Seyyid Sheikh
Mtungaji:-
Swahib Sujjada:
Sheikh Salim Bin Mbarak (Dar-wesh – Mti mkavu)
P. O. Box 8105,
Zawia kuu – Arusha,
Tanzania. (E.A).
i.
Swahib Sujjada,
Al habib Sheikh Salim Bin Mbarak.
(Dar-wesh Mti Mkavu). ii.
Seyyid Sheikh Abdul Qadir Jaylan
(Qad-dasa-Llahu Siral A`ziz).
First Addition Toleo la kwanza
iii.
iv.
Swahib Sujjada:
Al Habib Sheikh Salim Mbarak
(Mti - Mkavu).
Yaliyomo: No. Ukurasa.
1. Dibaji……………………………………….. vi.
2. Utangulizi…………………………………... vii.
3. Jina lake la kuzaliwa……………………….. 1.
4. Nasabu yake..………………………………. 2.
5. Makuzi yake na kusoma Qur an.………........ 2.
6. Kutafuta Ilmu ……………………………… 3.
7. Masheikh zake…………………………….. 4.
8. Umaarufu wake kwa kusoma……………… 5.
9 Kusomesha kwake Ilmu……………..…….. 7.
10. Namna ya Twariqa ilvyoenea….………….. 8.
11. Siri ya Ilmu ya Tasawfu ..………………..... 10.
12. Sifa za Seyyid Abdul Qadir…..…………… 11.
13. Wake zake na watoto wake……………….. 12.
14. Wasia wake kwa mwanawe A`bdul Razaq.. 13.
15. Karama zake……………............................ 13.
16. Kifo cha Seyyid Abdul Qadir Jaylani (Qsa).. 27.
v.
DIBAJI:
Sifa zote njema zinamstahiki ALLAH ambaye
amefundisha kwa wasta wa kalamu. Na akamfundisha Mwana
Adam lile asilolijua. Na Rehma na Amani Zimwendee Bwana
Mtume Saw na Ahly zake watukufu na Maswahaba wake watiifu.
Kwa ridhaa ya mtunzi wa kitabu hiki ambae ni kiongozi
mkuu na Mlezi wa Twariqatul-Qadiriya– Rrazziqiya–Jaylaniya Al
habib Sheikh Salim ibn Mbarak –(Dar-weish Mti mkavu) –
(Radhia ALLAH Anhu). Naandika Dibaji ya kitabu hiki kwa
munassaba wa kuya yakinisha yaliyomo kwenye kitabu hiki.
Kwa hakika kitabu hiki kimeelezea historia na sifa kadhaa
za Bwana wa Mawalii Seyyid Sheikh Abdul-Qadiri- Jaylani (Qada-sa-Llahu-Siral-Aziz)
Basi ukiwa utajaaliwa kusoma kitabu hiki utamjua vilivyo
alivyo Walii wa Mwenyezi Mungu na Uasili wa Twariqa kwa
ujumla.
Insha-Allah tunamuomba Allah amjaalie kila la kheri mtunzi
wa kitabu hiki Sheikh Salim amjaalie Mahaba zaidi ya kudarisisha
hususan kwa kutunga vitabu vingi zaidi vitavyotoa Ilmu na
muongozo wa ibada za Kitwariqa kwa misingi ya Kitassawfu. Aamiin Aamiin Aamiin wal-hamdulillahi Rabbil-A`alamiin
Khalifa Mohamed Omar.
Mwenyekiti wa Twariqatul-Qadiriya-Rrazziqiya-Al-Jaylaniya
Makao Makuu Ya Twariqa – Zawiya Kuu
S.L.P. 8105
Arusha.
Tanzania (E.A)
vi.
UTANGULIZI:
“Assalamu alay–kum warah–matullahi –Taala wabarakatuh”.
Namshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kunijaalia fikra
na utashi wa kuandika kitabu hiki nilichokitambulisha kwa jina la
Ghawth–l–A`adham, Seyyid Sheikh – Abdul – Qadir-Jaylani.
(Qad-sa-Llahu-Siral-A`ziz)
Makusudio yangu makubwa katika kuandika kitabu hiki ni
kuelezea sifa na mwenendo wa maisha ya Bwana wa Mawalii na
kipenzi cha Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume (Saw).
Ni Matarajio yetu Historia hii tuliyoiandika ndani ya kitabu
hiki itahifadhika na kujenga kumbukumbu juu ya maisha ya watu
wema kwa ujumla. Kuwakumbuka watu wema na kufuatisha
matendo mema ni ufunguo wa kheri hapa duniani na Akhera.
Insha Allah Mwenyezi Mungu amjaalie kila la kheri msomaji
wa kitabu hiki na amjaalie kuwa na matendo mema.
“Eee Mwenyezi Mungu tujaalie sote
mwishilio mwema na utujaalie kuwa
watu wa peponi”
(Aamiin).
Sheikh Salim Ibn Mbarak – (Dar-weish – Mti Mkavu).
S.L.P 8105
Zawiya Kuu – Arusha.
Tanzania (E.A).
vii.
viii.
i. Maisha ya Seyyid Abdul Qadir (Qsa).
Seyyid Abdul Qadir ni Muajemi. Naye ni mashuhuri si
katika Ardhi tu, bali hata Mbinguni pia. Yeye ni Sheikh wa
Waislam na ni kiigizo kwa Mawalii na watu wema. Seyyid Abdul
Qadir alikuwa Imamu wa Siddikin na A`arifiyn.
Sharafu yake kwa Mawalii wenzake ni kama Sharafu ya
Nabii Muhammad kwa Mitume wenzake.
ii. Kuzaliwa kwake:
Seyyid Abdul Qadir alizaliwa katika kijiji cha Jeilan huko
Iraq. Alizaliwa usiku wa kuamkia Mwezi mosi wa Ramadhani
mwaka 470. A.H.
Bi Fatma alichukua mimba ya mtoto huyo na hali ya kuwa
umri wake ni miaka 60. Wakati ambao hapana tamaa ya kupata
mtoto yeyote.
Siku hiyo aliyomzaa Seyyid Abdul Qadir ilizagaa Nuru
ambayo ilitapakaa kijiji kizima. Mambo hayakuwa hayo tu, lakini
hapakuwa na mtu yeyote aliyethubutu kuuangalia uso wake kwa
mng‟aro na haiba yake.
Tabia zake zafanana na zile za Seyydina Muhammad
(Saw). Uzuri wake ni ule kama wa Nabii Yusuf (A.s). Ukweli wake
unalingana na Seyyidna Abu-Bakar. (R.a) Haki yake ni kama ile ya
Seyyidna Omar (R.a), na upole wake wa Seyyidna Othman. (Ra).
iii. (a) Nasabu yake kwa kuumeni
Yeye ni Seyyid Abdul Qadir bin Mussa bin Abdillah
1.
bin Yahya bin Muhammad bin Daudi bin Mussa bin Abdillah Bin
Mussa bin Abdillahi bin Hassan bin Seyyid Hassan bin Ally bin
Abi Talib. Yaani nduguye Mtume (Saw).
(b). Nasabu yake kwa kukeni.
Yeye ni mtoto wa Bi Fatma Bint Seyyid Abdillah Sawmaiy
Bin Seyyid Mahmoud bin Issa Bin Muhammad Bin Ali Bin Mussa
Bin Jaafari Swadiq Bin Muhammad Bin Seyyidna Hussein Bin
Ally Bin Abi Talib.
Unapoangalia nasabu zake zote yaani kukeni na kuumeni, utaona
kama zimekutana kwa Seyyidna Ali bin Abi Talib; yaani nduguye
Mtume (Saw).
iv. Kukua kwake na kusoma Qur ani
Seyyid Abdul Qadir alikuwa akikua na akiishi katika hali
nzuri. Mji wake uliingia neema kubwa kabisa baada ya kuzaliwa
kwake. Seyyid Abdul Qadir alipewa Uwalii na hali ya kuwa ni
mtoto kama Nabii Isa alivyopata Utume katika hali hiyo hiyo.
Ishara zilizoonyesha kama yeye ni Walii ni nyingi na katika
hizo ni:-
(i) Kutamka „Hatifu‟ maneno siku ya mwanzo
alipopelekwa chuoni kusoma Qur an. Maneno
yenyewe ni haya “Mfanyieni nafasi ya kukaaWalii wa
Mwenyezi Mungu”.
(ii) Kusifiwa kwake na „Abdal‟ kwa kusema: “Mtoto
2.
huyu atakuwa na mambo matukufu
atakayosifiwa mwishoni kwake”.
(iii). Bishara ya Mtume aliyompa Baba yake
usingizini - “kwamba atamzaa mtoto ambaye
atakuwa na mambo matukufu atakayosifiwa
mwishoni kwake”.
v. Kutafuta Ilmu:
Seyyid Abdul Qadir alipotimia miaka 18, alimwomba
ruhusa mama yake kusafiri kwa kutafuta Ilmu ambayo ni wajibu
kwa kila Mwislamu mwanamke na mwanaume. Aliondoka kwenda
Baghdad pamoja na Nabii Khidhri. Lakini kabla ya kuingia ndani
ya Mji wa Baghdad; Nabii Khidhri alimpa Seyyid Abdul Qadir
sharti ambalo atakapolitekeleza ndipo atapompeleka kwa Masheikh
kusoma. Sharti yenyewe ni kukaa pale nje ya mji na kufanya ibada
kwa muda wa miaka mitatu kamili. Seyyid Abdul Qadir alikubali.
Tangu siku ile Nabii Khidhri hakupapita tena mpaka mwaka
ukamalizika.
Baada ya kutimia mwaka mmoja, Nabii Khidhri alikwenda
kumzuru Seyyid Abdul Qadir. Seyyid Abdul Qadir alipomwona
Nabii Khidhri alimsimamia. Lakini Nabii Khidhri alikataa
kunyanyukiwa na kumwambia akae kitako.
Siri ya kuwekwa Seyyid Abdul Qadir peke yake kwa
muda wote ule, apate kuitakasa roho yake na ile sehemu
inayoharibiwa na Shetani. Vitisho alivyokuwa akivipata mahala
pale havikuwa na mfano. Lakini Mwenyezi Mungu alimlinda Walii
wake na akamhifadhi na kila baya na vitisho. Ulipotimia mwaka
wa tatu. Nabii Khidhri alikwenda mahala pale kwa ajili ya
kumchukua Seyyid Abdul Qadir.
3.
Juu ya kuwa wamo ndani ya safari pamoja, Seyyid Abdul
Qadir kabisa alikuwa hamjui mtu anayefuatana naye. Lakini alikuja
kumjua baadaye hapo alipokwenda Baghdad kumkagua.
Seyyid Abdul Qadir alisoma kwa juhudi na ari kubwa na
aliwashinda wenzake wote kwa Ilmu na ufasaha wa lugha. Na
alikuwa jogoo mkubwa wa Madhehebu ya Shafi na Hambali. Na
alikuwa akijibu na akifutu masuali kwa Madhehebu hayo mawili.
Lakini yeye mwenyewe alikuwa akifuata madhehebu ya Hambal.
vi. Katika baadhi ya Ilmu alizosoma.
(i) Qur an (Tafsiri)
(ii) Fiqh
(iii) Hadith
(iv) Usuli-fiq
(v) Tarikh (historia)
(vi) Tasawuf
(vii) Lugha. n.k.
vii. Masheikh zake:
Seyyid Abdul Qadir amesoma Ilmu kwa Masheikh wengi
na kila mmoja katabahari katika fanni mbalimbali. Masheikh
wenyewe ni:-
1 Sheikh Abdil-Wafa Ali Bin Ukayl.
2. Sheikh Abi Said-al-Mubaraq.
3. Sheikh Abdil Khatib Mahfudh
Kaludhany.
4.
4. Sheikh Abi – Hassan Muhammad.
5. Sheikh Kadhi Abi Said.
6. Sheikh Yahya Bin Ali.
7. Sheikh Abi Ghalib Muhhamad bin Abdul
Karim.
8 Sheikh Abu Said Muhammad bin Abdul
Karim.
9. Sheikh Muhammed bin Muhammed
10 Sheikh Abubakar Ahmed bin Ahmed
11. Sheikh Abu Jafar bin Ahmed
12. Sheikh Abu Kassim Ali bin Ahmed
13. Sheikh Abu Talibu Abdul Kadir bin
Muhammad
14. Sheikh Abdul Rahman bin Yusuf.
15. Sheikh Abdul Rahaman bin Ahmed
16. Sheikh Abu - Barakat Hibatullah
17. Sheikh Abdul-Izzi Muhammed bi
Mukhtar.
18 Sheikh Abu – Nasri Muhammed
19. Sheikh Abu – Ghalib Ahmad
20. Sheikh Abu – Abdalla Yahya
21. Sheikh Abu – Hassan Mubarak
22. Sheikh Mansur Abdul Rahman
23. Sheikh Abu Barakat Taibat Akuly.
viii. Umaarufu wake kwa kusoma
Sifa za Seyyid Abdul Qadir zilizagaa kwa Ilmu yake.
Ingawa wengi walifurahi kwa mambo hayo, lakini mahasidi wake
walikuwa wakikereka - Nao ni katika nafsi ya wanachuoni
wenzake.
Siku moja walimjia wanachuoni 100 wakati alipokuwa
akisomesha ili kumhoji. Na kila mmoja katika hao alikuwa na
suala mbalimbali, na muradi wao ashindwe ili afedheheke.
5.
Wakati huo watapata kueneza kama hajui kitu kuliko wao. Mara tu
wale wanachuoni walipofika pale walikaa kitako kumsikiliza.
Baada ya kukaa, Seyyid Abdul Qadir alikiimanisha kichwa chake.
Na wakati huo lilimtoka pande la Nuru kifuani mwake
likanyakuwa yote waliyoyadhibiti katika vifua vyao. Mara wakawa
wanababaika na kuwayawaya, huku wanapiga makelele wakirarua
nguo zao mfano wa wenda wazimu. Wote walivua vilemba vyao na
wakamwendea Sheikh pale alipokaa. Kila mtu alikuwa akinyanyua
mguu wa Seyyid Abdul Qadir na kujiwekea kichwani kwake. Hii
ni ishara kuonyesha kama wameridhika na kukinai kuwa ni
Mwanachuoni na amewazidi. Na kila mtu alipokuwa akifanya hayo
yeye alikuwa akimkumbatia.
Waliporudi vikaoni mwao, yote waliyokuwa wameyasahau
wakayakumbuka tena. Seyyid Abdul Qadir alimwambia kila mtu
suala aliyokusudia kuuliza na akampa jawabu nzuri ambayo hata
yeye mwenyewe hakufikiria. Wote walistaajabu na walimpa heko.
ix. Muda wa kutoa waadhi
Seyyid Abdul Qadir alikuwa akitoa waadhi mara tatu kila
wiki kwa muda wa miaka 40. Masheikh, Mafaqih na wanachuoni
wengi wa Baghdad walikuwa wakimiminika kumsikiliza waadhi
wake.
Naam, Katika jumla ya wasikilizaji wa waadhi; Mayahudi
na Manasara walikuwamo.
Taathira kubwa ilipatikana kila waadhi aliokuwa akiutoa
kwani Mayahudi na Manasara wengi kabisa walisilimu. Na
miongoni mwa Waislamu wengi wafanyao maasi walitubu katika
maasi yao.
6.
Ama masomesho yake yalizidi kupatia utukufu. Kwani Bibi
mmoja alijitolea nafsi yake aolewe na Seyyid Abdul Qadir bila
mahari yoyote, isipokuwa alimpa sharti moja, nayo ni
kuwasomosha watu Ilmu kwa muda maalum. Muda ulipotimia,
Bibi yule aliolewa kama alivyotamani.
X. Kusomesha kwake Ilmu:
Katika chuo chake, Seyyid Abdul Qadir alikuwa
akisomesha Ilmu 13 za sheria. Na katika Ilmu hizo 13, aliweka
darsa moja kusomesha Madhehebu mbalimbali na darsa nyinginezo
alikuwa akisomesha Hitilafu za Wanachuoni. Baada ya sala ya
Alfajiri, alikuwa akisomesha Tafsir ya Qur an na akisomesha
Hadithi za Mtume (Saw) Darsa hizo zilikuwa zikisomwa na kila
mtu aliyetaka. Ama Ilmu za Madhehebu mbalimbali, Khitilafu za
Wanachuoni, Adabu, Fiq na Usuli Dini zilikuwa zikismwa na
Mawalii tu.
Wakati wa Adhuhuri, ilikuwa ikisomwa Qur an kwa Kiraa
(visomo) 7. Darsa ilikuwa ikihudhuriwa na wanafunzi 650
waliokuwa mahodari sana. Wasomaji wake wakubwa wa Qur ani
walikuwa Sheikh Masoud al Hashimiy na Sheikh Abdul Wahab bin
Abdul Qadir (mwanawe).
xi. Kufutu kwake masuala
Katika fatwa zake, Sheikh alikuwa halazi suala wala
alikuwa hafikiri, Bali alikuwa hanafutu mara moja tu. Kabla ya
kufutu au kujibu suala yoyote, ilikuwa ikisomwa Qur an. Jawabu
zake zilikuwa ama za kuandika au za mdomo. Na jawabu zake
zilikuwa zikiwafurahisha watu kwa ustadi wake.
7.
xii. Namna ya Twariqa ilivyoenea
Asili ya Twariqa inatokea kwa Mwenyezi Mungu. Yeye
akamfundisha Seyyidna Jibril As, na Seyyidna Jibril akamfundisha
Seyyidna Muhammad (Saw), tena Nabii Muhammad akamfundisha
Seyyidna Ali (R.a) Baadaye ikaendelea kwa Masheikh hawa hata
nao wakaifikisha hapa Tanzania na mwenginepo:-
1. Seyyidna Hassan al Busry.
2. Seyyidna Arif Samdany
3. Alhabibul Ajemy.
4. Daud Taiy
5. Maaruf al Karkhy.
6. Sharif Sakaty
7. Abi Kasim al Juneid
8. Abu Bakar Shily
9. Abu Fadhi Abdul Wahid
10. Abu Faraj Tusy
11. Seyyidna Abdul Hassan
12. Seyyidna Abu Said –al – Makhzumy.
13. Seyyid Abdul Kadir al Jeilany na kadhalika.
xiii. Siri ya Ilmu ya Twariqa
Ilmu ya twariqa imefanywa kwa Qur an na Hadithi za
Mtume (Saw) pamoja na mambo yafuatayo:-
(i) Kusafisha moyo
(ii) Ukarimu
(iii) Ustahamilivu
(iv) Kuwasamehe waliokuudhi
(v) Kuacha au kujiepusha na maasi
(vi) Kufanya Ibaada kwa jitihada.
8. .
Faida. i.
Hizi Twariqa ziko namna nyingi, nazo zinapata kama 17.
Katika hizo ni Qadiry, Shadhily, Nakshahabandy, Indarusy
n.k.
Ama Twariqa yoyote akiifuata mtu kama
inavyohitajia, basi itaweza kumfikisha kwa Mwenyezi
Mungu. Kwani lengo lao ni moja tu lakini kwa yote hayo
niliyoeleza inapasa kupatikana Sheikh Mwongofu wa
kukupa „Ijaza‟ na kukufundisha njia za kupita na kukupa
wasia. Huyu mtu anayepewa „Ijaza‟ na Sheikh huitwa
„Muridi‟ Kwa hivyo kila Murid ajitahidi sana kutekeleza
ahadi atakazopewa na Sheikh wake.
Faida ii. Yatakiwayo kwa Muridi
1. Kutubia kwa Mwenyezi Mungu.
2. Kufanya Ibaada kiasi ya uwezo wake.
3. Kufanya mambo yalio halali
4. Kuacha mambo yaliyo haramu.
5. Kumdhukuru Mungu
6. Kushikamamna na “Laa ila ha illa Llah” hasa baada
ya kila Sala mara 165 na wakati mwngine kiasi ya
kuweza kwake.
7. Kusoma sana Qur an kwa kila hali.
8. Kuwasamehe wenye kukuudhi.
9. Kuwa mstahamilivu.
10. Kuwa karimu
11. Kuacha husda, kijicho, choyo, uwongo wa
kuwasengenya watu.
12. Kudumu na udhu.
13. Kumsalia Mtume (S.a.w) kwa wingi.
9.
xiv. Siri ya Ilmu ya tasawuf:
Ilmu ya Tasawfu imefanywa kwa mambo yafuatayo:-
(i) Ukarimu.
(ii) Kuridhia hukumu ya Mungu.
(iii) Subira
(iv) Ishara
(v) Upweke
(vi) Kuvaa nguo za sufi
(vii) Kwenda sana
(viii) Umaskini.
Faida:-
Katika hizo sifa nane zilizotajwa hapo juu, zimechukuliwa
kutokana na Mitume wanane mbalimbali:-
1. Ukarimu: Ilikuwa sifa kubwa sana ya Nabii Ibrahim
(Asw).
2. Ridhaa: (kuridhia), ni sifa ya Nabii Is-haq. (As).
3. Subra: Ni sifa ya Nabii Ayub, (A.s)
4. Ishara: Ni sifa ya Nabii Zakaria (A.s)
5. Sufi: Ni kivazi cha Nabii Yahya (A.s)
6. Upweke: Ni sifa ya Nabii Yusufu (A.s)
7. Kwenda : Ni sifa ya Nabii Issa, (As) na ndio maana
akaitwa „Masihi‟
8. Umaskini: Ni sifa ya Nabii Muhammad (Saw). 10.
xv. Sifa za Seyyid Abdul Qadir (Qsa).
Seyyid Abdul Qadir alikuwa karim sana na mwenye sifa na
tabia nzuri za kupigiwa mfano. Alikuwa na kimo cha wastani, si
mrefu sana wa kuchusha wala hakuwa mfupi. Alikuwa mwekundu
wa weupe. Alikuwa na nyusi nzuri sana. Mwili wake ulikuwa
mwembamba, macho yake yalikuwa yenye haiba kubwa. Kifua
chake kilikuwa kipana chenye Ilmu nyingi. Alikuwa mkali kama
babu yake Sayyidna Ali bin Abi Talib. Ama ndevu zake zilikua
ndefu namna zile za Nabii Harun (As).
Seyyid Abdul Qadir alikua na cheo au makamo matukufu
mbelel ya Mwenyezi Mungu. Katika Ulimwengu alikuwa ni mtu
mwenye kusikilizwa sana sauti. Sauti yake iliokuwa nzuri na
nyororo kama lulu. Anaposema husema upesi upesi. Hakupata
kupenga makamasi wala kutema makohozi. Mwisho inzi hakupata
kumtua juu ya mwili wake.
Seyyid Abdul Qadir alikuwa mnyenyekvu na mkweli.
Alikuwa na kawaida ya kumtolea mtu salamu mwanzo kila
wanapokutana naye.
Aidha alikuwa akikaa na maskini kama alivyokuwa
akifanya Nabii Muhammad (Saw). Pamoja na utukufu aliokuwa
nao, alikuwa akiwasimamia watoto wadogo na alikuwa
akiwatukuza watu wazima kama ilivyokuwa ada yake Mtume
(Saw). Ingawa alikuwa akiwasimamia watoto lakini hakupata
kumsimamia mtu yeyote katika watu watukufu.
Seyyid Abdul Qadir hakupata kugonga mlango wa
Mfalme au waziri yeyote kwa kumtaka haja ya kilimwengu.
Kazi yake ilikuwa ni kuamrisha mema na kukataza maovu.
Alikuwa akila na wageni na marafiki zake.
Kadhalika alikuwa akiwapa nguo na chakula maskini.
Vile vile alikuwa akiwapa zawadi nzuri nzuri wanapomwendea
kwake. Kwa ukarimu wake hakupata kumrejesha mtu yeyote
aliyemwomba wakati wa shida, seuze wakati wa raha.
11.
Mavazi yake yalikuwa ya fahari, kama mavazi ya kifalme. Mavazi
hayo aliyavaa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Siku moja alipita mtu mwenye haja na akavua nguo hizo
akampa yeye. Alitoa Joho ambalo thamani yake yadi moja ni
Dinari 20; yaani Sh. 240/-Alitoa na kilemba ambacho thamanai
yake ni Dinari 70,000 yaani sh. 840,000/- .
xvi. Wake zake
Seyyid Abdul Qadir hapo mwanzoni mwake alikaaa muda
mrefu sana bila ya kuoa. Alikaa muda mrefu kwa Ibaada na
alichelea kuvaana na mambo ya ndoa asije akashughulika na
akapunguza Ibaada zake kwa mshughuliko wa wakeze. Siku moja
aliendewa na Mtume(Saw) akamwambia aoe. Kwa kupata nasaha
hiyo ndipo alipooa, na alioa wake wanne.
xvii Watoto wake:
Watoto aliozaa Seyyid Abdul Qadir ni 49. Katika hao 27
walikuwa watoto wanaume na 22 walikuwa wanawake.
Hawa wafuatao ni miongoni mwa hao watoto wa kiume wa
Seyyid Abdul Qadir aliowaacha baada ya kufa:-
1. Sheikh Abdul Wahab
2. Sheikh Abdul Razak
3. Sheikh Abdul Aziz
4. Sheikh Abdul Jabbar
5. Sheikh Abdul Ghafur
6. Sheikh Abdul Ghina
12.
Faida:- Sayyid Abdul Qadir alipokuwa akiumwa siki moja aliwahi
kuzimia. Wakawa wanawe na wakeze wanalia, Mara tu baada ya
kupata fahamu, alisema, “Msilie nitapona, kwani mgongoni
mwangu bado yuko mtoto mmoja Yahya” wale watu walidhania ati
maneno ya kigonjwa. Kumbe ni ya kizima. Kwani alipona katika
ule ugonjwa, na alimzaa huyo Yahya kama alivyosema. Mtoto
huyo alimpata kwa Suria wake Halima. Mtoto huyo ndiye
aliyekuwa kitinda-Mimba.
xviii Wasia wake juu ya mwanawe, Abdul-Razak.
1. Kumcha Mungu.
2. Kumtii Mungu.
3. Kufuata sharia
4. Kuhifadhi mipaka ya Mungu
5. Kuwatunza na kuwarehemu mafukara
6. Kuwatukuza Masheikh
7. Kuishi na ndugu kwa wema.
8. Kuacha kugombana ila kwa mambo ya Dini ikiwa
inavunjwa.
9. Kutomtegemea mtu kwa kumfanyia kazi zake.
xvii. Karama za Seyyid Abdul Qadir.
(maana ya karama). Karama ni mambo ya ajabu yenye kudhibiti kwa Mawalii.
Ama mambo kama hayo yanapotokana na Mitume huitwa
„Miujiza‟. 13.
Kwa hakika Seyyid Abdul Qadir alikuwa na karama nyingi mno.
Karama zilikuwa ni dalili za kuonyesha kama alikuwa ni Walii. Na
kila zikizidi ni ishara au ni dalili ya kuonyesha utukufu wa daraja
yake kwa Mwenyezi Mungu.
Kila Muridi wa Seyyid Abdul Qadir, ajue kama
amebahatika mno. Kwani Muridi wake hafi ila awe ametubia, kwa
Mungu, Na huko Ahera hatoingia Motoni.
Mwenyezi Mungu atudumishie mapenzi yetu kwa Seyyid
Abdul Qadir hasa, na Mawalii wengine kwa jumla.Tena Mwenyezi
Mungu atuepushe na madhambi makubwa na madogo pia.
Amin! Amin! Amin!
Hizi ni baadhi ya katika karama zake:
Kwenda mbinguni 1. Hekaya:-
Seyyid Abdul Qadir alikwenda Mbinguni, si kwa kiwili
wili na roho, bali ni kwa roho tu. Huko ni kusema alikwenda
Miiraji. Naye alisimama mahala pale pale „Kaaba kawsayn‟
ambapo alisimama Mtume wakati alipokwenda Miiraji, Huko
alimwona Seyyidna Israil, aliiona Lawhil-Mahfudh na Kursy, Si
tu; bali aliiona mpaka Nuru ya Mwenyezi Mungu (Jalla -Jalaluhu).
Wakati alipofika hapo “Kaaba Kawsayni” alipewa amri ya
kusimama na akaambiwa “Njoo, usiogope. Tumeyakunja mapazia
yetu. Hebu inama unywe upate kuniona.
“Neema iliyoje, mtu kuiona Nuru ya Mwenyezi Mungu”.
14.
Kuwasalisha Mawalii hewani:
2. Hekaya:-
Siku moja Seyyid Abdul Qadir alikuwa akitafutwa na
Masheikh wa Baghdad wa Twariqa ya Fawqany. Waliambiwa
kama amekwenda upande wa Mto Tigris. Huko walimwona
anakwenda juu ya maji na huku samaki wa mle mtoni
wanamwendea makundi makundi wakimtolea salam na wakimbusu
mkono wake kwa mboni za macho yao.
Mara tu waliponyanyua macho yao juu waliliona zulia
kubwa rangi ya kijani lililopambwa kwa dhahabu na fedha yenye
kung‟aa. Mtu yeyote akiliangalia atadhania kama labda ni lile zulia
la Nabii Suleiman. Na pale juu ya zulia palikuwa na kitabu
kielezacho utukufu wa Sayyid Abdul Qadir. (Q.s.a).
Ulipoingia wakati wa Adhuhuri kiasi cha saa 6.30; wale
Masheikh wa Baghdad waliwaona Mawalii wengi sana
wamefuatana na wakubwa wao wanakwenda kwenye zulia. Na
pale penye zulia walikuwa wamekaa “Rijalul – ghayb” (Mawalii)
na mkubwa wao yuko mbele. Ulipofika wakati wa kusali, yule mtu
aliyekaa mbele; alikimu Sala na walisimama Mawalii wote huku
wakitazamana nani atakayesalisha. Mara alipita mbele Seyyid
Abdul Qadir kusalisha. Aliwasalisha wale Mawalii pamoja na
mkubwa wao, pamoja na Masheikh wa Baghdad na mkubwa wao.
Baada ya kusali Seyyid Abdul Qadir alinyanyua mikono yake juu
kuomba. Aliomba hivi:- “Ewe Mola Mtukufu, ninakuomba
asife Murid wangu mwanamume au mwanamke mwenye
kunipenda ila awe ametubia kwa Mola wake”. Baada ya
kuomba, walisikia Malaika wakiitikia “Amiin”. Na walisikia sauti
isemayo:
“Furahi, hakika nimeikubali dua yako”.
Hakika Mungu ndiye Mtukufu, na humpa utukufu yeyote
amtakaye. Heri iliyoje ya kumwomba Mungu na akakujibu papo
kwa papo.
15.
Kumbusu mtume mkono wake. 3. Hekaya:
Seyyid Abdul Qadir alipokwenda Madina kumzuru Mtume
(Saw) muda wa siku 40 alisimama mbele ya kaburi. Ilipotimia siku
ya 40 alimwomba autoe mkono wake nje (kutoka kaburini) ili
aubusu. Pale pale Mtume (Saw) aliutoa mkono wake na Seyyid
Abdul Qadir aliushika na kuubusu. Tena alijiwekea juu ya kichwa
chake. Alhamdulillah, utukufu ulioje wa karama.
Kukutana na Mtume kwenye membari. 4. Hekaya:- Siku moja Seyyid Abdul Qadir alisimama kwenye
membari kutoa waadhi. Mara akashuka na akasimama kimya
kitambo hivi kwa adabu na heshima. Baadaye akasimama na
akatoa waadhi.
Mara alipokwisha kutoa waadhi, watu walimwuliza
yaliyomtokea. Alijibu ya kuwa wakati ule Mtume alikuja pale na
akampisha pale alipokaa. Na alipokuwa anaondoka alimwambia
asimame na atoe waadhi alioukusudia.
Kufuturu nyumba 70. 5. Hekaya:-
Siku moja Seyyid Abdul Qadir alipewa taarifa na watu 70
mablimbali, akafuturu kwao. Ulipofika wakati wa kufuturu, kila
mtu alifurahi kumwona Seyyid Abdul Qadir kuhudhuria kwake.
Habari hiyo ilitapakaa Baghdad nzima. Lakini mmoja katika
watumishi wake alikua akikanya kama
16.
si kweli, kwa sababu yeye alimwona kakaa juu ya takia lake wala
hakutoka. Mwisho mwenyewe SEyyid Abdul Qadir
aliyathibitisha maneno wayasemayo watu kuwa ni kweli.
Alimwambia yule mtumishi wake, “Ni kweli nimekwenda kufuturu
kwa watu 70. mmoja mmoja”.
Kumfufua maiti aliyekwisha kuoza
6. Hekaya:-
Siku moja Seyyid Abdul Qadir alipita katika kijiji, na
aliwakuta watu wawili wanashindana. Mmoja kati ya hao alikuwa
Mwislam na wa Pili alikuwa Mkristo. Seyyid Abdul Qadir
aliwauliza sababu ya kushindana kwao. Yule Mwislam alijibu
“Huyu Mkristo eti anasema kuwa Mtume wao ni bora kuliko
Mtume wetu. Na mimi nasema kuwa Mtume wetu ndiye bora
zaidi”. Seyyid Abdul Qadir alimwuliza yule Mkristo. “Dalili gani
uliyonayo inaonyesha kuwa Nabii Isa ni bora kuliko Nabii
Muhammad (Saw)?” Yule Mkristo alijibu, “ Mtume wetu alikuwa
akifufua maiti.” Tena Seyyid Abdul Qadir alimwambia Mkristo.
“Mimi vilevile nafufua maiti wala si mtume, bali ni mfuasi wake
tu. “Tena Seyyid Abdul Qadir. alimuliza Mkirsto, “Je nikimfufua
maiti utamwamini Nabii Muhammad?” “ Ndiyo, alisema Mkristo.
Tena alisema Seyyid Abdul Qadir alimwambia yule Mkristo,
“Nionyeshe kaburi la mtu aliyekufa zamani.”
Yule Mkristo alifuatana na Seyyid Abdul Qadir na yule
kijana kwenda kwenye kaburi ambalo mwenyewe keshaoza
zamani. Walipofika pale Seyyid Abdul Qadir alimuliza yule
Mkristo “Mtume wenu alikuwa akiwafufua maiti wenu kwa
maneneo gani?” Yule Mkristo alisema, “Alikuwa akimsemeza
maiti kwa kumwambia asimame kwa idhini ya Mungu. Seyyid
Abdul Qadir alimwambia Mkristo
“Mimi nitamfufua kwa idhini yangu” Mara baada ya kusema
17.
Vile, Seyyid Abdul Qadir alimwambia maiti “Simama kwa idhini
yangu”. Saa ile ile alitoka hali ya kuwa yu hai. Yule Mkirsto
kuona vile basi hakusita ila alitoa shabaha mbiombio, na
kumwamini Nabii Muhammad (Saw) mbele ya Seyyid Abdul
Qadir (k.s.a).
Haramia kumgeuza kuwa kutbu:
7. Hekaya:-
Seyyid Abdul Qadir alipokuwa anarudi Madina kwenda
Baghdad, alikumbana na haramia njiani akimngojea mtu ye yote
apitae amnyang‟anye vitu alivyokuwa navyo. Seyyid Abdul Qadir
alipofika pale alimwuliza yule mtu, “Nani wewe?” Yule mtu
alisema kuwa yeye ni haramia. Pale pale Seyyid Abdul Qadir
alikashfiwa na aliona jina lake ni miongoni mwa watu waovu.
Lakini yule mwizi ilimpitia katika roho yake na akawaza kuwa
asiwe huyu ndiye Seyyid Abdul Qadir. Mara tu alivyofikiri vile na
Seyyid Abdul Qadir alimwambia, “Mimi ndiye Abdul Qadir.” Yule
mtu aliposikia vile mara alianguka chini ya miguu ya Seyyid Abdul
Qadir na akasema, “Ewe Bwana wangu, Abdul Qadir kipenzi cha
Mungu.” Muda ule ule Seyyid Abdul Qadir alisikia akiambiwa,
“Ewe Ghawth Mtukufu, mfundishe huyo mwizi njia ya haki”. Tena
Seyyid Abdul Qadir alimfundisha njia ya haki yule mwizi na
mwishoni alikuwa ni mmoja katika Makutbu (Mawalii).
Kusilimu kafiri kwa kuona karama za seyyid
Abdul Qadir. 18.
8. Hekaya:- Mtu mmoja alitamani kwenda kumzuru Seyyid Abdul
Qadir, kwa wingi wa sifa zake anazozisikia. Pindi alipofika
Baghdad, alipita mahali ambapo, walikuwapo farasi 40 wakila
majani pasina kuchungwa. Farasi hao walikua wake Seyyid Abdul
Qadir. Alipozidi kuwaangalia aliwaona wanayo minyororo ya
dhahabu na fedha na matandiko yao ni ya hariri. Basi ikamjia fikra,
“Ala! Vipi Walii mkubwa kama huyu ashughulikie mambo kama
haya ya kilimwengu? Haya niliyoyaona kwake hata wafalme
hawana.”
Yule mgeni alipata maradhi makubwa sana kabla ya kufika
alikokusudia. Kwa hiyo ilimbidi afikie nyumba nyingine badala ya
nyumba ya Seyyid Abdul Qadir. Madaktari wengi walikwenda
kumwangalia kwa kutaka kumtibu.
Mwisho alikwenda Daktari mmoja wa Kinasara ambaye
alisema kama mgonjwa yule dawa yake ni maini ya Farasi wenye
sifa kadha. Watu walishughulika sana kuwatafuta. Lakini
aliyekuwa na Farasi hao ni Seyyid Abdul Qadir tu. Siku ya pli watu
walimwendea Seyyid Abdul Qadir kumwomba. Naye aliwapa bure
farasi mmoja na kunywa dawa nyingine, Yule mgonjwa alipata
nafuu kidogo. Kuona vile, watu walizidi kumwendea na
kumwomba tena na waliendelea mpaka farasi wote 40 wakesha.
Baada ya kupoa, yule mgeni alimuaga mwenyeji wake na
akaenda kumzuru Seyyid Abdul Qadir na kumshukuru kwa wema
aliomfanyia hata akapata nafuu. Seyyid Abdul Qadir alimwambia
yule mgeni “Ewe kijana, hao farasi mimi niliwanunua kwa sababu
yako wewe; kwa kuona unayo mapenzi makubwa juu yangu. Na
ulipotia azma ya kuja kunizuru mimi nilijua kama utaumwa na
dawa yako ni maini ya farasi. Lakini wewe pale ulipopita karibu
yao na ukawaona, roho yako iliharibika na ukaleta fikra mbaya juu
yangu.” Tena yule kijana alimwomba msamaha na kumtaka radhi
kwa tukio hilo.
19.
Seyyid Abdbul Qadir alimwita yule Daktari Mnasara akampa ile
minyororo ya dhahabu pamoja na yale matandiko ya hariri. Pale
yule Mnasara alisilimu mbele ya Sheikh Seyyid Abdul Qadir kwa
kuona mambo ya siri na karama zake.
Kufuturu chakula cha peponi:
9. Hekaya:-
Seyyid Abdul Qadir alikaa Riadha siku 40 kwa kufanya
Ibada. Siku zote hizo alikuwa ndani ya Siami (funga). Ilimpitia
rohoni mwake kutokufuturu kitu chochote isipokuwa maji mpaka
Mwenyezi Mungu amteremshie chakula cha peponi.
Ilipofika siku ya 38, aliona sakafu ya nyumba inapasuka na
alimwona mtu mwenye birika ya dhahabu katika mkono mmoja na
katika mkono wa pili alikuwa amechukua sahani ya fedha yenye
matunda. Tena hivyo vitu aliviweka mbele ya Seyyid Abdul Qadir.
Seyyid Abdul Qadir aliuliza, “Vitu gani hivi?” Yule
mtumishi alijibu, “Hivyo ni vyakula nimepewa nikuletee.” Seyyid
Abdul Qadir alisema: “Mtume amekataza kulia vyombo vya
dhahabu na fedha. Viondoe hivyo vitu“. Yule Rohani alitoka mbio
na vyombo vyake. Lakini ulipofika wakati wa kufuturu, alishuka
Malaika na sahani iliyojaaa chakula. Yule Malaika alisema: “Ewe
Ghawthil-A`adham, hii ni dhifa yako inayotoka kwa Mwenyezi
Mungu. Seyyid Abdbul Qadir alipokea kile chakula akala yeye
pamoja na wengi wa marafiki zake. Na Mwenyezi Mungu
humruzuku amtakae pasina kudhani kama ataipata riziki hiyo kwa
muda huo.
20.
Mtoto wa kike kugeuka mwanaume.
10.Hekaya:-
Mtu mmoja alimwendea Seyyid Abdul Qadir kumtaka
amuombee dua ili apate mtoto mwanamme. Ghawth alijibu,
“Nimeshakuombea kwa Mungu na atakupa huyo umtakaye”. Yule
Bwana alimpata mtoto, lakini alikuwa mwanamke. Kwa hivyo
alimchukua mpaka kwa Sheikh na kumwambia, “Mimi nilimtaka
mtoto wa kiume, si wa kike”. Seyyid Abdul Qadir alisema: “Basi
mfunike nguo na umrudishe nyumbani, utaona yatakayotokea“.
Mara tu alipofika nyumbani alimwona yule mtoto wa kike
amegeuka kuwa mtoto wa kiume. Kama alivyotaka hasa.
Tajiri kuwaona ngamia wake waliopotea:
11. Hekaya:-
Siku moja Tajiri mmoja alikuwa akisubiri msafara ili
afuatane nao kwenda kufamya biashara. Alikuwa na ngamia 6
ambao amewatwisha magunia ya sukari.
Walipofika katikati ya njia. Ngamia wake walipotea pamoja
na mizigo yao. Aliwatafuta sana, lakini hakuwaona. Basi akapiga
ukelele, “Ewe Seyyid Abdul Qadir, ngamia wangu wamepotea
pamoja na mizigo yao”. Kutazama mbele yake alimwona mtu
amevaa nguo nyeupe anampungia mkono, Alipokwenda kule
hakumwona yule mtu bali aliwaona wale ngamia wake pamoja na
mizigo yao.
Ndege kusikiliza maneno: 21.
12. Hekaya:-
Siku moja alikaa Seyyid Abdul Qadir, anazungumza. Basi
akasema: “Lau kama Mwenyezi Mungu angetaka kumleta Ndege
rangi ya kijani kusikilza maneno yangu, basi angekuja”. Baada ya
kumaliza kusema hivi, mara alitokea ndege mzuri wa rangi ile ile
ya kijani. Aliingia ndani ya mkono wa kanzu yake kusikiliza
maneno wala hakonekana tena mahala alikokwenda.
Kukatika ndege vipande vipande:
13. Hekaya:-
Siku moja Seyyid Andul Qadir alikuwa akizungumza, Mara
akaja ndege mzuri wa rangi ya kijani akatua mbele yake ili
kusikiliza maneno yake. Seyyid Abdul Qadir akasma, “Lau
ningemwambia huyu ndege kufa na kukatika vipande vipande basi
angalikufa.” Basi pale pale alianguka na akakatika vipande.
Kuhujumiwa simba mbele ya banda la farasi
14. Hekaya:-
Alikuwapo Walii mmoja jina lake Sheikh Ahmad
Zamdah. Sheikh Ahmad alikuwa akipanda simba na kutembea
naye anapokwenda kwa Mawalii wengine. Pale anapofika humtaka
mwenyeji wake ampe Ng‟ombe mmoja, yaani chakula cha simba
wake. Siku moja yule Sheikh Ahmad alifika Baghdad na akaenda
kwa Seyyid Abdul Qadir.
22.
Basi akamwambia: “Mimi ninayo desturi, pahala ninapofika
hupewa ng‟ombe na kumpa Simba wangu ale, Sasa unasemaje?”
“Nitampa ng‟ombe anayevuta maji”. Alisema Seyyid Abdul Qadir.
Alipokuwa anakwenda kwenye ng‟ombe alipitia pale penye
banda la Farasi wa Ghawth. Pale alikaa mbwa mmoja na
mwanawe. Alipopita Sheikh Ahmad walimfuata. Yule mbwa
alimweka pale alipokaa simba. Mara simba alitaka kumshambulia
mbwa wa Seyyid Abdul Qadir, lakini bahati mbaya mbwa
alimhujumu vikali simba yule na alimwua. Tena Sheikh Ahmad
alirudi kwa Seyyid Addul Qadir na kumtaka radhi kwa
yaliyotokea. Vile vile alitubia kwa Mwenyezi Mungu.
Kifo cha ndege mia:
15. Hekaya:- Ilitokea siku moja Seyyid Abdul Qadir alikaa pahala
akifanya Ibada zake. Juu kikapita kikundi kikubwa cha Ndege mia.
Walipomwona Seyyid Abdul Qadir wote walishuka wakatua na
wakamzunguka. Pale walipokaa wakawa wanafanya kelele. Seyyid
Abdul Qadir akatazama juu akasema, “Ewe Mola hawa ndege
wananishughulisha hapa”. Ndege wote walikufa saa ile ile.
Alipowaona wote ni maiti alisema “Ewe Mola unajua sababu ya
kifo chao”. Kusema vile mara wote walifufuka na kwenda zao.
Kujitenga kwenye magofu ya baghdad:
16. Hekaya:-
Seyyid Abdul Qadir alijitenga kwenye magofu kwa muda
23.
usiopungua miaka 25 akifanya Ibada. Siku moja alisikia sauti
iliyomwambia, “Rudi Mjini watu wanakuhitaji kwa manufaa ya
Akhera“. Alisema Seyyid Abdul Qadir:- "Mimi nimekuja huku
kufanya Ibaada kwa kutafuta salama ya Dini yangu, na kuepuka na
fitina za Baghdad“. Kusikia vile tena akaambiwa.“Rudi na
utasalimika Mungu akipenda“. Kusikia vile Seyyid Abdul Qadir
alirudi huku moyo wake umejaa siri za Mungu.
Maneno kujitokeza:
17. Hekaya:-
Kila alipokuwa akikaa Ghawth-A`adham walikuwa
hawaondoki Mawalii – Iwapo amekaa kimya basi maneno hutaka
kujitokeza na kufika mpaka kwenye koo. Basi yakifika hapo hua
hawezi tena kunyamaza bali huwapa siri katika elimu ya “Hakika”.
Unyayo wangu uko shingoni mwa kila walii:
17. Hekaya:-
Maneno haya alipewa idhini na Mtume kuyasema. Na siku
alipoyatamka Baghdad, Mawalii wote wa Ulimwengu mzima
waliyasikia na kila mmoja aliinamisha shingo yake kwa kuridhia
maneno yaliyotamkwa.
Yasemekana walii mmoja wa Damask, Sheikh Rasalam
alisema: “Ewe Mwenyezi Mungu, ninakushuhudiza wewe na
Malaika wako kuwa nimeyasikia maneno ya Bwana
24.
wa Mawalii na nimeyakaribisha. Tena akanyoosha shingo yake
kuonyesha kuwa ameridhia.
Nuru katika kidole chake.
18.Hekaya:-
Siku moja Seyyid Abdbul Qadir aliondoka usiku pamoja
na Masheikh watatu kwenda kuzuru kaburi la Imam Aba Hanifa,
Usiku huo ulikuwa na giza kubwa sana. Hapa na hapo huwezi
kupaona. Lakini Seyyid Abdul Qadir alipofika penye jiwe au mti
aliashiria kwa kidole chake. Na wakati huo lile jiwe au mti
hung‟ara sana mfano wa mbalamwezi kali. Waliendelea na hali
hiyo mpaka wakafika walikotaka na wakafanya waliyokusudia.
Wakati wa kurudi Seyyid Abdul Qadir alikuwa akiashiria
kwa kidole vile vile kwenye hatari na kutoka mwanga mkali
kwenye kile kitu. Tena walipofika
nyumbani kwa Seyyid Abdul Qadir, wale Masheikh waliaga na
wakaenda zao.
Mifupa kuigeuza kuku aliye hai:
19. Hekaya:-
Bibi mmoja alimpeleka mwanawe kwa Seyyid Abdul
Qadir kusomeshwa elimu. Mtoto huyo aliwekwa mahala maalum
kazi yake ni kufanya ibada tu kabla ya kusomeshwa Ilmu.
Siku moja mama yake yule mtoto kuja kumkagua. Lakini
hali alivyomwona nayo mwanawe kidogo haikumpendeza.
Alikuwa amedhoofu sana. Alipita ndani ili
25.
aonane na Seyyid Abduil Qadir. Kwa uchungu wa mwanawe
ilimtoka subra na akawa anamwandama Seyyid Abdul Qadir kwa
maneno. Alisema: “Ewe Ghawthil Aadham, unakula kuku na
unamwacha mwanangu anakula vipande vya mikate ya shairi hata
amekuwa mwembamba kama uzi?“ Seyyid Abdul Qadir hakujibu
chochote isipokuwa aliikusanya ile mifupa na akasema mbele ya
yule mwanamke: “Ewe kuku simama kwa idhini ya Mungu
mwenye kuhusisha mifupa iliyochakaa,” Mara tu baada ya kusema
vile mifupa iligeuka kuku ambaye alisimama mbele ya yule
mwanamke.
Naam hapo Seyyid Abdul Qadir ndipo alipomneneza yule
mwanamke kwa kusema: “Ninapenda mwanao aweze kama haya,
kwa kupata daraja kama hili, anaweza kula chakula chochote
akitakacho mwenyewe”. Mwisho yule bibi alimtaka radhi Seyyid
Abdulm Qadir na akamwambia, “Ewe Seyyid Abdul Qadir,
yaliyonipelekea kusema hayo ni uchungu wa mwanangu tu. Na
tangu sasa hivi nakupa uhuru ufanye utakavyo juu ya mtoto huyo.”
Kushiba kwa kufyonza kidole:
20. Hekaya:-
Sheikh Muhammad Shawry Sabty aliondoka Misri
kwenda kumzuru Seyyid Abdul Qadir. Alikaa huko kwa siku
nyingi. Sheikh Muhammad alipofunga safari ya kwenda nyumbani,
alipewa wosia na Seyyid Abdul Qadir. Wosia wenyewe ni huu:
"Usitake haja kwa mtu yeyote.“ Baada ya kuusiwa alipewa zawadi
na vyakula vya kula anapokuwa safarini. Lakini kabla ya kuondoka Seyyid Abdul Qadir alikitia
kidole chake ndani ya kinywa cha Sheikh Muhammad na
akamwambia akifyonze. Baada ya kufanya hivyo tena
26.
akashika njia akaenda zake. Jambo la kustaajabisha ni kuona kuwa
Sheikh Muhammad hakushikwa na njaa wala kiu mpaka akafika
kwake Misri. Na alipokitizama kile chakula alikiona kimeongezeka
wala hakikuharika. Baada ya kupumzika alikula chakula hicho
pamoja na watoto wake na Watu waliokuja kuonana naye.
Kifo cha seyyid Abdul Qadir (Qsa):
Seyyid Abdul Qadir alikufa siku ya Ijumaa, Mfungo saba,
mwaka 561 (A.H). Alizikwa kwenye chuo chake
“ Babuluzji”. Kafa na umri wa miaka 91. Watu wengi walimimminika mazikoni kwake, utasema
labda wanakwenda Arafa kwa vile watu walivyokuwa wengi
ilionekana ni bora zaidi awekwe ili azikwe usiku. Pamoja na hayo
hakubakia mtu yeyote katika Baghdad ila alihudhuria Maziko
yake. Katika majia, masoko na majumba yote yalijaa watu.
Seyyid Abdul Qadir alisalishwa na mwanawe Sheikh
Abdul Wahab na alisaliwa na watu wengi mno; Miongoni mwao
ni wanawe, wanfunzi wake na marafiki zake. Kifo chake Seyyid
Abdul Qadir kilitokea katika zama za Imam Yusufu bin
Muktafa. Wale watu waliokosa kumsalia Sheikh, walipewa nafasi
ya kumsalia wakati wa mchana ulipofunguliwa mlango.
27.
Jihad:
Kwa yeyote anayetaka kutabaruk katika Jihad hii ya
kuchangia katika kuchapisha vitabu vya Dhikri, Tawwasul n.k.
Kwa kuwa hiki ni toleo la kwanza, tunategemea kutoa matoleo
zaidi. Awasiliane na mtunzi wa kitabu hiki moja kwa moja kupitia
simu namba: 0755 547 771 au aitie michango yake kwenye
Account ya Benk:
NMB – CLOCK TOWER A/C. 4082300209. ARUSHA.
TWARIQATUL QADIRIA ARRAZZIKIA JAILANIA.
MAKAO MAKUU
ZAWIA KUU.
P. O. BOX 8105
ARUSHA.
Wabillahit Tawfiq.
28.
KIMETOLEWA NA:-
Mtungaji:-
Swahib Sujjada:
Al Habib Sheikh Salim Bin Mbarak.
(Dar-wesh – Mti mkavu)
P.O. Box 8105,
Zawia kuu.
Arusha - Tanzania.
(E.A)
Top Related