alikuwa mmoja ya mawaziri
katika serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Kikwete, sambamba na taswira iliyojengeka kuwa
CCM – chama ambacho Dokta Magufuli alipitia kugombea urais – kilikuwa ‘kichaka cha
kuhifadhi mafisadi, ulileta hofu baadhi ya Watanzania kuwa huenda utawala mpya usingeweza
kuleta mabadiliko yoyote ya maana.
Lakini kama ilivyoelezwa awali kwamba katika kampeni zake za kuwania urais, Dokta
Magufuli alionekana kuelemea zaidi kwenye maslahi ya taifa kuliko kuweka mbele itikadi za
chama chake CCM. Kadhalika, mwanasiasa huyo alionyesha ujasiri mkubwa kwa kukiri makosa
ya chama chake huku akienda mbali zaidi na kuonyesha jinsi angeweza kuyarekebisha makosa
hayo.
Na kama ilivyokuwa katika kampeni za urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010
ambapo ajenda kuu ilikuwa ufisadi uliokigubika serikali ya Kikwete na CCM kwa ujumla, huku
chama kikuu cha upinzani Chadema kupitia mgombea wake Dkt Slaa kikiwa kimejitanabaisha
kama wapambanaji wakubwa dhidi ya ufisadi, kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 nazo
zilishuhudia ajenda ya ufisadi ikiwa na umuhimu wa kipekee.
Kwa upande mmoja, wakati Dokta Magufuli alipata ujasiri wa kueleza bayana jinsi ufisadi
ulivyoshamiri ndani ya chama chake, jinsi unavyowaathiri Watanzania, na jinsi ambavyo
angeshughulikia tatizo hilo, kwa upande mwingine, umoja wa vyama vya upinzani wa UKAWA
‘ulipatwa na kigugumizi’ kuongelea suala hilo kwa sababu zilizo wazi. Itakumbukwa kuwa kwa
takriban miaka 9 mfululizo, vyama vya upinzani hususan Chadema vilikuwa vikimwandama
aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza katika serikali ya Kikwete, Lowassa, kuwa ni kielelezo cha
ufisadi ndani ya CCM. Na kwa hakika, ufuatiliaji wa Chadema ulichangia uamuzi wa Lowassa
kujiuzulu Uwaziri Mkuu mwaka 2008 kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Richmond.
Kutokana na uamuzi wa Lowassa kujiunga na upinzani baada ya kutofanikiwa azma yake ya
kuwania urais kupitia CCM, iliwawia vigumu UKAWA kuongelea ajenda ya ufisadi kwani wao
walikuwa na mchango mkubwa katika kujenga dhana kwamba ‘Lowassa ni fisadi.’
Kwa wapinzani kukwepa ajenda hiyo muhimu, ilimpa fursa nzuri Dokta Magufuli kuielezea
kama tatizo linalohitaji ufumbuzi na kueleza mikakati yake ya kukabiliana nalo.
Japo ni kweli kwamba nyota ya Lowassa ilikuwa inang’ara mno hadi wakati anajiondoa
CCM, Chadema na UKAWA kwa ujumla walijinyima fursa nzuri mno ya kuibana CCM kuhusu
ufisadi hasa ikizingatiwa kuwa jitihada za Chadema dhidi ya tatizo hilo zilikuwa zikiungwa
mkono na Watanzania wengi.
Kulikuwa na tatizo jingine kuhusu Lowassa. Katika vitabu vyangu viwili kuhusu uchaguzi
mkuu wa mwaka 2015, nilielezea kosa la kiufundi lililofanywa na Lowassa katika safari yake ya
kuwania urais. Ikumbukwe kuwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ilikuwa kama
kilichobaki ni suala la muda tu kabla mwanasiasa huyo kutangazwa rais. Kadhalika, kadri
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ulivyokuwa unazidi kujongea ndivyo umaarufu wa Lowassa
ulivyozidi kuongezeka.
Lakini badala ya kutumia fursa hiyo vizuri, mwanasiasa huyo alionekana kama
aliyebweteka, huku akikataa kutamka bayana iwapo angegombea urais. Aliendelea na hali hiyo
hadi katikati ya mwaka 2014 ambapo mwanasiasa kijana January Makamba alitangaza rasmi nia
yake ya kuwania urais. Ghafla, ile dhana kuwa ‘Lowassa ndio rais ajae wa Tanzania’ ikaingiliwa
na jina la mwana-CCM mwingine, yaani January.
Taratibu yakaanza kuibuka majina ya makada wengine wa chama hicho tawala waliotangaza
nia zao za kuwania urais. Lowassa alipoamua kutangaza rasmi nia yake, ule mvuto uliokuwepo
awali ulishaaza kupungua, huko wanasiasa kama January wakizidi kupaa kwa umaarufu.
Kwamba huenda Lowassa alijiamini kupita kiasi ndio maana hakuona umuhimu wa
kutangaza mapema dhamira ya kuwania urais, au iwapo maandalizi yake yalikuwa duni na
hatimaye kupelekea jina lake kutopitishwa na chama chake, ni vigumu kueleza kwa uhakika.
Lakini yayumkinika kuhitimisha kuwa Lowassa aliyejiunga na Chadema na baadaye kuwa
mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA hakuwa na umaarufu/mvuto mkubwa kama ule aliokuwa
nao baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Kwahiyo, kwa kiasi flani safari ya Dokta Magufuli ilirahisishwa na makosa ya kimkakati
yaliyofanywa na Chadema/UKAWA. Kadhalika, ajenda mbadala ya ‘mabadiliko’ ambayo
Lowassa alikuja nayo katika kambi ya upinzani haikuwa na mwelekeo, na hadi tarehe ya
uchaguzi mkuu ilipofika, ajenda hiyo ilibaki kuwa kauli-mbiu.
Tukiweka kando mazingira hayo yaliyomwingiza madarakani Dokta Magufuli, miaka
miwili ya uongozi wake imekuwa na mafanikio kadhaa na kasoro kadhaa pia. Sura hii itajikita
kwenye mafanikio pekee.
Moja ya mafanikio makubwa kabisa ya serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dokta Magufuli
ni vita dhidi ya ufisadi. Japo ni mapema mno kuhitimisha kuwa ushindi kamili umeshapatikana
katika vita hiyo, angalau kuna dalili za kuridhisha.
Mafanikio makubwa zaidi kwenye vita dhidi ya ufisadi ni ya kisaikolojia zaidi kuliko
kisheria. Hapa inamaanisha kwamba japo kuna idadi ndogo tu ya watu waliokamatwa au
kuondolewa madarakani kwa tuhuma za ufisadi, kwa mara ya kwanza na baada ya miaka mingi
Watanzania wameanza kupatawa na uoga wa kujihusisha na vitendo vya uhalifu kama ufisadi,
rushwa, ujangili, biashara ya madawa ya kulevya, na kadhalika.
Ni rahisi kumzuwia mtu asifanye kitendo flani lakini ni ngumu mno kumjengea mtu imani
kuwa kitendo hicho anachopaswa kutofanya sio kizuri. Kwa zaidi ya miaka 30 tangu Nyerere
ang’atuke, idadi kubwa tu ya Watanzania ilikuwa ikiishi kwa imani kwamba vitendo vya uhalifu
ni njia muhimu ya kumudu maisha yao. Na kwa upande mwingine, wengi wao waliamini kuwa
vitu kama rushwa ni majaliwa (fate) yao. Kwamba visingeondoka hata zingefanyika jitihada
kiasi gani.
Licha ya ukweli kwamba dhamira ya kupambana na ufisadi kwa dhati ilikuwa ndogo katika
zama za Mwinyi, Mkapa, na zaidi wakati wa Kikwete, asilimia kubwa tu ya wananchi
‘walisherehesha’ matendo ya kihalifu kama vile ufisadi na biashara ya madawa ya kulevya.
Kuthibitisha hilo, mafisadi walipewa heshima ya kuitwa ‘mapedejee’ badala ya ‘wala rushwa’ au
‘wabadhirifu,’ kama sio ‘wahalifu.’ Na kwa upande wao, wauza madawa ya kulevya walipewa
heshima mtaani kwa kuitwa ‘wazungu wa unga.’
Watu waliojihusisha na uhalifu huo waliheshimiwa mno katika jamii, na wananchi wengi
waliona ufahari kuwa karibu na wahalifu hao. Ilisikitisha zaidi kuona wauza unga
wakinyenyekewa licha ya ukweli kwamba biashara haramu waliyokuwa wakifanya ilikuwa
ikipelekea vifo vya mamia ya vijana wanaotumia madawa ya kulevya. Kadhalika, mafisadi
walioitwa ‘mapedejee’ pia walichangia majanga kadhaa katika jamii kwa sababu fedha
walizokwapua zilipangwa kutumika kuwahudumia wananchi.
Kutochukuliwa hatua stahili kwa wahalifu hao kulipelekea dhana kwamba kuwa fisadi, au
muuza madawa ya kulevya, au jangili, ni ‘kuwa mjanja,’ kitu kilichowafanya vijana wengi
kupainia kuingia kwenye magenge ya kiharamia kama hayo badala ya kufikiria vitu vya
maendeleo kama kujiendeleza kimasomo au kutafuta ajira.
Kwa upande mwingine, mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi, biashara haramu ya madawa
ya kulevya yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kurejesha heshima ya kazi halali. Katika kilele cha
matendo hayo ya kihalifu, kuwa mwajiriwa wa umma au sekta binafsi au hata kujiajiri
kulionekana kama ‘uwendawazimu.’ Waajriwa walioonekana ‘wenye akili’ ni wale waliokuwa
kwenye ‘sehemu za ulaji,’ yaani maeneo ya kazi yaliyowapa fursa ya kufanya ufisadi.
Sambamba na kuahidi kupambana na rushwa na ufisadi na uhalifu mwingine, Dokta
Magufuli pia aliahidi kuanzisha mahakama maalum ya kushughulikia kesi za ufisadi. Mahakama
hiyo imeshaanzishwa japo mwenendo wake hadi wakati ninaandika kitabu hiki bado ni
‘wakusuasua.’ Hata hivyo, hatua tu ya kuanzisha mahakama hiyo inaashiria kuwa dhamira ya
Dokta Magufuli kupambana na rushwa haikuwa hadaa zilizozoeleka katika kampeni za uchaguzi
mkuu.
Changamoto kwa mahakama hiyo ‘changa’ ni nyingi, kubwa zaidi ikiwa uwezo duni wa
wanasheria wa serikali ambao wana ‘rekodi nzuri tu’ ya kupoteza kesi muhimu. Lakini jingine ni
urasimu uliopo katika mchakato wa kuwafikisha watuhumiwa katika mahakama hiyo.
Sambamba na hilo ni mapungufu yanayoikabili Taasisi ya Kupambana na Kuzuwia Rushwa
(TAKUKURU), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali.
Hata hivyo, changamoto hizo zipo ndani ya uwezo wa serikali ya Dokta Magufuli kuzitatua.
Kwa vile kushamiri kwa vitendo vya kihalifu kama vile ufisadi, rushwa, biashara ya
madawa ya kulevya na ujangili kulikuwa na mchango mkubwa kuvunja moyo ari ya kuchapa
kazi, jitihada za Dokta Magufuli kupambana na vitendo hivyo kumewezesha kuamsha ari ya
uchapakazi miongoni mwa Watanzania wengi. Kwa upande mmoja, jitihada za serikali ya
Awamu ya Tano kupambana na vitendo hivyo kumefanikiwa kwa kiwango cha kuridhisha
kuziba mianya ya ‘watu kuishi kiujanja ujanja’ au kwa kutegemea njia zisizo halali. Taratibu,
kipato halali – hata kama ni kidogo – kinaanza kuonekana kuwa ndio njia sahihi ya kumudu
maisha.
Kwa upande mwingine, kuondoa utegemezi kwa njia zisizo halali kumechangia kwa kiasi
cha kuridhisha kurejesha heshima ya kazi halali, kitu kilichopotea kwa takriban miaka 30. Na sio
kurejesha tu heshima ya kazi halali bali pia jitihada hizo zimefanikiwa kwa kiasi cha kuridhisha
kurudisha nidhamu ya watumishi wa umma kuanzia ngazi za juu hadi chini.
Katika siku za mwanzo za urais wake, Dokta Magufuli alifanya ziara kadhaa za kushtukiza
ambazo zilipelekea kuwakumbusha watumishi wa umma wajibu wao, sambamba na kuchelewa
‘kutumbuliwa,’ msamiati uliopata umaarufu baada ya ujio wa kiongozi huo, na uliomaanisha
kuondoa wazembe, mafisadi na watu wasiotekeleza wajibu wao ipasavyo.
Hata kabla hajaunda Baraza lake la Mawaziri, Dokta Magufuli alifanya ziara mbili kubwa za
kushtukiza ambapo Novemba 6, 2015 ikiwa ni siku moja tu baada ya kuapishwa alitembea kwa
miguu kutoka Ikulu hadi Wizara ya Fedha ambako alipita katika ofisi moja baada ya nyingine na
baadaye alifanya kikao na watendaji. Novemba 9 alifanya ziara nyingine ya kushtukiza katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alivunja Bodi ya Wakurugenzi, alimwondoa Kaimu
Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Hussein Kidanto na kuamuru mashine muhimu za vipimo za
CT-Scan na MRI kutengenezwa haraka huku akitoa sehemu ya mshahara wake kumlipia
mgonjwa mmoja aliyekuwa anahitaji kufanyiwa kipimo cha CT-Scan.
Japo kuna waliotafsiri kuwa ziara hizo za kushtukiza ni za kusaka umaarufu, kiongozi huyo
alipata watetezi wengi walieleza bayana kwamba hata kama jitihada zake ni za kusaka sifa,
hakuna tatizo kwani matokeo mazuri yalianza kuonekana bayana. Ziara hizo za kushtukiza
ambazo baadaye zilifanywa pia na baadhi ya mawaziri wake baada ya kuunda baraza lake la
mawaziri, zilipelekea ‘watumishi wa umma waliojisahau’ kutambua kuwa zama zimebadilika na
wanapaswa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi.
Pia juhudi hizo za Dokta Magufuli zilipelekea ‘vigogo’ wa taasisi mbalimbali kama vile
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuswekwa ndani,
kusimamishwa, kutenguliwa teuzi zao na wengine kufikishwa mahakamani kwa makossa
mbalimbali, yakiwemo uzembe, rushwa na ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
Miongoni mwa waliokumbwa na rungu la Dokta Magufuli ni pamoja na aliyekuwa
Kamishna Mkuu wa TRA Rished Bade, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Dickson Maimu, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa
TAKUKURU Edward Hosea, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Sylvester
Ambokile, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Viwango (TBS), Joseph Masikitiko, Mkurugenzi
Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Raslimali za Meli (RAHCO) Benhadard Tito, na wengineo kadhaa.
Hatua hizo za Dokta Magufuli sio tu zimesaidia kurudisha nidhamu kwa watumishi wa
umma na kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi bali pia zimeiacha historia mpya
katika uwajibishaji, hasa ikizingatiwa kwamba kwa muda mrefu hatua iliyozoeleka katika
uwajibishaji ni kumhamisha kiongozi kutoka sehemu moja na kwenda sehemu nyingine.
Mafanikio mengine ya Dokta Magufuli ni utekelezaji wa ahadi yake ya ‘elimu bure’ kuanzia
chekechea hadi kidato cha nne. Kimsingi, sera hii ni kama inairejesha Tanzania katika zama za
itikadi ya Ujamaa ambapo elimu ilikuwa ikitolewa bure hadi kiwango cha chuo kikuu. Mageuzi
ya kiuchumi yaliyoanza katikati ya miaka 1980s yalipelekea serikali kujiondoa katika utoaji wa
baadhi ya huduma kwa jamii, sambamba na kuanzishwa kwa sera ya wananchi kuchangia
gharama za utoaji huduma kwa jamii (cost sharing). Miongoni mwa maeneo yaliyoathirika ni
pamoja na sekta ya elimu ambapo wazazi walitakiwa kuchangia gharama mbalimbali za masomo
ya watoto wao. Kutokana na kuzidi kuongezeka kwa umasikini, baadhi ya wazazi hawakuweza
kumudu gharama za kuwapelekea watoto wao shule au za watoto hao kuendelea na masomo
katika ngazi mbalimbali.
Kwahiyo, sera hii ya elimu bure kuanzia ngazi ya chekechea hadi kidato cha nne inairejesha
Tanzania katika zama ambazo fursa ya elimu ilikuwa kwa kila mwanafunzi bila kujali uwezo wa
kiuchumi wa mzazi wake. Wakati ni muhimu kuhakikisha elimu inayotolewa ni ya kiwango
sahihi, fursa kubwa kwa wanafunzi wengi kujiunga au kuendelea na elimu ni suala lenye
umuhimu kwa taifa.
Pengine ingekuwa vema sera hiyo ingesubiri kuboreshwa kwa miundombinu katika sekta ya
elimu lakini kufanya hivyo kungewanyima nafasi mamilioni ya watoto wa Kitanzania kuanza au
kuendelea na masomo yao. Uamuzi wa kutekeleza sera hiyo huku miundombinu katika sekta ya
elimu ikiboresha ni bora zaidi.
Yafahamika kwamba kuna changamoto nyingi, kubwa zaidi zikiwa uhaba wa nyenzo kama
madarasa, madawati, vitabu vya kiada, na kadhalika, sambamba na upungufu wa walimu
unaoambatana na maslahi duni ya walimu hao. Hata hivyo, changamoto hizo hazipaswi kugubika
ukweli kwamba sera ya elimu bure kuanzia chekechea hadi kidato ya nne ni ukombozi mkubwa
kwa Watanzania. Nyingi ya changamoto zinazoikabili sera hiyo zimekuwepo kwa muda mrefu,
na kinachohitajika ni jitihada endelevu za kuboresha sekta ya elimu kwa ujumla sambamba na
kufanyia kazi changamoto zinazoikabili sera ya elimu bure.
Eneo jingine ambalo Dokta Magufuli amefanikiwa ni kubana matumizi ya serikali. Katika
hotuba yake ya kuzindua Bunge, kiongozi huyo aliweka hadharani takwimu zilizoomyesha jinsi
pato la taifa lilivyokuwa likiteketea katika matumizi mbalimbali ya serikali yanayoweza
kukwepeka. Moja ya maeneo yaliyokuwa yakiligharimu mno taifa ni safari za nje za watumishi
wa serikali. Dokta Magufuli alipiga marufuku safari hizo isipokuwa zitakazoidhinishwa kwa
kibali maalumu na Katibu Mkuu Kiongozi.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na serikali, uamuzi wa Dokta Magufuli kubana safari
za watumishi wa serikali kwenda nje ya nchi umepelekea serikali kutumia shilingi bilioni 25 tu
katika miaka mwili iliyopita kulinganisha na zaidi ya shilingi bilioni 216 katika mwaka wa
fedha 2014/2015.
Hayo ni mafanikio makubwa hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba Tanzania ni nchi
masikini ambayo asilimia kubwa ya bajeti yake inategemea misaada ya nchi na mashirika
wahisani. Kwahiyo kila shilingi inayookolewa kupitia hatua za kubana matumizi ina faida
kubwa.
Sambamba na kubana matumizi ya serikali, serikali ya Dokta Magufuli imekuwa na
mafanikio ya kuridhisha katika ukusanyaji mapato hasa kupitia kodi mbalimbali. Miongoni mwa
sababu zilizokuwa zikichangia umasikini wa Tanzania ni pamoja na mianya lukuki ya ukwepaji
kodi sambamba na misahama mingi ya kodi iliyotolewa kwa ufisadi.
Katika mwaka wake wa kwanza madarakani, Mamlaka ya Mapato (TRA) ilikusanya wastani
wa trillion 1.1 kila mwezi kuanzia mwezi Novemba 2015 hadi Septemba 2016, ongezeko la
asilimia 28.1 kutoka wastani wa shilingi bilioni 867 kwa mwezi katika kipindi cha mwezi
Novemba, 2014 hadi Septemba 2015.
Jitihada za ukusanyaji mapato ya serikali zinazoendana na serikali kupunguza matumizi
yake zimechangia kuifanya Tanzania chini ya utawala wa Dokta Magufuli kuwa miongoni mwa
nchi zinazofanya vema kiuchumi duniani. Kwa mujibu wa takwimu Julai mwaka huu, nchi hiyo
ilikuwa miongoni mwa nchi 5 za Afrika zilizokuwa zikiongoza kwa kasi ya ukuaji wa uchumi
(Ivory Coast 7.9%, Tanzania 7.1%, Senegal 6.6%, Djibouti 6.5%, na Ethiopia 6.5%).
Kwa mujibu wa bajeti ya serikali ya mwaka 2017/2018 iliyosomwa Julai mwaka huu,
mapato ya serikali kuanzia Julai 2016 hadi Aprili 2017 yalikuwa shilingi trilioni 20,710.5 sawa
na asilimia 70 ya lengo la mwaka la shilingi trilioni 29, 536.9.
Kadhalika, matumizi ya serikali katika kipindi hicho yalikuwa shilingi trilioni 20,036.5
ambapo vipaumbele vikuu vya bajeti hiyo vilikuwa katika ujenzi na ukarabati wa barabara kuu
za mikoa na Halmashauri; miradi ya ujenzi wa barabara ikiwa ni pamoja na ulipaji madeni ya
wakandarasi na wahandisi washauri; miradi ya uzalishaji umeme; uboreshaji wa njia za kupitisha
umeme na usambazaji wa umeme vijijini; mikopo ya elimu ya wanafunzi wa elimu ya juu;
malipo ya awali ya ujenzi wa reli kwa kiwango cha ‘standard gauge’ awamu ya kwanza katika
eneo la Dar es Salaam hadi Morogoro; ununuzi wa ndege mbili na malipo ya awali ya ununuzi
wa ndege nne; usambazaji wa maji mijini na vijijini; na uboreshaji huduma za afya katika ngazi
zote ikiwa ni pamoja na ununuzi wa madawa.
Mafanikio mengine ya Dokta Magufuli na serikali yake ni vita aliyoanzisha dhidi ya
watumishi hewa na wale waliokuwa na vyeti vya kugushi. Japo zoezi hili lililaumiwa kwamba
lilifanywa kiubaguzi kutokana na ukweli kwamba liliwalenga watumishi wa umma wa kadi za
chini tu, lilisaidia serikali kuokoa jumla ya takriban shilingi bilioni 370. Katika kila shilingi
inayookolewa na serikali, ni muhimu kutazama kwa kuzingatia ukweli kuwa Tanzania bado ni
miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani. Kwahiyo kila shilingi inayookolewa ina umuhimu
mkubwa kwa wananchi.
Eneo jingine ambalo kwa muda mrefu limekuwa likiikosesha Tanzania fedha nyingi ni
katika raslimali zake mbalimbali hususan madini na maliasili. Dokta Magufuli na serikali yake
amefanikiwa kwa kiasi cha kuridhisha kupigania maslahi ya taifa katika sekta za madini na
maliasili. Hadi wakati huu ambapo kitabu hiki kinaandika, tayari serikali ya Dokta Magufuli
imefanikiwa kufikia makubaliano na kampuni kubwa ya madini duniani, Barrick Gold ya
Canada, ambayo ni yenye hisa kubwa kwenye kampuni kubwa zaidi ya uwekezaji katika sekta
ya madini nchini Tanzania, Acacia Mining.
Makubaliano hayo yalifikiwa kutokana na uamuzi wa Dokta Magufuli kuzuwia makontena
kadhaa ya makinikia yaliyokuwa yakisafirishwa kwenda nje, na baadaye kuunda tume mbili za
kuchunguza jinsi Tanzania ilivyokuwa ikikoseshwa mapato katika uwekezaji kwenye sekta ya
madini.
Katika makubaliano hayo, Barrick ilikubali kuilipa Tanzania hisa asilimia 16 na mgao wa
asilimia 50 ya mapato ya mauzo ya dhahabu kutoka migodi inayomilikiwa na Acacia. Mbali ya
malipo hayo, kampuni hiyo pia ilikubali kutoa dola milioni 300 kama malipo ya nia njema
kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kutokana na biashara za kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya moja ya tume hizo mbili, Tanzania ilikuwa imepoteza takriban
shilingi trilioni 188 katika kipindi cha miaka 19 kati ya mwaka 1998 hadi mwaka huu kupitia
usafirishwaji nje wa makinikia ya dhahabu na shaba.
Pamoja na hatua hiyo, serikali ya Dokta Magufuli imefanikiwa kuzifanyia marekebisho
sheria zinazohusiana na raslimali za taifa ili ziwe na manufaa stahili kwa Tanzania. Kadhalika,
jitihada hizo za kulinufaisha taifa kupitia raslimali zake zimeelekezwa pia kwenye sekta ya
maliasili na utalii ambapo hatua kadhaa zinachukuliwa, ikiwa ni pamoja na ‘kutumbuliwa’ kwa
aliyekuwa Waziri wa Maliasi ya Utalii, Profesa Maghembe.
Vilevile, kwa mara ya kwanza, mgogoro wa muda mrefu na uliotawaliwa na tuhuma
mbalimbali za ufisadi katika eneo la Loliondo unaelekea kupatiwa ufumbuzi baada ya Waziri
mpya wa Maliasi na Utalii, Dokta Hamis Kigwangalla kuamuru kufutwa kwa vibali vyote vya
uwindaji nchi nzima.
Mafanikio mengine yaliyopatikana ndani ya miaka miwili ya utawala wa Dokta Magufuli ni
pamoja na ujenzi wa hosteli mpya za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam zenye uwezo
wa makazi kwa wanafunzi 3840. Ikumbukwe kuwa moja ya adha kubwa za elimu katika chuo
kikuu hicho kikubwa kuliko vyote chini Tanzania ni uahaba wa makazi kwa wanafunzi.
Kadhalika, Novemba 2016 Dokta Magufuli alitoa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa
nyumba mpya zitakazotumika kwa makazi ya askari wa gereza la Ukonga, Dar es Salaam.
Pengine kutokana na ukweli kwamba huko nyuma Dokta Magufuli alikuwa Waziri wa
Ujenzi kwa muda mrefu, tangu aingie madarakani amekuwa na kiu kubwa ya kukufua Shirika la
Ndege la Tanzania. Tayari serikali yake imeshanunua ndege 2 na kutoa malipo ya awali ya ndege
nyingine 4. Kwa pamoja, gharama ni shilingi 234.9 kiasi ambacho kw upande mwingine
kimezua mjadala miongoni mwa Watanzania huku baadhi yao wakihoji iwapo ndege hizo ni
kipaumbele kikubwa zaidi ya sekta kama elimu na afya ambazo ‘zinasuasua’ kutokana na uhaba
wa fedha.
Katika suala la ujenzi na miundombinu, Dokta Magufuli amefanikiwa kuanzisha miradi
mbalimbali, kwa mfano, ujenzi wa flyover Tazara na Ubungo, jijini Dar; Upanuzi wa Uwanja wa
Ndege wa Mwanza; Upanuzi wa kisasa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius
Nyerere jijini Dar; upanuzi wa Barabara ya Morocco jijini Dar; kuzindua ujenzi wa reli yenye
kiwango cha ‘standard gauge’; barabara ya kuunganisha wilaya za Kibondo mkoani Kigoma na
Kauliua mkoani Tabora; Ujenzi wa barabara ya Mtwara -Tandahimba; ukarabati wa reli kati ya
Tanga na Moshi. Ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi bandari ya
Tanga.
Mradi mwingine mkubwa ni ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa huko Chato – eneo
analotoka Dokta Magufuli – na kama ilivyotarajiwa, mradi huo umezua ‘maneno’ kadhaa huku
kiongozi huyo akituhumiwa kulipendelea eneo analotoka, na baadhi ya wanasiasa wakidai kuwa
fedha za mradi huo hazikuidhinishwa na bajeti. Suala hili litajadiliwa kwa kirefu katika sura
ijayo.
Kwa kubana matumizi na kuongeza mapato ya serikali kwa kukusanya kodi sambamba na
kuwabana wakwepa kodi, serikali ya Dokta Magufuli imeweza kuboresha sekta mbalimbali za
huduma kwa jamii kama vile afya na maji hususan katika maeneo ya vijijini. Hata hivyo bado
kuna changamoto kubwa katika upatikanajai wa dawa mahospitalini sambamba na miundombinu
duni katika hospitali nyingi, huku uhaba wa madaktari na wauguzi ukiendelea kuathiri maeneo
mengi.
Kwa upande wa maji, huduma hiyo imeendelea kutokuwa ya uhakika sana huku taarifa
mbalimbali kwenye vyombo vya habari vikionyesha jinsi wananchi wanavyotaabika kupata maji.
Hata hivyo, serikali ya Dokta Magufuli imeendelea kufanya jitihada za kuanzisha au kuboresha
miradi kadhaa ya maji.
Kuna msemo wa Kiswahili usemao “Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni” ambao kwa
kiasi kikubwa unaweza kufaa kama wito kwa Watanzania wanapotathmini utendaji kazi wa
Dokta Magufuli, miaka miwili sasa tangu aingie madarakani Novemba 5, 2016. Kwamba,
pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo, angalau kuna jitihada za kuridhisha zilizofanyika,
zinazofanyika na zinazotarajiwa kufanyika kumkwamua Mtanzania. Kwa hakika safari hiyo
bado ni ndefu na ngumu lakini angalau imeanza.
Kadhalika, ni rahisi ‘kumhukumu’ Dokta Magufuli iwapo ‘mtoa hukumu’ atapuuzia hali
ilivyokuwa kabla ya kiongozi huyo kuingia madarakani, na hali aliyoikuta alipoingia
madarakani. Na yawezekana kwamba miongoni mwa sababu zinazochelewesha kasi ya
mafanikio ya jitihada za Dokta Magufuli na serikali yake ni masalio ya mfumo wa kifisadi
uliodumu kwa takriban miaka 30.
Katika kuhitimisha sura hii, ni muhimu kubainisha kuwa kuna idadi kubwa ya Watanzania
wenye matumaini kuwa jitihada za Dokta Magufuli zinaweza kuiondoa Tanzania kutoka katika
kundi la nchi masikini kabisa duniani, na tegemezi wa misaada, na kupiga hatua kimaendeleo
pengine hadi kufikia kiwango cha kuwa miongoni mwa nchi wahisani. Ukweli ulio bayana ni
kwamba nchi hiyo imejaaliwa utajiri mkubwa wa raslimali ambao ukisimamiwa na kutumika
ipasavyo unaweza kusaidia mno maendeleo ya taifa.
Sura Ya Sita
Magufuli 2.0
Kwa kuazima lugha ya kompyuta, ambapo maendeleo ya mtandao huangaliwa katika vizazi
– Web 1.0 (kizazi cha kwanza kati ya mwaka 1990 hadi 2000 ambapo mtandao ulitawaliwa na
maandishi, na mawasiliano yakiwa ya upande mmoja, kutoka kwa mwandishi kwenda kwa
msomaji), Web 2.0 (kizazi cha pili kati ya mwaka 2000 hadi 2010 ambapo mtandao ulitawaliwa
na social interaction kati ya mwandishi na msomaji) na sasa Web 3.0 kizazi cha tatu kati ya
mwaka 2010 hadi 2020 ambapo mtandao umekuwa ukitumia akili kama mwanadamu kwa mfano
kutekeleza majukumu wenyewe baada ya kujifunza kutoka kwa mwanadamu) – tathmini ya
miaka miwili ya utawala wa Dokta Magufuli inaweza pia kuangaliwa kwa namna hiyo.
Haihitaji uelewa mkubwa wa siasa za Tanzania kutambua kuwa kuna tofauti za msingi kati
ya Dokta Magufuli ‘wa mwanzo’ na ‘huyu aliyetimiza miaka miwili madarakani mwezi uliopita,
Novemba 2017. Lakini kutambua tofauti hizo ni kitu kimoja, ilhali kufahamu sababu
zilizopelekea kubadilika huko ni kitu kingine kabisa. Hadi wakati ninaandika kitabu hiki
hakujapatikana maelezo ya kujitosheleza kuhusu kitu gani hasa kimepelekea mabadiliko ya
kiongozi huyo.
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kwa kiasi kikubwa mwanasiasa
huyo alionekana kama mwanasiasa asiye na makuu, wa kawaida, anayesukumwa zaidi na hali
halisi na uchungu kwa nchi badala ya kuweka mbele itikadi za kisiasa. Hotuba zake mbalimbali
katika kampeni zilionyesha uelewa wake mkubwa kuhusu matatizo yanayoikabili Tanzania na
jinsi ya kuyatatua.
Japo kama mgombea urais alilazimika kuwanadi wagombea ubunge na udiwani kutoka
CCM lakini haikuwa vigumu kubaini kuwa kipaumbele chake kikubwa kilikuwa kuhusu
Tanzania zaidi kuliko chama chake. Na hilo lilileta matumaini makubwa baada ya ushindi wake
katika nafasi ya urais kwa sababu kwa muda mrefu itikadi za siasa zimekuwa zikiwekwa mbele
ya maslahi ya taifa.
Moja ya vitu vilivyoleta matumaini makubwa miongoni mwa Watanzania kuhusu urais wa
Magufuli ni hotuba yake aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa bunge la Jamhuri ya Muungano.
Katika hotuba hiyo, Dokta Magufuli alionyesha kuwa mtu anayezielewa vema shida za
Watanzania hususan janga la rushwa na ufisadi, na akaapa kushughulikia kwa nguvu zake zote.
Na alipoomba Watanzania wamwombee katika vita hiyo ngumu, yayumkinika kuhisi kuwa hata
miongoni mwa wale ambao hawakumpigia kura waliitikia wito huo wa kumfanyia maombi.
Baada ya hapo zikaja ziara ya kushtukiza - kama ilivyoelezwa katika sura iliyotangulia -na
taratibu Watanzania wengi wakaanza kuingiwa na matumaini mapya ya “mrithi halisi wa
Nyerere/Sokoine.”
Shangwe kuhusu Dokta Magufuli hazikuwa Tanzania pekee. Awali zilianza kusambaa
katika nchi jirani hususan Kenya ambapo baadhi ya wananchi walieleza waziwazi kuwa
walitamani wangeweza kumwazima kiongozi huyo asafishe nchi yao dhidi ya rushwa na ufisadi.
Kana kwamba hiyo haitoshi, umaarufu wa Dokta Magufuli ukasambaa takriban kila kona ya
dunia, na kilele kilifikiwa pale ilipoibuka alama #WhatWouldMagufuli Do iliyotamba kila kona
ya dunia. Kiongozi huyo aliwagiwa sifa lukuki kutokana na uchapakazi wake sambamba na
chuki dhidi ya rushwa na ufisadi.
Kwa kufurahishwa na kuridhishwa na utendaji wake, mwandishi wa kitabu hiki aliamua
kuandika kitabu cha tathmini ya urais wa Magufuli, siku 55 tu baada ya kiongozi huyo
kuapishwa kuwa Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Watu kadhaa walikosoa
uamuzi huo wa kuchapisha kitabu chenye tathmini ya kiongozi aliyeingia madarakani muda
mfupi tu uliopita. Wengi waliona kwamba haikuwa sahihi kwa mwandishi kufanya tathmini hiyo
mapema kiasi hicho. Hata hivyo, kwa hali ilivyokuwa wakati huo, ilikuwa rahisi kwa mwandishi
kudhani kwamba waliomkosoa kuhusu suala hilo walikuwa kama wenye chuki binafsi dhidi ya
‘mkombozi’ Magufuli.
Dalili ya kwanza kwamba huenda kuna walakini katika utawala wa Magufuli ni pale
alipotangaza baraza lake la mawaziri ambalo ilichukua wiki kadhaa kulisubiri. Lilipotangazwa,
sio tu lilikuwa kubwa kuliko ahadi yake kuwa angeunda serikali ndogo tu ili kupunguza gharama
za uendeshaji wa serikali, bali pia lilijumuisha baadhi ya sura ‘zenye utata.’ Miongoni mwa sura
hizo ni Profesa Muhongo, ambaye awali alilazimika kujiuzulu katika serikali ya Awamu ya Nne
kutokana na kuhusishwa na skandali ya Tegeta Escrow.
Kadhalika, kuna waliouona uteuzi wa makada kama Nape Nnauye na Mwigulu Nchemba
ulikuwa ni wa kisiasa zaidi, huku sura kama George Simbachawene, William Lukuvi na Profesa
Jumanne Maghembe zikijenga ishara kuwa huenda mambo hayajabadilika kama ilivyotarajiwa.
Kisha kukafanyika uteuzi wa mabalozi wa kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali
ambao ulionekana bayana kama kutumia nafasi hizo nyeti kuwaondoa watu flani kwenye
nyadhifa zao huko CCM. Baadhi ya watu wakaanza kujiuliza, “hivi hatujayashuhudia haya huko
nyuma?” Hata hivyo, hofu hiyo ilikuwa miongoni mwa watu wachache tu huku wengi
wakiendelea kuwa na matumaini kwa Dokta Magufuli.
Dalili ya kwanza kabisa kuwa pamoja na mazuri yake yaliyowavutia Watanzania wengi na
kona mbalimbali duniani, Dokta Magufuli ana mapungufu yake ni pale serikali yake kupitia
aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ilipozuwia haki ya
mamilioni ya Watanzania kusikiliza matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge. Awali
lawama kubwa zilielekezwa kwa Nape ambaye wadhifa wake ulimhusisha moja kwa moja na
zuwio hilo lililolaaniwa vikali na Watanzania wengi. Hata hivyo, baadaye Rais Magufuli alieleza
bayana kuwa uamuzi wa kuzuwia matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge ulikuwa
wake binafsi, na waziri alitelekeza tu maagizo ya Rais.
Baadaye likaja zuwio dhidi ya mikutano na maandamano ya vyama ya siasa. Awali baadhi
ya wananchi waliona kuna mantiki japo kidogo kwenye zuwio hilo, kutokana na hoja kwamba
“ah huu ni muda wa kuchapa kazi. Hayo maandamano na mikutano ni ya nini muda huu?”
Kujipa matumaini huko kulichangiwa pia na ukweli kwamba wananchi wengi wanaziona
shughuli za kisiasa kama mikutano na maandamano zikiwaathiri zaidi wao kuliko wanasiasa.
Kwahiyo, angalau kwa wakati huo, zuio hilo lilionekana kama lenye nia nzuri.
Kilichofanya zuwio hilo kuonekana kuwa mkakati wa dhati wa serikali ya Dokta Magufuli
dhidi ya vyama vya upinzani ni pale chama tawala kiliporuhusiswa kufanya maandamano na
mikutano bila kubughudhiwa huku vyama vya upinzani vikizuiliwa. Kwa maana hiyo, zuwio
hilo ni kama lililenga kuinufaisha CCM na wakati huohuo kuvikandamiza vyama vya upinzani.
Tukio jingine ambalo kwa hakika lilijenga picha isiyopendeza kuhusu Dokta Magufuli ni
pale Tanzania ilipokumbwa na janga la tetemeko la ardhi mkoani Kagera Septemba 2016.
Mshtuko wa tetemeko hilo ulisikika hadi Uganda, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Watu wa Kongo na Kenya. Kwa mujibu wa maelezo ya serikali, jumla ya watu 17 walipoteza
uhai huku wengine 240 wakijeruhiwa. Kadhalika, nyumba 2063 zilibomoka kutokana na
tetemeko hilo la ardhi.
Kwa kuwa pamoja na majukumu mengine aliyonayo Rais, yeye pia ni ‘mfariji mkuu, Dokta
Magufuli alitegemewa kwenda kuwafariji wahanga wa tetemeko hilo, na hasa ikizingatiwa kuwa
yeye pia anatoka Kanda ya Ziwa. Siku ya maombolezo ya kitaifa, Rais hakwenda na badala yake
aliwakilishwa na Waziri Mkuu Majaliwa.
Lakini wakati Watanzania wakiungana na wenzao wa Kagera walioathiriwa na janga hilo la
tetemeko la ardhi, Rais Magufuli alitoa kauli isiyopendeza kuhusu janga hilo akidai kwamba
“serikali haikuleta tetemeko hilo la ardhi.” Hata hivyo, hakuna rekodi yoyote inayoonyesha mtu
yeyote aliyedai kuwa serikali ndio iliyosababisha tetemeko hilo.
Baada ya miezi minne hivi, hatimaye Dokta Magufuli alifanya ziara mkoani Kagera na
kujionea mwenyewe uharibifu mkubwa uliosababishwa na tetemeko la ardhi. Hata hivyo, wakati
akiongea na wananchi ikiwa ni pamoja na wahanga wa tetemeko hilo, Dokta Magufuli alidai
kwamba “hakuna mahali popote duniani ambapo tetemeko likitokea serikali inaanza kujenga
nyumba za wananchi.” Haikuwa mwafaka kwa Rais kutoa kauli kama hiyo kwa sababu kwa
mujibu na mila za Kitanzania, lugha inayopaswa kutumika wakati wa majonzi ni ya kuliwazana.
Kadhalika, Rais Magufuli hakusema ukweli alipodai kwamba hakuna mahali popote duniani
ambapo tetemeko likitokea serikali inaanza kujenga nyumba za wananchi. Ukweli ni kwamba
hata katika nchi zilizoendelea kama Marekani, Italia na Japan ambazo asilimia kuwa ya wakazi
wake wanajimudu kiuchumi, serikali huwasaidia wananchi wake bila kujali uwezo wao
kiuchumi. Ndio Tanzania ni masikini na haina uwezo wa kumjengea nyumba kila mtu
aliyeathiriwa na janga hilo la tetemeko la ardhi lakini angalau lugha iliyotumika kufikisha
ujumbe kwa wananchi ilipaswa iwe ya kiungwana.
Baadaye zilisikika taarifa kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania kuhusu tishio la upungufu
wa chakula na dalili za uwepo wa baa la njaa. Lakini waliotarajia kwamba huenda wangepata
maneno ya faraja kutoka kwa Rais wao, Dokta Magufuli aliweka bayana msimamo wa serikali
yake kwamba haitotoa chakula kwa vile “haina shamba.”
Ni kweli inapendeza kuwa na kiongozi ‘asiyeuma maneno,’ na anayeeleza vitu kama
vilivyo. Ni kweli pia kwamba kwa muda mrefu, Tanzania ilikuwa ikiongozwa na ‘kauli tamu’ za
baadhi ya viongozi ambazo zilipendeza masikioni mwa wananchi lakini nyingi ziliishia kuwa
porojo tu. Kwahiyo, tabia ya Dokta Magufuli kusema ukweli kama ulivyo ni. Hata hivyo, kuna
tofauti kati ya kusema ukweli, na kusema ukweli katika lugha isiyokwaza watu. Ilikuwa sahihi
kwa Dokta Magufuli kueleza kwamba serikali yake haiwezi kugawa chakula kwa wananchi
wanaokabiliwa na uhaba wa njaa lakini kiungwana, haikuwa mwafaka kusema kuwa “serikali
haiwezi kuwasaidia kwa sababu haina shamba.”
Januari mwaka huu akiwa Magu, Dokta Magufuli akiwa kwenye ziara yake ya kikazi,
wananchi walisimamisha msafara wake na baadhi yao kumlalamikia kuwa wana tatizo la njaa.
Wananchi hao wanasikika wakipaza sauti za 'njaa…njaa'' wakati akisalimia na kutoa shukrani
zake kwa kumchagua kuwa Rais. Hata hivyo, baada za kelele za njaa kuzidi, Dokta Magufuli
alisikika akisema ''njaa, unataka mimi nikakupikie chakula ule,'' kauli ambayo japo iliibua
vicheko ingeweza kujenga taswira kwamba kiongozi huyo hajali matatizo ya wananchi
anaowaongoza.
Kama ilivyoandikwa awali, licha ya kuwa Amiri Jeshi Mkuu, Rais pia ni ‘mfariji mkuu’
kwa taifa. Kila linapotokea janga kubwa, inatarajiwa kuwa Rais atakuwa mstari wa mbele
kulifariji taifa sambamba na kuonyesha uongozi katika nyakati ngumu. Ni katika mazingira
hayo, uamuzi wa Dokta Magufuli kutokwenda ‘hapo kwa hapo’ Kagera kushiriki maombolezo
ya kitaifa ya wananchi waliouawa na tetemeko la ardhi ulizua minong’ono ya hapa na pale.
Aprili mwaka huu, askari polisi wanane waliuawa kwa mkupuo huko Kibiti mkoani Pwani.
Tukio hilo liligusa hisia za Watanzania wengi lakini katika mazingira ya kushangaza, Dokta
Magufuli hakushiriki katika kuaga miili ya askari hao jijini Dar na badala yake akaenda kwenye
hafla ya uzinduzi wa mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Amiri Jeshi
Mkuu ambaye pia ni mfariji mkuu kukosekana katika shughuli hiyo hakukujenga picha nzuri.
Mei mwaka huu, Tanzania ilikumbwa na msiba mkubwa kufuatia ajali iliyogharimu maisha
ya wanafunzi 33 wa Shule ya Lucky Vincent ya mkoani Arusha, walimu wawili na dereva
mmoja. Taarifa za ajali hiyo zilipata uzito mkubwa hadi kutangazwa na vyombo vya habari vya
kimataifa.
Hata hivyo, kwa mara nyingine tena, Dokta Magufuli hakuhudhuria maombolezo ya kitaifa
yaliyofanyika jijini Arusha na badala yake aliwakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan. Na kama ilivyokuwa katika tukio la Kagera na lile la polisi wanane, hakukutolewa
maelezo yoyote kwanini Rais hakuhudhuria katika maombolezo hayo.
Japo kuna hoja kwamba uwepo wa Rais katika matukio kama hayo hauwezi kurudisha uhai
wa waliopoteza maisha yao, mila na desturi zetu zinasisitiza mno umuhimu wa kuhudhuria
misiba, kitu ambacho husaidia kuwafariji wafiwa.
Septemba mwaka jana, zilipatikana taarifa za kupotea kwa kada mmoja maarufu wa
Chadema, Ben Saanane. Kada huyo alitokea kuivalia njuga shahada ya uzamifu ya Dokta
Magufuli, akidai kuwa ina walakini. Kijana huyo aliyekuwa na wafuasi wengi kwenye mitandao
ya kijamii pia aliunganisha ukosoaji wake huo na jitihada za Dokta Magufuli dhidi ya watumishi
wa umma waliogushi vyeti. Kwahiyo, Saanane alimtaka Rais athibitishe kwanza uhalali wa
shahada yake kabla ya kuwabana watumishi wa umma.
Hata hivyo, baadhi ya watu akiwemo mwandishi wa kitabu hiki walimsihi kada huyo kuwa
makini katika suala hilo kwani kulishaanza kuonekana dalili za Dokta Magufuli kutopenda
kukosolewa. Kwa bahati mbaya au makusudi, alipuuza ushauri huo.
Hadi wakati kitabu hiki kinaandikwa, haijulikani nini kimemsibu kijana huyo. Juhudi kubwa
zinazofanywa na familia yake, na Chadema kwa kiasi fulani, hazijazaa matunda. Jeshi la polisi
sio tu limekuwa halina msaada mkubwa katika kufuatilia ‘kupotea’ kwa kada huyo, lakini pia
limekuwa na wakati mgumu kupata ushirikiano kutoka Chadema hasa kutokana na mahusiano
mabaya kati ya jeshi hilo na chama hicho. Ugumu zaidi unatokana na ukweli kwamba jeshi hilo
linatuhumiwa na baadhi ya wafuasi wa chama hicho kuwa linahusika na kupotea kwa Saanane.
Hata hivyo, Chadema nao hawawezi kukwepa lawama katika suala hilo kwa jinsi
walivyozembea kulishughulikia. Kumekuwa na kauli zinazokinzana kutoka kwa baadhi ya
viongozi wa chama hicho kama ile ya mwenyekiti wa taifa, Freeman Mbowe kuwa Saanane
alitekwa huku Mbunge wa chama hicho Saeid Kubenea akidai kuwa kada huyo alikuwa
akionekana vijiweni. Haifahamiki kwanini chama hicho hakikuona umuhimu wa kuwabana
viongozi hao kufafanua kauli zao.
Kadhalika, taarifa alizonazo mwandishi wa kitabu hiki ni kwamba kiongozi mmoja wa ngazi
za juu wa chama hicho alifahamishwa na vyanzo vya kuaminika kuhusu kilichomsibu kada huyo
lakini hakuchukua hatua zozote.
Lakini kama kuna tukio lililompotezea heshima kubwa Dokta Magufuli ni lile la Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuvamia kituo cha redio na runinga cha Clouds akiwa
na askari wenye silaha, lakini siku chache baadaye, huku baadhi ya watu wakitarajia angemtimua
Makonda, Dokta Magufuli sio tu alimtetea Makonda na kumwita mchapakazi, pia aliwakebehi
wananchi waliotarajia angechukua hatua akieleza yeye ndo Rais, na hapangiwi kazi.
Tukio hilo liliwaacha midomo wazi Watanzania wengi kwani ilikuwa haiingii akilini kuona
Mkuu wa Mkoa huyo amevamia kituo cha habari, kitendo ambacho ni kosa la jinai, halafu Rais
anamtetea na kumsifu kuwa ni mchapakazi.
Uswahiba wa Dokta Magufuli na Makonda umechangia mno ugumu wa kuchunguza tuhuma
kuwa Mkuu huyo wa mkoa amegushi jina analotumia pamoja na cheti cha kuhitimu kidato cha
nne.
Katika hatua nyingine, Oktoba mwaka huu, Dokta Magufuli “alifunga rasmi mjadala kuhusu
vyeti na elimu ya Makonda” baada ya kusema kuwa anaridhishwa na utendaji wake na kwamba
kwake anamuona ni msomi mzuri.
Kauli hiyo ya Rais ilitafsiriwa kama jibu kwa tetesi kuwa Makonda alifeli kidato cha nne na
hivyo anatumia jina na vyeti vya mtu mwingine. Dokta Magufuli amekuwa akishauriwa angalau
kufanya uchunguzi kuhusu suala hilo, lakini mara zote amekuwa upande wa Mkuu wa Mkoa
huyo.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania
(ALAT), Dokta Magufuli aliwakosoa wanaomnyooshea kidole Makonda na kusema kwake yeye
ni msomi. “Wanasema hajasoma, mimi hata kama hajui A ila anakamata madawa ya kulevya,
kwangu ni msomi mzuri,” alisema Dokta Magufuli.
Kama kawaida yake, mkuu huyo wa nchi alimmwagia pongezi Makonda “kwa namna
anavyofanya kazi na kutatua changamoto za wananchi,” na kuwataka hatua wakuu wengine wa
mikoa kuja kujifunza kwake.
Hata hivyo, uswahiba kati ya Dokta Magufuli na Makonda umeendelea kuwakera watu
wengi, hasa ikizingatiwa kuwa Mkuu huyo wa Mkoa amekuwa akiutumia ipasavyo upendeleo
anaopewa na Rais, na hiyo kumpa jeuri ya kufanya dharau za waziwazi kama ile ya kupigiwa
saluti na vingozi wa ngazi za juu wa jeshi la polisi huku amevaa kofia aina ya ‘kapelo.’ Hiyo ni
dharau ya hali ya juu kwa vyombo vya dola.
Kwa upande mwingine, miaka miwili ya utawala wa Dokta Magufuli ilitawaliwa na wakati
mgumu kwa vyombo vya habari. Pengine dalili kwamba kiongozi huyu si rafiki wa vyombo vya
habari ni ukweli kwamba katika muda wote wa kampeni zake za urais mwaka 2015 hakufanya
mahojiano na chombo chochote cha habari.
Na hata baada ya kushinda kiti cha urais, Dokta Magufuli amefanya mkutano na waandishi
wa habari mara moja tu. Hata hivyo, kwa wananchi wengi, la muhimu sio kiongozi kusikika
mara kwa mara bali jinsi gani anawatumikia.
Ndani ya miaka miwili ya utawala wake, serikali yake imeshayafungia magazeti matano.
Agosti mwaka jana, serikali ililifungia gazeti la Mseto kwa miezi 36, kisha Juni mwaka huu
ikalifungia gazeti la Mawio kwa miaka miwili. Serikali ya Dokta Magufuli iliweka rekodi ya
aina yake kwa kufafungia magazeti matatu ndani ya kipindi cha takriban mwezi mmoja, ambapo
Septemba mwaka huu iliyafungia ya Raia Mwema (siku 90) na Mwanahalisi (miaka mwili) kisha
Oktoba mwaka huu ikalifungia gazeti la Tanzania Daima kwa siku 90.
Lakini hata kabla ya kuchukua hatua hizo zinazokandamiza uhuru wa vyombo vya habari
sambamba na kuwanyima wananchi haki ya kuhaharishwa, Dokta Magufuli alishavitahadharisha
vyombo vya habari kwamba uhuru walionao una mipaka.
''Serikali ya kutumbua majipu haiwezi kuacha kutumbua magazeti yanayofanya mambo ya
uchochezi hatuwezi kuiacha Tanzania ikawa dampo la eneo la kuweka maneno ya uchochezi
chini ya utawala wangu," alisema Dokta Magufuli.
"Hilo halitakuwepo kuna magazeti mawili tu kila ukisoma wao ni kuchochea tu
ikizungumzwa habari hii wao wanageuza hii nasema na nataka wanisikie siku zao zimeshafika
kama wanasikia wasikie wasiposikia wasisikie lakini magazeti mengine na vyombo vyote
vingine vinatoa uchambuzi mzuri sana,” alitahadharisha kiongozi huyo katika kauli iliyotafsiriwa
kama yenye lengo la kuvitisha vyombo vya habari ili viandike habari zinazompendeza Rais
pekee.
Haya yametokea wakati Tanzania bado ipo kwenye mshtuko kufuatia jaribio la kumuua
mwanasiasa ambaye amekuwa mpinzani mkubwa wa Dokta Magufuli, mbunge wa Chadema
Tundu Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria cha TLS. Chuki inayopandikizwa
dhidi ya wapinzani imepelekea asilimia kubwa ya viongozi wa serikali na chama tawala CCM
kuogopa kwenda kumjulia hali Lissu huko Nairobi alikolazwa.
Kama ilivyokuwa kwa kada wa Chadema Ben Saanane ambaye ‘alipotea’ baada ya
kumwandama Dokta Magufuli kuhusu shahada yake ya uzamifu, Lissu nae alikumbana na
jaribio hilo dhidi ya maisha yake baada ya kujitokeza kuwa mwanasiasa mpinzani mkuu wa
Dokta Magufuli. Japo upinzani wao dhidi ya mkuu huyo wa nchi haumaanishi kuwa anahusika
dhidi ya yaliyowakuta, lakini haijengi picha nzuri.
Pengine kipimo halisi cha mambo kwenda kinyume na matarajio ya baadhi Ya Watanzania
kuhusu Dokta Magufuli ni kwamba katika miaka mwili ya utawala wake, zaidi ya viongozi na
wanachama 400 wa Chadema wamekamatwa na polisi. Japo tangu kuruhusiwa kwa mfumo wa
siasa za vyama vingi mwaka 1992, vyama vya upinzani vimekuwa vikiendesha shughuli zake
katika mazingira magumu, chini ya utawala wa Dokta Magufuli hali imekuwa ngumu zaidi.
Imefika mahala, wakuu wa wilaya wanakamata viongozi wa Chadema kila wanapojisikia.
Na pengine kibaya zaidi ni ukweli kwamba taratibu jamii inaanza kuzowea kuona viongozi na
wanachama wa upinzani – hususan Chadema – wakidhalilishwa na kukamatwa kiholela.
Jambo jingine la kusikitisha kuhusu utawala wa Magufuli ni utitiri wa sheria kandamizi
dhidi ya uhuru wa habari. Licha ya sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 ambayo ni
kazi ya Rais mstaafu Kikwete, kuna sheria mpya ya Huduma za Habari na kinachoitwa ‘Kanuni
za Maudhui ya Mitandao ya Kijamii,’ ambazo kwa kiasi kikubwa zinafanya uhuru wa habari na
mawasiliano kuwa suala la hisani ya serikali badala ya haki ya kikatiba.
Kwa kufuatilia jitihada zilizopo dhidi ya uhuru wa habari, na kwa kuzingatia ukweli
kwamba vyombo vya habari ‘vya asili’ kwa maana ya magazeti, redio na runinga zimedhitiwa
vyema na serikali, eneo ambalo linaweza kuwa mlengwa wa jitihada mpya na zaidi ni mitandao
ya kijamii.
Ikumbukwe kuwa Septemba mwaka jana, Dokta Magufuli aliweka wazi ‘hasira zake’ dhidi
ya mitandao ya kijamii aliposema kuwa anatamani malaika washuke na kuifunga mitandao hiyo
kwa mwaka mmoja. Uwepo wa mkataba kati ya serikali na kampuni moja ya Korea ya Kusini
inayoshughulika na teknolojia ya ‘kudhibiti mtandao’ unaweza kuashiria kuwa siku za uhuru wa
mitandao ya kijamii zinahesabika.
Kwa upande mwingine, huku Chadema ikishuhudia viongozi na wanachama wake
wakinyanyaswa mfululizo, kuna dalili kuwa mgogoro unaoendelea ndani ya chama cha CUF una
mkono wa serikali hasa kwa kuzingatia mwenendo wa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
(taasisi ya serikali) kuibeba waziwazi kambi ya mwanachama aliyejiuzulu kwa utashi wake
Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye alijiuzulu kwa hiari yake kabla ya kurudi chamani na kudai
yeye bado mwenyekiti wa taifa wa chama hicho cha upinzani.
Wiki chache kabla ya kuchapishwa kitabu hiki, Dokta Magufuli ‘alitoa siri’ kwamba kuna
siku aliombwa ushauri na Spika wa Bunge la Jamhuri, Job Ndugai kuhusu uteuzi wa wajumbe
wa kamati moja ya bunge. Hiyo ina maana kuwa bunge limewekwa mfukoni na mhimili wa
serikali.
Kadhalika, kauli za Jaji Mkuu ‘mpya’ Profesa Ibrahim Hamis Juma baada ya jaribio la
mauaji dhidi ya Tundu Lissu yanajenga taswira ya mhimili wa mahakama nao kuwekwa mfukoni
na mhimili wa serikali.
Siku 15 baada ya Lissu kupigwa risasi na watu wasiojulikana, Jaji Mkuu aliitisha mkutano
na waandishi wa habari na kueleza kuwa mahakama haijalifumbia macho tukio hilo kwa kuwa ni
jambo ambalo litafikishwa mahakamani. Haikueleweka alikuwa na uhakika gani kama suala hilo
litafikishwa mahakamani ilhali hakuna juhudi zozote kwa upande wa vyombo vya dola kuwatia
nguvuni waliohusika na tukio hilo.
Jaji Juma alidai kwamba kwa mujibu wa kanuni jambo litakalofikishwa mahakamani kwa
ajili ya kutolewa ushahidi halipaswi kuongelewa au kutolewa maoni na kwamba tukio hilo la
Lissu litafikishwa mahakamani baada ya taratibu zote kukamilika.
Profesa huyo pia aliwataka wananchi wenye ushahidi unaohusiana na tukio hilo kuwasilisha
katika mamlaka husika badala ya kusambaza mitandaoni. Kwa tafsiri nyepesi, kauli za kiongozi
huyo wa mhimili wa mahakama zilikuwa kama zinazolenga kuwaziba mdomo wananchi
kuongelea suala hilo.
Lakini pengine cha kusikitisha zaidi ni ukweli kwamba hadi wakati kitabu hiki kinaandaliwa
kuchapishwa, Jaji Juma alikuwa hajaenda kumjulia hali Lissu, ambaye katika wadhifa wake
kama Rais wa TLS, ana mahusiano ya karibu kikazi na Jaji Mkuu.
Jambo jingine ambalo limetia doa miaka miwili ya utawala wa Dokta Magufuli ni uchaguzi
mdogo wa madiwani uliofanyika mwezi Novemba mwaka huu katika kata 43. Uchaguzi huo
utaingia katika vitabu vya historia kama uliotawaliwa na unyanyasaji, uonevu, vitisho na kila
aina ya uhuni dhidi ya vyama vya upinzani hususan Chadema.
Kana kwamba zuwio dhidi ya vyama vya upinzani kutofanya shughuli za kisiasa halitoshi,
kampeni za Chadema ziliandamwa na uonevu wa waziwazi uliofanywa na jeshi la polisi dhidi ya
viongozi, wagombea, mawakala na wanachama wa chama hicho.
Hadi wakati kitabu hiki kinaandaliwa kuchapishwa, kuna lundo la viongozi na wanachama
wa Chadema wenye kesi mbalimbali, nyingi kati ya kesi hizo zikiwa na dalili ya uhasama wa
kisiasa unaozidi kukua ndani ya CCM ya Dokta Magufuli dhidi ya vyama vya upinzani, hususan
Chadema.
Wakati wa kampeni zake za kuwania urais, na hata katika hotuba zake baada ya kushinda
urais, Dokta Magufuli amekuwa akimtaja sana Mungu, na kuwataka Watanzania kuendelea
kumwombea. Hilo ni jambo jema kwa sababu kiongozi mcha Mungu anakuwa katika nafasi
nzuri ya kuwatumikia anaowaongoza.
Hata hivyo, ‘ucha-Mungu’ wa Dokta Magufuli unashangaza kidogo kwa sababu wakati ni
ruhusa kwa wananchi kumwombea (kama anavywasihi mara kwa mara), serikali yake ilifikia
hatua ya kupiga marufuku maombi ya kiroho kwa ajili ya Lissu anayeugulia majeraha ya risasi
kufuatia jaribio la kumuuwa.
Japo Makamu wa Rais Samia na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi wamemtambelea mbunge
huyo wa Singida Mashariki, inaelezwa kuwa msimamo wa Dokta Magufuli kwa wabunge na
viongozi wa CCM dhidi ya ushirikiano na viongozi wa upinzani ni miongoni mwa sababu
zilizopelekea viongozi wengi wa chama hicho tawala kushindwa kumtembelea Lissu huko
Nairobi.
Kuna suala jingine ambalo japo halijaibuka waziwazi, linaweza kuzua maswali dhidi ya
utawala wa Dokta Magufuli. Suala hilo ni operesheni iliyoendeshwa na vyombo vya dola katika
maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji (MKIRU) ambayo yalikumbwa na mauaji mfululizo.
Serikali haijatoa taarifa rasmi kuhusu idadi kamili ya ‘magaidi’ waliouawa.
Hivi karibuni, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro alinukuliwa akieleza kuwa jumla
ya watoto 1,300 wa eneo la MKIRU hawajulikani walipo. Lakini cha kushangaza, mkuu huyo
wa jeshi la polisi aliwataka wazazi na walimu washirikiane kuwatafuta watoto hao. Watoto
ELFU MOJA NA MIA TATU watafutwe na wazazi na walimu?
Rekodi ya utendaji wa vyombo vya dola hata pale vinapopaswa kusimamia tu usalama
kwenye shughuli za vyama vya upinzani sio ya kupendeza. Kwahiyo kuna uwezekano kwamba
operesheni yao huko MKIRU ina mengi ambayo wananchi hawayafahamu japo ni haki yao
kufahamishwa.
Kwa upande mwingine, kumekuwa na manung’uniko japo hayajasambaa sana kuhusu dalili
za ukabila, ukanda na udini. Tangu aingie madarakani, Dokta Magufuli amezuru zaidi Kanda ya
Ziwa, eneo ambalo ni asili yake. Hata hivyo pengine ni mapema mno kumlaumu kwani bado
amekuwa madarakani kwa miaka miwili tu na bado ana takriban miaka mitatu kabla
hajahitimisha muhula wake wa kwanza.
Kingine kinachoongelewa kuhusu Dokta Magufuli ni hofu kuwa huenda akabadili Katibu
huko mbeleni ili aendelee kubaki madarakani. Japo yeye mwenyewe ameshaahidi kuheshimu
ukomo wa muda wa urais, ‘marafiki zake’ kama Rais Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri
Museveni wa Uganda – wapinzani wakubwa wa ukomo wa muda wa urais – wanaweza
kumshawishi aendelee kubaki madarakani. Pengine kingine kinachochangia katika hofu hiyo ni
ukweli kwamba Dokta Magufuli ameweka msimamo wake bayana kuwa marekebisho ya Katiba
sio miongoni mwa vipaumbele vyake.
Sura hii ilijikita katika kuangalia upande mwingine wa Dokta Magufuli, mwanasiasa
aliyeingia madarakani wakati Tanzania ikiwa katika hali mbaya katika takriban kila nyanja,
akafanikiwa kurejesha matumaini ya Watanzania huko wengine wakimfananisha na Baba wa
Taifa Julius Nyerere, lakini tathmini ya miaka miwili ya utawala wake inaonyesha upande
mwingine usiopendeza.
Hitimisho
Kitabu hiki kimeandikwa kwa nia nzuri ya kutathmini utandaji kazi wa Rais Magufuli katika
kipindi cha miaka miwili tangu aingie madarakani. Mwandishi amekuwa akifuatilia kwa karibu
siasa za Tanzania, na kimsingi, kitabu hiki ni mwendelezo wa vitabu vingine viwili: kimoja
kilichoandikwa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 uliomwingiza madarakani Rais
Magufuli, na kingine kilichoandikwa siku 55 baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani.
Ni vigumu kufanya tathmini kwa kuangalia upande mmoja tu, na hilo lilikuwa kosa kuu la
kitabu cha pili cha mwandishi huyu ambacho japo pia kilikuwa kikifanya tathmini, kwa kiasi
kikubwa ilielemea kuangalia ‘mazuri’ tu. Lengo la kitabu hiki, kama ilivyokuwa kwa viwili
vilivyomtangulia katika mfululizo huu wa ufuatiliaji wa karibu wa siasa za Tanzania, si
kumchukiza au kumpendeza mtu flani,
Kwa vile kitabu kimeshaonyesha alikotoka Rais Magufuli, mchakato wa kuchaguliwa
kwake, siku za mwanzo za utawala wake na hali ilivyo miaka miwili tangu aingie madarakani.
Katika hitimisho hili, mwandishi anajaribu kueleza kwa kifupi kuhusu matarajio ya huko
mbeleni, na mustakabali wa Tanzania kwa ujumla.
Ndani ya CCM, Dokta Magufuli amefanikiwa kukamata hatamu za uongozi baada ya
kufanikiwa kufanya ‘mapinduzi ya mtu mmoja,’ kwa maana ya kuwezesha mabadiliko makubwa
ndani ya chama hicho peke yake, kwa kiasi kikubwa.
Moja ya mitihani mikubwa ya uenyekiti wake wa CCM Taifa ulikuwa kukabiliana na
makundi makubwa mawili: ‘masalia’ ya kambi ya Lowassa ndani ya chama hicho tawala na
wana-CCM wengine wenye nguvu katika chama hicho lakini ni wahanga wa sera mbalimbali za
Dokta Magufuli kama vile vita dhidi ya ufisadi.
Japo sio matumizi mazuri ya raslimali za taifa, taarifa zinaonyesha kuwa Idara ya Usalama
wa Taifa imekuwa na ufanisi mkubwa katika utekelezaji wa ajenda za Dokta Magufuli ndani ya
chama chake na serikalini.
Wakati CCM inaelekea katika hatua za mwisho za chaguzi zake za ndani, yayumkinika
kuhitimisha kuwa kiongozi huyo amefanikiwa kutengeneza mfumo aliohitaji katika kufikia
mageuzi ndani ya chama hicho. Na kama ilivyo serikalini, amefanikiwa kwa kiwango fulani
kurejesha nidhamu ndani ya chama hicho tawala.
Kumudu kufanikisha ajenda ya kutenganisha kofia mbili, yaani kiongozi wa chama asiwe na
majukumu mengine ‘full-time,’ kumemaanisha pia kwamba baadhi ya wanasiasa wenye nguvu
ndani ya chama hicho wamebaki wananachama wa kawaida tu licha ya baadhi yao kuwa na
madaraka makubwa serikalini.
Kwamba mabadiliko hayo yatakuwa na ufanisi kwa chama hicho itategemea mwelekeo wa
Dokta Magufuli ukoje. Na kwa hakika ni vigumu kubashiri kwa sababu kama sura mbili
zilizopita na hii zilivyoonyesha, kiongozi huyo sio mtu wa kutabirika kirahisi.
Mageuzi anayofanya ndani ya chama chake pia yanamaanisha kuwa nafasi yake ya
uenyekiti wa taifa wa chama hicho ipo salama, na licha ya utaratibu uliozoeleka wa rais aliyepo
madarakani kutopata mpinzani ndani ya chama hicho, nguvu kubwa aliyokwishatengeneza ndani
ya CCM inamwondolea wasiwasi wa kuibuka upinzani dhidi yake katika kinyang’anyiro cha
kuwania tiketi ya urais kupitia chama hicho tawala.
Kwa upande mwingine, Dokta Magufuli anaendelea kunufaika na ‘sintofahamu’
inayovikabili vyama vya upinzani. Tukiweka kando ukweli kwamba vyama hivyo vinafanya kazi
katika mazingira magumu kutokana na kunyimwa fursa ya kufanya shughuli zake za kisiasa,
bado kuna kukosekana kwa dira kwa takriban vyama vyote vikuu vya upinzani.
Kwa upande wa Chadema, ukweli tu kwamba chama hicho kimeipa kisogo demokrasia kwa
kutofanya uchaguzi wake mkuu kwa miaka kadhaa sasa, inakiweka katika mazingira magumu ya
kufanya mabadiliko ya ndani ambayo ni muhimu kwa maendeleo na ustawi wa chama hicho.
Pamoja na mchango wake mkubwa kwa Chadema na siasa za upinzani kwa ujumla, lakini
kuna dalili zinazoashiria kuwa mwenyekiti wa taifa wa chama hicho Mbowe ‘ameishiwa pumzi.’
Haimaanishi aondoke madarakani lakini pengine apambane na changamoto mpya kutoka kwa
viongozi au wanachama wengine kupitia sanduku la kura, kwa maana uchaguzi mkuu wa chama
hicho.
Kwa kiasi kikubwa, Chadema imeshindwa kabisa kurudi zama zile ilipokuwa ‘mwiba’ kwa
CCM na serikali yake kutokana na kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ufisadi.
Ajenda hiyo sio tu ilikifanya chama hicho kifahamike zaidi bali pia ilipelekea kikubalike
miongoni mwa Watanzania wengi kwani kilikuwa ‘msemaji’ wao, sambamba na kuonekana
mbadala wa kweli wa CCM.
Tangu kuisha kwa uchaguzi mkuu uliopita, Chadema kimekuwa zaidi chama cha kudandia
hoja kuliko kuanzisha hoja zake zenyewe. Hivi chama hicho kimeshindwa hata kulifanya suala la
kupotea kwa kada wake Saanane au jaribio la mauaji dhidi ya Lissu kuwa mijadala ya kitaifa?
Chama hicho kinapaswa kutambua kwamba kisipokuwa makini, kitakuwa katika wakati
mgumu kwenye uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020. Kwamba Dokta Magufuli ‘havipendi’ vyama
vya upinzani sio suala la mjadala, matendo yake yamejidhihirisha bayana. Kutarajia miujiza
kwamba labda atalegeza uzi ili vyama vya upinzani vifanye shughuli zake za kisiasa bila
bughudha ni ndoto ya alinacha.
Kama alivyosema aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dokta Willbrord Slaa,
mabadiliko ya kweli – kama ilivyokuwa ajenda kuu ya Chadema katika uchaguzi mkuu uliopita
– yataletwa na mikakati makini itakayotekelezwa na watu makini. Lakini kuilaumu tu CCM pasi
kufanya kitu mbadala kinachoweza kuwashawishi wananchi kuwa ‘hawa nafuu,’ hakuna ufanisi
wowote.
Mara kadhaa mwandishi wa kitabu hiki amekuwa akiwakumbusha wafuasi wa Chadema
kwamba ‘mabaya ya CCM hayamaanishi mazuri ya Wapinzani.’ Na kwa hakika, wapigakura
wanaweza kukubali kukivumilia chama kibaya lakini wanachokifahamu vema kuliko kukipatia
fursa ya majaribio chama ‘kizuri’ lakini kisichoeleweka kinasimamia nini.
Kubwa ambalo Chadema na vyama vingine vya upinzani vinapaswa kupigani ni Katiba
mpya. Kwamba Dokta Magufuli ameshaeleza kuwa Katiba hiyo sio kipaumbele chake, sio
sababu ya muhimu kukwaza jitihada za kudai Katiba mpya. Ikumbukwe tu ni jitihaza za
Chadema zilizoibuka suala la Katiba mpya kabla CCM hawajalipora na kulifanya ajenda yao.
Kadhalika, kama ilivyoelezwa awali, tangu kuanza kwa mfumo wa siasa za vyama vingi,
vyama vya upinzani vimekuwa vikifanya shughuli zao za kisiasa katik mazingira magumu, huku
takriban awamu zote za serikali za CCM zikifanya jitihada za kuvikandamiza vyama hivyo.
Mkazo mkubwa kwa vyama vya upinzani unapaswa kuwa kwenye kundi muhimu la wapiga
kura nchini Tanzania, yaani watu wasiojihusisha na chama chochote. Ni kwamba, CCM haihitaji
kuwashawishi wanachama wake kuipa kura wala haijihangaishi sana na wanachama wa
upinzani. Walengwa wakuu wa kampeni za CCM huwa kundi hilo la watu wasio na vyama.
Ili kuweza kulishawishi kundi hilo, ni muhimu vyama vya upinzani vionekane vina cha
tofauti kulinganisha na CCM. Ugumu wa kukiondoa chama tawala madarakani huchangiwa na
hofu ya wapigakura kwamba ‘angalau huyu ni jini tunaye,mjua’ kwa maana angalau
wanakifahamu vema chama tawala pamoja na mapungufu yake. Kwa upande wa wapinzani,
huangaliwa kama ‘wageni’ fulani ambao hakuna mwenye uhakika iwapo wakiaminiwa
wataweza kufanya vitu tofauti na chama tawala.
Lakini pasipo Katiba mpya, hata kama vyama vya upinzani vitafanikiwa kumnasa kila
Mtanzania asiye na chama na kuwa na uhakika kuwa atavipigia kura vyama vya upinzani, pasipo
Katiba mpya itakuwa sawa na ‘kutwanga maji kwenye kinu.’ Kwahiyo jitihada za kupania
kuiondoa CCM madarakani sharti ziendane na jitihada ya kushinikiza kupatikana kwa Katiba
mpya.
Kwa upande mwingine, ni vigumu kuona mwana-CCM yeyote akijaribu kumshawishi Dokta
Magufuli kuhusu umuhimu wa vyama vya upinzani kwa siasa za Tanzania. Kuna dalili nyingi tu
za kuuangamiza upinzani hasa kupitia wimbi lililokuwa likiendelea wakati wa uandaaji kitabu
hiki, la viongozi mbalimbali wa upinzani kuhamia chama tawala.
Kwa vile Dokta Magufuli amefanikiwa ‘kupora’ sera ya vita dhidi ya ufisadi kutoka
Chadema, hakuna dalili zozote kwamba kukipa uhuru chama hicho cha upinzani, na vinginevyo,
kutamwathiri yeye binafsi au chama chake. Sana sana, ili kuepuka kupotea kwenye ramani ya
siasa, vyama vya upinzani vinaweza kuwa washirika muhimu wa Dokta Magufuli katika
utekelezaji wa sera mbalimbali kwa manufaa ya taifa. Siasa haipaswi kuwa uadui ilhali wote ni
Watanzania.
Kwa kumalizia kitabu hiki, pamoja na kusisitiza umuhimu mkubwa kwa serikali ya Dokta
Magufuli kuruhusu nafasi kwa vyama vya upinzani kufanya shughuli zake bila kubughudhiwa,
serikali yake pia ina wajibu wa kuwaelewesha Watanzania kuhusu jitihada mbalimbali
zinazofanyika katika kuiondoa kutoka katika mfumo wa uchumi wa kifisadi kuelekea uchumi wa
‘kila mtu atakula kwa jasho lake halali.’
Kwamba ili kufikia japo karibu na mahali Tanzania inapaswa kuwepo basi ni lazima
kutakuwa na machungu kadhaa ambayo ni lazima kuyapitia kabla ya kufika eneo kusudiwa.
Badala ya kuhangaika kuwahadaa wananchi kuhusu takwimu zinazoashiria kuwa uchumi upo
vizuri ilhali wao wanaoteseka, ni vema kuwa wakweli na kuwaelewesha wananchi kuwa hatua
zinazopitiwa ni lazima zitawathiri lakini kwa nia njema.
Kumwita ‘mpiga dili’ kila mtu anayelalamikia ugumu wa maisha sio kuwatendea haki
mamilioni ya wachapakazi wa Kitanzania ambao ufisadi pekee wanaofahamu ni ule unaofanywa
na vyama vya ushirika dhidi ya mazao yao.
Vitabu vingine vya mwandishi huyu
1. Uchaguzi Mkuu Tanzania 2015: Magufuli vs Lowassa
2. Dokta John Magufuli: Safari Ya Urais, Mafanikio Na Changamoto Katika Urais Wake
3. Afisa Usalama wa Taifa Ni Mtu Wa Aina Gani? Na Anafanya Nini?
4. Makala Za Evarist Chahali Zilizovuma Magazetini: Toleo La Kwanza
5. Makala Za Evarist Chahali Zilizovuma Magazetini: Toleo La Pili
6. Mwongozo Wa Kitabibu Wa Jinsi Ya Kuacha Sigara Na Ushauri Wa Mvutaji Mstaafu
Ungana Na Mwandishi Mtandaoni
Ungana nami Facebook: http://facebook.com/evarist.chahali.1
Ungana nami Twitter: http://twitter.com/chahali
Ukurasa wangu Smashwords: https://www.smashwords.com/profile/view/Evarist
Blogu yangu: http://www.chahali.com
Nisikilize hapa (audio): https://www.spreaker.com/user/chahali