Wanawake Katika Kazi Ya Mungu -...

18
Wanawake katika Kazi ya Mungu Diocese-Based Leadership Training Program Mennonite Churches of East Africa (KMC/KMT) Joseph and Gloria Bontrager Theological Education Coordinators, 2015 ©2015 Gloria Bontrager

Transcript of Wanawake Katika Kazi Ya Mungu -...

Wanawake katika Kazi ya Mungu

Diocese-Based Leadership Training Program Mennonite Churches of East Africa (KMC/KMT)

Joseph and Gloria Bontrager Theological Education Coordinators, 2015

©2015 Gloria Bontrager

2

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

Yaliyomo

Soma la 1 Utangulizi – Wanawake Katika Kazi ya Mungu 3

Somo la 2 Wanawake katika Kanisa la Kikristo 5

Somo la 3 Washiriki katika Mwili wa Kristo 6

Somo la 4 Wanawake na Karama Zao 7

Somo la 5 Kazi za Wanawake Kanisani 8

Somo la 6 Changamoto katika Vikundi vya Ushirika vya Wanawake 10

Somo la 7 Makusudi na Utekelezaji 12

Somo la 8 Mahitaji ya Kimwili na ya Kiroho 13

Somo la 9 Utamaduni, Miiko, Maadili na Fedha 15

Somo la 10 Mafunzo Shirikishi – Kusaidia watu Wajifunze 17

Nukuu 18

Madhumuni ya Somo

1. Kuwasaidia wanawake kutambua nafasi yao katika kufanya kazi ya Ufalme wa Mungu.

2. Kulihimiza kanisa katika kutumia vipaji vya wanawake kanisani na ndani ya jamii.

3. Kutoa changamoto kwa vikundi vya ushirika vya wanawake viweze kupanua wigo wa

maono kwa kuiendea jamii wanamoishi.

Mwandishi: Gloria Bontrager Watafsiri: Rhoda Mtoka, Mch. Emmanuel Matuntera, Mch. Joseph Bontrager

3

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

Soma la 1 Utangulizi – Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Soma Mwanzo 12:1-5 Agano la Mungu na Abraham lilimhusu Sara naye. (Nitakubariki na kupitia kwako mataifa yote yatabarikiwa) Sara mke mwaminifu wa Abrahamu alifuatana naye na hatimaye kuwa mama wa taifa kufuatia ahadi ya Mungu (Mwanzo 12:5; I Petro 3:5-6; Waebrania 11:11). Hivyo, Mungu anataka kuwatumia wanawake na wanaume kuendeleza kazi yake ulimwenguni. Kabla ya misingi ya dunia kuwepo, Mungu alituchagua na kutufanya wanawe na warithi kupitia Yesu Kristo. Tumepokea wingi wa neema yake na twatumwa kuonyesha sifa ya utukufuu wake kwa wengine. Mpango wa Mungu wa kukomboa watu wote na kurudisha tena mahusiano yake na mwanadamu unatuhusu na sisi wanawe wote.

Katika Agano la Kale wanawake waliitwa na Mungu kutenda kazi yake ulimwenguni:

Mariamu alitumia kipaji cha uongozi akishirikiana na kaka zake Haruni na Musa katika kuwaongoza Waisraeli kutoka Misri (Kutoka 15:20, Micah 6:4).

Mama yake Musa (Jochabed) alimwamini Mungu na kuamua kuasi amri ya mfalme. Tendo la kumwokoa mwanawe lilimtayarisha mtu, ambaye alitumiwa na Mungu kuwatoa Waisraeli kutoka Misri ingawa alikulia katika nyumba ya kifalme (Kutoka 2:1-10; Waebrania 11:23).

Debora alikuwa nabii mke na mwamuzi katika Israeli alienda vitani pamoja na Baraka kwa maelekezo ya Mungu (Waamuzi 4:4-10). Kupitia uongozi wake, Mungu aliwapa Waisraeli ushindi na pumziko la kutokuwa na vita kwa miaka 40 (Waamuzi 5:7, 31).

Esta ni mwanamke aliyetumika kuwaokoa watu wa Mungu wakati mfalme alitaka kuwaangamiza. Ingawaje alikuwa ni mgeni katika nchi, tena ni mwanamke, alitumia nafasi ya umalkia kwa ujasiri. Kwa maombi ya watu wa Mungu alimwamini Mungu aliyempa hekima.

Wakati wa Yesu, wanawake walitumiwa na Mungu:

Mariamu, mama wa Yesu, na Elizabeti, mama wa Yohana Mbatizaji, ambao walionyesha maisha ya utakatifu, walichaguliwa kuwazaa mtangulizi wa Masihi na Masihi mwenyewe. (Luka 1:28-38)

Baadhi ya wanawake walioponywa na Yesu walikuwa ni wafuasi wake, na walimhudumia Yesu na wanafunzi wake kila siku wakitumia mali zao (Luka 8:2-3). Hao wanawake walikuwa ni pamoja na Mariamu Magdalene, Yoana na Susana. Walishuhudia maisha na huduma ya Yesu, na pia kifo na kufufuka kwake.

Mwanamke Msamaria akawa mwinjilisti aliwawezesha wanakijiji wengi kumfahamu Yesu. Yesu hakujali kabila lake wala maisha yake alikubali kuongea naye. (Yohanna 4:39-42.)

Yesu aliinua hadhi ya wanawaake kwa jinsi alivyowakubali wafanye huduma naye. Yesu alitaja mifano ya wanawake wa imani katika mafundisho yake. Alijenga daraja la usawa kati ya wanaume na wanawake.

Wanawake wa Biblia walimtumikia Mungu katika maisha yao ya kila siku, bila kujali hali ya mazingira ilivyowakabili. Walimwamini Mungu wakati wa mahitaji. Walimheshimu Mungu na kumtumikia katika maisha yao ya utakatifu, utiifu na kukubali mapenzi yake. Kupitia hawa wanawake, Mungu alionyesha nguvu na utukufu wake za ajabu.

4

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

Maswali ya Majadiliano

1. Je, lengo la Mungu kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu lilikuwa ni nini? (Waefeso 1:3-4)

2. Chagua mfano mmoja wa mwanamke wa Agano la Kale ambaye ni changamoto kwako. Jadili kwa nini umemchagua.

3. Taja mfano wa mwanamke aliyetumiwa na Mungu katika tendo dogo tu, lakini akawa ni baraka kwa wengi kwa sababu alimwamini Mungu.

4. Orodhesha sifa muhimu zinazoonyesha tabia za wanawake wa Biblia.

Je, wanawake wa leo waweza kuwa na tabia hizo ili kumtumikia Mungu vizuri?

5. Taja uwezo au kipaji ulicho nacho mwanamke ambacho Mungu anaweza kukitumia.

5

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

Soma la 2 Wanawake katika Kanisa la Kikristo

Wanawake walikuwepo wakati Yesu alipotoa Agizo Kuu kwa wanafunzi wake, “Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi” (Mathayo 28:19-20).

Wanawake walikuwepo wakisali pamoja na wanafunzi, wakisubiri kuja kwa Roho Mtakatifu (Matendo 1:14).

Soma Matendo 2:42-47.

Waumini wa kwanza walianza kuona maajabu ya Mungu yaliyofanyika ndani ya kanisa. Walizoea kukutana kila siku katika ushirika, kwa fundisho la mitume, kuumega mkate, na kusali. Ili kukidhi mahitaji, waliuza mali zao na vitu vyao na kuvileta kanisani, na kuwagawia watu wote kulingana na mahitaji. Mungu alibariki jambo hili, na kupitia hali hii, watu wengi waliokolewa na kuwa wa imani. Katika kanisa la asili wanawake walihusika na huduma za kanisa wakisaidiana na mitume.

Kikundi cha wanawake cha maombi ndicho kiliwapokea wamisionari wa kwanza (Matendo 16:13) na kuwa waanzilishi wa kanisa la Filipi (Wafilipi 4:1-3).

Lidia, mwanamke mfanyabiashara katika Filipi, aliwakarimu Paulo na Sila, na baadaye aliwahudumia walipotoka gerezani (Matendo 16:12-15, 40).

Prisila aliyefanya pamoja na mumewe, Akila, walimsaidia Apolo kuielewa njia ya Mungu kwa usahihi zaidi (Matendo 18:18, 24-26).

Mabinti wa Filipo walitabiri (Matendo 21:8-9).

Paulo alimtaja Fibi kama mhudumu aliyesafiri akizunguka kati ya makanisa akiwa mwangalizi (Warumi 16:2).

Paulo anatuma salaamu zake kwa Mariamu, “aliyejitaabisha sana kwa ajili yenu” (Warumi 16:6).

Yunia, jamaa wa kike wa Paulo, aliyefungwa pamoja na Paulo, na “ni maarufu miongoni mwa mitume” (Warumi 16:7).

Maswali ya Majadiliano

1. Elezea kwa maneno yako, jinsi kanisa la asili lilivyoweza kuona mahitaji ya wengine na walijitoa kushirikishana mali na vitu kwa ajili yao.

2. Je, kuna mahitagi gani kati mwetu? Tunawezaje kusaidiana? (Kum. 15:11; Warumi 12:13).

3. Je, yalikuwaje matokeo ya kushirikisha mali yao na wenye mahitaji?

4. Je, tunawezaje kutambua zaidi mahitaji yaliyoko kati ya majirani wetu, na kuwa na nia ya kutoa mali ili tusaidie wengine?

5. Je, ilikuwa ni faida gani Paulo kufika katika kikundi cha maombi na cha wanawake hasa?

6. Je, ni mambo gani mengine waliofanya wanawake katika kanisa la asili?

7. Je, unafikiri, ni kwa nini kanisa la asili halikuwatenga wanawake katika ushiriki wa kazi za kanisa?

6

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

Soma la 3 Washiriki katika Mwili wa Kristo

Soma Waefeso 5:23-32.

Waraka wa Paulo kwa Waefeso unafananisha kanisa na mwili wa Kristo, ambapo Kristo ni kichwa. Katika upendo wake anataka kupeleka kanisa takatifu na bila mawaa kwa Mungu . Kama vile mwili ulivyo na viungo vingi tofauti vinahitajiana ili mwili ufanye kazi yake vizuri, hivyo kanisa nalo linahitaji washiriki wote washirikiane ili kujenga mwili (1 Wakorintho 12:12-13; Warumi 12:4-5). Na kwa sababu “tulibatizwa kwa Roho mmoja katika mwili wa Kristo,” sote tunapewa heshima na neema katika mwili (Wagalatia 3:28; 1 Wakorintho 12:13). Hakuna anayeweza kusema kuwa ni bora kuliko mwingine, au muhimu zaidi. Hata kama viungo vingine ni dhaifu au visivyo na heshima katika mwili vinapaswa kuheshimiwa, kulindwa katika madhara. Kama mshiriki mmoja akiumia na asifanye sehemu yake, mwili wote huumia. Mwamini mmoja akifanikiwa, wote hufurahi.

Wanawake kama viungo vya mwili wamepewa kazi na vipawa vya kiroho vinavyofaa kuhudumia kanisa. Wanawake waliagizwa pamoja na wanafunzi wengine ili waende na kufanya watu wote kuwa wanafunzi, na kuwabatiza na kuwafundisha (Mathayo 28:19-20). Kusudi la Yesu ni kutuma wanafunzi wote katika mavuno (Mathayo 9:37).

Yesu alihubiri Ufalme wa Mungu, lakini alivuka taratibu za Wayahudi kwa jinsi alivyotambua na kuwahudumia wanawake sawa na wengine. Akizungumza na Mwanamke Msamaria kisimani (Johana 4), alivunja taratibu zote za nyakati zile. Lakini baada ya mazumgumzo kuisha, mwanamke alifurahi sana na alikwenda kuwaambia wengine juu ya Masihi. Mwanamke mwenye dhambi, lakini aliyebadilishwa, akawa ni mwinjilisti wa kwanza! Yesu hakumwambia, “Hiyo si kazi yako!” bali Yesu alikubali ushuhuda wake na jinsi ulivyowasaidia wengine.

Hata kabla ya misingi ya ulimwengu kuwepo, mpango wa Mungu ulikuwa ni kuwaleta watoto wake wote katika familia moja, ambayo Yesu ndiye jiwe kuu la pembeni. Tunapoungana pamoja, tunakua katika hekalu takatifu na maskani ya Mungu katika Roho (Waefeso 2:19-22). Lakini, kila moja inatubidi tuitoe miili yetu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu ya kumpendeza Mungu (Warumi 12:1). Kujitoa kwetu katika huduma ni namna ya kumwabudu Mungu.

Maswali ya Majadiliano

1. Je, kanisa linafananaje na mwili wa Kristo? Na, je, washiriki wa mwili wa Kristo wanatoaje heshima kwa kichwa chao?

2. Je, kanisa linafanyaje kazi kama mwili?

3. Je, kuna tofauti za umuhimu katika mwili? Je, ziko kazi tofauti za viungo vya mwili?

4. Je, ni lipi muhimu zaidi, ni kazi ya kila mwamini, au ni jinsi gani kazi ya kila mmoja husaidia kazi ya mwili kwa jumla?

5. Ni mifano ipi mingine inayoonyesha jinsi Yesu alivyovunja taratibu za Wayahudi kuhusu wanawake?

6. Je, ni kwa njia zipi wanawake wanaweza kuwa dhabihu iliyo hai kwa Mungu?

7

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

Soma la 4 Wanawake na Karama Zao

Soma Warumi 12:4-8; I Wakorintho 12:1-11. Roho Mtakatifu hutoa karama kwa waumini ili kujenga umoja katika mwili na kuhudumia kanisa.

Kila mshiriki wa mwili wa Kristo amepewa karama (1 Wakorintho 7:7; 12:7).

Paulo alimwonya Timotheo asiache kuitumia karama aliyopewa (I Tim. 4:14).

Karama za aina mbalimbali zimeorodheshwa katika sehemu kadhaa za Biblia. Warumi 12:6-8 inataja unabii, imani, huduma, kufundisha, kuonya, ukarimu, uongozi, rehema, na furaha.

1 Wakorintho 12:4-11 inataja hekima, maarifa, imani, uponyaji, miujiza, unabii, kupambanua roho, kunena kwa lugha, tafsiri ya lugha.

1 Wakorintho 12:27-3 inataja huduma au kazi ndani ya kanisa, mitume, manabii, walimu, viongozi, miujiiza, karama za kuponya, wasaidizi, viongozi, na kunena kwa lugha.

Tukiishatambua karama zetu tulizo nazo, ndipo tutaelewa namna Mungu anavyotaka kututumia kanisani. Ni rahisi wakati mwingine kutambua karama ya mwingine kuliko yako mwenyewe. Pengine tunavutiwa na yale tunayoona jinsi mwingine anavyohudumia kanisa, nasi tunatamani tuweze kubariki wengine. Njia nzuri ya kutambua karama yako ni kujitoa kufanya kazi ndogo ndogo, au kufanya huduma za kubariki wengine kufuatana na uwezo wako. Katika kufanya huduma hizo kwa Bwana, utaweza kuelewa ni huduma zipi zinakuridhisha zaidi. Na pia sikiliza wengine wanavyoizungumzia huduma yako. Wala si kujivuna, bali kuelewa kwa uhakika kuwa, Mungu amekupa karama hiyo kuhudumia wengine.

Kumbuka, mtu anayetoa huduma si lazima apewe sifa au utambulisho maalum kutoka kwa watu. Hakika, ni muhimu sana kutambuliwa na mpaji wa karama hiyo, ambaye ni Mungu. Anafurahi sana unapowabariki wengine, hata katika shughuli za kawaida za kila siku, kupitia karama aliyokupa. Kwa kawaida, wanawake hutafuta kulinda mahusiano, wakionyesha karama za huruma, na malezi, na ukarimu. Kanisa lahitaji karama hizi. Lakini, Roho Mtakatifu hutoa pia karama za kiroho kwa wanawake za kuimarisha kanisa. Wanawake wanazo nguvu sana katika huduma ya maombi, pia kuwatia moyo na kuwashauri wenye mahangaiko. Wanawake huwa wanatafuta ushirikiano na wengine kwa manufaa ya wote, wala si kutumia mamlaka au ukuu wanapowaendea watu. Wanazoea kushirikiana na kushirikishana maisha na kazi zao binafsi bila kuficha, hivyo wengine hujifunza na kufaidika tutokana na hali hiyo. Hivyo wanaweza kuwafundisha wengine na kuwaelekeza.

Maswali ya Majadiliano

1. Je, ni ipi shabaha ya Mungu ya kutoa karama kwa kila mtu kanisani?

2. Je, ni tofauti gani iliyopo kati ya uwezo wa kibinadamu na karama za kiroho?

3. Katika kugawa kazi kanisani, je, tugawe kazi kufuatana na nafasi zilizopo, au kugawa kazi kufuatana na karama za waumini? Eleza jibu lako.

4. Karama nyingine zinaonekana zaidi mbele za watu, kama uponyaji, unabii, au kufundisha. Je, karama hizo ni muhimu zaidi kuliko karama za ukarimu au utoaji?

5. Je, umeweza kutambua karama ya mwingine na kumtia moyo aitumie? Chukua muda kusaidiana kutambua karama zenu na kutiana moyo.

8

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

Soma la 5 Kazi za Wanawake Kanisani

Mara nyingi, kanisa halijahusisha wanawake katika huduma za kanisa kwa kiasi inavyostahili. Tunatakiwa kufikiria upya kazi za wanawake kanisani, ili karama zao walizo nazo ziweze kutumika, kwa manufaa ya kanisa na jamii. Katika kitabu cha Rosalia Oyweka, Kuwaendea Wanawake wa Afrika, anasema “Swala la msingi si wanawake kuchukua mamlaka ndani ya kanisa, bali ni kuwawezesha kutumia karama na vipaji kuendeleza Ufalme wa Mungu pamoja na wanaume.”1

Mila na desturi za dunia wakati mwingine zinashusha hali na heshima ya wanawake kuwa chini ya wanaume. Ila inabidi kanisa lizidi dunia na kuwainua wanawake kuwa sawa na wanume. Biblia inafundisha kuwa, wanawake na wanaume wote waliumbwa katika sura ya Mungu na walipewa karama zinazohitajika kanisani (Mwanzo 1:27; Wagalatia 3:28). Hivyo wana haki sawa na wanaume, siyo kushindana nao bali kufanya kazi ya Mungu pamoja2.

Kazi za wanawake na wanaume katika familia zinaweza kutofautiana, lakini hali hiyo haimpi mmoja mamlaka juu ya mwingine kanisani. Katika mafunzo mengine ya Biblia, mwanamume amepewa kazi ya uongozi na mwanamke kazi ya usaidizi katika ndoa na ndani ya nyumba. Mwanamke anatakiwa kuwa mnyenyekevu ili kudumisha na kuiendesha familia kwa utulivu akishirikiana na mumewe. Hata hivyo, kila mmoja katika kazi yake, anatakiwa kumheshimu mwenzake, kwa sababu wote pamoja ni warithi wa Ufalme wa Mungu (Mwanzo 2:18; 1 Petro 3:7; Waefeso 5:21-22,25).

Katika Agano la Kale wanawake wengine kama Debora na Mariamu waliochaguliwa kushika uongozi katika kazi maalum sambamba na wanaume (Waamuzi 4, Mika 6:4). Walipewa karama fulani zilizotumika kukamilisha malengo ya Mungu. Hata leo hii, wanawake wanaitwa kuimarisha karama zao na kuzitumia katika kazi ikiwa uongozi au kazi nyingine ili kuhudumia kanisa. Agano Jipya nalo limetoa vielelezo vingi vya wanawake waliofanya kazi sambamba na viongozi wanaume katika kanisa la kwanza (Matendo 16:12-15; Warumi 16; Matendo 21:8-9). Kumnyima mwanamke nafasi katika kanisa, kwa sababu tu ni mwanamke, inamaanisha, kanisa linaacha nje uwezo mkubwa wa karama ya kiroho aliyopewa na Mungu, pia kuwanyima sehemu kubwa ya waumini (yaani, wanawake) wasishiriki katika kazi za kanisa. Kutambua na kutumia karama za wanawake ni lazima na muhimu ili kanisa lifanikiwe kikamilifu kama mwili wa Kristo.

Je, tunaweza kueleza vipi maagizo ya Paulo kwa kanisa la Korintho (1 Korintho 14:34-35) na kwa Timotheo (1 Timotheo 2:11-12) kuhusu wanawake kuwa watulivu kanisani? Nyaraka hizo za Agano Jipya ziliandikwa na Paulo ili kuyatia moyo makanisa mapya yalioanzishwa. Makanisani mengi yalipatwa na matatizo kwa sababu maisha yalifuata bado misingi ya utamaduni wao wa nyuma. Hivyo Paulo alishugulikia matatizo yaliyokuwa yamejitokeza, kama vile vurugu katika taratibu za ibada na baadhi ya wanawake kujiingiza kwa namna isivyostahili. Kwa hiyo Paulo alihisi, katika hali hiyo ni vizuri zaidi wanawake wajifunze kusikiliza kimya kuliko kushiriki katika mijadala. Kwa bahati mbaya, kwa miaka mingi mistari hiyo imesisitizwa kwa nguvu na wanaume kanisani, kwa vile wanayo mamlaka kanisani. Wala hawakusoma maneno mengine katika Biblia yanayowaruhusu wanawake kuzungumza, na yanayowatia moyo watumike kufuatana na karama zao.

Huenda tatizo hili limesababishwa na tafsiri na ufafanuzi wa maneno haya kutoka katika lugha ya asili. Mafundisho ya Paulo ni kujifunza katika hali ya utulivu na amani, wala si kumnyima mtu sauti ya kusema. Na anawaonya juu ya utawala kwa nguvu, wala si kumnyima kazi zote za uongozi. Endapo mistari hiyo ingesomwa hivyo, ingeruhusu

9

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

wanawake wenye tabia njema na karama, kuwa washiriki kamili katika kanisa na kuthaminiwa huduma wazitoazo.

Maswali ya Majadiliano

1. Je, ni sahihi, kibiblia, kusema kwamba hadhi ya mwanamke si sawa na ya mwanamume?

2. Katika mawazo yetu kanisani, je, tunaona tofauti gani kati ya huduma na cheo? Kwa jinsi gani mawazo hayo yameleta utata katika uongozi wa kanisa?

3. Je, tabia na mtazamo wa mwanamke uwe ni wa namna gani, anapohudumu kanisani?

4. Je, inastahili mwanamke mwenye karama ya uongozi au aliyekomaa zaidi kiroho, apewe nafasi ya uongozi kanisani?

5. Je, ni katika hali gani mwanamke mwenye uwezo ateuliwe ili kuwekewa mikono?

10

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

Soma la 6 Changamoto katika Vikundi vya Ushirika vya Wanawake

Washiriki wengi wa kanisa ni wanawake na changamoto nyingi katika jamii ya kiafrika yanawahusu. Wanawake wanapokutana kwa maombi na ushirika, wanayo nafasi pekee ya kuwapelekea wenzao mafunzo ya kimsingi juu ya maisha3. Mara nyingi baada ya ushirika, wanawake hawana haraka ya kurudi nyumbani, bali huzungumzia masuala ya maisha yao. Majadiliano hayo hutoa nafasi nzuri kushauriana na kusaidiana kutatua matatizo yao. Mabadiliko mazuri hutokea hapo wanawake wanaposhirikiana kuimarisha jamaa na jamii. Inabidi wanawake wa kanisa kuelewa namna ya kujiletea maisha bora katika jamii zao kwa kutumia rasilimali walizo nazo. Wanawake wenyewe wanao uwezo wa kuhudumia wenzao kanisani au wengine wanaokutana nao nje ya kanisa, hivyo wanaweza kuleta mafanikio makubwa katika kanisa.

Faida ya ushirika wa wanawake inazidi vikundi vingine vinavyokutana. Vikundi vya wanawake vinakaza mahusiano kuliko taratibu, wakiwakaribisha wanawake wa asili na imani tofauti. Ushirika hulenga kuimarisha imani, na ushirikiano huo unawaunganisha kuliko taratibu inayowekwa. Biblia ikiwa msingi wa mafunzo, wanawake hupata nuru juu ya maisha yao na kupokea nguvu ya kufanya mabadiliko katika ya maisha yao (Tito 2:3-5). Kujua habari za wanawake na wanaume katika Biblia, huimarisha imani na kutoa mwongozo kwa maisha. (1 Petro 3:1-6) Wanawake wanapojifunza pamoja wanatambua maisha yao yalivyo na kusaidiana kutatua matatizo. Mafundisho ya Biblia yahusu maisha yote, kama vile afya, malezi na utunzaji wa familia, na utunzaji wa mazingira.

Ziko changamoto nyingine ambazo ushirika hukutana nazo. Changamoto moja ni ile ya kutoamini viongozi wao. Baadhi ya wanawake hasa wa vijijini wapewapo uongozi, baada ya muda mfupi huutumia kwa kujinufaisha wenyewe. Kwa kawaida, vikundi vimejengwa katika miradi midogo ya fedha yenye kusudi la kuboresha maisha yao. Hali hii imeweka msisitizo mkubwa juu ya fedha4. Endapo fedha inawekwa kuwa msingi wa kikundi, huleta matatizo mengi, kama vile, wivu au viongozi kutumia fedha vibaya. Panapotokea kutoaminiana ndani ya kikundi, hutokea ushindani badala ya ushirikiano, na hupunguza uwezo wa kuleta mabadiliko mazuri katika jamii. Inafaa kwamba, badala ya kuwa na vikundi vidogo vya miradi ya fedha, vikundi vya ushirika vinapaswa kupanua wigo ili kuwa na nia ya kuwasaidia wengine kwa kuwajengea uwezo wao binafsi waweze kutatua matatizo yao wenyewe. Pia, kutoaminiana huweza kutokea katika uongozi wa kanisa, ikiwa kikundi kitapata mafanikio na kanisa linahisi shughuli hizo zifanyike chini ya uongozi wake.

Changamoto nyingine iliyoko ni ile ya jinsi ya kujiongoza. Kwa miaka mingi, wanawake wa kanisa wamepewa kazi za huduma na hawakupewa kazi za uongozi, hivyo hawajiamini katika uongozi. Hali hiyo huleta mkanganyiko na uongozi dhaifu. Wanawake wapaswa kutazama mifano mizuri ya uongozi, tena wawe na hekima ya kuwachagua watu walio na uwezo wa kuongoza vema, wala si kufuatana na urafiki au undugu. Wanaume wanapoingilia shughuli za wanawake na kuwaambia jinsi ya kufanya, huongeza matatizo na kuwanyima wanawake udhibiti wa kutoa maamuzi yao wenyewe.5 Wanawake wapewe nafasi kufanya utafiti kuhusu mawazo na mipango yao na kuitekeleza. Wanapaswa kujua namna ya kupata maarifa na vifaa ili kujua hali yao halisi ilivyo na kuishughulikia inavyotakiwa. Wanapaswa kujijengea hali ya kujiamini na ufanisi katika uongozi. Wawe na uwezo wa kupuuzia malalamiko yanayoletwa bila msingi, lakini pia kukubali ushauri utakaowasaidia.

11

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

Maswali ya Majadiliano

1. Jadili tofauti kati ya wanawake kufundisha wanawake na wanaume kufundisha wanawake. Je, ni kwa nini mafunzo yanayotolewa na wanawake kwa wanawake yanafanikiwa kuliko yale ya wanaume kwa wanawake?

2. Taja baadhi ya sababu zinazofanya vikundi vya ushirika kuwa mahali pazuri pa kutoa mafundisho na kujadili masuala ya maisha ili kuleta mabadiliko.

3. Inawezekanaje mafundisho ya Biblia yaweze kuleta mabadiliko katika masuala ya maisha ya kila siku?

4. Je, ni kwa nini fedha ni changamoto katika vikundi vya wakawake vya ushirika? Je, twawezaje kuhakikisha kwamba mkazo wa kikundi ni kuboresha maisha ya kila siku juu ya kukaza fedha?

5. Je, tunawezaje, kama wanawake, kuboresha uwezo wetu wa kujitawala na kujiongoza wenyewe?

6. Je, tunawezaje kujenga hali ya kuaminiana ndani ya vikundi vyetu vya ushirika?

7. Wakati tunapochagua viongozi, je, ni hali na tabia gani inafanya mtu kuwa kiongozi mwema?

12

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

Soma la 7 Makusudi na Utekelezaji

Ili wanawake waweze kuwaendea wengine, ni muhimu kwanza kujua makusudi yao. Kitabu cha Nehemia ni kielelezo kizuri cha jinsi kusudi na mpango ulivyojengwa ili kufikia mahitaji. Nehemia ni mfano wa hatua zinazotakiwa katika kufaulu kusudi na utekelezaji. Nehemia 1:3. Taarifa ya mahitaji miongoni mwa watu wake inamhuzunisha. Nehemia 1:6. Nehemia analeta hitaji kwa Mungu wakati akiomba na kufunga. Nehemia 1:8-10. Anaomba Mungu msaada kwa ajili ya watu wake na katika kuunda

mpango. Nehemia 2:5. Anaomba msaada na baraka za Mfalme. Nehemia 2:17-18. Anakusanya watu na kupata utashi wao wa kujenga tena ukuta. Nehemia 2:19. Wanawekewa vipingamizi lakini wanaamini Mungu atawafanikisha. Nehemia 3:1. Utaratibu unawekwa ukijumuisha na kuhusisha kila mtu kuanzia kuhani

mkuu hadi mabinti wa akida Shalumu (Neh. 3:12). Sura zinazofuata zinaelezea taarifa za maendeleo ya ujenzi, pamoja na matatizo yao na

jinsi mradi wa ujenzi ulivyokamilika.

Kwanza, lazima ushirika wa wanawake uelewe kuwa, nao ni washiriki katika kazi ya ufalme wa Mungu. Wanawake wakishajua kuwa kazi yao ni kazi ya ufalme wa Mungu, watahitaji kubuni malengo machache ya huduma katika jamii. Malengo hayo yatakuwepo tu, iwapo watatambua na kuelewa mahitaji ya familia na jamii inayowazunguka. Mahitaji ni ya kiroho, kimwili na kijamii. Mahitaji ya kiroho yatashughulikiwa katika mafunzo ya kawaida ya Biblia na majadiliano katika vikundi. Mafunzo mengi ya maendeleo yatalenga shuguli za wanawake za kila siku. Hivyo watapata uwezekano wa kufanya kazi pamoja ili kuboresha maisha.6 Ni wanawake hasa ni wakulima, wapanda mazao, wavunaji, wapeleka mazao sokoni kuuza au kununua, walishao familia, na watafutaji fedha kwa ajili ya elimu ya watoto wao. Wawajibika kwa afya ya watoto wao na waangalizi wa ardhi. Kazi hizi za uzalishaji, ni muhimu kuziboresha ndani ya jamii ili kupata afya bora ya jamii. Lengo lisiwe kuondoa hizi kazi kwa wanawake bali kutafuta njia za kurahihisha kazi zao ili kuleta ufanisi na tija zaidi. Hili litainua kiwango bora cha maisha na kuwapa wanawake nafasi ya udhibiti zaidi wa maisha yao ya kila siku.

Makusudi lazima yaendane na mahitaji ya watu wa sehemu husika, mafunzo yatolewe kulingana na hali ya watu ili yaeleweke vizuri. Mabadiliko hutokea kwa hatua ndogo, lakini mafanikio hupatikana tu kama wanawake wataelewa na kuweza utekelezaji. Mabadiliko makubwa yanayohitaji utalaamu au msaada wa nje, mara nyingi hayadumu au kuendelezwa na wanajamii kwa sababu ni ya utegemezi. Lengo liwe, kama vile wanavyofundishwa watu kuboresha maisha yao, walazimike kushirikisha wengine kwa yale waliyojifunza, hao nao wafanye hivyo kwa wengine (2 Tim.2:2).

Maswali ya Majadiliano 1. Taja hatua alizochukua Nehemia katika kuweka mipango na kutekeleza. 2. Je, makusudi na mipango yetu yawekwe kufuatana na nini? 3. Karama ya uratibu na taratibu ni lazima ili kuweka mpango fanisi. Ni nani katika kikundi

chako aliye na karama hiyo? 4. Je, itatosha kushugulika na mahitaji ya kiroho tu katika vikundi? 5. “Kushugulikia hitaji, anza na hatua ndogo kinachoweza kikundi chako.” Je, huu ni usemi

sahihi? 6. Je, lengo letu ni lipi, kutokana na 2 Tim. 2:2?

13

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

Sura ya 8 Mahitaji ya Kimwili na ya Kiroho

“Waafrika wana namna ya kuuona ulimwengu kuwa ni jumla ya vyote katika kitu kizima. Mtazamo huu huitwa mtazamo wa kiujumla. Ulimwengu wa kiroho na ule wa kimwili unaonwa ni ulimwengu mmoja wala hazitengwi.”7 Vitu vyote katika maisha na katika ulimwengu vinahusiana na vingine na kuwa kimoja. Kwa hiyo inafaa katika mtazamo wa kiafrika kuunganisha mafundisho kuhusu mahitaji ya kimwili pamoja na ya kiroho. Neno la Kiebrania, Shalom linaeleza hali ya afya na uzima, ya kiroho pamoja na ya kimwili, ambayo Mungu alidhamiria kwetu, watoto wake. Katika vikundi vya ushirika wa wanawake mafundisho hutakiwa kujenga “shalom” kwa wanawake katika kushugulikia mahitaji ya kimwili, kiakili, kijamii na kiroho. (Soma Mathayo 22:37-40; Marko 2:1-12; 1 Wathesalonike 5:23)

Kutokana na mwandishi Oyweka, baadhi ya mada za kawaida muhimu katika jamii inayotuzunguka ni pamoja na afya ya mtoto, afya na usafi, madawa ya kuzuia, matibabu ya huduma ya kwanza, mazingira ya nyumbani, bustani, uzalishaji na utunzaji wa chakula, maji safi, na kujihisi vizuri kama wanawake.8 Magonjwa mengi yatapunguzwa kwa kujifunza chanzo cha ugonjwa na jinsi ya kuuzuia au kuudhibiti. Vikundi vya ushirika ni mahali sahihi kwa mafunzo juu ya malaria, homa ya matumbo (typhoid), kifua kikuu (TB), magonjwa ya watoto, pepo punda, kupooza (polio), uzazi wa majira na ukimwi. Wafanyakazi wa afya jamii au wanakikundi walio na taaluma wa masuala ya afya ya msingi wanaweza kufundisha. Mafunzo yaambatane na ushauri wa vitendo, kama vile matumizi ya vyandarua, umuhimu wa chanjo, namna ya kuipatia familia chakula na maji safi, n.k. Wafundishwe juu ya tabia na matendo hatarishi ya kusabibisha magonjua. Wanawake waeleweshwe dawa za huduma ya kwanza na ya kiasili za kuwa nazo nyumbani za kusaidia kuharisha, homa na minyoo. Lazima wafundishwe njia rahisi zingine za kiafya, kama vile utayarishaji wa maji ya chumvi ya kuzuia watoto kuishiwa maji mwilini na usimamizi na tiba ya awali ya homa. Mafunzo ya aina hii yanasaidia kuokoa maisha na kupunguza gharama ya madawa na utunzaji afya. Wanawake wanapojadili pamoja na kushirikishana juu ya maisha yao, wanapata mafunzo mengi watakayotumia.

Zaidi ya mafunzo ya afya, wanawake wapewe mafunzo yanayohusu utunzaji wa rasilimali kama nishati na maji, uvunaji maji, upandaji miti, uboreshaji njia za mapishi na majiko. Vidokezo kuhusu matumizi ya mbolea, uhifadhi wa unyevunyevu katika bustani n.k. Haya ni mambo yaliyo ndani ya uwezo hata wa watu walio wa hali ya chini katika kuboresha maish yao. Wafundishwe juu ya namna ya kutunza, kugawa, na kuuza mazao. Mafunzo yote yafanyike kwa nia njema, kutoa muda wa kutosha wa majadiliano na kushirikishana mawazo, ili kujenga nia ya umoja na ushirikiano.

Wanawake wanaojifunza kuboresha maisha yao na kutatua matatizo yao wenywe wanaanza kujihisi vizuri na kujithamini. Wanajivunia kazi zao wanazozifanya na wanaona thamani ya kujifunza na kusaidiana ili kuishi vizuri zaidi. Mafunzo ya vitendo na yale ya kiroho yanapounganishwa, mtu mzima hujengwa na hatimaye watu hufikia hatua ya juu ya Shalom.

14

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

Maswali ya Majadiliano

1. Jadili mifano ya jinsi Waafrika tunavyoshika mtazamo wa jumuisho (yaani, hali ya kiroho inavyohusiana hali ya kimwili na kijamii, na hali ya kimwili inavyohusiana na hali ya kiroho). Je, nguvu ya mtazamo huo ni nini? Na udhaifu wake ni nini?

2. Je, unakubaliana na orodha ya masuala yanayohitaji kushughulikiwa katika jamii za Kiafrika? Orodhesha masuala unayoyaona katika kijiji au mji wako kuwa ni muhimu.

3. Je, utaanzaje kushughulikia maswala hayo. Je, yuko mtu katika kikundi chako aliye na taaluma kuhusu swala fulani na aweza kufundisha na kuongoza majadiliano?

4. Ni jinsi gani wanawake wanaojiheshimu wenyewe huongeza heshima yao katika jamii?

5. Katika uumbaji, mwanadamu alipewa mamlaka ya kutunza ardhi. Ni kwa njia zipi tunaweza kutunza na kuhifadhi rasilimali za nchi?

15

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

Soma la 9 Utamaduni, Miiko, Maadili na Fedha

Katika tamaduni nyingi za Kiafrika zimewabana na kuwafunga wanawake kwa kazi au shughuli maalum. Wanawake wanaonwa mara nyingi kuwa ni wa daraja la pili, wanaomilikiwa na wanaume, hata kama mtumwa kwa bwana wake. Katika mafunzo, tumeona kuwa huo si msimamo wa Biblia, ingawa makanisa mengine yanafundisha na kutenda kulingana na mtazamo huo wa utamaduni. Sisi Wakristo tunatakiwa kuwa tayari kufanya mabadiliko katika desturi za utamaduni wetu ili kuleta uhuru wa kweli kwa wanawake.9 Miiko ndani ya utamaduni husababisha kupinga mafunzo yanayoweza kuokoa maisha na kuleta maendeleo sahihi katika jamii. Miiko hii inakuwa na uzito kwa sababu inaambatana na vitisho na hofu. Hata hivyo, Wakristo hawashikwi na hofu hizo kupitia imani katika uwezo wa Yesu.

Mwandishi Rosalia Oyweko amegawa imani na desturi za kitamaduni katika makundi matatu: desturi zinazosaidia, desturi zisizosaidia wala kudhuru, na desturi zinazodhuru.10 Anelezea kuwa desturi zinazosaidia zikubalike hata ingawa zinafuatwa kwa sababu zisizo sahihi. Desturi zisizo na upande, zinaweza kupuuzwa kwa sababu hazisaidii wala hazidhuru. Lakini, desturi na miiko yenye madhara, iangaliwe kwa uangalifu na kushughulikiwa. Hayo yahitaji kubadilishwa kwa msingi wa mafunzo ya Biblia. Mafunzo hayo ni kama vile yahusuyo utunzaji wa miili yetu kama hekalu ya Roho Mtakatifu ( Soma 1 Kor.6:19); na kuhusu kutokuwa na hofu (Zaburi 34:4: Zaburi 46:2; Isaya 41:10; 51:12-13); na kuhusu mafunzo mengine ya kiroho, kama vile uhuru tuliyo nayo katika Kristo.

Baadhi ya mafunzo yanayohusu miiko yenye madhara ni:11

Jinsi kukatazwa kula vyakula fulani, huleta madhara kwa wajawazito.

Lazima watoto wenye surua waogeshewe ili kusaidia kupunguza homa.

Haja ya kupunguza kuliko kuongeza joto la mtu mwenye homa.

Haja ya kupewa vyakula vya maji maji au vimiminika kwa mtoto anayeharisha.

Umuhimu wa ushirika ni kwa mafunzo, lakini pia hutia moyo wanawake wale wanaoondokana na mfumo wa utamaduni, miiko na desturi zisizofaa. Jamii ya imani inaweza kutoa ujasiri unaotakiwa katika kupingana na masuala ya tamaduni zisizotakiwa.

Kutokana na msingi wa mafunzo ya Biblia yanayotolewa, ushirika wa wanawake unao nafasi pekee ya kushughilikia masuala ya maadili katika jamii. Sheria za Mungu zilipewa ili kuweka mazingira yaliyo mazuri kwa ajili ya binadamu aliowaumba. Kwa mfano, mafunzo ya Amri Kumi za Mungu, na kupenda jirani yako, na ndoa ya Kikristo hutoa msingi wa uadilifu katika jamii yetu leo. Mtazamo wa Biblia kuhusu masuala ya ngono ni mafunzo ya lazima ndani ya kanisa ili kubadilisha tabia na fikira za watu zinazowapelekea magonjwa ya zinaa na ukimwi.

Kwa watu walio wengi, hata katika makanisa yetu, maendeleo huambatana na fedha. Hata hivyo, katika maeneo ya vijijini palipo na rasilimali pungufu, miradi ya fedha haifanikiwi, na mara nyingi huishia kwa watu wachache sana. Kuna njia mbadala ya mtazamo huo mahali ambapo pesa haiongezeki. Njia hiyo ya maendeleo ni kufanya fedha iliyopo itoshe kwa matumizi zaidi pamoja na kupunguza matumizi mengine ya fedha. Hii inaitwa mapato yasiyo fedha. Baadhi ya mifano ya mapato yasiyo fedha ni pamoja na: uzalishaji wa chakula katika mashamba yao, uzuiaji wa magonjwa ili kupunguza gharama za matibabu, kurekebisha nguo badala ya kununua mpya, kutumia majiko sanifu, kupanda miti ya kuni, na kujifunza kutengeneza sabuni, mafuta ya mwili na mishumaa kutokana na vitu vinavyopatikana.

16

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

Mkakati huu huimarisha vikundi vya ushirika na kupunguza mategemeo katika jamii kwamba fedha ni suluhu ya matatizo yote.12

Maswali ya Majadiliano

1. Je, ni lazima tuangalie kwa mashaka desturi zote ya utamaduni?

2. Ni nini mwongozo wetu tunaposhughulika na masuala ya tamaduni na miiko?

3. Kumbuka baadhi ya tamaduni na miiko iliyoleta athari mbaya katika jamii yako. Je, wanawake katika kikundi wanaweza kufanya nini?

4. Ni yapi baadhi ya masuala ya maadili unayoyaona katika jamii yako? Ni jinsi gani wanawake wa kikundi chako wanaweza kuyazungumzia?

5. Je, unafikiri msisitizo juu ya fedha umeangamiza vikundi vya wanawake? Toa mifano.

6. Je, ni jinsi gani unafikiria mapato yasiyo fedha yanaweza kusaidia katika jamii yako?

17

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

Somo la 10 Mafunzo Shirikishi – Kusaidia watu Wajifunze

Soma Mathayo 13:3-9.

Kama ilivyo ardhi inavyohitaji utayarishaji kabla ya kupanda mbegu ili mavuno mengi yapatikane, vivyo hivyo mafunzo yanahitaji sifa fulani za kuwezesha mbegu za mafundisho kuota na kusitawi katika mioyo ya watu. Mfano wa mpanzi unakumbusha kwamba, tusipoangalia kuhusu mahali na jinsi ya kupanda mbegu za ukweli na mabadiliko, mazao yanayotarajiwa hayatavunwa. Mafundisho yetu yanaweza kupata ugumu katika kuota au kusongwa na matatizo na kufa kabla ya kukomaa. Soma hili linafundisha jinsi ya kutayarisha ardhi na kuwasaidia watu kujifunza kutokana na mafunzo yatolewayo katika vikundi vya ushirika vya wanawake.

Wataalamu wa mafunzo ya elimu ya watu wazima wamegundua kwamba mafunzo shirikishi ndiyo njia nzuri zaidi ya kuleta ufanisi katika kujifunza. Watu wazima wanayo hazina kubwa ya uzoefu, wanaweza kutumia uzoefu huo kama rasilimali, wao kwa wao katika kujifunza. Nguvu ya mafunzo shirikishi ni kukusanya maarifa na kushirikishana maarifa hayo kupita mijadala katika vikundi vidogo. Watu wazima hujifunza haraka kama mambo yanayoletwa yana mahusiano na maisha yao. Uwezo wao wa kuchunguza na kufikiria umekomaa na unaweza kuwa wa manufaa kama watapewa heshima kuhusiana na mitazamo na uzoefu wao. Elimu ya namna hiyo hukaza umuhimu wa mtu kujifunza badala ya maneno ya kufundishwa tu. Pia inasisitiza kwamba suluhisho ya matatizo itokane na wahusika wenyewe badala ya mwingine kuwaambia namna ya kutoa suluhisho kwa matatizo yao. Katika mchakato huu wa mafunzo, watu wanasaidiwa kuelewa tatizo, na kutafuta uwezekano wa suluhisho, na jinsi ya kutekeleza suluhisho hilo.

Mafunzo shirikishi yanafanikiwa katika vikundi vidogo vya watu 4-12 wakiongozwa na mtu asiyefundisha tu, bali anaendesha mjadala na kutoa nafasi kwa kila mtu kushiriki. Washiriki washauriwe kukaa katika mduara ili kila mchangiaji aonekane na kusikika vizuri. Watu wote wapewe moyo wa kuchangia mambo mapya, bila kurudiarudia au mtu mmoja kuutawala mjadala. Watu washawishiwe kuzungumzia simulizi zao au mifano, hadithi zilizo na uhusiano na somo. Maonyesho na mazoezi ya vitendo yanaweza kwa wakati fulani kutumika ili kuimarisha mchakato wa mafunzo. Maswali yaliyotayarishwa kabla ya mazungumzo yatasaidia kupata mawazo ya kikundi na kuelekeza mjadala. Maswali yanayojitokeza ndani ya mjadala yaelekezwe na kujibiwa na washiriki wala siyo na kiongozi tu. Mafunzo yanapofanyika kwa mtindo huo yanawezesha wanawake kujiona wanao uwezo wa kufanya na kufuatilia masuala yao kwa vitendo kuliko wanavyoambiwa suluhu tu kwa matatizo yao.12

Inapotokea wakati kikundi cha ushirika kinahitaji mtu mtaalamu kutoka nje ya kikundi kuwezesha mambo fulani ambayo kikundi hakina uwezo nayo. Hapo waalikwe watu wengine wenye taaluma kusaidia mafundisho kuhusu mambo magumu. Kikundi kiwe tayari kusikilizana na kuwasiliana na vikundi vingine, kujenga mahusiano na kuwa tayari kujifunza na kupata ujuzi kwa manufaa ya kikundi. Isipokuwa, kikundi chako kisianze kuwategemea kikundi kingine na kiache kutafuta suluhu zake wenyewe.

Maswali ya Majadiliano

1. Je, kwa nini maandalizi ya fikira za watu kwa ajili ya mbegu za mafunzo ni muhimu sana?

2. Ni kwa jinsi gani na kwa nini mafunzo ya watu wazima ni tofauti na elimu ya watoto?

3. Ni zipi kanuni za msingi za mafunzo shirikishi?

18

Wanawake Katika Kazi ya Mungu

Diocese Based TEE, Kanisa la Mennonite Tanzania, Kenya Mennonite Church, ©2015 Gloria Bontrager

4. Buni baadhi ya maswali ya kuuliza wakati unapozungumzia tatizo fulani.

5. Ni namna gani mjadala unaweza kuendeshwa?

6. Kwa nini ni muhimu mafunzo yanayoendeshwa yawe kwa manufaa ya kikundi?

Nukuu

Nukuu zifuatazo zimetokana na maandiko kutoka kitabu cha Oyweka, Rosalia Achien’g, Reaching Out to the Women of Africa: Holistic Teaching Through Church Women’s Fellowships, REAP, 2000. (tafasiri: Kuwaendea Wanawake wa Afrika: Mafunzo ya Kiroho na ya Kimwili Kupitia Vikundi vya Wanawake Kanisani)

(1) Uka. 25 (2) Uka. 30 (3) Uka. 39, 53 (4) Uka. 20 (5) Uka. 20 (6) Uka. 56 (7) Uka. 54 (8) Uka. 70 (9) Uka. 80 (10) Uka. 82 (11) Uka. 83 (12) Uka. 86