MASHARTI YA CHAMA - CRDB Saccos YA CHAMA.pdf · 2014-01-09 · mpaka akidhi masharti yote ya kuwa...
Transcript of MASHARTI YA CHAMA - CRDB Saccos YA CHAMA.pdf · 2014-01-09 · mpaka akidhi masharti yote ya kuwa...
Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
CRDB WORKERS’ SAVINGS AND CREDIT COOPERARIVE SOCIETY LIMITED
MASHARTI
YA
CHAMA
CRDB WORKERS SACCOS LTD
i Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
YALIYOMO
SEHEMU YA KWANZA
JINA, FUNGAMANO, ANWANI NA USAJILI ....................................................................................... 1
1. Jina, Fungamano na Anwani ............................................................................. 1
2. Usajili wa Chama ............................................................................................. 1
3. Ufafanuzi wa Maneno ....................................................................................... 1
SEHEMU YA PILI
MADHUMUNI, MAMLAKA NA WAJIBU WA CHAMA .......................................................................... 2
4. Madhumuni ya Chama hiki yatakuwa ................................................................. 2
5. Mamlaka ya Chama yatakuwa ........................................................................... 3
6. Wajibu wa Chama ............................................................................................ 3
SEHEMU YA TATU
SIFA, UTARATIBU, URITHI NA UKOMO WA KUWA MWANACHAMA ............................................ 4
7. Sifa za Kuwa Mwanachama ............................................................................... 4
8. Utaratibu wa kujiunga na Chama ....................................................................... 4
9. Ukomo wa Uanachama ..................................................................................... 4
10. Kuachishwa Uanachama ................................................................................... 5
11. Haki ya Mtu Aliyekoma Uanachama ................................................................... 6
12. Mrithi Wa Mwanachama ................................................................................... 6
SEHEMU YA NNE
WAJIBU NA HAKI ZA MWANACHAMA ................................................................................................ 6
13. Wajibu wa Mwanachama .................................................................................. 6
14. Haki za Mwanachama ....................................................................................... 7
15. Daftari la Wanachama ...................................................................................... 7
SEHEMU YA TANO
KIINGILIO, HISA, AMANA NA AKIBA ZA CHAMA ............................................................................. 8
16. Kiwango Cha Kiingilio, Hisa, Amana na Akiba ..................................................... 8
17. Kiingilio ........................................................................................................... 8
18. Hisa ................................................................................................................ 8
ii Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
19. Akiba .............................................................................................................. 9
20. Amana ............................................................................................................ 9
SEHEMU YA SITA
VYANZO NA UWEKEZAJI WA FEDHA ZA CHAMA ........................................................................... 10
21. Vyanzo vya Fedha ya Chama ni ........................................................................ 10
22. Uwekezaji wa Fedha za Chama ........................................................................ 10
SEHEMU YA SABA
MWAKA WA FEDHA, MAHESABU YA CHAMA NA MGAO WA ZIADA ........................................... 10
23. Mwaka wa Fedha ............................................................................................ 10
24. Mahesabu ya Chama ....................................................................................... 11
25. Mgao wa Ziada ............................................................................................... 11
SEHEMU YA NANE
FEDHA ZA CHAMA .............................................................................................................................. 12
26. Kuhifadhi Fedha za Chama............................................................................... 12
SEHEMU YA TISA
AKIBA NA AMANA ............................................................................................................................... 13
27. Taratibu za Uwekaji Akiba ................................................................................ 13
SEHEMU YA KUMI
MIKOPO ................................................................................................................................................ 14
28. Taratibu za Mikopo ......................................................................................... 14
SEHEMU YA KUMI NA MOJA
MIKUTANO YA CHAMA ....................................................................................................................... 14
29. Aina ya Mikutano ndani ya Chama .................................................................... 14
30. Mkutano Mkuu wa Mwaka ................................................................................ 15
31. Mikutano Mikuu ya Kawaida ............................................................................. 15
32. Mkutano Mkuu Maalum ................................................................................... 16
33. Taarifa za Mikutano ......................................................................................... 16
34. Muda wa Matangazo ....................................................................................... 16
35. Mahudhurio kwenye Mikutano .......................................................................... 17
36. Uendeshaji wa Mikutano ya Chama .................................................................. 18
iii Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
SEHEMU YA KUMI NA MBILI
BODI NA KAMATI ZA CHAMA ........................................................................................................... 18
37. Bodi ya Chama ............................................................................................... 18
38. Kamati Ndogo ya Mikopo ................................................................................. 21
39. Kamati ya Usimamizi ....................................................................................... 22
SEHEMU YA KUMI NA TATU
USIMAMIZI WA SHUGHULI ZA CHAMA ........................................................................................... 23
40. Usimamizi wa Shughuli za Chama ..................................................................... 23
41. Meneja ........................................................................................................... 23
42. Mhasibu ......................................................................................................... 23
43. Wawakilishi wa Chama .................................................................................... 23
SEHEMU YA KUMI NA NNE
KUFUTWA KWA CHAMA NA MENGINEYO ....................................................................................... 25
44. Kufutwa kwa Chama ....................................................................................... 25
45. Mengineyo ..................................................................................................... 25
1 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
SEHEMU YA KWANZA
JINA, FUNGAMANO, ANWANI NA USAJILI
1. Jina na Anwani:-
(a) Jina la chama litakuwa: CRDB WORKERS’ SAVINGS AND CREDIT
COOPERATIVE SOCIETY LIMITED, kwa
kifupi “CRDB Workers SACCOS Limited”;
(b) Fungamano: Wafanyakazi wa Benki ya CRDB na kampuni
zake tanzu (Benki) au Waajiriwa wa CRDB
Workers SACCOS Limited;
(c) Anwani ya Chama: S.L.P 268, DAR ES SALAAM;
(d) E-mail: [email protected]
(e) Eneo la shughuli za Chama: Mahali popote zilipo ofisi na Matawi
ya Benki
(f) Makao Makuu ya Ofisi za Chama: KATIKA OFISI ZA MAKAO MAKUU YA
CRDB BANK PLC
2. Usajili wa Chama:-
(a) Tarehe ya kuandikishwa: 11/01/2014
(b) Nambari ya kuandikishwa: 5410
(c) Idadi ya wanachama waliofanya maombi: 1,412
3. Ufafanuzi wa Maneno:
Maneno yafuatayo yanapotumika katika masharti haya yatakuwa na maana
kama inavyoelezwa hapa: -
(a) “Benki” itamaanisha “Benki ya CRDB” na kampuni zake tanzu;
(b) “Bodi ya wakurugenzi” (Board of Directors) yaani Kamati ya kuongoza
shughuli zote za kawaida zenye kuhusu chama hiki;
(c) “CRDB Workers SACCOS” AU “CRDB Workers SACCOS Limited”, AU
“Chama”, inamaanisha CRDB WORKERS SAVINGS AND CREDIT
COOPERATIVE LIMITED;
2 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
(d) “Kanuni za Uhasibu” inamaanisha kanuni za kiuhasibu kulingana na
“Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA)”, “Sheria za Kimataifa
za Ukaguzi wa Mahesabu (IFRS)”; na Kanuni na Taratibu za kiuhasibu
kulingana na Sheria ya Ushirika;
(e) “Kiongozi” (Leader) yaani Wajumbe wote wa Bodi na Wajumbe wa
Kamati ya Usimamizi;
(f) “Mrajisi” (Registrar of Cooperative Societies) yaani Mrajisi wa Vyama
vya Ushirika Tanzania Bara;
(g) “Mtoto au Mtoto mdogo” mwenye umri chini ya miaka 18;
(h) “Mwajiri” ni CRDB Workers SACCOS Limited au Benki;
(i) “Savings and Credit Cooperative Society Limited” yaani Chama cha
Ushirika cha Akiba na Mikopo;
SEHEMU YA PILI
MADHUMUNI, MAMLAKA NA WAJIBU WA CHAMA
4. Madhumuni ya Chama hiki yatakuwa:-
(a) Dhumuni kubwa la Chama ni kustawisha na kuinua hali ya kiuchumi ya
Wanachama;
(b) Kuhamasisha na kupokea viingilio vya uanachama, Hisa, Akiba, Amana
na michango mbalimbali kutoka kwa Wanachama kwa mujibu wa
Sheria ya Ushirika;
(c) Kuweka viwango vya faida juu ya Hisa, na riba juu ya Amana na Akiba;
(d) Kutoa mikopo inavyohitajika na wanachama wake;
(e) Kukuza na kulinda fedha ya wanachama kwa:-
(i) Kuwahamasisha wafanyakazi wa Benki kujiunga kwa kununua
hisa, na kuweka akiba na amana katika Chama;
(ii) Kuwahamasisha Wanachama kuongeza hisa, amana na akiba
zao;
(iii) Kuweka kinga ya majanga (BIMA) dhidi ya fedha na rasilimali
nyingine za Chama;
3 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
(iv) Kuwekeza sehemu ya rasilimali ya chama katika maeneo
yanayoongeza tija na faida zaidi kwa wanachama;
(f) Kutoa elimu ya Ushirika na mambo mengine ya msingi kwa
Wanachama na wafanyakazi ili kukijenga Chama katika misingi ya
Ushirika;
(g) Kufanya shughuli nyingine halali kwa manufaa na ustawi wa Chama na
Wanachama;
5. Mamlaka ya Chama yatakuwa:-
(a) Kukopa fedha kutoka kwenye taasisi za fedha kwa ajili ya kuwekeza
katika maeneo yanayoleta tija;
(b) Kuanzisha na kuendeleza shughuli zozote za kiuchumi kwa manufaa ya
Wanachama kama itakavyokubaliwa na Mkutano Mkuu na kuidhinishwa
na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika;
(c) Kufanya kazi kwa kusudi ya kufikia na kutimiza madhumuni yake kama
yalivyo ndani ya Masharti;
(d) Kutoza faini (adhabu) kwa Wanachama watakaoshindwa kurejesha
mikopo kulingana na taratibu zilizopo za Chama;
(e) Chama kitakopa baada ya kupata idhini ya Wanachama na Mrajisi wa
Vyama vya Ushirika kwa kuzingatia mambo yafuatayo:-
i. Chama hakiwezi kukopa Mkopo zaidi ya robo (1/4) – yaani
asilimia ishirini na tano (25%) ya jumla ya rasilimali zote za
Chama;
ii. Chama kitakopa kwa uamuzi wa angalau robo tatu (3/4) ya
Wanachama wake;
6. Wajibu wa Chama kwa Wanachama:-
(a) Kulinda maslahi ya Wanachama wakati wote;
(b) Kulinda Akiba, Hisa na Amana za Wanachama;
(c) Kuweka Masharti na Sera muafaka ili kulinda na kukuza rasilimali za
Chama;
4 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
SEHEMU YA TATU
SIFA, UTARATIBU, URITHI NA UKOMO WA KUWA MWANACHAMA
7. Sifa za Kuwa Mwanachama:-
(a) Awe ni mtu mwenye akili timamu na anayeaminika na wenzake;
(b) Awe ni mfanyakazi wa Benki; aliyeajiriwa kwa masharti ya kudumu au
kwa mkataba usiopungua mwaka mmoja (1), AU awe mwajiriwa wa
CRDB Workers SACCOS Limited;
(c) Awe tayari kufuata na kuheshimu masharti ya Chama na Sheria ya
Vyama vya Ushirika;
(d) Awe ametimiza umri usiopungua miaka 18;
(e) Kama ni Kikundi au Taasisi, lazima Bodi ijiridhishe Wanachama wake
wana sifa zilizotajwa hapo juu.
8. Utaratibu wa kujiunga na Chama:-
(a) Mtu anayetaka kuwa Mwanachama atajaza fomu ya maombi ya
kujiunga na chama na kuiwakilisha ofisi za CHAMA moja kwa moja au
kupitia kwa Wawakilishi wa Matawini;
(b) Bodi itajadili maombi hayo, na inaweza kukubali au kuyakataa;
(c) Mapendekezo ya Bodi yatajadiliwa na Wanachama katika Mkutano
Mkuu;
(d) Mwombaji akikubaliwa kujiunga na Chama, atalipa michango yote kwa
mujibu wa Sera na Taratibu za wakati husika;
9. Ukomo wa Uanachama:
(a) Mwanachama ataweza kukoma uanachama kwa sababu zifuatazo:-
i. Kwa mwanachama kujiuzulu mwenyewe kwa taarifa ya
maandishi;
ii. Kuachishwa uanachama kwa azimio litakaloungwa mkono na
Wanachama wasiopungua theluthi mbili (2/3) ya Wanachama
waliohudhuria katika Mkutano Mkuu huo;
iii. Mwanachama Kuchukua hisa zake zote;
5 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
iv. Kufariki kwa mwanachama;
v. Mwanachama kupoteza uwezo wake wa kiakili uliothibitishwa na
daktari;
vi. Mwanachama anapostaafu, kuachishwa au kufukuzwa kazi na
Mwajiri;
vii. Kwa sababu zozote zilizotajwa katika kifungu cha 25 cha kanuni
za Vyama vya Ushirika (Rules), 2004.
(b) Barua ya Mwanachama ya kuacha Uanachama itajadiliwa na
kuamuriwa na Bodi ndani ya kipindi cha miezi mitatu na taarifa
kupelekwa kwenye Mkutano Mkuu.
10. Kuachishwa Uanachama:
(a) Mwanachama anaweza kuachishwa uanachama kwa sababu zifuatazo:-
i. Kushindwa kutoa michango ya lazima ndani ya Chama kwa
kipindi cha miezi mitatu mfululizo bila sababu ya msingi
itakayokubalika na Bodi ya Chama; na taarifa kupelekwa kwa
kwa Mkutano Mkuu;
ii. Kutoa rushwa kwa kiongozi au mtumishi wa Chama hiki kwa nia
ya kufanyiwa upendeleo wowote ndani ya chama hiki, au
kupokea rushwa kutoka kwa kiongozi au mtumishi kwa sababu
yoyote ile;
iii. Kufanya kitendo chochote ambacho Bodi itajiridhisha kuwa ni
cha kutokuwa mwaminifu au ambacho ni kinyume na
madhumuni ya Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo;
iv. Kushindwa kulipa mkopo wake katika muda muafaka, bila ya
kuwa na sababu zinazokubalika na Bodi ya Chama;
(b) Kabla ya Mwanachama hajaachishwa uanachama wake, atapewa nafasi
ya kujitetea kwa maandishi kwa Bodi na mbele ya Mkutano Mkuu;
6 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
11. Haki ya Mtu Aliyekoma Uanachama:-
(a) Mwanachama ambaye uanachama wake umekoma:-
i. Atarudishiwa hisa na akiba zake ndani ya siku tisini (90) baada
ya kutolewa kwa maandishi ya kuacha Uanachama;
ii. Hatarejeshewa hisa zake mpaka madeni yake na ya wanachama
aliowadhamini yawe yamelipwa yote, au wadhaminiwa
kubadilisha wadhamini;
iii. Na yule ambaye kaachishwa/kaacha au kafukuzwa kazi na
Mwajiri atarudishiwa fedha zake zote mara moja baada ya
kuhakikisha hana deni na chama;
(b) Mtu aliyeacha au kufukuzwa uanachama anaweza kuomba kujiunga
tena kwa mujibu wa masharti ya Chama;
12. Mrithi Wa Mwanachama:-
(a) Kila Mwanachama atamteua mrithi wake ambaye atakuwa na haki ya
kulipwa akiba, hisa na faida zote ndani ya Chama;
(b) Mwanachama atakuwa na haki ya kubadilisha jina la mrithi pale
anapotaka;
(c) Mrithi wa Mwanachama hawezi kurithi kuendelea kuwa Mwanachama,
mpaka akidhi masharti yote ya kuwa Mwanachama katika kipengele
cha 7 cha Masharti ya haya.
SEHEMU YA NNE
WAJIBU NA HAKI ZA MWANACHAMA
13. Wajibu wa Mwanachama:-
(a) Kuwa mwaminifu na kushiriki kikamilifu katika shughuli zote za
maendeleo ya Chama;
(b) Kununua Hisa, kuweka Akiba na Amana mara kwa mara;
(c) Kukopa na Kurejesha kwa mujibu wa Masharti na Sera za Chama;
7 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
(d) Kuhudhuria Mikutano yote ya Wanachama kama ilivyoainishwa ndani
ya Masharti
14. Haki za Mwanachama:-
(a) Kuchagua au kuchaguliwa kwenye uongozi;
(b) Kupata taarifa zote za maendeleo ya Chama;
(c) Kutoa Maoni Binafsi kwa Maendeleo ya Chama;
(d) Kupata Mikopo kutoka kwenye Chama kulingana na Masharti;
(e) Kupata Stakabadhi za malipo yote anayolipa kwenye Chama;
(f) Kukishtaki Chama au Uongozi wa Chama pale anapoona kuna
ukiukwaji wa taratibu za Chama au kupotea kwa mali za Chama;
(g) Kupata riba itokanayo na Akiba na Amana zake ndani ya Chama;
(h) Kupata gawio kwenye Hisa zake zilizo ndani ya Chama
15. Daftari la Wanachama:-
(a) Chama kitakuwa na Daftari la Wanachama wote likiwa na taarifa
zifuatazo:
i. Majina ya Mwanachama
ii. Tarehe ya Kujiunga na Chama
iii. Nambari ya Uanachama
iv. Idadi na Nambari ya Stakabadhi ya Hisa na Thamani zake
v. Picha ya Mwanachama
vi. Nambari ya Shahada ya Mwanachama
(b) Taarifa hizi katika Daftarti la Wanachama zitakuwa zinaboreshwa mara
kwa mara
8 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
SEHEMU YA TANO
KIINGILIO, HISA, AMANA NA AKIBA ZA CHAMA
16. Kiwango Cha Kiingilio, Hisa, Amana na Akiba:-
(a) Viwango vya Kiingilio, Hisa na Akiba vitakuwa vikipangwa na Bodi ya
Chama na kuidhinishwa na Mkutano Mkuu;
(b) Kiwango cha Amana kitakuwa kulingana na uwezo wa Mwanachama
atakavyojiweza.
17. Kiingilio:-
(a) Mtu atakayekubaliwa kujiunga na Chama atawajibika kulipa ada ya
Kiingilio;
(b) Mwanachama hatarejeshewa Kiingilio chake endapo uanachama wake
utakoma;
(c) Kiwango cha Kiingilio kitakuwa TZS 10,000/= (Shilingi za Kitanzania
Elfu Kumi Tu);
18. Hisa:-
(a) Hakuna Mwanachama atakayeruhusiwa kumiliki hisa zaidi ya moja ya
tano (1/5) – yaani asilimia ishirini (20%) ya hisa zote za Chama;
(b) Kwa mujibu wa kifungu cha 9(a) na (b) cha masharti haya,
mwanachama anayetaka kuchukua hisa na akiba zake au sehemu,
anatakiwa kutoa taarifa ya siku 90 kwa maandishi;
(c) Mwanachama haruhusiwi kupunguza hisa zake hadi kufikia chini ya
hisa kumi;
(d) Mwanachama anaweza:-
i. Kurithisha hisa zake;
ii. Kuuza hisa zake kwa Mwanachama mwingine;
iii. Kuzihamisha kwenda kwa Mwanachama mwingine;
(e) Kila Mwanachama atakuwa na hati yake ya Hisa (Share Certificate) na
kuingizwa kwenye daftarti la Wanachama
9 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
19. Akiba:-
(a) Kila Mwanachama atatakiwa kuweka Akiba mara kwa mara ili itumike
kama kigezo cha kukopea mkopo;
(b) Mwanachama atapata faida inayotokana na Akiba zake mara moja kwa
Mwaka, kwa kadri itakavyopendekezwa na Mkutano Mkuu;
(c) Kiwango cha lazima cha Akiba cha kila Mwezi kitakatwa moja kwa moja
kutoka kwenye mshahara wa Mwanachama; ila Mwanachama anaweza
kuweka kiwango cha ziada moja kwa moja kwenye akaunti yake ndani
ya Chama;
(d) Mwanachama aliye na mkopo, hataruhusiwa kupunguza akiba zake
chini ya nusu (1/2) ya madeni yake ndani ya Chama.
(e) Kila mwanachama atatakiwa kuweka kiwango cha lazima cha Akiba;
ingawa anaruhusiwa kuweka kiwango chochote juu ya hapo kadri
awezavyo ili kuongeza Akiba zake;
(f) Mwanachama anaweza kuweka kiwango cha ziada moja kwa moja
kwenye Akaunti ya Chama iliyo Benki;
(g) Taratibu na viwango mbalimbali vya Akiba vitatajwa katika Sera na
Taratibu za Bidhaa na Huduma (Policy and Procedures for Products and
Services);
20. Amana:-
(a) Kila Mwanachama anahimizwa kufungua Akaunti na kuweka Amana
zake ndani ya Chama;
(b) Kutakuwa na aina mbalimbali za amana kulingana na mahitaji ya
wanachama;
(c) Kila Akaunti ya Amana itakuwa inalipwa faida kila mwisho wa kipindi au
mwisho wa mwaka, kulingana na Sera na Taratibu za Bidhaa na
Huduma;
(d) Viwango, gharama, utaratibu na aina mbalimbali za Amana zitakuwa
kwenye Sera na Taratibu za Bidhaa na Hududma.
10 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
SEHEMU YA SITA
VYANZO NA UWEKEZAJI WA FEDHA ZA CHAMA
21. Vyanzo vya Fedha ya Chama ni: -
(a) Akiba na Amana za wanachama;
(b) Hisa za Wanachama;
(c) Fedha zinazotokana na viingilio na michango maalum au ruzuku, na
misaada mbalimbali;
(d) Mikopo kutoka Mabenki au Taasisi nyingine za fedha;
(e) Adhabu zinazotolewa kwa wanachama;
(f) Ziada halisi ya Chama;
(g) Akiba ya lazima na malimbikizo mengine;
(h) Mapato kutokana na Vitega uchumi (investments);
(i) Mapato yatokanayo na mikopo mibaya;
(j) Mapato yatokanayo na gharama za mikopo.
22. Uwekezaji wa Fedha za Chama:-
(a) Kutoa Mikopo kwa Wanachama;
(b) Kuweka Amana kwenye Mabenki;
(c) Kuwekeza katika Hisa au vitega uchumi vingine ili kuongeza faida
katika Chama;
SEHEMU YA SABA
MWAKA WA FEDHA, MAHESABU YA CHAMA NA MGAO WA ZIADA
23. Mwaka wa Fedha:-
(a) Mwaka wa fedha wa Chama utakuwa kuanzia tarehe 01 Januari hadi
tarehe 31 Disemba ya kila mwaka;
(b) Mwaka wa fedha unaweza kubadilishwa na wanachama katika Mkutano
Mkuu
11 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
24. Mahesabu ya Chama:-
(a) Chama kitaandika vitabu na mahesabu kutunza kumbukumbu muhimu
kulingana na Sheria ya Ushirika na Kanuni za Kiuhasibu kulinga na Bodi
ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu;
(b) Wajumbe wa Bodi ya Chama watapitia mfumo wa hesabu na utunzaji
wa kumbukumbu za Chama kila mwaka kwa kushirikiana na Mkaguzi
wa Vyama au Mkuguzi mwingine atakayependekezwa na Bodi; na
kuidhinishwa na Mkutano Mkuu;
(c) Wajumbe wa Kamati ya Usimamizi watakagua vitabu na kumbukumbu
za Chama wakati wowote;
(d) Chama kitaanda taarifa za fedha kwa ajili ya ukaguzi kulingana na
Kanuni za Uhasibu;
(e) Gharama za Ukaguzi wa Chama zitalipwa na Chama;
(f) Chama kitakuwa na Sera na Mwongozo wa Kutunza Vitabu na
Kumbukumbu, na Utaratibu Maalum wa Fedha (Accounting and
Finance Manual);
(g) Chama kitafuata taratibu za uhasibu kama zinavyoainishwa na Bodi ya
Uhasibu na Ukaguzi (NBAA) katika kutunza vitabu vya hesabu na
kumbukumbu nyingine.
25. Mgao wa Ziada:-
(a) Kila mwaka Chama kitatenga kiasi kisichopungua asilimia thelathini
(30%) kutokana na faida halisi kwa ajili ya akiba ya lazima ambayo
itaweza kutumika kwa kufidia hasara zisizoweza kuepukika;
(b) Chama kitatenga asilimia kumi (10%) ya faida halisi kwa ajili ya mfuko
wa Elimu;
(c) Asilimia kumi na tano (15%) ya faida halisi itatengwa kwa ajili ya
kukombolea hisa;
(d) Asilimia kumi na tano (15%) ya faida halisi itatengwa kwa ajili ya
Madeni mabaya (bad and doubtful debts);
(e) Akiba ya lazima itabakia kuwa ni mali ya Chama hiki na haitaweza
kugawanywa isipokuwa kama Chama kimevunjwa;
12 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
(f) Bodi ya Chama inaweza kupendekeza kwa Mkutano Mkuu kuongeza
mifuko mingine iwapo Chama kina Mapato halisi ya kutosha;
(g) Baki itagawanywa kwa mgawo kwa kutumia kiwango cha hisa na
nyingine kwa ajili ya mipango ya maendeleo;
(h) Ziada iliyobaki, yaani asilimia thelathini (30%) itagawanywa kama
gawio la kwenye hisa (dividends) na shughuli mbalimbali za maendeleo
baada ya vitabu kufungwa na ukaguzi kufanywa. Hii ni pamoja na
kutoa faida kwa akiba za wanachama;
(i) Gawio sio lazima liwe kwa fedha taslimu; bali linaweza kulipwa kwa
kuongeza akiba au hisa za Mwanachama;
SEHEMU YA NANE
FEDHA ZA CHAMA
26. Kuhifadhi Fedha za Chama:-
(a) Wanachama, kupitia katika Mkutano Mkuu, wataidhinisha
mapendekezo ya Bodi juu ya Benki itakayotumika kuhifadhi Fedha za
Chama;
(b) Malipo yote ya Chama, yatafanyika kwa njia ya hundi, TISS, Internet
Banking, nk; hata hivyo Bodi inaweza kutenga kiasi chochote kidogo
(petty cash) ili kukidhi matumizi madogo ndani ya Chama;
(c) Fedha yote ya Chama isipokuwa ile inayohitajika kwa matumizi
madogomadogo itahifadhiwa kwenye Akaunti ya Chama ndani ya
Benki;
(d) Fedha ambayo haitumiki kwa mikopo kwa Wanachama yaweza
kuwekwa katika:
i) Benki.
ii) Kuwekeza katika rasilimali kama Bodi itakavyoona inafaa;
13 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
iii) Mikopo au hisa za Vyama vingine vya akiba na mikopo,
lakini visizidi asilimia ishirini na tano (25%) ya jumla ya
rasilimali ya Chama.
SEHEMU YA TISA
AKIBA NA AMANA
27. Taratibu za Uwekaji Akiba:-
(a) Kila Mwanachama atakayejiunga na Chama atapatiwa kitabu cha akiba
(pass book) ambacho kitaonyesha kiasi cha akiba na amana
alichoweka, kiasi cha mkopo alichokopa na baki ya hisa zake ndani ya
Chama;
(b) Vitabu vya akiba vitawekwa nambari zinazofuatana na mara moja
vitatolewa kwa Wanachama. Nambari ya vitabu hivi itaandikwa kwenye
daftari la Wanachama na kadi/leja yake ya akiba, amana na mikopo;
(c) Tarehe ya malipo ya hisa na kiingilio vilivyolipwa na Mwanachama
mpya viingizwe kwenye safu ya kitabu inayohusika na kuwekwa sahihi
na Meneja au mtu mwingine aliyeidhinishwa kupokea fedha; kisha
kitabu hicho apewe mwanachama kikiwa kama stakabadhi yake rasmi
na kumbukumbu ya shughuli zake zote za baadaye;
(d) Vitabu vya akiba na amana vitatunzwa na Wanachama wenyewe.
Kitabu kikipotea na upotevu huo ukathibitishwa na Bodi ya chama
kitabu kingine kitatolewa na Mwanachama atatakiwa kulipa ada ya
kiasi kitakachowekwa na Bodi ya chama;
(e) Kitabu cha akiba na amana ni budi kionyeshwe wakati wote wa kuweka
na kuchukua fedha ili watendaji waweze kuingiza kiasi kilichowekwa au
kuchukuliwa;
14 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
(f) Chama kitakuwa na Sera na Taratibu ya Bidhaa na Huduma za Akiba
na Amana itakayoelezea aina, faida na sifa za Bidhaa za Akiba na
Amana
SEHEMU YA KUMI
MIKOPO
28. Taratibu za Mikopo
(a) Mikopo itatolewa kwa Wanachama wa Chama tu;
(b) Mwanachama mpya hataweza kukopeshwa mpaka atakapokuwa na
muda wa miezi mitatu kwenye Chama kama mwanachama kamili, au
vinginevyo kwa idhini ya Bodi;
(c) Mkopo hautatolewa kwa Mwanachama yeyote zaidi ya mara tatu ya
akina zake alizonazo kwenye Chama, na hataweza kukopeshwa zaidi ya
asilimia tano (5%) ya mali yote ya chote;
(d) Chama kitakuwa na Sera na Taratibu za Bidhaa na Huduma za Mikopo
zitakazobainisha aina ya mikopo, sifa za mkopaji, utaratibu na
mchakato mzima wa kutoa mikopo kwa Wanachama.
SEHEMU YA KUMI NA MOJA
MIKUTANO YA CHAMA
29. Aina ya Mikutano ndani ya Chama:-
(a) Mkutano Mkuu wa Mwaka;
(b) Mkutano Mkuu wa Kawaida;
(c) Mkutano Mkuu Maalum
15 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
30. Mkutano Mkuu wa Mwaka:-
(a) Madaraka Makuu yanayohusu Chama yatakuwa mikononi mwa
Wanachama katika Mkutano Mkuu;
(b) Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama utafanyika mara baada ya
kufunga mwaka wa chama na ndani ya miezi tisa (9) baada ya mwisho
wa mwaka wa hesabu;
(c) Mambo yafuatayo lazima yajadiliwe katika Mkutano Mkuu wa mwaka:-
i. Kusoma na kuthibitisha mambo ya mkutano uliopita.
ii. Kupokea na kujadili taarifa ya mwaka ya mahesabu ya mkaguzi
(Auditor)
iii. Kupokea na Kujadili taarifa ya:
I. Bodi
II. Kamati mbalimbali
iv. Kujadili na kupitisha mgawo wa ziada kwa kuzingatia masharti
ya chama, kanuni na sheria ya Vyama vya Ushirika ya 2003;
v. Kuidhinisha ununuzi/au uuzaji wa mali ya Chama ambayo
hayakuwa kwenye yenye thamani inayozidi shilingi
10,000,000/= (Shilingi za Kitanzania Milioni Kumi Tu);
vi. Kuidhinisha makisio ya mapato na matumizi kwa mwaka
unaofuata;
vii. Kupanga posho mbalimbali kwa wasio waajiriwa wa chama;
viii. Kuzungumzia mambo mengine yanayohusu maendeleo ya
Chama kwa jumla na kutoa maelekezo ya utekelezaji kwa Bodi
ya Chama;
ix. Kuangalia na kupanga idadi ya wajumbe wa bodi ya chama.
31. Mikutano Mikuu ya Kawaida:-
(a) Kutakuwa na Mkutano Mkuu wa Kawaida angalau mara moja
utakaofanyika wakati wowote katika mwaka wa fedha wa Chama.
(b) Mambo yafuatayo yatajadiliwa katika Mkutano Mkuu wa kawaida:
i. Kuthibitisha muhtasari wa Mkutano uliopita.
ii. Kupokea na kujadili taarifa ya maendeleo ya utekelezaji kutoka
kwa Bodi ya Chama.
16 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
iii. Kuthibitisha kuingizwa na kufukuzwa kwa wanachama.
iv. Kuweka ukomo wa madeni chini ya sheria ya vyama vya
Ushirika ya 2003.
v. Kuchagua, kuwasimamisha au kuwafukuza wajumbe wa Bodi ya
chama.
vi. Kuchagua wajumbe wa kuwakilisha Chama katika Vyama na
Taasisi nyingine zinazohusika na maendeleo ya chama.
vii. Kuzungumzia mambo yote yanayohusu maendeleo ya chama.
32. Mkutano Mkuu Maalum:-
(a) Mrajisi au mtu Mwingine na aliyeidhinishwa na Mrajis anaweza kuitisha
na kusimamia Mkutano Mkuu au Mkutano Maalum;
(b) Kutakuwepo na Mkutano Mkuu Maalum wakati wowote iwapo
utaitishwa na Mrajisi kwa maombi ya maandishi ya wanachama
wasiopungua theluthi moja (1/3);
(c) Kwa Mkutano Mkuu Maalum ulioombwa na wanachama maombi lazima
yataje sababu za kutaka mkutano huo ufanyike na waombaji lazima
waweke sahihi zao na kupeleka kwa mwenyekiti wa chama na nakala
kwa Afisa Ushirika;
(d) Mkutano Mkuu Maalum hautazungumzia mambo zaidi ya yale
yaliyotakiwa kuzungumzia katika mkutano huo;
(e) Gharama zote za mkutano zitalipwa na chama.
33. Taarifa za Mikutano:-
(a) Matangazo ya Mkutano yatabandikwa katika ofisi ya Chama na
kutumwa kwenye matawi yote ya CRDB Bank LTD kwa kutumia
taratibu zinazokubalika katika sehemu hiyo. Tangazo hili litabidi
lionyeshe waziwazi tarehe ya Mkutano, saa, mahali pa mkutano na
mambo yatakayozungumziwa.
34. Muda wa Matangazo:-
(a) Muda wa matangazo ya mikutano utakuwa:
i. Kwa Mkutano Mkuu wa Mwaka si chini ya siku 21.
17 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
ii. Kwa Mkutano Mkuu ya Kawaida si chini ya siku 21.
iii. Kwa Mkutano Mkuu Maalum si chini ya siku 7.
(b) Wanachama watakumbushwa kwa njia ya simu na barua pepe kuhusu
siku ya mkutano pale itakapowezekana;
35. Mahudhurio kwenye Mikutano:-
(a) Mahudhurio katika mikutano ya chama yatabidi kuwa si chini ya nusu
ya Wanachama wote au wanachama 100, ukichukulia idadi yoyote iliyo
ndogo;
(b) Kwa mkutano maalum uliothibitishwa na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika
idadi yoyote ya Wanachama waliohudhuria wataendesha mkutano na
yote yatakayozungumzwa ni halali;
(c) Kwa mikutano mikuu ya mwaka na kawaida, ikiwa mahudhurio
hayatoshi baada ya saa 1.30 ya saa zilizopangwa, mkutano
utaahirishwa kwa siku saba na mambo yatakayozungumzwa ni yale
yale ya mkutano ulioahirishwa. Iwapo mahudhurio hayatoshi tena
maazimio yanaweza kutolewa kwa idadi isiyopungua (2/3) ya
waliohudhuria; na maamuzi yatakayofanywa yatakuwa halali;
(d) Kwa Mkutano Mkuu maalum ulioitishwa na wanachama, Mkutano
utafutwa kabisa iwapo mahudhurio hayatoshi;
(e) Wanachama waliopo Makao Makuu ya CRDB Bank PLC na matawi
yaliyopo Dar es salaam watachukua dhamana ya kuendesha shughuli
zote za chama. Wanachama katika matawi nje ya Makao Makuu
wataendelea kuhudumiwa na Chama na mambo yafuatayo
yatazingatiwa: -
i. Viongozi wa Chama watatoka katika Makao Makuu ya Chama na
matawi yaliyopo Dar es salaam.
ii. Mikutano ya Wanachama itafanyika iwapo waliohudhuria mkutano
huo ni zaidi ya nusu ya wanachama waliopo Makao Makuu na
matawi ya Dar es salaam, au Wanachama 100, namba yeyote iliyo
chini;
18 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
iii. Kwa Mkutano Mkuu wa Mwaka, wanachama walioko kwenye
Matawi nje ya Dar es Salaam, ikiwa tawi lina Wanachama angalau
kumi (10), watamchagua mwakilishi mmoja kutoka tawi hilo ili
kuwawakilisha wenzake;
iv. Wawakilishi wa Wanachama walioko nje ya Mkoa wa Dar es
Salaam, watakuwa wanachaguliwa mara moja kwa Mwaka, na
muda wao utaisha pale tu Mkutano Mkuu wa Mwaka na Mkutano
Mkuu wa Kawaida inapomalizika
36. Uendeshaji wa Mikutano ya Chama:-
(a) Mwenyekiti wa Chama ataendesha mikutano yote isipokuwa ule
Mkutano Mkuu Maalum ulioitishwa na Mrajis, ambao utaendeshwa na
Mrajis mwenyewe au mtu atakayeteuliwa na Mrajis kuwa Mwenyekiti.
(b) Mwenyekiti akiwa hayupo, makamu wake ataongoza mkutano, na
iwapo wote wawili hawapo katika muda wa dakika 15 baada ya
mkutano kuanza mtu yeyote katika waliohudhuria atachaguliwa kuwa
mwenyekiti wa muda na ataongoza mkutano huo;
(c) Utaratibu utakaofanywa katika kuendesha mikutano mikuu ni kama
ilivyo katika kanuni ya 27 na 28 ya sheria ya Vyama vya Ushirika.
SEHEMU YA KUMI NA MBILI
BODI NA KAMATI ZA CHAMA
37. Bodi ya Chama:-
(a) Kutakuwa na Bodi ya Chama ambayo itachaguliwa na Mkutano Mkuu
wa Wanachama;
(b) Wajumbe wa Bodi hiyo watashika madaraka yao kwa muda wa miaka
tisa, theluthi moja ya Wajumbe wa Bodi watajiuzulu baada ya miaka
mitatu (3). Nusu ya Wajumbe waliobaki watajiuzulu baada ya miaka
sita [(Act Sec.63 2-3)].
19 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
(c) Utaratibu wa kujiuzulu kwa Bodi hiyo utakuwa kwa zamu na itapangwa
katika mkutano wa kwanza baada ya kuandikishwa chama. Wajumbe
wanaojiuzulu wanaruhusiwa kugombea tena nafasi ambazo zitakuwa
wazi;
(d) Hakuna mjumbe wa Bodi atakayekuwa na haki ya kudai malipo ya
mshahara au posho, isipokuwa kama ilivyoelezwa katika masharti
haya;
(e) Bodi ya chama itakuwa na wajumbe si chini ya watano na hawatazidi
tisa akiwemo mwenyekiti na makamu wake (S. 63);
(f) Bodi ya Chama itafanya mikutano yake ya kawaida mara moja kila
mwezi.
(g) Bodi inaweza kufanya mkutano usio wa kawaida wakati wowote.
Mahudhurio ya wajumbe wengi wa Bodi ya Chama yatahitajika kwa kila
mkutano;
(h) Mwenyekiti au Makamu wake wataongoza Mkutano wa Bodi. Kama
wote hawapo kikao kitamchagua mwenyekiti wa muda miongoni mwa
wajumbe waliopo;
(i) Mjumbe wa Bodi ataacha madaraka kama atafukuzwa na Mkutano
Mkuu, au sababu yoyote kama ilivyo katika kanuni ya 49 ya Kanuni za
Vyama vya Ushirika ya mwaka 2004;
(j) Mjumbe wa Bodi atakishindwa kuhudhuria vikao vitatu mfululizo bila ya
sababu inayokubaliwa na Bodi ya Utendaji, anaweza kuachishwa
uongozi na kuteuliwa Mwanachama mwingine badala yake hadi
Mkutano Mkuu unaofuata;
(k) Bodi inaweza kuchagua kamati ndogondogo kama itakavyoona inafaa,
kwa ajili ya utekelezaji bora zaidi wa kazi za Chama;
(l) Bodi ya Chama itakuwa na mamlaka ya kusimamia shughuli za kawaida
za chama, mali na kazi ambazo kwa jadi hufanyika na Bodi ya Chama
cha Ushirika;
(m) Bodi ya Chama itakuwa na wajibu wa kufanya mambo yafuatayo kwa
mujibu wa kanuni ya 44 Kanuni za Vyama vya Ushirika ya mwaka
2004:-
20 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
i) Kueneza elimu ya uwekezaji wa akiba na mikopo, kuwaelimisha
wanachama kuhusu matumizi bora ya mapato yao.
ii) Kupokea na kujadili maombi ya wanachama wapya na
kuyafikisha mbele ya Mkutano Mkuu ili kuidhinisha.
iii) Kuhakikisha kuwa wakopaji wanalipa madeni yao kama
walivyoahidi na kuwachukulia hatua za kisheria wakopaji wasio
waaminifu.
iv) Zitokeazapo nafasi katika Bodi ya Ushirika au Kamati ya Mikopo
au usimamizi kutakuwa na mtu wa kuteuliwa kwa wingi wa
kura za wajumbe walioko katika Bodi ya Utendaji ya wakati ule.
Wanakamati watakaoteuliwa vilevile watashika nafasi hizo
mpaka Mkutano mwingine mkuu wa mwaka ambako nafasi
zilizo wazi zitajazwa kwa kura na wanachama.
v) Kuweka taratibu za uendeshaji wa shughuli za akiba na mikopo
ila kwa masharti kwamba taratibu hizo zisikiuke sheria na
kanuni za vyama vya ushirika.
vi) Kuajiri kulingana na matakwa ya usimamizi wa Chama,
kusimamia na kufukuza watumishi pale inapohitajika;
vii) Kusimamia matumizi yote ya Chama isipokuwa kazi ya
kuidhinisha maombi ya mikopo kulingana na masharti ya utoaji
mikopo yaliyowekwa na Bodi hii na Mrajisi wa Vyama vya
Ushirika.
viii) Kufikisha mbele ya Mkutano Mkuu wa mwaka mapendekezo ya
makisio, na hesabu ya mapato na matumizi, mizania na taarifa
ya ukaguzi aliyothibitishwa na Mrajisi wa Vyama vya ushirika.
ix) Muhtasari wa majadiliano na maazimio yote ya Mikutano ya
Bodi ya Ushirika ni budi yaandikwe katika kitabu cha
kumbukumbu za mikutano na kutiwa sahihi na Mwenyekiti,
Katibu wa Wajumbe wote waliohudhuria.
x) Katika kuendesha shughuli za Chama, Bodi itatumia busara
kama wafanyabiashara wa kawaida, hasara yoyote itakayotijea
Chamani kutokana na Bodi kutojali wajibu wao na madaraka
waliyopewa na wanachama, itawalazimu kufidia hasara hiyo.
21 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
xi) Kusimamia kazi ya urejeshaji wa mikopo kutoka kwa
wanachama na kuidhinisha ufutaji wa mikopo ambayo
imeshindikana kabisa kulipwa.
xii) Kutoa mapendekezo ya kusimamisha uanachama wanachama
au mjumbe yeyote wa kamati ya mikopo na ya usimamizi
kutokana na tabia mbaya au kushindwa kutimiza wajibu wake
wa kazi na kupeleka mapendekezo kwa mkutano mkuu
unaofuata ili uamuzi wa mwisho utolewe.
xiii) Bodi ya Chama cha Ushirika itakuwa na madaraka kuongoza
shughuli za maendeleo ya chama hiki.
38. Kamati Ndogo ya Mikopo:-
(a) Itakuwa ni juu ya Kamati ndogo ya mikopo kuyapitia maombi yote ya
mikopo, kuhakikisha kwamba mkopo huo utakuwa na manufaa kwa
mkopaji na kuchunguza kama dhamana iliyotolewa kwa uamuzi wao
itatosha na mapatano yaliyofanywa kama ni sawa;
(b) Idadi ya Wajumbe wa Kamati ya Mikopo itakuwa ni watatu (3) ambayo
itachaguliwa na wajumbe wa Bodi kutoka miongoni mwao;
(c) Wajumbe wa kamati ndogo ya mikopo watachaguliwa kwa muda wa
miaka mitatu, ingawa wanaweza kuchaguliwa tena kwa kipindi kingine
kama ataendelea na ujumbe wa Bodi;
(d) Wajumbe wa kamati ndogo ya mikopo watachagua miongoni mwao
mwenyekiti. Katibu wa kamati hii atakuwa ni Afisa Mikopo ambaye
atatengeneza na kuweka kumbukumbu sahihi za mambo yote
yatakayofanywa na kamati ya mikopo;
(e) Shughuli za mwenyekiti na katibu zinaweza kufanywa na mtu mmoja.
(f) Kamati ya mikopo itafanya mikutano kama vile shughuli za Chama hiki
zitakavyohitaji lakini siyo chini ya mara moja kwa kila mwezi. Taarifa ya
mikutano hiyo itatolewa kwa wanachama jinsi itakavyoamuliwa na
kamati hiyo mara kwa mara.
(g) Idadi ya juu ya jumla ya wanakamati wote itatosha kuendesha
shughuli katika mikutano.
22 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
(h) Kwa wingi wa kura, Kamati ya Mikopo inaweza kumchagua Afisa au
Maofisa wa Mikopo kufanya kazi kama itakavyohitajika na Kamati na
kumpa uwezo wa kuidhinisha mikopo kwa kadri ya kiasi
kitakachowekwa na Kamati.
(i) Mchakato na undanii wa kazi za Kamati ya Mikopo utabainishwa katika
Sera na Taratibu za Bidhaa na Huduma ya Mikopo
39. Kamati ya Usimamizi:-
(a) Kamati ya usimamizi itachaguliwa na Wanachama na itakuwa na
Wajumbe wasiozidi watatu ambao ni Wanachama wa Chama;
(b) Mwanachama yeyote wa Kamati ya Mikopo au mtumishi yeyote wa
Chama hiki hatastahili kuchaguliwa katika Kamati hii;
(c) Wajumbe wa Kamati hii watashika madaraka yao kwa muda wa miaka
mitatu, na wanaweza kuchaguliwa tena;
(d) Theluthi moja ya wajumbe itajiuzulu kila mwaka na wanaweza
kuchaguliwa tena.
(e) Wajumbe wa Kamati ya usimamizi watatengeneza utaratibu wao wa
kutosheleza kazi za Kamati hiyo. Katibu atatengeneza, atahifadhi na
atazichunguza kumbukumbu zote pamoja na hatua zitakazochukuliwa
na Kamati hiyo. Kazi ya Mwenyekiti na Katibu inaweza kushikwa na
mtu mmoja.
(f) Kamati hii itakuwa na kazi zifuatazo:
i) Usimamizi na ukaguzi wa fedha na rasilimali zote za Chama kwa
niaba ya Wanachama;
ii) Itakuwa na uwezo wa kuamuru ufanyike uchunguzi pamoja na
ukaguzi wa vitabu wakati wote itakapoona inafaa;
iii) Kutayarisha taarifa ya maandishi juu hali ya fedha na huduma
zitolewazo kwa Wanachama kwa Kamati ya Utendaji na Mkutano
Mkuu na nakala kwa Afisa Ushirika wa Wilaya, Mrajis wa Mkoa,
mara mbili kwa mwaka.
23 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
SEHEMU YA KUMI NA TATU
USIMAMIZI WA SHUGHULI ZA CHAMA
40. Usimamizi wa Shughuli za Chama:-
(a) Bodi itaajiri watu wenye uwezo ili wasimamie shughuli za kila siku za
Chama, akiwemo Meneja;
(b) Shughuli zote za Chama zitasimamiwa na Meneja;
(c) Bodi itaweza kuajiri wafanyakazi mbalimbali kulingana na mahitaji ili
kuendesha shughuli za Chama kwa ufanisi zaidi;
41. Meneja:-
(a) Chama kitamwajiri Meneja ili kusimamia kazi za kila siku za chama kwa
niaba ya Bodi ya Chama.
(b) Kazi za meneja zitakuwa ni kwa mujibu wa kanuni ya 50 ya Kanuni za
Vyama vya Ushirika ya mwaka 2004, na zitabainishwa katika Sera na
Taratibu za Ajira kwa Watumishi wa Chama;
42. Mhasibu:-
(a) Chama kitakuwa na Mhasibu mwenye sifa na ujuzi wa kutunza hesabu
na kumbukumbu za Chama;
(b) Kazi za Mhasibu zitabainishwa katika Sera na Taratibu za Ajira kwa
Watumishi wa Chama.
43. Wawakilishi wa Chama Mikoani:-
(a) Ili kusimamia kwa karibu shughuli za Chama, kutakuwa na Wawakilishi
wa Chama katika Matawi ya Benki yaliyo Mikoani;
(b) Tawi lililo Mikoani lenye wanachama angalau kumi (10) litakuwa na
Mwakilishi mmoja wa Chama atakayekuwa anachaguliwa na
wanachama wenzake tawini, kila mwanzo wa Mwaka wa fedha;
(c) Kwa matawi ambayo hayajafikisha wanachama kumi (10) au idadi ya
wafanyakazi ni ndogo, Mwakilishi wa Chama katika tawi la karibu
24 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
lililokidhi idadi ya wanachama, itampasa kuhudumia matawi haya,
mpaka pale yatakapokuwa na Mwakilishi wao;
(d) Wawakilishi wa Chama watakuwa ndo wawakilishi wa Wanachama
katika Mkutano Mkuu wa Mwaka;
(e) Wawakilishi wa Chama watalipwa posho kulingana na uwezo wa
Chama;
(f) Wasimamizi watapewa Hadidu za Rejea na malengo wanayotakiwa
kufikia kwa Mwaka;
(g) Wasimamizi wa Shughuli za Chama watakuwa na kazi zifuatazo:-
i. Kuhamasisha wafanyakazi wote walio kwenye tawi kuwa
wanachama katika Chama;
ii. Kuelimisha wanachama na wasio wanachama kuhusiana na
utaratibu, bidhaa, sera na masharti ya Chama ili kuongeza
muamuko katika kushiriki kwenye shughuli za Chama;
iii. Kutoa maelezo juu ya maswali mbalimbali wanayouliza
wanachama, au wafanyakazi wengine wa Benki, kuhusiana na
Chama na kuwasilisha maoni kwa Meneja wa Chama;
iv. Kuhamasisha wanachama kutumia bidhaa mbalimbali za Chama
– kuongeza Akiba, kuweka Amana, kukopa na kununua Hisa
zaidi;
v. Kutoa taarifa ya hali ya Ushindani dhidi ya bidhaa za Chama
katika Tawi au Taasisi nyingine zinazowahudumia wafanyakazi
wa Benki Tawini;
vi. Kuwawakilisha wanachama katika Mkutano Mkuu wa Mwaka;
vii. Kuandaa au kuratibu mafunzo ya kwa wanachama katika
matawi yao;
viii. Kuratibu mawazo mapya kutoka kwa wanachama na wasio
wanachama kwenye tawi juu ya uboreshaji wa shughuli na
bidhaa za Chama;
25 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
SEHEMU YA KUMI NA NNE
KUFUTWA KWA CHAMA NA MENGINEYO
44. Kufutwa kwa Chama:-
(a) Chama hiki kinaweza kufutwa katika daftari la vyama kwa amri ya
Mrajis chini ya kifungu cha 100 cha sheria ya Vyama vya Ushirika ya
2003.
45. Mengineyo:-
(a) Sera na Taratibu za Chama – Chama kitakuwa na Sera na Taratibu
mbalimbali katika kuhakikisha kinasimamia rasilimali na kuendesha
shughuli zake, kama ifuatavyo:-
i) Sera na Taratibu za Bidhaa na Huduma za Mikopo;
ii) Sera na Taratibu za Bidhaa na Huduma za Amana na Akiba;
iii) Sera na Taratibu za Fedha na Hesabu ya Chama;
iv) Sera na Taratibu za Ajira kwa Watumishi wa Chama;
v) Sera na Taratibu za Uendeshaji wa Chama;
(b) Siri juu taarifa za Chama – wajumbe wa Bodi, Kamati mbalimbali, na
watumishi wa Chama, watatunza siri kuhusu maisha binafsi ya
Wanachama, isipokuwa masuala ya utoaji na ukusanyaji wa mikopo
ambayo Bodi ya Chama inaweza kuchukua hatua zozote za lazima dhidi
ya wasiokuwa waaminifu;
(c) Bima ya Uaminifu – Chama kitakata bima ya Uaminifu (Fidelity
Insurance) kulinda rasilimali za Chama dhidi udanganyifu na wizi
utakaoweza kufanywa na Wajumbe wa Bodi, Kamati ya Usimamizi na
Watumishi wa Chama;
(d) Upatikanaji wa Taarifa za Chama – Vitabu vya hesabu na kumbukumbu
nyingine za Chama hiki zinaweza kuchunguzwa wakati wowote na
wajumbe wa Kamati mbalimbali za Chama. Mwanachama yeyote
atakuwa na haki ya kutazama masharti, mizania, muhtasari ya
mikutano mikuu na nyaraka za Mrajis.
26 Copyright ©2014. CRDB Workers SACCOS Limited
(e) Migogoro au Malalamiko – migogoro au malalamiko yoyote kuhusu
masharti au huduma za Chama hiki kwa wanachama wa sasa au wa
zamani na kati ya wanachama ipelekwe kwa Mrajisi wa Vyama vya
Ushirika ambaye uamuzi wake kuhusu shauri lolote utakuwa wa
mwisho.
(f) Uzembe katika Uendeshaji – Iwapo chama kitapata hasara kutokana na
uzembe, ubadhirifu au matumizi mabaya ya fedha, Wajumbe wa Bodi
watawajibika kufidia hasara yote iliyotokana na utendaji wao;
(g) Mapitio ya Masharti – Masharti haya, kama kuna marekebisho au
maboresho yoyote, yatapendekezwa na kupitishwa na wanachama
katika mikutano ya Wanachama. Mapitio ya Masharti haya yatakuwa ni
mara moja kwa mwaka.
(h) Mapendekezo ya masharti haya yameandaliwa na Wajumbe wa Bodi na
Kamati ya Usimamizi – kama walivyooredheshwa hapa chini, kwa ajili
ya kupitishwa na wanachama:-
Na. Jina la Mjumbe wa
Bodi Cheo Saini
1 JOHN FIDELIS KOMBA Makamu Mwenyekiti wa Bodi
2 OMARY KILIMA Mjumbe wa Bodi
3 LEONARD KOSIA Mjumbe wa Bodi
4 MAKAYE MAO Mjumbe wa Bodi
5 THEOPHIL AKARO Mjumbe wa Bodi
6 HAMISI MHINI Mjumbe wa Bodi
7 ANNA MSOFE Mjumbe wa Bodi
8 BENJAMINI KOMBA Mjumbe wa Bodi
9 GODWIN SEMUNYU Mjumbe wa Bodi
10 Leevan Maro Mjumbe Kamati ya Usimamizi
11 John Mtindo Mjumbe Kamati ya Usimamizi
12 Negwako Mvungi Mjumbe Kamati ya Usimamizi