The Standard: Enock Maregesi
-
Upload
enock-maregesi -
Category
Career
-
view
137 -
download
5
Transcript of The Standard: Enock Maregesi
ENOCK MAREGESI MSHINDI WA PILI WA TUZO YA
KISWAHILI YA MABATI-CORNELL YA FASIHI YA KIAFRIKA 2015
MWANDISHI WA KOLONIA SANTITA
MAHOJIANO
Ulianzaje kuandika?Nilianza kuandika kwa kujijengea
utamaduni. Utamaduni wa kuandika. Popote pale nilipoona kitu ambacho nilidhani kilifaa kuandikwa mahali,
nilikiandika bila kusita au kuchelewa kwa namna yoyote ile. Nilianza kwa kuandika
insha na kitu chochote kile kama vile barua kwa rafiki yangu wa kike wa kipindi kile, marafiki na kwa familia
yangu pia. Hicho ndicho kilichoniingiza katika biashara hii ya uandishi wa vitabu.
Hadithi yangu ya kwanza kabisa kuandika iliitwa Magaidi wa Namba
One – Namba One likiwa jina la sehemu – hadithi fupi ya kijasusi
iliyohusu genge la kijambazi, lililokuwa na maskani yake mjini
Dodoma. Magaidi wa Namba One ilikuwa na urefu wa kurasa 15.
Niliiandika nikiwa na umri wa miaka 15 au 16 hivi, katika Shule ya
Sekondari ya Bihawana ya mkoani Dodoma.
Hadithi hii ilihusu kikundi cha kigaidi kilichoitwa Namba One.
Kikundi hiki kilikuwa na makao yake makuu nje ya Dodoma, katika pori
la Namba One, kama unaelekea Iringa. Lilifanya shughuli zake ndani na nje ya Dodoma hadi siku moja mkubwa wake alipokamatwa; na
baadaye kupata adhabu ya kifungo cha maisha jela kilichoambatana na
kazi ngumu, katika gereza lenye ulinzi mkali la mkoani Shinyanga.
Baada ya hapo, viongozi wote wakubwa wa kikundi hicho walikamatwa na kukabidhiwa vifungo kulingana na
makosa waliyoyafanya.
Nini kilikusukuma kuwa mwandishi wa vitabu?Nilihamasishwa na watu wengi na
matukio mengi kuwa mwandishi wa vitabu: Ngugi wa Thiong’o, Ben Mtobwa,
Euphrase Kezilahabi, Penina Mlama, Shafi Adam Shafi, sinema za mapigano kama vile The Big Boss ya Bruce Lee na
Missing in Action ya Chuck Norris, hadithi kutoka kwa wazee na watu wengine wakubwa, na kadhalika.
Hata hivyo, hamasa kubwa zaidi kushinda zote ilitoka kwa Shaaban
Robert – mzalendo wa kweli wa Tanzania na kinara wa lugha ya
Kiswahili – ambaye vitabu vyake vilinipa nguvu (na tumaini) kuandika riwaya yangu ya kwanza ya Kolonia Santita,
ambayo awali iliitwa Salina Cruz.
Salina Cruz ni mji wa mwambao wa kusini-magharibi mwa Meksiko, katika jimbo la Oaxaca, kateli ya Kolonia Santita ilipoanzishwa.
Nilipomaliza masomo yangu ya sekondari mwaka 1992 nilianza kuandika
Kolonia Santita. Kipindi hicho nilikuwa nikisubiri majibu ya mtihani wa taifa wa
kidato cha nne. Siku moja (nilipoanza rasmi kuandika, miaka 23 iliyopita) niliijiwa ghafla na ndoto ya mchana
nikiwa katika bustani ya nyumbani kwetu Kijitonyama, Dar es Salaam. Vita kubwa ya mawazo iliendelea kichwani mwangu kwa muda mrefu bila kukoma, kuhusiana
na dhana fulani ambayo nilikuwa bado sijaielewa sawasawa.
Ndoto hiyo ikawa msingi wa taaluma yangu ya uandishi wa vitabu na msingi
wa utetezi wangu wa lugha ya Kiswahili. Ikanikumbusha uzuri wa kipaji na uwezo
wa talanta nilivyopewa na Mungu na jinsi gani nivitumie, na ikanikumbusha jinsi gani nilivyoweza kuwa na uwezo mkubwa kuburudisha na kuelimisha
watu kwa nguvu ya neno.
Ujasiri wa kujaribu au jeuri ya kufanya kitu na kujiamini na tumaini, ulinipa
msingi wa kufikiri vyema na kuandika kwenye karatasi dhana mbalimbali na
mawazo kadha wa kadha kutoka katika dunia niliyoigundua. Nilikuwa na
uwezo, nilidhani, wa kuwa mojawapo kati ya watoa burudani bora na
waandishi bora wa vitabu Tanzania.
Bustanini nilitamani sana kuchapisha kitabu changu nje ya Tanzania na Afrika,
mathalani Uingereza au Marekani, ambapo uchapishaji wa vitabu ni wa
kimataifa na wa daraja la kwanza. Kichwa changu kilifikiria riwaya ambayo
ingesimulia mandhari ya miji zaidi ya minne ulimwenguni kote, ambayo baadaye ingekuwa ya kwanza kwa
mauzo hapa Afrika ya Mashariki na Kati.
Nilitamani hadithi yangu ichapishwe nje kupata ubora wa kitabu, na ubora wa huduma za
uchapishaji wa vitabu.
Hadithi ya Kolonia Santita niliiandika kwa miezi mitatu mfululizo hadi
nilipokamilisha rasimu ya kwanza kabisa ya muswada wenyewe. (Nilikuwa na
umri wa miaka 20 nilipofanya hivyo). Kila nilipodhani muswada umekamilika ili
niupeleke kwa wachapishaji, niligundua bado ulihitaji marekebisho.
Mwaka 1999 hata hivyo nilidhani umekamilika, na niliupeleka Popular
Publications Ltd (PPL) kwa ajili ya mkataba wa uchapishaji wa vitabu.
Lakini PPL waliukataa muswada huo. Waliukataa kutokana na ripoti iliyokuwa na mchango mkubwa kwangu ya Hayati Saifu D. Kiango, ambaye kipindi hicho
alikuwa mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Tanzania (BAKITA).
Kiango alishauri katika ripoti yake masahihisho mengi katika muswada
wangu, ambayo yote nilikubaliana nayo, kabla sijaurudisha kwa wachapishaji
lakini nikashindwa kufanya hivyo. Nilishindwa kuurudisha kwa
wachapishaji.
PPL walipoteza baadhi ya sura za muswada wa Kolonia Santita (sura ya 7,
8 na 9) na sikufurahishwa na majibu niliyopewa na Ndg. Mhando (nimesahau
majina yake mengine) kwamba yeye/ofisi hawakujua hizo sura
zilipokwenda na kwamba yeye/ofisi walipeleka muswada BAKITA ukiwa
umekamilika kabisa. Mhando alikuwa mhariri mwandamizi wa PPL.
Kwa sababu hiyo niliuondoa muswada wangu PPL na kuweka nadhiri ya kusahihisha kila kosa
aliloliona Kiango na kushauri nilisahihishe, na nadhiri ya
kuchapisha kitabu hicho mimi mwenyewe nje ya Afrika kama
ningepata nafasi.
Mnamo mwaka 1992 hadi 1999 nilipata nafasi ya kuandika miswada mingine mitano. Miwili kati ya miswada hiyo ilikuwa imekamilika. Mitatu ilikuwa
bado. Mitatu ni ya kipelelezi. Miwili ni ya kimapenzi. Septemba 2004 nilihamia
London nchini Uingereza. Huko nilipata nafasi nzuri zaidi ya kufanya utafiti
yakinifu, wa miswada yangu yote sita, kwa kiwango nilichokitaka.
Katika maisha yangu yote nilitamani sana kuwa mtetezi wa lugha na
utamaduni wa Kiswahili. Nadhani tunahitaji wote kuwa watetezi wa
lugha hii na lugha zingine za Kiafrika kwani hizi ndiyo utambulisho wa
bara letu.
Kutokana na hamu hiyo, mwaka 1995 niliweka nadhiri ya kupigania
lugha ya Kiswahili maisha yangu yote yaliyobakia. Lakini nilijua hilo
lisingewezekana bila kwanza kufanikisha elimu.
Mwaka 2010 nilijiunga na chuo cha ubunifu wa kifasihi cha Manchester (The
Writers Bureau) nchini Uingereza, kwa lengo la kutimiza ndoto zangu na kupata
taaluma ya uandishi wa vitabu. The Writers Bureau walinipa moyo wa
kujiamini. Nilikuwa nikiishi shimoni, gizani. Hata hivyo, baada ya kupitia
vitabu vichache vya kozi niliona nuru upande wa pili wa tobwe.
Nilijua, kutokea kipindi hicho kwamba, endapo ningesoma kwa bidii ningepata uzoefu na utaalamu na mwongozo hasa
niliyoutaka. Nilitamani kuwa mwandishi bora wa vitabu na
nilitamani kuwaelimisha watu na kuwaburudisha pia. Nilitamani kuwa
mojawapo ya waandishi bora wa vitabu na wauzaji bora wa vitabu nchini
Tanzania, na nje ya hapo.
Ulishindaje?
Habari ya Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika niliipata kwa mshangao
mkubwa. Kwanza, niliipata kutoka kwa Mkurugenzi wa CDEA (Culture for Development
East Africa) Ayeta Anne Wangusa mwezi wa tatu 2015 ofisini kwake Dar es Salaam. Kisha
nikaandaa muswada wangu vizuri na kuutuma kupitia tovuti ya tuzo kwa waamuzi wa tuzo,
kwa ajili ya mashindano.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya
Fasihi ya Kiafrika Profesa Abdillatif Abdalla aliponipigia simu kunijulisha kwamba muswada wangu ulishinda
nafasi ya pili nilifurahi sana. Nilifurahi sana kiasi kwamba nilijifungia chumbani kwangu hotelini na kucheza muziki kwa masaa matatu mfululizo, na nimekuwa
na furaha kuanzia kipindi hicho na kuendelea.
Sababu kubwa ya muswada wangu kushinda ni kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu WOTE. Ni uvumilivu,
uchapakazi na nidhamu.
Nini ushauri wako kwa waandishi chipukizi?
Ushauri wangu pekee ninaoweza kutoa kwa waandishi chipukizi ni elimu! Hutaweza kufikia malengo
yako kikamilifu bila msaada wa wataalamu – Hata kama una kipaji
au ujuzi kiasi gani.
Ukiwa na kipaji nenda shule kurekebisha kipaji chako, ukiwa na ujuzi nenda shule
kurekebisha ujuzi wako.